Tumbaku: Mtazamo wa Uislamu - 1

mtugani wa wapi huyo

JF-Expert Member
Dec 5, 2012
1,239
1,475
UVUTAJI SIGARA: SUMU YA KIJAMII

Utangulizi;

Uvumbuzi Wa Tumbaku
Tumbaku ilivumbuliwa na mabaharia wa Kispanioli kwenye fukwe za Marekani mnamo miaka ya 1500 (900 H). Tokea kuvumbuliwa kwake, jinamizi la uvutaji sigara limeendelea kuenea duniani kote. Katika wakati wetu wa leo, ni nadra kukuta nyumba ikiwa haijaathirika nayo.

Mwanzoni mwa Karne ya Kumi na Saba, nchi za Ulaya zilitambua hatari za uvutaji sigara na kuipinga. Sheria zilitungwa nchini Uingereza, Urusi, Denmark, Sweden, Austria na nchi nyenginezo, zikizuia uvutaji sigara na kuwaadhibu wenye kukiuka.

Hivi sasa, nchi za Magharibi zinaendelea na majaribio yao ya kuwalinda watu wao kutokana na madhara ya uvutaji sigara. Wanatumia vyombo vya habari, kutunga sheria na kanuni, na kutumia nyanja nyenginezo kuwahamasisha watu kuacha uvutaji sigara. Kwa sababu hiyo, asilimia kubwa ya wavutaji sigara imepunguwa ndani ya nchi hizo.

Uvutaji Sigara Miongoni Mwa Waislamu;
Uvutaji wa sigara ulianzishwa na Wazungu ndani ya nchi za Waislamu mnamo miaka ya 1000 H. Ueneaji wake miongoni mwa Waislamu unafanana kabisa na ule wa Magharibi. Ukweli usiotarajiwa ni kwamba, hata hivyo ndani ya nchi za Waislamu, hakuna taratibu za uzuiaji zilizotumika kuwalinda watu kutokana nayo. Kinyume chake, vyombo vya habari vinaendelea kuupamba uvutaji sigara na kuwahamasisha watu kuvuta sigara. Hili limesababisha madhara ya uvutaji sigara kuendelea kukua ndani ya nchi hizo kwa hatua ambayo imefika kuwa ni vigumu kuidhibiti.

Tabia ya uvutaji sigara imekuwa ni desturi, na kuachana nayo ni hitilafu. Kawaida, watu wanamuangalia kwa mshangao na kumshusha hadhi mtu anayepatiwa sigara akakataa, akiikataa sigara kwa maelezo kwamba havuti sigara.

Kuwakaribisha sigara wageni imekuwa ndio miongoni mwa kanuni za mwanzo za ukarimu. Yeyote asiyempa mgeni wake au kumuhimiza kuvuta sigara atakuwa anakiuka maadili ya ukarimu na uungwana!

Juu ya hivyo, baadhi ya wanaojidai kujinasibisha na Diyn ndio afiriti wa uvutaji sigara. Wanapofuatwa au kukumbushwa na wapinzani wao, wanajibu kwa kutoa dharura dhaifu ili kuthibitisha kwa jina la Uislamu. Wanatoa maelezo ya mzaha kwamba hakuna andiko linalokataza uvutaji sigara moja kwa moja. Hivyo, wanahitimisha kwamba uvutaji sigara sio haramu bali ni makruuh (isiyopendeza). Kwa mtindo huu, wanatoa udhuru mwepesi kwa wasioelewa, na kuanzisha mfano mbaya kwa wengine.

Waislamu wengi wamekumbwa na matamshi kama hayo, wakitumbukia kwenye mtego wa uvutaji sigara usioweza kutokeka. Hili linadhihirika duniani kote. Mfano mkuu ni kwamba ndege zote za Marekani zinazuia uvutaji sigara, mpaka kwa safari za kimataifa; kwa upande mwengine, kwa ndege za Waislamu, mtu anaweza kusafiri katika hali ya kubanwa na pumzi, hata katika safari fupi, kwa sababu ya idadi kubwa ya wavutaji sigara.

Hivyo, inakuwa ni kazi pevu kuandika makala inayotoa ushahidi kuhusiana na hukumu ya uvutaji sigara ndani ya Uislamu. Tunataraji kwamba hili litawanufaisha kaka na ndugu zetu Waislamu; na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuikubali kazi hii kutoka kwetu kama ni tendo lenye kufungamana kupata radhi Zake.

Maana
Uvutaji inamaanisha tendo la kuwasha sigara, kiko, biri, ugoro (tumbaku iliyosagwa) wa puani au mdomoni, kiko ya maji (shisha), kutafuna tumbaku kwa chokaa, popoo, tambuu, au aina nyengine yoyote inayotokana na tumbaku au kitu kinachofanana na hicho chenye taathira sawa. Kitu hicho baadaye kinanyonywa kwenye midomo kwa lengo la kuchimbua moshi. Moshi huu unaingizwa ndani ya kifua na baadaye kutolewa nje kupitia pua na mdomo kwa mtindo wa moshi mweupe. "Uvutaji" hivi sasa una maanisha tendo la kuzalisha moshi huu katika lugha ya Kiingereza, Kiarabu, na lugha nyengine.

Ushahidi Wa Kuzuia Uvutaji Sigara
Kuna sababu nyingi, moja kati ya hizo yatosha kuthibitisha kwamba uvutaji hauruhusiki. Muhimu zaidi ni kwamba, ina madhara katika njia nyingi. Ina madhara kwa Diyn, afya, mazingira, familia, udugu na mahusiano ya kijamii, fedha (mali) n.k. Maelezo yafuatayo yataeleza kwa ufupi ubaya na madhara yake.

Haramu Kwa Diyn
Uvutaji sigara unaharibu matendo ya ibada ya mtu na yanampunguzia malipo. Kwa mfano, inaharibu Swalah, ambayo ni nguzo ya Diyn. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Yeyote anayekula kitunguu thomu au kitunguu maji, akae mbali na sisi na misikiti yetu, na akae nyumbani mwake. Malaika hakika wanaumia kwa mambo ambayo yanawaumiza wanaadamu.)) [Imesimuliwa na Jaabir na Maswahaabah wengine. Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].

Wale wenye unadhifu na maumbile yasiyochafuliwa, hapana shaka yoyote kwamba harufu mbaya inayotoka mdomoni mwa mvutaji sigara inakirihisha na imeoza zaidi kuliko ile inayotoka kinywani mwa mtu aliyekula kitunguu thomu au maji. Hivyo, mvutaji sigara yupo baina ya hiari mbili, aidha kuwadhuru watu wanaoswali kwa harufu yake iliyooza na pia malaika, au kuikosa Swalah ya jama'ah.

Uvutaji sigara pia unaharibu funga.
Swawmu ni ngumu sana kwa mvutaji sigara. Pale tu siku inapomalizika, anakimbilia kuivunja funga yake kwa uovu wa sigara badala ya utamu wa tende au maji safi. Hata kama akifunga katika mwezi wa Ramadhaan, mvutaji ana kuwa dhaifu wa kufunga siku zengine. Hivyo, anapoteza malipo bora ya yule anayefunga angalau siku moja kwa ajili ya Allaah.

Madhara Kwa Mwili Wa Binaadamu
Hakuna mtu atakayeweza kukataa kwamba uvutaji sigara una madhara kwa mwili wa binaadamu. Ushahidi wa kiafya kwa hili umeshatambuliwa na unajulikana sana. Kwa sababu ya hili, sheria ndani ya Marekani na nchi nyenginezo zinalazimisha kuwepo tangazo la onyo kwenye matangazo ya biashara za sigara.

Uvutaji sigara una kemikali za sumu, kama vile nicotine, tar, carbon monoxide, arsenic, benzopyrene na nyenginezo; kwamba mvutaji sigara anameza (sumu hizi) angalau kwa kiwango kidogo. Madhara yake yanajumuisha kufika wakati ambapo athari yake ni kuua kidogo kidogo viungo vya mwanaadamu na nyama nyama (tissues) za mwanaadamu.

Madhara ya kutisha ya uvutaji sigara kwenye afya ni mengi sana na ni vigumu kuyaorodhesha yote. Miongoni mwa madhara yake yanayokubalika kuwa yanatokana na uvutaji wa sigara ni saratani, kifua kikuu, magonjwa ya moyo, pumu, kukohoa, kuzaa kabla ya kufika wakati, mimba isiyodunga vyema, madhara kwenye mfumo wa mkojo, presha ya damu, kuwa na hamaki, maradhi kwenye mdomo na meno n.k.

Maradhi haya huwenda yasitokee kwa wakati mmoja, hata hivyo mvutaji sigara anaweza kwa kiwango kikubwa kuathirika na baadhi ya maradhi hayo kwa kiwango kibaya mno, na kuugua kwake kunaongezeka kila akiwa mzee. Juu ya hivyo, takwimu zinaonesha kwamba umri wa mvutaji sigara, ni, kwa kukisia, miaka kumi pungufu kuliko watu wengine.

Hili latosha kuharamisha sigara. Uislamu unazuia tendo lolote ambalo litasababisha madhara kwa mtu mwenyewe au kwa watu wengine. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

{{Wala msijiue (wala msiue wenzenu.)}} [An-Nisaa, 4: 29]

{{Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.}} [Al-Baqarah, 2: 125]

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((Hakuna madhara yanayoweza kufanywa kwa mtu mwenyewe au kwa wengine.)) [Imesimuliwa na Ibn 'Abbaas na 'Ubaaday. Imepokewa na Ahmad na Ibn Maajah. Imesahihishwa na al-Albaaniy na wengineo].

Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mguu wa mwanaadamu hautaondoka Siku ya Hukumu kutoka katika kisimamo mbele ya Mola wake hadi aulizwe kuhusu mambo matano: maisha yake – namna alivyoyatumia, ujana wake – namna alivyoutumia, mali yake – wapi alipoipata na vipi aliitumia, na namna gani alifuata kile alichokuwa anakijua.)) [Imesimuliwa na Ibn Mas'uud na Abu Barzah. Imepokewa na at-Tirmidhiy. Imesahihishwa na al-Albaaniy].

Na amesema:

((Yeyote anayekula sumu, akijiua mwenyewe kwa hiyo (sumu), basi atakula sumu ndani ya moto wa jahannam, na itamuingia ndani ya tumbo lake daima na kuendelea milele.)) [Imesimuliwa na Jaabir. Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

Madhara Kwa Akili Na Hamasa
Uvutaji sigara una madhara kwa akili ya mwanaadamu na namna ya kutoa hoja. Maelezo ya kina katika hili ni kwamba mtu ambaye ameathirika na sigara anapitia vipindi vibaya vya kuhitaji kuvuta sigara kila wakati, na kumfanya kuwa mgumu wa kufikiri, kuwa makini, kusuluhisha tatizo, au kufanya jambo lolote muhimu, hadi avute sigara.

Pale mtu anapovuta sigara, misuli yake inajiachia, na anapita kipindi cha mapumziko mafupi ya kutokwa na akili yanayogubika tatizo lililomkumba. Mfumo wake wa kutuliza tumbo (digestion) pia unaathirika, na kumsababisha kuathirika na vipindi vya kuwa na wasi wasi kila mara na kupapatika mikono. Anapitia vipindi vya kufurahi ama kuhamaki kwa haraka kabisa na kukosa usingizi.

Hivyo, badala ya kuwa mtumwa wa Allaah, mvutaji sigara anakuwa mtumwa wa sigara. Anaendelea kuwa dhaifu wa kuzidhibiti hisia zake na namna ya kufikiri kwake. Sehemu ya kuwaza ndani ya kichwa, ni sehemu iliyo safi na huru, na ni moja kati ya fadhila Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa watu. Yeye (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameisifu sehemu mbali mbali ndani ya Qur-aan; na Amewataka watu kuitumia kuona ukweli na kumtii Yeye katika njia bora kabisa. Allaah Anawataka waumini kuwa wakakamavu na uwezo wa kudhibiti kutotawaliwa na nafsi. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

{{Na Mwenyezi Mungu Anataka kukukhafifishieni. Lakini wanaofuata matamanio (yao) wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa (ulio khalifu haki).}} [An-Nisaa, 4: 27]

Mvutaji sigara anatoa sumu yake mbele ya uso wa rafiki zake, mkewe, watoto wake, na mazingira. Ni jambo linalojulikana kwamba moshi wa pili takribani una madhara sawa kama ule moshi wa kwanza. Hivyo, iwapo wanapenda au hawapeni, watu wa karibu wa mvutaji sigara wanalazimika kumeza moshi na kuwa wao wenyewe ni wavutaji sigara.

Zaidi ya sumu hiyo ya kawaida inayobebwa ndani ya moshi, iwapo mvutaji ni mwenye maradhi ya kuambukiza, kama vile kifua kikuu na kamasi, moshi wake anaoutoa na kukohoa kwake unabeba maradhi hayo hadi kwa wanaomzunguka.

Juu ya hivyo, mvutaji anawakera watu kwa harufu na sumu yake mbovu ya uvutaji sigara. Iwapo wataugua maradhi ya pumu au madhara mengine, wanalazimika kumtenga. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Yeyote anayemuamini Allaah na Siku ya Mwisho asimuudhi jirani yake.)) [Al-Bukhaari]

Hivyo, uvutaji sigara una madhara yaliyo wazi kwa watu wengine; hili limekatazwa, kama ilivyoeleza ndani ya Hadiyth iliyonukuliwa hapo mwanzo.

Halikadhalika, hakuna shaka yoyote kwamba mvutaji sigara ni rafiki mbaya wa kukaa naye, kama ilivyochorwa ndani ya Hadiyth ifuatayo:

((Mfano wa jaliys (mtu unayeambatana naye) mwema na jaliys mbaya ni kama mfano wa mbebaji miski na mfua chuma (anayevuvia kipulizo). Mbebaji miski ima atakupa au utanunua kutoka kwake au utapata harufu nzuri kwake. Na mfua chuma (anayepuliza kipulizo), ima atachoma nguo zako au utapata harufu mbaya kutoka kwake)) [Al-Bukhaari na Muslim]

Madhara Kwa Mali
Mvutaji sigara anapoteza mali yake kwa kitu ambacho kina madhara na hakina manufaa; ataulizwa kuhusu mali yake na namna alivyoitumia, hili limenukuliwa hapo mwanzo ndani ya Hadiyth. Mali zake ni milki ya Allaah, anadiriki vipi mtu basi kuipoteza kwa kumuasi Yeye? Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

{{Wala msiwape wapumbavu mali zenu (mali zao mlizonazo) ambazo Mwenyezi Mungu Amezijaalia kwa ajili ya maisha yenu (nyote).}} [An-Nisaa, 4: 5]

Na pia:

{{Na umpe jamaa (yako) haki yake, na maskini na msafiri aliyeharibikiwa, wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu.}}

{{Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa maShaytwaan (wanamfuata Shaytwaan). Na Shaytwaan ni mwenye kumkufuru Mola wake.}} [Bani Israaiyl, 17: 26-27]

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Allaah Anachukia mambo matatu: kusengenya, kuomba na kupoteza pesa.)) [Al-Bukhaari na Muslim]

Juu ya hivyo, kuna kesi mbali mbali za kuungua mazulia, fanicha, na hata nyumba nzima na imetambuliwa kwamba umetokana na jambo hili la kuangamiza (sigara).

Uharibifu Wa Maadili
Uvutaji sigara ni mfumo wa kuharibu maadili. Imeenea zaidi miongoni mwa wasio na maadili. Inanasibiana na kufuata kwa upofu watu wasio kuwa Waislamu. Inatumika zaidi ndani ya baa, kumbi za disko, kamari/kasino, na maeneo mengine ya dhambi. Mvutaji anaweza kuomba ama kuiba iwapo hana pesa za kununulia sigara. Ni mtu mwenye tabia mbovu kwa marafiki zake na familia yake, haswa pale anapokosa kupata dozi yake ya kawaida kwa wakati wake.

Jambo Ovu
Uvutaji sigara unahusisha matumizi ya kitu kiovu (khabiyth). Ina harufu mbovu, ladha mbovu, na ni yenye madhara kwa mwili. Hili linatosha kuiharamisha, kwasababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

{{(Mtume) ambaye anawaamrisha mema na anawakataza yaliyo mabaya, na kuwahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao (yaani sharia ngumu za zamani na mila za kikafiri).}} [Al-'Araaf, 7: 157]

Kujifananisha Na Watu Wa Motoni
Mvutaji sigara anaingiza mwilini moshi ambao haumpatii shibe yoyote. Hili linafanana na tendo la watu wa Motoni wanaokula mimea inayochoma na isiyo na manufaa:

{{Hawatakuwa na chakula isipokuwa cha miba.}}

{{Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa.}} [Al-Ghaashiyah, 88: 6-7]

Mfano Mbaya
Mvutaji sigara, iwapo atapenda au kutopenda, anakuwa ni mfano kwa watoto wake na wengine kumuiga. Anawaongoza kutenda jambo hili ovu. Matendo mara nyengine yana madhara zaidi kuliko maneno. Hivyo, hata kama akiwashauri kutovuta sigara au kuwazuia kuvuta sigara, ushiriki wake katika uvutaji sigara unawapatia hoja zaidi ya wao kuvuta sigara.

Tatizo ni baya zaidi pale mvutaji anapokuwa ni mtu mwenye kuheshimika ama mwenye elimu. Katika kesi kama hizo, madhara yake yanahamasishwa zaidi, kwasababu watu wengi wanamchukulia kama ni kiongozi wa kufuatwa na mfano wao, na hivyo wanaongozwa kutokana naye kuelekea njia potofu.

Uadui Mbele Za Watu Wema
Watu wengi wema wanakimbia uvutaji sigara na wanakaa mbali na wavutaji sigara. Hivyo, mvutaji sigara atalazimika kukaa mbali nao – angalau pale anapovuta sigara. Anajiweka mwenyewe katika sehemu ya kutengwa, anavumbua sehemu ya mbali na anajenga uadui baina yake na watu wema, na badala yake ana kuwa karibu na watu waovu. Athari ya hili linakuja wazi zaidi na lenye kuonekana kila wakati unapokwenda mbele. Kuwa makini kwamba hili linatumika sawa kwa dhambi yoyote ambayo mtu anafanya, iwapo ni ndogo au kubwa.

Uwezo Mdogo Wa Kuhimili Matatizo
Mvutaji sigara anajidanganya nafsi yake, kwasababu anahisi kwamba sigara ndogo inampa nguvu. Akitambua udhaifu wake kabla ya matamanio, hili linamfanya kuwa na hisia ya kushindwa anapokutana na matatizo.

Maamuzi Ya Wanachuoni
Tokea uvutaji wa sigara ulipoanza kujulikana kwa Waislamu, wanazuoni wote wakubwa wenye uwezo wa kutoa Ijtihaad (kutoa maamuzi kwenye mazingira mapya) wanakubaliana kuhusu uharamu wake. Hivyo, hakuna thamani ya maamuzi yasiyokuwa na msingi, kwa kutofautisha na hili, maamuzi ya kukubali sigara yanatolewa na wanazuoni wa chini wenye kufuata matakwa ya nafsi zao.

Tahadhari;
Katika mjadala wa mada hii ya kuzuia matumizi ya sigara, kuna baadhi ya indhari muhimu zinahitaji kutajwa:

1. Kama ilivyoelezwa kabla, uzuiaji wa uvutaji sio tu kwa sigara, bali unahusu vitu vyengine vyenye athari zinazofanana kama vile sigaar, kiko, kiko za maji, tumbaku ya kutafuna au ya kunusa, n.k.

2. Hoja zilizotajwa hapo juu kuhusu uzuiaji wa matumizi ya sigara zinatumika pia, na zaidi, kwa aina nyenginezo za madawa ya kulevya na hashishi kama vile marijuana na –ghaat.

3. Uharamu wa sigara sio tu katika kuivuta, bali pia kwa wale wenye kuitoa, kukaa na wale wenye kuvuta sigara, au kuinusa. Yote haya yanahusisha na kuwasaidia watu kutenda madhambi, ambayo yanazuiwa, kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anavyosema:
{{Na saidianeni katika wema na taqwa, wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.}} [Al-Maaidah, 5: 2]

Pia, Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika pale Allaah Anapozuia kitu, Anazuia kula thamani yake.)) [Imesimuliwa na Ibn 'Abbaas. Imepokewa na Ahmad na Abu Daawuud. Imesahihishwa na al-Albaaniy]

Kutibu Maradhi Ya Uvutaji Sigara
Baadhi tu ya wale walioathirika vibaya na uvutaji sigara wanaweza kuachana nayo. Sababu ya wengi kushindwa kuacha uvutaji sigara ni nyingi, miongoni mwao ni kama zifuatazo:

a. Asili ya sumu isiyoachika iliyokuwemo ndani yake.
b. Wavutaji hawajajikubalisha kwamba sigara ni haramu.
c. Hawana azma ya kweli kuachana na uvutaji huo.

Ufuatao ni baadhi ya ushauri unaoweza kumsaidia mtu kuacha kuvuta sigara:

1. Mtegemee Allaah kikweli kweli, ukiwa na azma ya moja kwa moja kutorudia kuvuta sigara, kwa kuridhia amri ya Allaah:
{{Na ufungapo nia mtegemee Mwenyezi Mungu (tu ufanye hili uliloazimia).}} [Aali-'Imraan, 3: 159]

2. Achana nayo mara moja badala ya kudai kwamba ni bora kuacha kidogo kidogo. Mtindo wa kuacha kidogo kidogo ni njia ya yule ambaye haamini uwezo na nguvu ambazo Allaah Amempatia. Chukua mfano kutoka kwa Maswahaabah (Radhiya Allaahu ‘Anhum), ambao mara tu baada ya amri ya kuharamishwa ulevi kuwafikia:
{{Hakika Shaytwaan anataka kukutilieni uadui na bughudha baina yenu kwa ajili ya ulevi na kamari na anataka kukuzuilieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na (kukuzuilieni) kusali. Basi je, mtaacha (mabaya hayo)?}} [Al-Maaidah, 5: 91]

Hapo hapo walimwaga pombe yote waliyokuwa nayo na kusema: "Tunajisalimisha kwa Bwana wetu, tunajisalimisha!" Walifanya hili ingawa ukweli ni kwamba pombe ilikuwa imegandana na damu zao kwa wale wenye kuinywa.

3. Epuka kuwa karibu na makundi ya wavutaji sigara na mazingira yatakayokusukuma kuvuta sigara ambayo yamejaa harufu ya sigara.

4. Badili mfumo wako wa chakula kwa kuepuka vyakula na vinywaji ambavyo vitakufanya kuvuta sigara kama vile viungo vikali (spices), nyama, chai na kahawa; na badala yake kula matunda na mboga mboga kwa wingi.

5. Tumia zana za kiafya zilizojaribiwa na kukubalika za kusaidia kuacha kuvuta sigara, kama zilivyoelekezwa na tabibu, kwa mfano nicotine patches, nicotine gums, n.k.

6. Epuka na kunong'onezwa kwa siri na Shaytwaan ambaye anaendelea kumuamrisha mwanaadamu kwamba ni dhaifu na asiyeweza kuacha kutenda dhambi, kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anavyosema:
{{Huyo (aliyekutieni khofu ile) ni Shaytwaan ambaye anakuogopesheni marafiki zake, basi msiwaogope bali niogopoeni Mimi mkiwa Waislamu (kweli).}} [Aali-'Imraan, 3: 175]

{{Basi piganeni na marafiki wa Shaytwaan. Hakika hila za Shaytwaan ni dhaifu.}} [An-Nisaa, 4: 76]

Itaendelea In shaa Allaah…
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom