Idimi
JF-Expert Member
- Mar 18, 2007
- 15,297
- 11,082
Ujenzi wa kiwanda cha magadi Ziwa Natron ni wa kuutilia shaka
2007-10-11 10:18:38
Na Johnson Mbwambo wa JET
Mwingereza mmoja mwenye asili ya Ireland, John Nolan, alipata kunukuliwa na gazeti moja kubwa la nje akisema kwamba; Tanzania ndiyo nchi pekee duniani ambayo Mzungu anaweza kuingia akiwa mikono mitupu na kuondoka akiwa bilionea!.
Mzungu huyo ndiye yule aliyeendesha mapambano makubwa dhidi ya Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) ambacho kilikuwa kikipinga mpango wake wa kufungua mashamba ya kamba (prowns) katika Delta ya Rufiji, mpango ambao kama ungetekelezwa ungewaacha mamia ya wavuvi masikini katika Delta hiyo kuwa masikini zaidi.
Pamoja na serikali ya awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa kuupitisha mradi huo Ireland, JET na wanaharakati nchini, wakiungwa mkono na jumuiya za kimataifa, walisimama kidete kuupinga mradi huo na hatimaye serikali ikasalimu amri.
Ni vigumu kutoikumbuka kauli hiyo ya John Nolan unapotafakari kasi ya sasa ya kukaribisha uwekezaji wa kigeni katika maeneo mbalimbali nchini bila kujali athari za muda mrefu za mazingira ya maeneo hayo.
Moja ya mambo yanayosaidia sana kuitangaza Tanzania nchi za nje na kuiingizia mamilioni ya pesa za kigeni, kwa miaka mingi tu, ni vivutio vyake vya kitalii.
Mungu ameijalia nchi hii kwa kuipa mbuga, maziwa, misitu na hata milima yenye viumbe hai ambavyo havipatikani sehemu nyingine duniani.
Na ni mbuga hizo na viumbe hai hivyo ambavyo vimekuwa, kila mwaka, vikiwavuta kuja nchini watalii na watafiti kutoka sehemu mbalimbali duniani, na kwa njia hiyo kuliingizia taifa mamilioni ya pesa za kigeni.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Maliasili na Utalii, zilizotolewa bungeni, hivi karibuni, kwa mwaka 2006 tu Tanzania ilipata watalii 644,124 walioiingizia nchi jumla ya dola za Kimarekani milioni 862.
Kinachowaleta watalii hao hapa nchini ni wanyamapori na viumbehai wengine wasioonekana kwingineko duniani; lakini sasa Tanzania imenasa katika mtego wa uwekezaji wa kigeni katika mbuga na maeneo mengine yenye maliasili hizo kiasi kwamba miaka si mingi wanyama na viumbe hai hivyo vitakimbia na kuufanya uwepo wao hapa nchini kubakia kuwa ni historia.
Lengo la Serikali, kwa mujibu wa bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2007/2008, ni kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 1.2 ifikapo mwaka 2012.
Mkakati mkuu wa Serikali katika kulifikia lengo hilo ni kuongeza idadi ya hoteli za nyota tano katika mbuga za wanyama.
``Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji wenye uwezo wa kujenga hoteli za nyota tano katika mbuga zetu na katika maeneo yanayozunguka mbuga zetu,`` ndivyo Waziri wa Wizara hiyo,Prof. Jumanne Maghembe alivyoliambia Bunge wakati akiwasilisha bajeti yake, Julai mwaka huu.
Lakini sote tunajua kwamba huwezi ukajenga hoteli kubwa za kitalii za nyota tano katika mbuga za wanyama, ukajenga na barabara kubwa na hata viwanja vya ndege vikubwa ndani ya mbuga hizo, na kisha ukatarajia wanyamapori waendelee kuwepo hapo.
Lakini hivyo ndivyo serikali ya Tanzania inavyofanya. Mwekezaji na tajiri wa Uarabuni ameruhusiwa kujenga hoteli kubwa ndani ya mbuga, na sasa kuna mpango wa kujenga barabara kubwa ndani ya mbuga ya Serengeti na pia kualika wawekezaji wengine wa nje kujenga hoteli nyingine zaidi za nyota tano ndani ya mbuga hizo.
Huhitaji kuwa mtaalamu wa mazingira kujua kwamba vyote hivyo vitafanya shughuli za binadamu ndani ya mbuga hizo kuongezeka, na hivyo kuwafanya wanyama kuhamia kwingineko (Kenya?!).
Je, bila kuwepo kwa wanyama hao, mtalii gani atatembelea hoteli hizo za nyota tano ndani ya mbuga? Nani kaiambia Serikali ya Tanzania kwamba watalii wanafuata hoteli za nyota tano ndani ya mbuga za wanyama?
Si kweli kwamba kwao wana hoteli nzuri zaidi kuliko zilizopo hapa nchini? Si kweli kwamba wanachokifuata nchini ni wanyamapori katika mazingira yao ya asili na si hoteli za kifahari?
Ni jambo linaloeleweka wazi kwamba kadiri shughuli za binadamu zinavyoongezeka katika maeneo ya pori, ndivyo pia wanyamapori na viumbe hai vingine vinavyozidi kuyakimbia maeneo hayo kuwakwepa binadamu.
``Mradi wowote ule ambao huhusisha kusafisha eneo kubwa la ardhi na kuondoa forest cover, si wa kuuendekeza; vinginevyo, tutamaliza uoto wa asili na kuwafanya wanyamapori wetu na viumbe hai vingine kuondoka,`` anasema Rais wa Chama cha Wataalamu wa Misitu Tanzania (TFA), Dk. Felician Kilahama.
``Mbuga ya Serengeti imeingizwa katika orodha ya maeneo ambayo ni Urithi wa Dunia (World Heritage Site), na pia ni moja ya maajabu saba ya dunia.
Ni wazi itapoteza sifa hizo kama shughuli za binadamu zitaruhusiwa kuongezeka ndani ya eneo la mbuga hiyo na kusababisha wanyama kutoweka,`` alisema Dk. Kilahama alipotembelea ofisi za JET, mjini Dar es Salaam, hivi karibuni.
Lakini si Serengeti tu. Kama zitajengwa barabara kubwa za lami ndani ya maeneo ya mbuga na kisha kuwakaribisha wawekezaji wa kigeni kujenga hoteli za nyota tano ndani ya mbuga hizo, shughuli za binadamu ndani ya mbuga hizo zitaongezeka na wanyamapori watatoweka moja kwa moja.
Na kama wanyamapori watakimbilia kwingineko kukwepa shughuli za binadamu, ni mtalii gani atatembelea mbuga hizo zisizo na wanyama? Je hoteli hizo za nyota tano ndani ya mbuga hazitaishia kuwa ``white elephants``?
Mfano mwingine wa jinsi Serikali inavyoendekeza uwekezaji wa kigeni unaofukuza wanyama au viumbe hai vinavyovutia watalii nchini, ni huu unaohusu ujenzi wa kiwanda cha magadi katika Ziwa Natron lililopo mkoani Manyara karibu na mpaka wa Kenya.
Licha ya kwamba Ziwa Natron ni eneo la hifadhi ya Ramsar (Ramsar Site) kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Ramsar ambao Tanzania imeuridhia, Serikali imeingia makubaliano ya awali (MOU) na kampuni ya Tata Chemicals Limited ya India kujenga kiwanda cha magadi katika eneo la ziwa hilo.
Wadau mbalimbali wa mazingira, ndani na nje ya nchi, ikiwemo JET, inaupinga mradi huo si tu kwa sababu ni eneo la hifadhi la Ramsar, lakini pia kwa sababu ujenzi wa kiwanda hicho utawafukuza ndege aina ya Lesser Flamingo kuondoka katika eneo hilo. Asilimia 75 ya ndege hao waliosalia duniani wanapatikana Tanzania katika Ziwa Natron.
``Ujenzi wa kiwanda cha magadi karibu na Ziwa Natron utatibua mazingira ya ndege aina ya Lesser Flamingo na kuwasababisha waondoke.
Ziwa Natron ndilo eneo pekee lililosalia katika Afrika Mashariki ambako ndege hao hutaga mayai,`` anasema Naibu Mkurugenzi wa East African Wildlife Society (EAWLS), Hadley Becha.
``Lesser Flamingo wanatoweka kwa kasi duniani. Wamo katika orodha ya IUCN ya ndege wanaotoweka kwa kasi duniani. Ni ndege wanaohitaji mazingira tulivu mno kuweza kutaga mayai yao na kutotoa.
Tanzania imebahatika kwamba bado inao ndege hao; lakini ni dhahiri ujenzi wa kiwanda hicho utafanya waondoke,? anasema Becha.
Kwa mujibu wa andiko la mradi huo, kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani 500,000 za magadi kwa mwaka.
Aidha wakati wa ujenzi kitakuwa na wafanyakazi 1,225 na kikianza uzalishaji kitakuwa na watumishi 152. Kitatumia megawati 11.5 za umeme na lita 106,000 za maji kwa saa na kutoa maji machafu lita 10,000 kwa saa.
``Kiwanda kitakuwa na wafanyakazi wengi na hivyo shughuli za binadamu zitaongezeka katika eneo la ziwa.
Kutakuwa na kelele za malori yakiingia na kuondoka yakiwa na shehena za malighafi au magadi.
Haya yote yatawafanya ndege hao kuondoka kabisa na kuhamia nchi nyingine,`` anasema Andrew Wairu wa African Conservation Centre (ACC), moja ya asasi za mazingira zinazoupinga mradi huo.
Si siri kwamba moja ya sababu za watalii kuja Afrika Mashariki, hususan, Tanzania ni kuwaona Lesser Flamingo. ``Hiyo maana yake ni kwamba ndege hao wakishatoweka, watalii nao watapungua kuja``, alisema Wairu.
Hilo ndilo pia limewafanya wanamazingira wa Kenya kujitosa katika kampeni ya kupinga kuanzishwa kwa kiwanda hicho cha magadi, kwani ndege hao wa Lake Natron ndiyo pia huvuka mpaka na kuingia Kenya ambako watalii pia huweza kuwaona.
Ingawa wakati wa kikao cha bajeti Waziri anayeshughulikia Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Deodatus Kamala, aliwaambia wanamazingira hao wa Kenya kwa kusema kwamba Lake Natron ni mali ya Tanzania; hivyo lazima kiwanda hicho kitajengwa, lakini Waziri alisahau kwamba ziwa hilo ni trans-boundary; yaani uwepo wake unahusu au unagusa nchi zaidi ya moja.
Ni dhahiri Dk. Kamala alisahau kwamba ingawa Ziwa Natron lipo Tanzania, lakini mto unaoingiza maji katika ziwa hilo unaanzia Kenya. Je Kenya nao ikiuzuia mto wake kutakuwa tena na Ziwa Natron?
Hivi sasa kampuni ya Tata Chemicals Limited tayari imeshatoa zabuni kwa kampuni ya Nor Consult Tz kufanya tathmini ya athari za muda mrefu za mazingira (Environmental Impact Assessment - EIA) ya mradi huo, lakini haitarajiwi ripoti yake kuwa kinyume na matarajio ya `mtoa kazi`; yaani Tata Chemicals Limited.
Katika hali hiyo, matumaini ya mwisho ya wanamazingira wa Tanzania na Kenya yamo katika EIA itakayofanywa na Baraza`la Taifa la Mazingira (NEMC).
Matarajio ni kwamba NEMC litafanya uchunguzi wake likizingatia hofu zilizotolewa na wadau wa Ziwa Natron katika kikao kilichohusu mradi huo, kilichofanyika Julai 12 mwaka huu, mjini Dar es Salaam.
Lakini hata kabla NEMC haijafanya utafiti wake na kutoa ripoti yake ya EIA, kilifanyika kikao kingine, Agosti 13 mwaka huu, mjini Mumbai, India kati ya viongozi wa Tata Chemicals Limited na Shirika la Kimataifa la Mazingira - IUCN (Asia) na kutolewa ripoti ya `kujikosha`.
Ripoti yao inasema kwamba kampuni hiyo itazingatia maoni ya wadau wa Ziwa Natron yaliyotolewa katika kikao cha Julai 12, lakini wanamazingira hawana uhakika na utekelezaji wake.
Yawezekana Serikali ya Tanzania katika kuukubali mradi huo ilisukumwa na hamu yake ya kuongeza ajira. Lakini nini faida ya kutengeneza ajira za muda mfupi kwa kuua maliasili ambayo ingedumu vizazi na vizazi?
Tata Chemicals Limited ilikuwa na viwanda viwili vya magadi nchini Kenya, lakini kimoja tayari kimeshafungwa baada ya maji kukauka (viwanda vya namna hiyo hutumia sana maji).
Kwa maana hiyo, ajira walizoahidiwa nazo zinakuwa za muda mfupi.
Wanamazingira wanaamini kwamba kama Tanzania ikiendekeza uwekezaji huu wa kigeni unaoua maliasili, kwa sababu tu ya `faida ndogo za muda mfupi`, hakuna tena kitakachobakia kitakachowavuta watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja nchini. Huwezi kula keki yako na ukaendelea kuwa nayo!
Hii ndiyo changamoto kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri katika ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Profesa Mark Mwandosya na waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba.
SOURCE: Nipashe
Maoni Yangu
Kwa ninavyojua, eneo la Ziwa Natron linalindwa na mkataba wa Ramsar,ambao lengo lake ni kulinda maeneo oevu yote duniani, hivyo kuweka mradi eneo hili ni kukiuka mkataba huo.
Maelezo zaidi yanapatikana katika tovuti yao "www.ramsar.org"