Tuambizane ukweli, ufisadi hauna dini

eliesikia

JF-Expert Member
Oct 29, 2010
787
755
Uchaguzi Mkuu umekwisha, kilichobaki ni historia iliyowekwa na uchaguzi huo. Rais Jakaya Kikwete akizindua bunge la kumi amesema; uchaguzi huu umeacha majeraha kadhaa, kubwa sana likiwa la udini.

Walio karibu naye wanasema kuwa hata katika maandalizi ya hotuba yake hiyo alikuwa ametaja watu anaodai wanahusika na jeraha hili wakiwamo viongozi wa dini na wana habari. Kwa kuwa hakudiriki kuwataja kwenye hotuba yake, si vema kumhukumu kwa hili.

Kazi moja ya watu walio karibu na Rais ni kueneza uvumi na hili la kutaja majina ya watuhumiwa wa udini linaangukia mlengo ule ule wa kujipendekeza kwa Rais. Lakini pia ni vema kujiuliza kwa nini Rais amechagua jeraha la udini wakati kuna majeraha mengi yameachwa na uchaguzi huu.

Lipo jeraha la wizi wa kura ulioanzia katika kura za maoni; lipo jeraha la donda ndugu la rushwa katika uchaguzi; lipo jeraha la tume ya uchaguzi kuelemewa na mashinikizo ya dola na chama tawala ili kutangaza matokeo yenye utata; lipo la kutumia vyombo vya dola kuwapiga na kuwajeruhi wapiga kura kana kwamba wamefanya makosa kupiga kura; lipo la idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura; na lipo la chama tawala kuwazuia wagombea kushiriki midahalo ya wazi ili wapiga kura wapate kuwahoji.

Yako majeraha mengi, lakini Mheshimiwa Rais amechagua jeraha la udini. Makala hii inajadili dhana hii ya udini kama ilivyojitokeza katika hotuba za Rais, wakati wa kampeini na wakati anazindua bunge.

Nirudie tena kusisitiza mambo machache ya msingi kuhusiana na mjadala huu. Kwanza, Jakaya Kikwete alikuwa Mwislamu alipogombea mwaka 2005. Ndani ya CCM aligombea na Wakiristo lakini akachaguliwa yeye. Katika uchaguzi nkuu wa mwaka huo, akagombea na Wakiristo, akashinda kwa kishindo kikubwa akiwaacha mbali sana Wakiristo.

Mwaka huu, Jakaya bado ni Mwislamu yule yule. Amegombea akipambana na baadhi ya Wakiristo. Hakushinda kwa kishindo kama alivyotegemea. Dai lake la udini yawezekana linaanzia hapa. Kwa dhati naamini kuwa wapiga kura walimjua kuwa ni Mwislamu 2005 na 2010. Kilichobadilika ama ni ufahamu wa wapiga kura au uwezo wa kuongoza wa Jakaya.

Ninapata shida kuamini kuwa mabadiliko haya kama yana uhusiano na dini ya Jakaya au dini ya waliopiga kura.

Jambo la pili, nashawishika kuamini kuwa Jakaya anapotamka neno “viongozi wa dini” katika hotuba zake anamaanisha “maaskofu, mapadre na wachungaji”. Nitaeleza. Mara kadhaa amelalamika katika vikao vya ndani ya chama kuwa maaskofu hawampendi.

Hivi sasa kamati za siasa za CCM katika wilaya na mikoa yote zinafanya tathmini ya uchaguzi, na inavyoelekea kuna maelekezo maalumu yaliyotolewa “kuwashughulikia” maaskofu na wachungaji wanaodaiwa kutokuiunga mkono CCM.

Siku chache kabla ya uchaguzi, wakuu wa mikoa waliagizwa kuwaita “viongozi wa dini” ili kuwatisha na kuwaeleza masikitiko ya Jakaya juu ya udini. Badala yake, walioitwa ni maaskofu tu.

Kuna malalamiko kutoka pande zote za nchi kuwa wakuu wa wilaya wanakataa kutoa barua za utambulisho kwa madhehebu ya Kikiristo kwa ajili ya misamaha ya kodi. Kwa ujumla tathmini ya uchaguzi mkuu ndani ya CCM imegeuka zoezi la kutafuta mchawi aliyesababisha ushindi mdogo kwa CCM.

Jakaya Kikwete anaujua ukweli lakini anaukwepa. Mwaka 2005, watu wengi walikuwa hawajamjua Jakaya kwa undani. Miaka mitano ya utawala wake, imeonyesha nyufa za kutisha katika uwezo wake wa kufanya maamuzi ya kuwaletea watu maisha bora aliyoyaahidi.

Hata ndani ya CCM, upo mgawanyiko mkubwa wa maoni juu ya uwezo wa Jakaya katika kukiongoza chama na serikali yake. Kwa hiyo, waliopiga kura kumkataa Jakaya mwaka huu, waliukataa uwezo wake mdogo wa kuongoza, hawakuikataa dini yake. Wapo waliokataa chama cha Jakaya lakini hawana tatizo na Jakaya.

Chama chake kinakabiliwa na matatizo makubwa na sehemu nyingi nchini sasa hakikubaliki. Waliokikataa chama si kwa sababu ya udini kwa sababu CCM haina dini ya kukataliwa.

Liko kundi jingine japo ni dogo ambalo halina shida na Jakaya, halina shida na CCM kama taasisi, lakini lina shida na umakini wa sera za CCM. Hawa nao hawakumchagua Jakaya kwa sababu labda kwa bahati njema safari hii waliona sera zinazovutia katika chama kingine. Hawa nao hawakuongozwa kufanya hivyo na kiongozi yeyote wa dini.

Ni uzembe wa hali ya juu kufikiri na hatimaye kusema kuwa makundi haya matatu hapo juu, yana udini.

Liko suala la ufisadi katika mjadala wa kitaifa. CCM walidhani litapita kama yalivyowahi kupita mengine. Jitihada za kuwafikisha baadhi ya vigogo mahakamani hazijasaidia kuzima mjadala huu. Uamuzi wa kupuuza suala la ufisadi katika kampeni za CCM hazijasaidia kuufanya mjadala usishabikiwe na wapiga kura.

Propoganda za makada wa CCM kuwa CHADEMA hakina agenda nyingine zaidi ya ufisadi, hazikusaidia kuzima kiu ya watu kutaka kujua undani wa ufisadi. Hii ni kwa sababu, ufisadi hauna dini wala itikadi hata kama unaweza kukumbatiwa bila shida na chama fulani.

Kwa bahati mbaya, hata ndani ya CCM wamo waliojeruhiwa na ufisadi. Wapo waliofukuzwa kazi au kunyimwa haki fulani kwa sababu tu walishabikia mjadala huu. Kwa maneno mengine, agenda ya ufisadi inawaunganisha Watanzania bila kujali dini zao.

Kwa kuwa maisha ya Watanzania kiuchumi yanazidi kuwa mabaya, wapiga kura wengi lazima wapige ramli kutafuta sababu ya kuwapa usingizi wa muda. Na sababu nyepesi inayovutia ni ufisadi uliotamalaki kila sekta ya umma katika taifa letu.

Uamuzi wa CHADEMA kuufanya ufisadi kuwa moja ya agenda kuu katika kampeni zake, uliiweka CCM mahali pagumu sana kwa sababu, wanaoitwa mafisadi katika taifa letu ni wana CCM.

Kutokana na kuwa CCM imekuwa madarakani kwa nusu karne, ni wazi kuwa mafisadi na wahujumu wa uchumi, watakuwa ni wale walio au waliowahi kuwa katika tabaka tawala. Mpaka hapa, ni vigumu kuitakasa CCM na ufisadi kwa kutumia maneno matupu.

Liko kundi kubwa la wapiga kura walioamua kutoipigia CCM kwa sababu ya jinsi CCM inavyoshughulikia suala la ufisadi nchini chini ya Jakaya. Hawa nao walipiga kura kuukataa ufisadi, si dini ya Jakaya wala ya wagombea wa chama cha Jakaya.

Nayasema haya kwa sababu, wagombea wa CCM walioanguka kwa ngazi za udiwani na ubunge, wamo Waislamu kwa Wakiristo. Hali kadhalika walioshinda ni wa dini zote mbili.

Ni matusi kwa wapiga kura kuanza sasa kuwasingizia dhambi ya udini eti tu kwa sababu CCM imeonekana kukataliwa katika sehemu mbalimbali hapa nchini. Dhambi ya udini haiwezi kuonekana kwa kuikataa CCM tu, na pale CCM inaposhinda ionekane hakuna udini.

Anayepalilia fikra hizi ndiye anayepandikiza fikra za udini na Watanzania tuwe macho naye.

Imefikia mahali ikakubalika kuwa kupiga vita ufisadi ni kuipinga CCM na Jakaya amekwama katika fikra hizi nyepesi! Hata maaskofu anaowakamia Jakaya ni wale waliowahi kusimama na kukemea ufisadi na ndipo Jakaya na wenzake wakadhani maaskofu hao wanaipinga CCM.

Ikiwa sasa imekubalika kuwa ufisadi maana yake ni CCM, na kuwa maaskofu walipinga ufisadi wakadhaniwa wanaipinga CCM, basi nawashauri wakubali “kushughulikiwa” na serikali ya Jakaya kwa sababu thawabu yao ni kubwa mbele za Mwenyezi Mungu na waja wake walio hapa Tanzania.

Nayasema haya kwa sababu naamini kwa uthabiti wa moyo wangu kuwa ufisadi hauna dini.

Wako pia wanaohoji kwa nini chini ya utawala wa Jakaya, mijadala ya kidini ndipo imeibuka na kupoteza muda mwingi wa watu. Hivi sasa ofisi ya Waziri Mkuu inatumia muda mwingi na fedha nyingi kuratibu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi na fedha nyingi za walipa kodi zimeishatumika bila kuwajulisha Watanzania kuwa mahakama hii imo mbioni kuanzishwa kwa gharama za serikali japo inadaiwa kuwa ikianzishwa “haitaendeshwa” na fedha za serikali.

Kama serikali haitaiendesha mahakama hiyo kwa nini imetumia mabilioni kuianzisha?

Ni wakati wa Jakaya suala la kujiunga na OIC limechukua sura mpya na sasa Wizara husika iko mbioni kurasmisha hatua za kujiunga.

Kwa wenye akili wangedhani madai ya CHADEMA ya kuharakisha Katiba mpya yangekubaliwa haraka ili Katiba hiyo sasa itamke kuwa Serikali yaTanzania ina dini kuliko ilivyo sasa inapotamka kuwa haina dini wakati inatumia fedha kuanzisha taasisi za kidini!
 
Kina Chenge, Balali, Mramba, Kikwete, Lowassa dini yao moja ufisadi tuu. Wasijifanye kuanzisha udini wakati watu wanakufa kwa kukosa huduma wakati wao wanaiba tuu. Hakuna udini Tanzania ila ufisadi upo, ndio namuunga mkono Rais udini umeanza kwa kasi na udini huo ni ufisadi na wala si uislamu au ukristo. Dini yao mpya ya kina Kikwete ni ufisadi
 
Back
Top Bottom