Tumemsikia Kinana kupitia kwa Nape; CCM wamealika mapambano na Watanzania Oktoba, hofu

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,071

Kinana kupitia kwa Nape ni kualika mapambano, hofu ya kuondoka madarakani

Kwa siku za karibuni, ukitaka kujua uwezo wa kufikiria na kupanga alionao Katibu Mkuu wa CCM, Kinana ambaye anawakilisha utendaji wa chama hicho kupitia sekretarieti, hauhitaji kuwa mwajiriwa au kutembelea ofisi za chama hicho Lumumba- Dar es Salaam au Dodoma. Unatakiwa kutega sikio tu kusikiliza kila anachoropoka, kwa bahati mbaya au makusudi msemaji wake, Nape Nnauye.

Imefikia mahali hata sekretarieti ya chama hicho chini ya Kinana ikitaka kuendeleza mchezo wa magenge ya chama hicho katika kushughulikiana kwa maslahi binafsi, Nape ndiye huwa anatumwa kusema lolote analoambiwa. Kuropoka. Anathibitisha kwa vitendo lile jina alilowahi kupewa na Mwenyekiti Mstaafu wa BAVICHA, John Heche, aliyemwita 'vuvuzela'.

Ni kupitia Nape, CCM imekuwa ikitoa kauli tenge zinazoendelea kukitafuna chama hicho, ikiwemo ile ya kuwatakia kifo cha haraka akina Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Agustino Ramadhan na wengine waliokuwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa sababu tu walizingatia maoni ya wananchi juu ya muundo wa Muungano wa Serikali Tatu.

Ni kupitia huyo huyo, CCM iliwahi kuzunguka nchi nzima kuutangazia umma wa Watanzania kuwa chama chao kinatakiwa kujivua gamba la ufisadi kwa kuwafukuza makada 3 ndani ya siku 90 vinginevyo kitazidi kukataliwa na watu. Kila mtu anajua kuwa magamba yaligoma kuvuka. Waliotakiwa kufukuzwa leo ndiyo wanapewa hadhi ya viti vya mbele kwenye chama hicho hicho. Nape anaendelea kuropoka.

Kauli ya juzi aliyotumwa Nape kuropoka akiwa Kijiji cha Nyehunge, Jimbo la Buchosa, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza kama ilivyoripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa CCM itashinda uchaguzi na kurudi ikulu hata kwa 'goli la mkono' yaani kwa kuiba kura, kama walilenga kutisha vyama vya upinzani, basi wamekosea mkakati.

Ni kauli ambayo imekuja kwa wakati mwafaka na itatumika kuwaamusha na kuwandaa Watanzania wanaowaka moto wa mabadiliko kujihami dhidi ya uporaji huo unaoandaliwa. Nape kawazindua wananchi na katoa mwaliko wa mapambano ya kutetea sanduku la kura, kulinda kura na kuhifadhi heshima ya demokrasia ya uchaguzi.

Kama tujuavyo uchaguzi huru na haki ni moja ya misingi muhimu katika demokrasia ya ushindani wa vyama vingi. Ni fursa ya wapiga kura kuzungumza mahitaji yao. Kupaza sauti zao ambazo huwa zinapuuzwa kabla ya uchaguzi.

Kuheshimu sauti ya wananchi katika uchaguzi ni kiwango cha juu cha ukomavu wa demokrasia kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Kinyume chake ni kualika vurugu za kisiasa ambazo zimedhihirisha kuwa kikwazo cha ustawi wa jamii nyingi katika nchi za Bara la Afrika hususan zile ambazo zimekuwa chini ya watawala wenye kibri kama CCM, wanaothubutu kupuuza chaguzi na kudharau sanduku la kura.

Kauli hiyo ya Nape kwa Watanzania waliohamasika kiasi cha kukesha na kushinda vituoni, wanaonunua nafasi na kuweka mawe kwenye foleni wajiandikishe kwenye BVR ili wapate nguvu ya kudhihirisha na kuwakumbusha waliopewa dhamana ya kuwa madarakani kwamba mamlaka kuu ya kuongoza nchi iko na inatoka kwa wananchi, si tu inaalika mapambano makubwa bali pia ni matusi kwa wanyonge wanaosubiri kwa hamu kuzungumza kupitia kura.

Kwa mwamko mkubwa na kiu ya mabadiliko ambayo wananchi wameendelea kuionesha kwa vitendo; mifano mizuri ikiwa ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na Serikali za Mitaa mwaka 2014, ambapo wananchi walisimama kidete dhidi ya mitutu ya bunduki, magari ya kuwasha, mabomu ya machozi na uhuni wa Green Guard, kulinda heshima ya sanduku la kura dhidi ya uporaji wa uchaguzi, CCM wasijidanganye kuwa uhuni wanaopanga kufanya utakuwa ni dhidi ya vyama vya siasa! Chochote watakachofanya isivyo halali, wajiandae kupambana na wananchi.

Ndiyo! Kwa dhana ya umuhimu wa uchaguzi ambayo Watanzania wameanza kuielewa baada ya kazi kubwa ya elimu ya uraia na kupiga kura kuenezwa kila mahali nchini, ni wazi kuwa wananchi wapiga kura hawatakubali tena kuendelea kubezwa. Wataitetea haki yao. Ukweli na uhalisia wa yanayoendelea nchini unadhihirisha hilo na historia imekuwa mwalimu mzuri. Hivyo CCM ijiandae kupambana ambayo imeyaalika yenyewe.

Kama CCM wanajiandaa kufunga goli kwa mkono, kwamba wanajiandaa kufanya faulo kwenye uchaguzi yaani kuiba kura na mbinu zingine za kuvuruga uchaguzi, wanawaambia Watanzania kuwa kura zao watakazopiga kuchagua kadri ya uelewa wao hazitakuwa na maana. Kwa hiyo wapiga kura watakuwa na wajibu wa kuzifanya hizo kura ziwe na maana. Kuzitetea na kuzilinda.

Kama huo ndiyo ujumbe wanaopeleka kwa wapiga kura miezi miwili kabla ya uchaguzi, tafsiri iliyofichwa katikati ya maneno yao ni kwamba CCM imeshasahau kuwa msingi wa mamlaka unatoka kwa wananchi na kwamba kiwango cha kibri chao kujiweka juu ya Watanzania sasa kimefikia hatua ya kubeza uchaguzi hadharani kwamba si tendo la maana tena.

Hivyo inawaalika wananchi watafute njia mbadala za kuhakikisha sanduku la kura linaheshimiwa. Kuna njia gani ya kudhibiti uporaji ambao mporaji kwa bahati mbaya au makusudi ameshakutangazia kuwa anajiandaa kuja kupora? Mapambano.

Kupitia mamlaka yao yanayotoa uhalali wa kisiasa na kisheria, mapambano hayo na wananchi, CCM wajiandae kulazimika kuchagua mambo mawili tu; democracy au democazy. La kwanza likitokana na uhalali wa kisiasa na kisheria, la pili likiwa ni tunda la kupuuza wapiga kura na kudharau uchaguzi.

Aidha kwa uropokaji wa Nape anayetumiwa au kutumwa na Katibu Mkuu wake Kinana, CCM si tu kwamba hatimaye wamejivua nguo hadharani kuhusu uovu wao katika kila uchaguzi, bali pia imedhihirisha kile ambacho kimesemwa kwa muda mrefu sasa kuwa chama hicho kinakabiliwa na hofu kubwa mno ya kushindwa uchaguzi wa mwaka huu na kuondolewa madarakani.

Kwa mara ya kwanza chama hicho na wagombea wake wanakwenda kushiriki uchaguzi mkuu bila kuwa na uhakika wa kushinda mahali nafasi yoyote, iwe urais, ubunge, uwakilishi wala udiwani. Hajawahi kukutana na upinzani mkali kama uliopo sasa. Tena wakiwa wamebanwa mfululizo kutoka uchaguzi mmoja kwenda mwingine. Kila mahali. Vijijini na mijini. Mitaani na vitongojini.

Hofu, hofu tupu ya CCM kuondoka madarakani. Hofu humfanya mhusika atokwe na fahamu kwa kiwango cha kujisemea hata ambalo hakukusudia kulisema, kufanya asichokuwa na uwezo nacho. Ya sirini anayaweka hadharani. Kinana na Nape ambao wanajaribu kuisaidia CCM kushika matawi ya mwisho mwisho yanayoteleza wanaujua uhalisia wa hali ngumu inayokikabili chama hicho.

Wanajua katika mizunguko hiyo jinsi ambavyo wananchi wana hasira za kuiondoa CCM. Uelewa wa wananchi kuhusu haki zao uko juu. Wanahusisha maendeleo mabovu na utawala mbovu wa CCM. Wanaunganisha ufisadi, umaskini, ujinga na maradhi na kufeli kwa sera za CCM.

Baada ya muda mrefu kutegemea mbinu ya kusomba watu kwa magari, kuwapikia chakula ili kuhudhuria mikutano yao, imefikia mahali viongozi hao wanalazimika kuwa na 'maonesho' kwenye mikutano yao ili kuwavuta watu. Hali ni mbaya.

Kutokana na ukweli wa namna ambavyo CCM imepoteza uhalali wa kisiasa na ushawishi wa hoja kwa wananchi, wamejikuta wanajawa na hasira iliyowatia hofu na kujikuta wakiropoka kwamba watashinda hata kwa goli la mkono. Hii ni kauli ya mtu asiye na uhakika wa ushindi. Vinginevyo chama hicho kingelikuwa kinakubalika, kauli ya wasiwasi wa kushindwa imetoka wapi?

Unaweza kuiona hofu hiyo ya CCM hata kupitia kwa watia nia wote waliojitokeza kuwania uteuzi wa urais ambao wanalazimika 'kukopi' na 'kupesti' karibu kila kitu ambacho kilisemwa na wapinzani dhidi ya Serikali ya CCM.

Kutokana na hofu ya kushindwa uchaguzi na kuondoka madarakani, CCM wamejikuta sasa wanaalika mapambano na wananchi. Tusubiri tuone.

Makene






 
Ukawa tupo tayari kwa lolote ikiwa jaribio la kuiba kura au ishara yoyote ya kutaka kukisaidia chama cha majambazi CCM itafanyika, tutajibu kila dalili au ishara kwa nguvu ile ile.

Mwaka huu Bora punda afe mzigo ufike.
 
Makene mwaka huu lazima mchimbe shimo mjifukie kinana siyo mwepesi kama zitto kama zitto kawazingua kiasi hicho sijui kinana itakuwaje.
 
Makene mwaka huu lazima mchimbe shimo mjifukie kinana siyo mwepesi kama zitto kama zitto kawazingua kiasi hicho sijui kinana itakuwaje.

Asante. Hofu ile ile umetoa siri hapo katikati ya maneno yako. Alas! Kwa hiyo kumbe hao wawili wanafanya kazi moja sehemu moja, ila tulifanikiwa kushughulika na mmoja ambaye unasema ni mwepesi au siyo?

Hii hofu ya kuondoka madarakani mliyonayo itawafanya mseme yote mwaka huu.

 

Asante. Hofu ile ile umetoa siri hapo katikati ya maneno yako. Alas! Kwa hiyo kumbe hao wawili wanafanya kazi moja sehemu moja, ila tulifanikiwa kushughulika na mmoja ambaye unasema ni mwepesi au siyo?

Hii hofu ya kuondoka madarakani mliyonayo itawafanya mseme yote mwaka huu.




Makene ni mwepesi sana kapiga bonge la ngonjera na inaelekea maneno yote kamezeshwa na bwana zake teh teh jamani wana JF kama vipi nawapa namba yake muwe mnampigia simu hata kumshauri aache kuweweseka maadamu amechagua kula kwenye siasa ajiandae pia kuwa kichaa!
 
Niko tayari kufa kuliko kuona CCM inaiba kura mwaka huu.Kuna maana gani kuwepo kwa uchaguzi wkt chama kimoja wapo kinaiba kura?
 
Makene mwaka huu lazima mchimbe shimo mjifukie kinana siyo mwepesi kama zitto kama zitto kawazingua kiasi hicho sijui kinana itakuwaje.

Makene ni muongo sana kama walivyo hao ndugu zake unakumbuka issue ya hati za muungano Walisimama kuuaminisha umma wa watanzania kuwa hati zile ni fake baada ya kuonyeshwa na Serikali wakazimia, hizi ni propaganda za kitoto aisee na wewe makene ni Kanjanja! Najua utakuja na Id nyingine kutukana!
 
makene ni mwepesi sana kapiga bonge la ngonjera na inaelekea maneno yote kamezeshwa na bwana zake teh teh jamani wana jf kama vipi nawapa namba yake muwe mnampigia simu hata kumshauri aache kuweweseka maadamu amechagua kula kwenye siasa ajiandae pia kuwa kichaa!

mchumba tulia ushughulikiwe
 
naumia sana wakati naona kuna watu wanachochea na kushabikia kauli zinazoweza kuharibu Amani .
 
Niko tayari kufa kuliko kuona CCM inaiba kura mwaka huu.Kuna maana gani kuwepo kwa uchaguzi wkt chama kimoja wapo kinaiba kura?

Bora ufe tu utupunguzie watu wasio na uelewa wanaoongozwa na kiongozi Mwepesi sana Anayejua kuapa na kukana kiapo chake hadharani teh teh Dr.Slaa.
 
Makene ni muongo sana kama walivyo hao ndugu zake unakumbuka issue ya hati za muungano Walisimama kuuaminisha umma wa watanzania kuwa hati zile ni fake baada ya kuonyeshwa na Serikali wakazimia, hizi ni propaganda za kitoto aisee na wewe makene ni Kanjanja! Najua utakuja na Id nyingine kutukana!

Nape na CCM italeta machafuko
 
Back
Top Bottom