Tukijua kutenda haki tutajua mipaka yetu inaanzia wapi na mipaka ya watu wengine inashia wapi

Shayu

Platinum Member
May 24, 2011
608
1,653
Ni MUHIMU kuheshimu kila mtu Mipaka yake. Tusivuke mistari. Kuna mambo yanayotuhusu sisi tujishughulishe nayo hayo. Tusiingilie mambo ya wengine. Ingawaje wakati fulani tunakuwa sahihi na tungependa wengine wawe kama sisi katika maisha yetu , lakini ni ngumu mno kumbadilisha mtu. Nimejifunza kukaa kimya na kuufunga mdomo na kufuli kwa mambo ambayo hayanihusu.


Tuache kila mtu afuate njia yake anayotaka na kipimo chake ni matokeo ya njia zetu na matendo yetu. Ni muhimu kufahamu matendo yetu huzaa matunda. Hakuna kitu kinachokuja bahati mbaya katika maisha. Sisi ni matokeo ya matendo yetu. Kwahiyo kuchagua maisha mema au mabaya ni uchaguzi wetu.


Lakini mtu anapovuka mipaka yake na kuingilia mipaka ya mtu mwingine ni tatizo. Kila mtu lazima aheshimu mipaka yake. Uovu wako usivuke mipaka ukamfikia jirani yako na kutaka kuharibu misingi yake. Ukijua hili utakuwa umefanya jambo la msingi sana.


Kila mtu ana haki ya kufikiri na kutenda kile anachofikiri. Kila mtu ana haki ya kujitawala na kufanya maamuzi yake mwenyewe. Kujenga na kuitazama familia yake mwenyewe kwa mtizamo wake bila kuingiliwa. Hata kama sisi watu wa nje tunaona familia yake aiangalii inavyotakiwa. Tunachoweza tu ni kushauri kwa busara. Akikaataa shauri yake. Maneno ya busara ni kama spider web. Mtu asipoyasikiliza hunaswa.


Hii pia inaenda sawa katika nchi. Kila nchi ina haki ya kujiamulia na kujiendeshea mambo yake bila kuingiliwa. Ni Kukosa busara kuingilia mambo ya nchi nyingine. Ni busara kutia mdomo kufuli na kuangalia mambo yanavyoenda. Kama hujaombwa ushauri hauna haja ya kunyanyua mdomo. Wakati mwingine ni busara kukaa kimya kuliko kuongea.


Kwahiyo mara kwa mara tumekuwa watu wa kuvuka mipaka yetu. Kuna watu wanavuka mipaka na kuingilia ndoa za watu wengine. Hakuna uovu mkubwa kama huu. Unaharibu familia na amani katika nyumba.


Watu wanakuwa hawako wamoja na kuongeza kutokuelewana. Na kuvunja umoja wa familia ambao ni muhimu sana katika ukuaji wa familia na malezi ya watoto.


Kwa baba yeyote mwenye akili attention yake ya kwanza ni familia yake. Kuhakikisha familia ni moja na kuwa tayari kuilinda. Mwanaume wa namna hii hawezi kukuacha akikukuta na mke wake , anakupeleka moja kwa moja kuzimu. Ni muhimu kuheshimu mipaka wengine lakini mtu akiingia kwenye mpaka wako usimwache.


Watu hawa wamesaini mkataba na kula kiapo cha kuishi mme na mke na kuanzisha familia. Ambayo kwa uhakika ni sehemu ndogo ya taifa. Na stability katika familia inaendana kabisa sambamba na stability katika jamii zetu. Ndoa zikiyumba hakuna jamii itakayosimama. Kama familia ikiyumba unaharibiwa mustakabali wa maisha yako yote. Kwahiyo usikubali mtu achezee familia yako. Usikubali watu wavuke mipaka yao na kuingilia himaya yako. Ni muhimu kuheshimiana.


Kwa wanaume tunatakiwa kuwa na busara na hekima. Tunatakiwa pia kuwa imara kama wanaume na kusimamia misingi. Tusikubali kuyumbishwa kwenye mambo ya msingi ambayo yanahusu future ya familia. Lakini pia future ya jamii zetu na taifa letu.


Kwasababu haya mambo yanaendana. Binadamu haishi katika kisiwa anaishi na binadamu wengine katika jamii yake na ndani ya taifa. Kwahiyo kama unatakiwa kuwa na busara unatakiwa kuwa na busara ndani ya familia yako pamoja na kwenye jamii yako na taifa.


Uongozi unaanza ndani ya familia na kwenye jamii inayotuzunguka. Leadership skills zinaanza huko hakuna sehemu nyingine. Mtu ambaye ataweza kutawala familia yake vyema na ku galvanise watu katika jamii yake vyema kukabiliana na changamoto wanazokabiliana nazo kisha kuifanya jamii hiyo kuwa productive ni kiongozi wa kweli.


Kiongozi wa kweli ni yule mwenye uwezo wa kutatua matatizo ya watu kwa kushirikiana nao. Kwahiyo anahitajika kuwa na maarifa. Lakini pia kujua mipaka yake. Kufahamu watu wana uhuru wao. Ingawaje wanawajibika kutoa sehemu ya uhuru wao kwa manufaa ya taifa.


Kwahiyo ni muhimu kufahamu hata serikali ina mipaka yake na hairuhususiwi kuingilia uhuru wa watu kama watu hao hawavunji sheria ambazo jamii wamejiwekea. Kwahiyo serikali ni muhimu kujua mipaka yake. Na kujua raia wana uhuru wao na uhuru huo unapaswa kulindwa.


Raia wana haki ya kutoa maoni bila kuingiliwa. Wana haki ya kujikusanya na kuongelea matatizo yao na jinsi wanavyoongozwa. Majaliwa ya taifa lao yako mikononi mwao. Kwahiyo wanawajibu wa kushiriki moja kwa moja na kutoa maoni bila kuzuiwa. Kujua mwelekeo wa taifa lao ni haki yao ya msingi. Raia wanapoona serikali yao inawapeleka siko wana haki ya ki msingi kuongea. Na serikali inawajibika kuheshimu hilo na kujua mipaka yake.


Kwahiyo kupiga na kuonea raia wanaotoa sauti zao sio jambo sahihi na ni uvukaji wa mipaka. Kama vile raia wanavyowajibika kutovunja sheria za nchi. Ambayo matokeo yake ni kupelekwa mahakamani na inapothibitika mtu hufungwa jela.


Kwahiyo tukijua kutenda haki tutajua mipaka yetu inaishia wapi na mipaka ya watu wengine inaanzia wapi. Ni jambo la muhimu sana kufahamu. Na taifa lolote linalotenda haki ni taifa lenye utulivu wa kudumu.
 
Back
Top Bottom