comrade igwe
JF-Expert Member
- Jan 12, 2015
- 7,295
- 3,945
SIKU chache baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kupiga kura kulaani ujenzi wa makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi na Yerusalem Mashariki, Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amehoji ufanisi wa chombo hicho, akisema ni ‘genge la watu wakusanyikao na kupiga soga’.
Alitoa kauli hiyo baada ya jaribio lake la kutaka kupinga azimio lililokemea mpango wa Israel kuendelea kujenga makazi katika ardhi ya Wapalestina kushindikana.
Baraza la Usalama la UN (UNSC) limesema Israel inakiuka sheria za kimataifa kwa kujenga katika ardhi ya Wapelestina.
Azimio hilo lilipitishwa Ijumaa iliyopita, huku Trump akitoa onyo kuwa mambo yatakuwa tofauti wakati atakaposhika rasmi hatamu za uongozi wa Marekani.
Uamuzi wa utawala wa Rais Barack Obama kujiweka kando wakati UNSC ilipopiga kura hiyo ilihali ina kura ya turufu yenye uwezo wa kuitetea Israel, umekosolewa na Trump na kulaaniwa vikali na Israel.
Awali Desemba mwaka jana, Trump aliwahi kukaririwa akisema angependa kutoegemea upande wowote katika masuala ya Israel na Palestina.
Lakini msimamo wake ukawa ukibadilika kadiri kampeni za urais zilipoendelea akiegemea Israel zaidi.
Licha ya shutuma za Trump kwa UN, chombo hicho kwa miaka mingi kinashutumiwa na baadhi ya Serikali za magharibi kukosa ufanisi, huku mataifa yanayoendelea yakisema kinaburuzwa na mataifa tajiri.
Chanzo: BBC