TUCTA: JK acha woga

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,029
TUCTA: JK acha woga

na Waandishi Wetu, Dar, mikoani
Tanzania Daima~Sauti ya Watu

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limemtaka Rais Jakaya Kikwete, kuacha woga wa kuwashughulikia viongozi mafisadi waliopo serikalini pamoja na kuwabeba wawekezaji wasio na uwezo.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa TUCTA Mkoa wa Dar es Salaam, Everist Mwalongo kwenye sherehe za Sikukuu ya Wafanyakzi kwa Mkoa wa Dar es Salaam zilizofanyika Uwanja wa Taifa.

Alisema mpaka sasa viongozi mafisadi hawajafikiwa na wanaendelea kutafuna rasilimali za nchi kwa masilahi binafsi.

Mwalongo alisema ni aibu kwa kiongozi ambaye amekuwa akisimama katika majukwaa na kuwaahidi Watanzania maisha bora, lakini huku nyuma amekuwa akihujumu rasilimali za wanyonge kwa tamaa zake.

Alisema mtandao wa ufisadi ni mkubwa sana nchini na unahitaji mtu jasiri, hivyo ni vema Rais Kikwete, akaachana na woga na kuwawajibisha viongozi husika.

“Mpaka sasa viongozi mafisadi hawajaguswa wala kufikiwa, ndiyo tunamtaka Rais Kikwete aache woga na awe jasiri kuwashughulikia viongozi mafisadi,” alisema Mwalongo.

Aidha, alisema mtandao huo ndio unaokwamisha maendeleo ya kiuchumi kwa taifa na kuifanya serikali kushindwa kuwahudumia Watanzania ambao kila kukicha gharama za vyakula na maisha vinazidi kupanda.

Alisema kama Rais Kikwete atashindwa kuwashughulikia viongozi hao, kuna kila dalili za kutokea machafuko kama yanayotokea nchi jirani na kwengine duniani.

“Sisi wafanyakazi tunajua kazi hiyo ni ngumu, lakini tunaahidi kumpa ushirikiano wa kuwafichua na kupambana nao wote waliobaki mpaka wamalizike,” alisema Mwalongo.

Alisema fedha zilizoibwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zingetosha kuwalipa mishahara mizuri wafanyazi kwa kipindi cha miaka kadhaa ijayo.

Aidha, wafanyakazi hao walimuonya Rais Kikwete kuwa makini na malumbano ya kisiasa na kuyatatua bila upendeleo, ili kuleta demokrasia ya kweli kwa kizazi hiki na kijacho.

Alisema malumbano hayo yanaweza kuleta athari kwa ufanyaji kazi nchini pamoja na vizazi vijavyo, hivyo ni vema yakatafutiwa ufumbuzi sahihi.

Mwalongo, alisema itikadi za vyama zisipewe kipaumbele katika kupanga watumishi kwa lengo la kutimiza matakwa ya siasa, bali yafanywe hivyo kulingana na matakwa ya kazi.

Alisema mtu yeyote ambaye atapewa nafasi kwa itikadi ya chama atafanya kila njia kutekeleza maagizo ya aliyemchagua badala ya wananchi.

“Wafanyakazi wanaochaguliwa kwa itikadi za siasa ndio wanaosababisha migomo, maandamano ya kila mara ambayo husababisha kudumaa kwa uchumi na hatimaye kuzua vurugu nchini,” alisema Mwalongo.

Naye Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Dar es Salaam, Burhan Semvua, alisema mtindo wa kuwabeba wawekezaji wasio na uwezo ndio umelifikisha taifa hapa lilipo.

Alisema wawekezaji matapeli huja nchini bila mtaji, lakini hubebwa na serikali na kupata mitaji, na hatimaye huanza kuwanyanyasa wafanyakazi ambapo wakati mwingine huajiri wafanyakazi kutoka nje, huku kuna Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi hizo.

“Hawa wawekezaji matapeli ndio chanzo cha kutowalipa wafanyakazi malipo yanayotakiwa, hivyo ni vema tukaachana na tabia ya kuwabeba ambayo kwa namna moja au nyingine imepunguza wigo wa ajira kwa Watanzania,” alisema Semvua.

Aidha, alisema hali ya sasa ya wafanyakazi ni ngumu mno kulinganisha na miaka 12 iliyopita ambako ilikubalika kima cha chini kiwe sh 84,000 lakini utekelezaji wake umekuwa ukipigwa danadana.

Alisema ni aibu mpaka sasa kima hicho hakilipwi na serikali imekuwa ikiwasikiliza wafanyabishara wenye viwanda (CTI) kuliko TUCTA na Chama cha Waajiri Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo, alikiri wafanyakazi kupata mishahara midogo pamoja na kufanya kazi katika mazingira magumu.

Alisema mishahara midogo si kigezo cha kusema serikali inawanyanyasa au kuwadhalilisha, bali ni mgawanyo wa fedha ambapo serikali hulazimika pia kuwahudumia watu wa vijijini ambao wanakadiriwa kufikia asilimia 80.

Aidha, alisema suala la ufisadi linahitaji mabadiliko ya kila mtu na kufanya uadilifu na uzalendo katika kazi zao, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Kila siku watu wanakaa kupiga soga kuhusu ufisadi na wanasahau kuwa nao wanafanya ufisadi kwa kutokufanya kazi kwa saa walizopangiwa, sasa tubadilike ili tuweze kupambana na ufisadi,” alisema Kandoro.

Wakati huohuo, habari kutoka Iringa zinaeleza kuwa Rais Kikwete ameahidi kutafuta nafasi ya kukutana na viongozi wa vyama vya wafanyakazi wakati wowote baada ya kurejea nchini.

Rais Kikwete alirejea nchini jana baada ya kumaliza ziara ya kikazi nchini Ethiopia alikohudhuria mkutano muhimu wa Umoja wa Afrika (AU) na baadaye akaenda nchini Uganda.

Pamoja na kuahidi kukutana na viongozi hao, pia amewataka wafanyakazi kote nchini kuacha tabia ya kufanya migomo kama njia pekee ya kupata haki, kwani kufanya hivyo kunasababisha shida kwa wananchi wasio na hatia.

Kikwete alitoa kauli yake hiyo jana kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyemwakilisha wakati wa sherehe za kitaifa za Mei Mosi zilizofanyika mkoani Iringa.

Alisema kitendo cha wafanyakazi kugoma kinahatarisha maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia na kuongeza kuwa wananchi wengi hupata matatizo wakati wa migomo hiyo, ambayo imekuwa ikitokea sehemu za kazi ambazo ni reli, afya na ualimu.

Pinda alisema wanapogoma walimu husababisha wanafunzi kukosa masomo, na wanapogoma watu wa afya husababisha maumivu na mateso kwa wagonjwa.

Alisema kugoma kunadumaza shughuli za uchumi, na kwamba ufumbuzi wa tatizo lolote ni mazungumzo ambayo yanawezekana hata kwa rais.

“Yanapotokea matatizo njooni tuzungumze, ikibidi hata kwa Mheshimiwa Rais, lakini si kugoma ambako uhatarisha maisha na kudumaza uchumi wetu,” alisema Pinda.

Aliwataka waajiri nchini kutambua matatizo ya wafanyakazi wao, ili kuepusha mateso na adha kwa wasiostahili, kupata haki zao na pia kuepusha migomo isiyo ya lazima.

Aidha, alisema serikali inaendelea kuwajali na kuwahudumia wafanyakazi na waajiri, ili waweze kuzalisha na kutoa huduma zaidi katika kuleta maendeleo ya taifa.

Pia alitaka wafanyakazi kukataa kupokea na kutoa rushwa kwa kuwa wafanyakazi wa umma bado wananung’unikiwa na wananchi kwa vitendo hivyo.

Alisema kuwa agizo hilo kwa wafanyakazi dhidi ya rushwa ni jambo moja kati ya matatu aliyoyasema Rais Kikwete katika waraka alioutoa wakati wa kumteua yeye kumwakilisha katika Mei Mosi ya mwaka huu.

Mambo mengine mawili ni kuwa, wafanyakazi wakatae kutumika kufanikisha vitendo vya rushwa na wasaidie kutoa taarifa za vitendo vya rushwa, ili zifanyiwe kazi na wahusika wabanwe.

“Endapo haya yatafanyika, serikali itaweza kuboresha maslahi ya wafanyakazi na ya wananchi kwa jumla,” alisema.

Aidha, habari kutoka mkoani Arusha zinaeleza kuwa wafanyakazi mkoani humo wameeleza kuishangaa serikali kwa kutolipa madeni ya watumishi wa umma mpaka wasubirie mgomo, wakati fedha wanazo za kumaliza madeni hayo.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama Cha Walimu (CWT), wilayani Arumeru, Nuru Shenkorwa na kusema pamoja na serikali kupunguza kiwango cha madeni ya walimu, wameitaka kuhakikisha madeni hayo yanalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha, kinyume na hapo watachukua hatua zaidi.

Alisema mbali na madeni ya walimu, wameitaka serikali kuhakikisha inalipa madeni ya watumishi wa umma bila kusubiri migomo mikubwa inayoingiza nchi katika misukosuko isiyo ya lazima.

Aidha, alisema serikali iepuke kubagua wafanyakazi ambao wote wanalitumikia taifa wakati wa kulipa madeni, kwani wote ni watumishi wa Serikali Kuu.

Alisema wafanyakazi wanaishi maisha yasiyo na matumaini, kutokana na mishahara midogo, badala yake serikali inawakopa nguvu zao pasipo sababu za msingi.

Taarifa hii imeandaliwa na Salehe Mohamed (Dar), Godfrey God (Iringa) na Violet Tillya (Arusha).
 
aaggggggghhhhh....., nachoka hata kumfikiria JK kwa uzwembe wake, baada ya kusoma hii yani imenitonyesha tuu kidonda aaaaghhhh.....
 
Ni vizuri sana watanzania wanapoweza kujenga ujasiri kama huu na kuweka wazi yanayowakera moyoni.

Kikwete is being watched, itafika siku tutampa dossier yenye risala zote hizi na kumuuliza alizifanyiaje kazi?
 
JK ana wakati mgumu kama Mugabe na Zimb .Lakini ukimuona JK ana smile utadhani Muhimbili mtu hajaliwa hadharani.Kisa si uchawi ni maisha magumu kisa cha ugumu ni ufisadi wa Serikali yake .Sijui wanajiandaa na maneno gani mwaka 2010 .Oh watasema walijiuzuru baada ya kutakiwa na Rais ama ?
 
Viongozi wanatakiwa kubadilika na kufanya chochote kulinusuru taifa letu kwani hali ni mbaya sana hasa kwa wananchi wakawaida maisha yamekuwa magumu mnno na hii yote inasababishwa na ufisadi wa maliasili ya taifa letu unaofanywa na viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza.
 
Kinacho nisikitisha ni pindi ukimwona kiongozi anaelezea swala la hali ngumu ya maisha kwa wananchi,maelezo yake yanakuwa kama mtu ambaye hajafika tz kabisa.
 
hivi kuna mkakati wowote wa kuwaelimisha wananchi kuinyima kura ccm 2010?? maaana tunapoelekea sio kuzuri
 
Back
Top Bottom