Tukiacha kulumbana, watatuburuza! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Tukiacha kulumbana, watatuburuza!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by BAK, Apr 9, 2009.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Apr 9, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,918
  Likes Received: 83,433
  Trophy Points: 280
  Tukiacha kulumbana, watatuburuza!

  Lula wa Ndali-Mwananzela Aprili 8, 2009

  Raia Mwema~Muungwana ni Vitendo

  WIKI chache zilizopita tumeshuhudia viongozi mbalimbali wakizungumza na wananchi na kuliasa taifa kuwa malumbano yanayoendelea nchini sasa hivi hayana maana, ni kupoteza muda na kwa hakika yanapaswa yakome.

  Viongozi hao wa CCM kuanzia aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) John Malecela hadi Rais Jakaya Kikwete wote wametaka wananchi (na hasa wanasiasa wenzao) waache malumbano.

  Malumbano au mazungumzo ya majibizano ya wazi ni jambo geni na kwa kiasi kikubwa limechochewa na kuwapo kwa vyombo vingi vya habari kama mzee Malecela alivyodokeza. Kuwapo vyombo hivyo vyote kumetoa nafasi ya watu mbalimbali kushindanisha hoja zao mbele ya jamii na kwa kufanya hivyo kutoa nafasi kwa hoja nzito, nyepesi, za kiakili na za kijinga kutolewa hadharani.

  Majibizano hayo ya hoja wakati mwingine yamegeuka kuwa mashambulizi binafsi ya mtu na mtu na hivyo kuondoa ladha yote ya majadiliano ya kiungwana.

  Malumbano hata hivyo ni muhimu. Nchi yoyote inayotaka utawala wa kidemokrasia ni lazima ijenge utaratibu na mazoea ya kulumbana ili hoja dhaifu ziweze kuonekana na hoja zenye uzito ziweze kupata nafasi. Katika kulumbana na kubishana katika uwanja wa fikra basi tunapata nafasi ya kupima na kutambua ni yupi anamwaga sera na yupi anamwaga pumba.

  Kuweza kuelewa umuhimu wa malumbano ya kisiasa na tuangalie kwa karibu sababu zilizotolewa na mzee Malecela alipokuwa akizungumzia suala hili karibu wiki mbili zilizopita.

  Sababu ya kwanza iliyotolewa na mzee Malecela ni kuwa malumbano haya yanapaswa kukomeshwa “kwa sababu yanawavuruga wananchi na yanavuruga mawazo ya wananchi”.


  Sababu hii haipaswi kuzingatiwa. Binadamu wana uwezo wa kuona, kufikiri, kuamua na kutenda. Kinachomtofautisha mwanadamu na viumbe wengine ni uwezo wa kupima matokeo ya matendo yanayotokana na fikra zake, aidha, kabla ya matokeo hayo au baada ya matokeo hayo. Hivyo, anajipa nafasi ya kupanga na kuchagua vizuri maamuzi yake au kuyarekebisha baadaye.

  Hivyo, malumbano basi hayavurugi wananchi wala kuvuruga mawazo yao. Malumbano kimsingi, yanatupa nafasi ya kuweza kusikiliza hoja mbalimbali na kuweza kuzipima hoja hizo na pia uwezo na nafasi ya kuwapima wale wanaotoa hoja hizo na kuona kama wana msingi katika kuzitoa. Hivyo, kama jamii hatupaswi kuzuiwa kusikiliza mawazo mbalimbali, kuyakubali yanayotushawishi na kuyakataa ambayo hayana ushawishi.


  Hata hivyo, zaidi ni kuwa si jukumu la Mzee Malecela au kiongozi yoyote kuamua wananchi wafikiri kitu gani. Uwezo huo hawana na hatuwezi kuwapa. Hakuna kiongozi ambaye anaweza kuliambia Taifa hili nini watu wake wawaze au wasiwaze; ni kwenye nchi yenye utawala wa kiimla ndipo kiongozi anaweza kusema “mawazo haya mabaya! Na yanavuruga watu!”

  Kwa upande mwingine, inapotokea kiongozi (awe Rais au mtu mwingine) anafikia mahali pa kusema ni mawazo gani yanavuruga wananchi kwa kweli ni kejeli kwa watu wazima katika Taifa. CCM na Serikali yake si wazazi wetu kiasi cha kutuamualia ni nini tufuatilie, magazeti gani tununue na watu gani tuwasikilize. Na kwa hakika hawana haki wala uwezo wa kutuamulia ni malumbano gani yaendelee au yasiendelee.

  Kila mtu ana nyumba yake na familia yake na mipaka ya nini mtoto aangalie au asiangalie inabakia kwa wazazi isipokuwa pale ambapo sheria halali zilizowekwa zinapovunjwa. Nje ya hapo, haiwezekani hata kidogo kwa mtu mzima mmoja kuwaambia watu wazima wengine kuwa mawazo yao yanavurugwa na malumbano ya watu wazima wengine!

  Sababu nyingine ambayo mzee Malecela aliitoa ni kuwa “mimi kwa kweli sioni kwamba haya mambo yanafaida kwa mtu yeyote”. Kwa maneno mengine mzee wetu na bila ya shaka kundi la watu wanaomuunga mkono, hawaoni faida ya malumbano haya. Kwao wanachokiona bila ya shaka ni hasara tu. Je ni kweli malumbano haya hayana faida?

  Ninaamini malumbano haya yana faida kubwa sana katika demokrasia yetu changa. Kwanza, ni kwa sababu yanatuonyesha fikra za watawala wetu. Zamani malumbano kama haya yalikuwa ni siri zao kwenye vikao vyao lakini leo hii malumbano haya yanatufanya tuweze kuwapima viongozi wetu. Mara nyingi utaona kuwa mtu akikaa kimya unaweza ukamdhania ana hekima; lakini siku akifungua kinywa basi ndipo unapojua hekima yake imeishia wapi.


  Ukweli ni kuwa malumbano haya yametusaidia kuwajua ni viongozi gani ambao kwa kweli fikra zao ni duni mno na hawastahili muda wa kusikilizwa. Kuna maneno ambayo yamekuwa yakizungumzwa na watawala wetu hadi tunashindwa kuelewa kama wameingiwa na “pepo” au ndivyo walivyo! Fikiria yule kiongozi aliyetaka watu wauawe papo kwa papo kwa sababu ana uchungu tu! Tusingelumbana wakati ule bila ya shaka leo ingekuwa moto mtupu!

  Au yule kiongozi aliyesema Tanzania inapaa kiuchumi; tulipolumbana tuliweza kuwekana katika msingi sahihi wa fikra za hoja.

  Malumbano haya pia yanafaida ya kuchochea mijadala ya kifikra. Tangu enzi za wanafalsafa wa zamani wa Ugiriki (kina Plato, Aristotle na Socrates na wengine katika historia) malumbano na ujengaji hoja umekuwa ni chanzo cha kutafuta njia bora za kufanya jambo au kupata mwanga wa kulielewa jambo fulani au tatizo fulani kwa mapana yake.

  Hivyo, malumbano ya hoja kimsingi yanatusaidia kuweza kubadilishana mawazo, kushindanisha mapendekezo ya jambo gani bora lifanywe na zaidi ya yote yanatupa nafasi ya kufikiri nje ya mawazo yetu sisi wenyewe. Yanatulazimisha kuwasikiliza wengine. Hivyo malumbano yana faida sana katika jamii.

  Jambo la tatu ambalo mzee Malecela alilitolea sababu ya kwa nini malumbano yakome ni kwa sababu jukumu la vyombo vya habari si kutukanana bali kuelemisha jamii. Kwa maoni yake vyombo vya habari vimekuwa vikitumiwa hivi leo kurusha malumbano na kile alichokielezea kuwa malumbano haya “yamefikia mahali… watu wanaanza kutukanana matusi ya nguoni, maneno ya ovyo ya mtu mwingine binafsi wanayafanya makubwa”.

  Sasa kwa kiasi kikubwa nakubaliana na mzee Malecela kuwa malumbano haya yamevuka mpaka wa uungwana na kuwa malumbano ya kushambuliana nafsi na nafsi.

  Katika ulimwengu wa watoa hoja, mashambulizi ya nafsi ya mtu kwa maneno ni mtindo dhaifu kabisa wa hoja. Mtu yeyote anayeamua kumtukana au kumwita majina mpinzani wake mtu huyo anakiri kushindwa kwenye uwanja wa hoja.

  Tatizo lililopo katika malumbano ya Tanzania ni kuwa Serikali na vyombo vyake wamevumilia sana lugha chafu, habari za kizandiki na mwelekeo duni wa habari nchini. Kwa muda mrefu sasa magazeti mbalimbali yamekubaliwa kuwa ni ya “udaku” lakini si udaku wa kawaida bali yamejikita katika kudhalilisha kijinsi mtu mwingine. Mapicha yanayopamba kurasa za mbele, vichwa vya habari vyote vimezunguka kwenye mambo ya ngono, kukashfiana na kuumbuana.

  Naamini hapo ndipo tatizo la malumbano yetu lilipo. Hatulumbani kushindanisha hoja za uongozi bora, utawala, usawa, haki, n.k bali nani kafanya nini, nani katuhumiwa nini, na nani anashukiwa nini. Malumbano yetu hayajajikita kwenye suala la utawala wa sheria, mwelekeo wa kikatiba, au mwelekeo wa fikra na itikadi za taifa. Matokeo yake tumeacha kulumbana kwenye vitu vya muhimu tumebakia kulumbana kwenye vitu vya kijinga.

  Haya yote, hata hivyo, yanatokana na Serikali ya CCM kuvumilia upuuzi huu kwa kadiri ya kwamba ulikuwa unawahusu kina “Juma na Rosa” wa mitaani au wasanii fulani fulani. Sasa kilipogeuka na kuanza kuwauma wao watawala ndipo watu wanataka “malumbano yakome”. Kama vyombo vya habari vinaonekana kutumika kutukana watu, je matusi hayo yanauma wanapotukanana wanasiasa na viongozi tu? Kwa nini tuwe na viwango viwili, kile cha “viongozi na kile cha watu wengine”?

  Hivyo, binafsi ningeona mzee wetu ana hoja kama angejikita kukemea malumbano na matumizi mabaya ya vyombo vya habari hata kwa watu wa kawaida na kutaka maadili ya vyombo hivyo yazingatiwe akiwa mtetezi wa hata watu wa kawaida badala ya wanasiasa wenzake.

  Vinginevyo, kwa kadiri malumbano na matusi ya watu wa kawaida yanaendelea kuvumiliwa basi wanasiasa nao wajiandae kupewa kikombe hicho hicho cha matusi ambacho watu wa kawaida wananyweshwa kila siku.

  Pamoja na hayo naamini kuwa malumbano ya sasa hayajanoga vya kutosha. Malumbano haya yanatakiwa kuwa ni ya kiakili, ya kisomi, na ambayo yanavuka mpaka wa malumbano na kuwa midahalo ya wazi.

  Ninafahamu kuwa watawala wanaogopa midahalo ya wazi na malumbano ya kisomi. Enzi za Mwalimu watu walikuwa wanakutana pale Ukumbi wa Nkrumah Chuo Kikuu Mlimani na kufanya midahalo ya kila aina na ya kisiasa huku wasomi na watu mahiri mbalimbali wakigonganisha vichwa vyao kwa mada motomoto. Leo hii, imebakia “mihadhara na warsha mbalimbali”. Hakuna tena malumbano ya kisomi!

  Fikiria itokee mjadala pale Chuo Kikuu kati ya Nape Nnauye na John Mnyika, Dk. Slaa na mzee Makamba, au Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba! Midahalo hiyo ndiyo watu wanaiihitaji kuiona na kuisikia. Fikiria mdahalo wa wakongwe kama mzee Edwin Mtei na Mzee Malecela! Patakuwa patamu hapo.

  Tatizo leo hii hakuna taasisi au chombo ambacho kinaweza kuthubutu kuandaa midahalo ya namna hiyo. Sababu ni kuwa inaogopwa.


  Wanaogopa midahalo ya wazi namna hiyo kwa sababu wanajua hawana hoja zaidi ya vitisho na ya kuwa kwa kuruhusu watu wao kulumbana hadharani basi udhaifu wao utaonekana. Ni nani atathubutu kuandaa malumbano ya hoja katika mazingira ya kiungwana? Kwa nini hoja zisishindanishwe kwa hoja ili hoja yenye uzito iweze kuonekana?

  Hivyo, nimalize kwa kusema kuwa Watanzania hawana sababu ya kusitisha malumbano au kukomesha. Ni muhimu wayaendeleze na kupanua wigo wake. La maana ni kuyafanya malumbano haya yawe ya kiungwana, ya kidugu, na pale inapobidi yawe ya kisomi, kwani kufanya hivyo tunachochea fikra za wananchi wetu, kushawishi akili, na kutafuta njia mbadala za kufanya mambo.

  Katika utawala wa demokrasia malumbano ni kiungio kizuri cha utawala bora. Pale wananchi wanapokubaliana kutokubaliana na kugongana bila kuvunjana na kubishana bila kupashana ndivyo ambavyo fikra zetu zinanolewa, viongozi wazuri wanaonekana, wale wabangaizaji wanajulikana na kutoka hapo tunashiriki kwa pamoja katika kujenga fikra mpya za taifa letu.

  Hivyo, malumbano yasikome bali yaendelee; wakiwauliza semeni nimewapa ruhusa kwani hakuna sababu ya kukomesha malumbano isipokuwa kwa wale wanaoogopa maana ya malumbano hayo kwao na kwa maslahi yao.

  Kwani hakuna kitu kinachowatisha watawala kama mwananchi mwenye fikra huru, anayeweza anavyotaka yeye na mwenye kuthubutu kuhoji kile kilichokubaliwa. Hii ndiyo sababu pekee inayomfanya mzee Malecela na viongozi wengine kuogopa roho ya malumbano ambayo imezidi kupamba moto!

  Twende na tulumbane, kwani tusipolumbana nao, watatuburuza!
   
 2. S

  S.M.P2503 JF-Expert Member

  #2
  Apr 9, 2009
  Joined: Nov 25, 2008
  Messages: 463
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 35
  malecela naye ni kichaka cha mawazo duni... kama si kichako kwa nini awaambie watu waache kulumbana ili hali akifahamu kwamba malumbano ni faida hata ndani ya familia yake...
  malumbano achachilia mbali ya taifa sema ya ndani ya nyumba kuhusu chochote kile husaidia kukuza pia kuiimarisha familia kwa kuijengea ewezo wa kupambanua migogoro na matatizo mbalimbali...

  huyu mzee anapoteza heshima zake bure na namshauri ajipumzishe na siasa zilizokwisha kumzidi kimo ingawaje mwenyewe bado anazing'ang'ania bila kuona kwamba yeye ni zilipendwa...
   
 3. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #3
  Apr 9, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,395
  Trophy Points: 280
  Ukweli wanaoogopa malumbano ni kwa sababu hawana hoja!
   
 4. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #4
  Apr 9, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0

  - Mkuu acha mawazo mufilisi, Malecela amesema na wewe sema yako, mbona mna uoga sana na mawazo duni au ni kwa sababu unajua kua ndio yatakayofuatwa? Na yakifuatwa kosa ni la nani? Yaani mimi ninasema mawazo yangu halafu yanafuatwa wakulaumiwa ni mimi au wanaofuata?

  Acheni hizi siasa za alinacha, huwezi kubadilisha sysytem ya siasa ya taifa lolote bila kubadilisha mawazo ya wananchi kwanza, mpaka mtkapolielewa hili tutaendela kuwasindikiza CCM tu tena tukiamuliwa na hata wastaafu wa CCM, msikimbie vivuli wakuu saidieni kuelimisha wananchi kwanza ambao hawafiki huku kwenye internent, ama sivyo hivi vilio havitakuja kuisha.

  FMES!
   
 5. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #5
  Apr 9, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  - Kumbe ndio maana Mwalimu alikuwa hapendi malumbano?

  FMES!
   
 6. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #6
  Apr 9, 2009
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 105
  Trophy Points: 145
  Wakati mwingine Udikteta mzuri sana.
  Malumbano ambayo hayana msingi ni kuyasigina tu na kufunga kufuri midomo.
  Watu wanaacha kulambana kimaendeleo nini kifanyike kwa nn barabara hazipitiki kweli tunasafari ndefu sana.
   
 7. Azimio Jipya

  Azimio Jipya JF-Expert Member

  #7
  Apr 9, 2009
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 3,370
  Likes Received: 14
  Trophy Points: 135
  Kama :

  Kiogozi wetu Mkuu angekuwa na Ujasiri wa kuyakabili MAGUGU yote yanayo karibia kulimeza taifa.......

  Kama :

  Viogozi mbalimbali wa Taifa la Tanzania wangekuwa HONESTY mionyoni mwao kulitetea, kulitumikia na kulilinda Taifa......

  Na Kama :

  Watanzania wenye MIOYO jasiri na ya Ukweli katika kusimamia Ustawi wa kweli wa Utu na Maendeleo yake wangejitokeza......

  Viogozi na sereakali iliyoko madarakani ingekuwa imeshalumbana constractively na hilo lingekuwa limeshamalizika na mavuno yake yangetumika kuendeleza wananchi wote wa jamii yetu.

  Kwa kuwa wao hawana Thamani hiyo..... Kwa kuwa wamekosa heshima hiyo...

  Ni kweli na ni hakika ...

  Tukiacha kulumbana, Watatuburuza vibaya sana.
   
 8. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #8
  Apr 9, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  - Malumbano ya bongo bado hayawezi kutusaidia kwa sababu yanajali udini, ukabila, undugu na interest, mapaka tutakapoachana na haya ndipo tutalisaidia taifa letu na malumbano, ingawa sio dhambi pia kua nayo kwa sasa, haya ya mfano wa what to come huko mbele ya safari.
   
 9. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #9
  Apr 9, 2009
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,918
  Likes Received: 83,433
  Trophy Points: 280
  Juzi juzi tumeona malumbano ya ununuzi wa Dowans yalivyoiepusha nchi kuingia mkenge wa kununua mitambo chakavu ya Dowans kwa shilingi bilioni 60, Watanzania tungeamua kukaa kimya fisadi Rostam angekuwa anakenua gego to gego on his way to Bank na kutuona sisi ni wapumbavu wa hali ya juu. Lakini kutokana na ushindi katika malumbano ya kutonunua au kununua mitambo hiyo hatimaye kambi ya kutonunua iliibuka na ushindi katika malumbano hayo. Angekuwa ameishaifisadi nchi yetu shilingi bilioni 300 (Kagoda 40 billioni, Richmond/Dowans billioni 240).

  Hivyo sikubaliani na dhana kwamba malumbano hayatusaidii Watanzania kuna mafanikio mengi tumepata kutokana na malumbono huu ni mfano mmoja tu.
   
 10. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #10
  Apr 9, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,364
  Likes Received: 6,395
  Trophy Points: 280
  Kama watu wa kulumbana nao ndiyo walikuwa hawa.. hata mimi nisingeyependa!
   
 11. Field Marshall ES

  Field Marshall ES JF-Expert Member

  #11
  Apr 9, 2009
  Joined: Apr 27, 2006
  Messages: 12,659
  Likes Received: 69
  Trophy Points: 0
  - Got you....Bwa! ha! ha! ndio maana nikasema bado hatujawa na malumbano sahii kwa taifa letu, lakini one day tukiendelea hivi tutayafikia.

  Respect.

  FMES!
   
Loading...