Tuache mahakama ifanye kazi yake

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
3rd June 2009

Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi.

Tanzania ni taifa ambalo limejijenga juu ya misingi ya utawala wa sheria. Kila kitu tufanyacho sharti kizingatie taratibu na msingi ya sheria, kwa kuwa hayo ndio makubaliano yetu kama taifa.

Tunasema haya kwa nia ya kukumbusha wadau wote wa maendeleo ya nchi hii kwamba kila mwananchi ana haki zake ambazo zinalindwa kisheria, utaratibu wa kupata haki iliyodhulumiwa au kunyimwa ni kupitia mahakama zetu ambazo ni vyombo huru vilivyoundwa mahususi kwa kazi hiyo.

Hivi karibuni Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, alikumbusha kuwa kuna baadhi ya watu wamekuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao aliwapa sifa ya mafisadi papa, hawa walikuwa watano. Baada ya kukumbusha umma kuhusu watuhumiwa hao, taifa limekumbwa na taharuki kuu. Mawaziri na vyombo vya dola vinavyoshughulika na usalama navyo vimeingia katika taharuki hiyo.

Mengi mwenyewe amekaririwa akilalamika kwamba anaandamwa na vyombo hivyo, kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru); Kamati ya Usalama; Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na vyombo vingine vya dola vya kufuatilia uhalifu!

Kwa maoni ya Mengi, anaandamwa hivyo si kwa sababu nyingine yoyote ile ila kwa sababu tu alikumbusha umma kwamba kuna watu hao wanaoitwa mafisadi na kuwaongezea sifa ya kuwa ni mafisadi papa!

Tunajua kwamba waliotajwa na Mengi ni watu ambao kila kukicha kwa takribani miaka mitatu iliyopita wamekuwa kwenye kurasa za mbele za magazeti wakituhumiwa kwa ufisadi. Wametajwa kwenye mitandao ya kompyuta, wametajwa kwenye mikutano ya hadhara, na kila walipotajwa, si wao wala vyombo vya dola vilijisumbua kuchukua hatua yoyote.

Lakini, ni jambo la kushangaza kwamba pamoja na ukweli kwamba waliokumbushiwa na Mengi ni watu binafsi na ambao wana haki ya kwenda mahakamani kushitaki kama wanaamini wamekashifiwa, na bila kusahau kwamba suala lenyewe ni la madai juu ya staha na hadhi ya watuhumiwa, serikali imeamua kulivaa suala hilo kana kwamba ina wajibu wa kuwasaidia.

La muhimu zaidi, wakati juhudi hizi zote zikifanywa na vyombo mbalimbali vya dola dhidi ya Mengi, kuanzia mawaziri na taasisi zote za kuzuia uhalifu, ipo kesi ya madai Mahakama Kuu iliyofunguliwa na Mengi dhidi ya mdaiwa mmojawapo wa mafisadi papa. Kesi hii ipo mahakamani kihalali kabisa na kwa misingi ya sheria za nchi hii.

Hapana shaka, vyombo vya dola vinavyomwandama Mengi kila kukicha vikimwita huko na huko, vinajua wazi kabisa kwamba kesi hii ipo; na ni dhahiri vinajua si busara wala utawala wa sheria kuchokonoa jambo ambalo lipo mahakamani na uamuzi wake wa mwisho haujafikiwa.

Katika mlolongo wa mambo haya sisi kama wadau wa utawala bora wa nchi hii, tukiwa na dhima ya kuelekeza na kuikumbusha jamii yetu juu ya mustakabali mwema wa nchi yetu, tunapatwa na tabu kuamini kama vyombo vya dola vya nchi hii vimeamua kupuuza misingi ya kuheshimu uhuru wa mahakama na hivyo kuacha kuchokonoa kile kilicho mbele yake.

Tunasema haya kwa uwazi bila kutaka kumwonea yeyote aibu, kwamba kwa mwenendo wa mambo, kama aliyosema Mengi ni hivyo, kuwa anaandamwa na vyombo mbalimbali vya dola, tunasema wazi kwamba huko ni kumtisha na kwa kweli vitisho katika taifa hili na katika zama za sasa havina nafasi katu.

Tunasisitiza kwamba mahakama zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria za nchi, hakuna chombo chochote chenye uwezo wa kuhoji suala lolote ambalo liko mahakamani, kama watendaji wa vyombo hivi vya dola vinavyomwandama Mengi wamesahau, basi sisi tunawakumbusha kwamba wasiingilie uhuru wa mahakama. Waiache mahakama ifanye kazi zake kwa uhuru kamili.

Pamoja na haya yote, tunawasilisha pia masikitiko yetu juu ya kukosekana kwa weledi miongoni mwa watendaji wa vyombo vya dola katika kushughulikia mambo magumu na yenye maslahi ya kitaifa; ushabiki, jeuri na kiburi vilivyoonyeshwa havilengi kujenga nchi ila kuongeza matatizo na kushindwa kwa serikali kutatua kero za kweli ambazo zimekuwa kikwazo cha kufikiwa kwa maendeleo ya kweli ya wananchi.

Hakuna taifa hata moja lilikofanya masihara na ufisadi likasimama, umma ukifika mahali ukaona kwamba wahalifu wanaopora rasilimali za nchi wanaendelea kutanua na kupuuza sheria na hakuna lolote dhidi yao linalotendeka, basi nao wataamua kufanya watakavyo na hapo hatuamini kama taifa litasimama tena. Tuache kuchezeana, sheria ziheshimiwe.

CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom