THINKING ALOUD; BUNGE, Serikali kudandia mgongoni mwa Mahakama na Rufaa ya John Mnyika

Chief Isike

JF-Expert Member
Jan 17, 2010
445
462
Wanajamvi kwa wale wanaofuatilia vikao vya bunge, hasa katika Bunge hili chini ya Spika Makinda, Naibu Spika Ndugai na vijana wao, Wenyeviti Mabumba na Mhagama, kumeibuka tatizo ambalo kwa hakika linahitaji mjadala wa hoja za kina ili kusaidia ustawi wa jamii yetu.

Kwa kutumia uongozi wa bunge wa viongozi hao, bunge linaonekana kujikabidhi mikononi mwa serikali na wote wawili sasa, bunge na serikali, wanadandia mgongo wa mahakama (kwa hiari au bila hiari ya mahakama). Mahakama sasa imekuwa kichaka cha kufichia na kuulia mijadala yenye afya, ambayo kwa namna moja ama nyingine, inagusa maslahi na mstakabali wa jamii yetu.

Mifano ipo mingi...more recently ni mgogoro wa serikali na madaktari ambao umepelekea kwenye kadhia hii inayoendelea kumaliza maisha ya Watanzania kimya kimya, mgomo wa madaktari.

Bunge lilipoamua kujikabidhi mikononi mwa serikali, kisha pamoja kudandia mgongoni mwa mahakama, kukwepa 'bahari' ya mjadala wa kina kuokoa maisha ya Watanzania na kusaidia maboresho ya dhati katika sekta ya afya, ambayo kama ilivyo elimu, maji, umeme, miundombinu n.k, inazidi kudorora na kutishia mstakabali wa uhai wa wananchi.

Kwa kweli bunge, kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kushindwa kujadili mgogoro wa madaktari mpaka sasa, kwa 'kisingizio' kuwa suala liko mahakamani, ni nafasi inayopaswa kujutiwa na kila mtu mpenda maendeleo katika nchi hii.

Juzi pia tumeona bunge kwa kushirikiana na serikali (AG) wameua mjadala wa Dowans ulioibuliwa na David Kafulila kwa sababu tu eti 'suala hilo liko mahakamani'. Jana pia tumeona/kusikia Mbunge mmoja, Mangungu, CCM-Kilwa, akilalama kuomba mwongozo kwa nini Halima Mdee alizungumzia suala la yule tajiri wa Big Bon, aliyekodi jeshi lake kwenda kuwabomolea wananchi maskini makazi yao pale Tegeta Namanga.

Wanabodi, dhana ya separation of powers katika uendeshaji wa serikali ni muhimu sana. Lakini kwa namna inavyotumiwa na serikali yetu kupitia bungeni na bunge lenyewe, inapoteza maana nzima ya dhana hii.

lifikia mahali hata mbunge akitaja hata jina tu la Dkt. Ulimboka anaambiwa suala hilo liko bungeni. Lakini tunajua some elements za suala fulani in its totality zinaweza kuwa ziko mahakamani, lakini some offshots zingine katika suala hilo hilo, zisiwe sehemu ya suala lililoko mahakamani. Lakini kwa akili za wabunge, hasa uongozi wa sasa, hili halionekani.

Ukifika hapa, ndiyo unapata umuhimu wa tafakuri ya John Mnyika, ambaye ameamua kukata rufaa. Nimeiona hii tafakuri katika Jukwaa la Wanabidii, katika mjadala wa Msimamo wa SIKIKA katika suala la mgomo wa madaktari.

Tunaweza kupanua mjadala huu, huku tukijadili kwa kina pia Rufaa ya John Mnyika Mbunge wa Ubungo, juu ya suala hili la Serikali bungeni kudandia juu ya mgongo wa Mahakama na kuharibu mantiki nzima ya dhana ya separation of powers kwa manufaa ya nchi hii, hasa demokrasia kuwa moja ya nyenzo za maendeleo endelevu ya kwa watu!


Wananchi wenzangu;

Nimesoma msimamo wa SIKIKA na maoni ya wachingiaji wengine na nimeshawishika kuchangia mjadala huu baada ya kusikiliza majibu ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda bungeni kwenye maswali ya papo kwa papo kuhusu sekta ya afya ya umma nchini. Nilitarajia Waziri Mkuu kwa kuwa ametoka kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri angetoa tamko la hatua nzito za kibajeti ambazo serikali imepanga kuzifanya kurekebisha udhaifu uliojitokeza ama walau kutangaza kurejea kwenye meza ya majadiliano.

Badala yake Waziri Mkuu amelieleza bunge na taifa masuala matatu; Mosi, Serikali ilishaboresha hospitali za rufaa na hospitali maalum nchini ikiwemo kupandisha hadhi Hospitali ya Lugalo kuwa ya rufaa. Pili, Serikali ilishatoa upendeleo maalum kwa watumishi wa sekta ya afya hususan madaktari, wauguzi na wafamasia kuliko watumishi wengine wa umma nchini, hivyo wale wasiotambua ni muhimu wakapewa elimu Tatu, ameeleza kwamba watumishi wa sekta ya afya hawapaswi kujiingiza kwenye migomo na wale wasiotambua wajibu ni muhimu elimu ikatolewa kwa umma na changamoto zilizopo ziendelee kushughulikiwa kwa majadiliano.

Mengine wengine mnaweza kuongezea kwa kadiri ya mahitaji ya mjadala. Majibu hayo ya Waziri Mkuu yamedhihirisha kwamba upande wa serikali unaendelea kuzungumzia bungeni hoja zilizomo kwenye madai ya mgogoro wake kati yake na madaktari kwa maelezo ya upande mmoja bila kuzuiwa kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani. Lakini wabunge na bunge linapotaka kujadili masuala hayo na kupata pia maelezo ya upande wa pili kupitia Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii haraka kinatolewa kisingizio kwamba suala hilo halipaswi kujadiliwa kwa kuwa liko mahakamani.

Majibu hayo ya Waziri Mkuu bungeni kwa mara nyingine tena yanajenga uhalali wa ombi langu nililowasilisha kwa uongozi wa bunge kwamba wabunge tupewe nakala ya taarifa za kamati ya bunge ili tuwianishe na majibu ya serikali na bunge lipewe nafasi ya kujadili masuala husika ili liweze kuishauri na kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Aidha, ukilinganisha msimamo wa SIKIKA na majibu ya Waziri Mkuu utaona kwamba mgogoro wa mtizamo uliopo ambao pengine unazaa mgogoro wa wazi unaojitokeza katika madai na matishio ya migomo ni kwamba wakati ambapo Madaktari, wananchi na wadau wengine wanaona kwamba bajeti katika Sekta ya Afya haitoshi na ile inayotolewa haitumiki kwa ufanisi;

Serikali kwa upande wake inaona bajeti inatosha pamoja na kukiri kuwepo kwa changamoto kidogo na inaamini kwamba kuna matumizi yenye ufanisi katika utekelezaji wa bajeti husika. Mgogoro huu unadhihirisha umuhimu wa pendekezo nililowaandikia uongozi wa bunge kwamba chanzo cha mgogoro huu ni bajeti na matishio ya migomo ni matokeo tu, hivyo kwa kuwa serikali haishughulikii chanzo ni wakati muafaka wa bunge kwa niaba ya wananchi kama chombo chenye mamlaka ya kuisimamia serikali kupanga mipango ya maendeleo na kuridhia bajeti kupokea taarifa toka kwenye kamati yake na kujadili ili kupitisha maazimio ya kuelekeza serikali hatua za kuchukua.

Pamoja na kuwa bajeti kuu ilishapitishwa, bado bunge likijadili sasa linaweza kuishauri na kuisimamia serikali kufanya marekebisho ya msingi kwenye bajeti ya Wizara ya Afya kabla haijawasilishwa kuidhinishwa bungeni ili kupata nyongeza ya kushughulikia sehemu ya madai yaliyotolewa na madaktari. Katika muktadha huo; nawaomba mijadala hii inayoendelea iliwezeshe bunge kuingilia kati kujadili bungeni hali tete ya sekta ya afya nchini na kauli tata za serikali katika kushughulikia hali hiyo.

Tuungane kukataa visingizio vya serikali vya kutumia mahakama kuathiri haki, kinga na madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali juu ya suala la madaktari na hali ya sekta ya afya nchini. Kwa upande wangu juzi tarehe tarehe 3 Julai 2012 niliwasilisha rasmi kwa Katibu wa Bunge kwa mujibu wa masharti ya kanuni ya 5 (4) rufaa dhidi ya maamuzi ya Spika, Naibu Spika na wenyeviti ya kutumia kanuni ya 64 (1) (c) kudhibiti Bunge kutumia uhuru na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya nchi; sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge na kanuni nyingine za Kanuni za Kudumu za Bunge.

Kwa kipindi cha takribani miezi minne nimetumia njia za kawaida za kibunge kutaka suala la madai ya madaktari lijadiliwe bungeni ili kushughulikia chanzo badala ya matokeo hata hivyo hitaji hilo la kikatiba limekuwa likipuuzwa na kusababisha bunge lizembee kuchukua hatua kwa wakati kuepusha mgogoro na mgomo. Izingatiwe kwamba katiba ya nchi ibara ya 63 (2) inatamka kwamba “Sehemu ya pili ya bunge (yaani wabunge) ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano, ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba”.

Hivyo, umma na wadau wa haki za binadamu tuungane pamoja kutaka Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyoshughulikia suala la madai ya madaktari itolewe bungeni na hadharani na bunge liruhusiwe kutumia mamlaka yake ya kuisimamia serikali kujadili taarifa hiyo na kupitisha maazimio maalum ya kuupatia ufumbuzi mgogoro unaoendelea na pia kuboresha hali ya huduma katika hospitali, vituo vya afya na zahanati inayoendelea kutetereka. Kanuni ya 64 (1) (c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge inayoelekeza kwamba “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika bunge, mbunge hatazungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama”; inatumiwa vibaya na serikali kuficha udhaifu na kudhibiti mamlaka ya bunge kwa kisingizio cha mahakama.

Muongozo wa jana tarehe 4 Julai 2012 wa Mwenyekiti wa Bunge Sylvester Mabumba wa kuendelea kukataa suala la hali tete ya sekta ya afya nchini kutokana mgogoro unaoendelea kati ya serikali na madaktari unaendelea kudhihirisha kwamba tumefika hapa tulipo kwa sababu ya uzembe wa bunge katika kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ya katiba ya nchi kuweza kuisimamia serikali. Badala ya kuendelea kutoa miongozo ya kulinda uamuzi wa Spika, ni muhimu uongozi wa bunge ukazingatia kwamba maamuzi hayo ya Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa bunge tayari yameshakatiwa rufaa hivyo kinachotakiwa katika hatua ya sasa ni kuitishwa kwa dharura kwa kikao cha kamati ya kanuni kuweza kubatilisha uamuzi huo ili wabunge watumie uhuru wa kikatiba wa ibara ya 100 kuwawakilisha wananchi katika kuisimamia serikali juu ya suala husika.

Nimewasilisha rufaa hiyo kwa katibu ambayo inapaswa kujadiliwa na kamati ya kanuni za bunge baada ya kutopokea majibu ya barua zangu mbili za kumshauri Spika kurekebisha miongozo iliyotolewa awali kuliwezesha bunge kutumia ipasavyo madaraka na mamlaka yake kwa mujibu wa katiba na kanuni za bunge kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma za afya nchini, jaribio la mauji ya Dkt. Ulimboka Steven na kushughulikia chanzo cha mgogoro unaoendelea kati ya serikali na madaktari wenye athari kwa nchi na maisha ya wananchi.

Ikumbukwe kwamba tarehe 27, 28, na 29 Juni 2012, na tarehe 2, 3 na 4 Julai 2012 ambapo kwa nyakati mbalimbali kumetolewa miongozo, maamuzi, majibu na Mheshimiwa Spika Anne Makinda, Mheshimiwa Naibu Spika Job Ndugai na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge Sylvester Mabumba Jenister Mhagama kwamba suala la madai ya madaktari na mgogoro uliotokana na madai hayo ni masuala ambayo hayapaswi kujadiliwa bungeni kwa kuwa kanuni ya 64 (1) (c) ya kanuni za bunge toleo 2007 inamkataza mbunge kuzungumzia jambo lolote ambalo linasubiri uamuzi wa mahakama. Katika rufaa yangu kwa kuzingatia masharti ya kanuni ya 5 (4) nimewasilisha maelezo ya kutoridhika na maamuzi yaliyofanyika sababu tatu za kutoridhika na maamuzi hayo kama ifuatavyo:

SABABU YA KWANZA;


Taarifa za Vyombo vya habari zimeeleza kwamba kesi iliyopo mahakamani imefunguliwa dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na si Jumuiya ya Madaktari Nchini pamoja na vyama vingine vya watumishi na wataalamu katika sekta ya afya na masuala mengine ya sekta husika. Aidha, ukiondoa suala la madai ya madaktari ambayo ni kati ya hoja zilizo mahakamani masuala mengine yanayoendelea si sehemu ya madai yaliyopo mahakamani, mathalani hali ya hivi sasa ya kudorora kwa huduma katika hospitali za umma nchini na jaribio la mauaji ya Dr Ulimboka Steven.

Hivyo, Spika kukataza masuala husika ni kinyume na kanuni 5 (1) na ni kuingilia masharti ya ibara ya 100 ya katiba ya nchi yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge. Irejewe kwamba Waziri Mkuu alilieleza bunge kuwa Serikali imejipanga kuziba pengo kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea kwa kupeleka madaktari kwenye hospitali za rufaa kutoka wizarani, kurejesha madaktari wastaafu, kupeleka wagonjwa wa rufaa katika hospitali za Jeshi na kupunguza idadi ya wagonjwa wa rufaa kutoka hospitali za wilaya na mikoa.

Na Rais katika hotuba yake kwa taifa ya tarehe 30 Juni 2012 iliyotolewa tarehe 1 Julai 2012 alijadili suala hilo na kueleza hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ikiwemo kufukuza madaktari; hata hivyo tarehe 2 Julai 2012 viongozi wa madaktari ikiwemo madaktari bingwa wametoa kauli kwa umma kwamba Rais alipotoshwa na timu aliyoituma kufanya majadiliano na madaktari. Kauli hizi zinaashiria kwamba bado mgogoro huo unaendelea na tayari tarehe 3 Julai 2012 vyombo mbalimbali vya habari vimeeleza athari za mgogoro unaoendelea ikiwemo migomo baridi katika baadhi ya hospitali nchini; tarehe 4 na 5 Julai pamoja na baadhi ya vyombo vya habari kueleza kwamba hali ya utoaji huduma imeanza kuimarika bado upo umuhimu wa bunge liwezeshwe kuingilia kati kulinda maisha ya wananchi na kuboresha sekta ya afya nchini.

SABABU YA PILI;


Hata masuala yanayosubiri uamuzi wa mahakama ambayo yamewekewa masharti kwa mujibu wa kanuni 64 (1) (c) yanaweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni kwa muongozo na utaratibu utakaowezesha majadiliano kufanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kwa kuzingatia kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Kanuni ya 5 (1) inaeleza kuwa katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa na ibara ya 84 ya katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazijatoa mwongozo, basi spika atafanya kazi kwa kuzingatia katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya awali ya maspika wa Bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.

Kwa kuwa maneno “jambo lolote linalosubiri uamuzi wa mahakama” hayajapewa tafsiri kwa mujibu wa kanuni, sijaridhika na miongozo ya Spika iliyotafsiri maneno hayo kudhibiti bunge kujadili masuala niliyoyaeleza. Hivyo, nimeiomba kamati ya kanuni itoe tafsiri sahihi kwa kuzingatia masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba na sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa kurejea pia maamuzi ya awali ya maspika wa bunge pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa bunge la Tanzania.

Nimemjulisha Katibu wa bunge kuwa niko tayari kuwasilisha maelezo na vielelezo zaidi wakati malalamiko yatakapokuwa yanajadiliwa na kikao cha Kamati ya Kanuni, hata hivyo kwa maelezo ya awali nimeiomba kamati irejee nyaraka toka maktaba ya Bunge la Uingereza ambalo lina utaratibu kama wetu wa kibunge ( “Separation of Powers- Standard Note: SN/PC/06053) ambayo katika ukurasa wa saba imeeleza yafuatayo kuhusu kanuni hiyo ya kukataza majadiliano bungeni kuhusu masuala yaliyo mahakamani ambayo kwa kiingereza huitwa “Sub Judice”:

“The Sub Judice rule is intended to defend the rule of the law and citizens’ right to fair trial. Where an issue is awaiting determination by the courts, that issue should not be discussed in the House in any motion, debate or question in case that should affect decisions of the court.
However, the sub judice rules are not absolute: The chair of proceedings of the House of Commons enjoys the discretion to permit such matters to be discussed. Morever, sub judice does not affect the right of parliament to legislate on any matter. The 1999 Joint Committee on Parliamentary Privilege explained that sub judice rules are intended to “strike a balance between two sets of principles. On the one hand, the rights of parties in legal proceedings should not be prejudiced by discussion of their case in Parliament, and Parliament should not prevent the courts from exercising their functions. On the other hand, Parliament has a constitutional right to discuss any matter it pleases”

Maelezo hayo yanathibitisha kwamba bunge linaweza kujadili masuala yaliyo mahakamani ilimradi mjadala huo usilenge kuathiri maamuzi ya kesi iliyo mahakamani, na pia Spika anayo mamlaka ya kutoa uhuru wa majadiliano kwa masuala yaliyo mahakamani bila kuingilia uhuru wa mahakama na kwamba kesi kuwa mahakamani hakuwezi kulizuia bunge kutumia haki na madaraka yake ya kikatiba.

SABABU YA TATU;


Spika badala ya kudhibiti mjadala huo bungeni kwa kutumia kanuni 64 (1) (c) angetoa muongozo wa kuwezesha kutolewa kwa hoja ya kutengua kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 150 kuruhusu mjadala kwa kuzingatia masharti ya ibara ya 63 (2) na Ibara ya 100 ya katiba ya nchi. Hivyo, sijaridhika na uamuzi wa kukataliwa kuahirishwa kwa shughuli za bunge ili kujadili jambo la dharura kwa mujibu wa kanuni ya 47 ambayo ilitolewa na kuungwa mkono lakini ikakataliwa kujadiliwa. Hata hivyo, ni muhimu kamati ya kanuni ikazingatia kuwa hatua zilizochukuliwa mpaka sasa ikiwemo za kufukuza madaktari hazijaweza kurekebisha hali iliyopo kwa kuwa nikiwa mbunge wa Dar es salaam kwa mkoa wetu pekee hatua hizi hazijaweza kuziba kwa ukamilifu hali ambayo inahitaji chombo chenye madaraka ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi kuingilia kati kupata ufumbuzi wa kudumu.

Aidha, serikali imetangaza kwenye vyombo vya habari kuwa imeweka mpango wa kuwahamishia wagonjwa katika hospitali binafsi suala ambalo linazua maswali mengi ikiwemo ukweli kwamba iwapo Serikali ina uwezo wa kugharamia matibabu katika hospitali binafsi ni kwanini isitumie fedha hizo kuboresha huduma katika hospitali za umma ikiwemo maslahi ya madaktari, madawa na vifaa tiba masuala ambayo ni chanzo cha mgogoro. Pia, kutumia fedha za umma zilizopitishwa na bunge kwa ajili ya hospitali za umma kulipia hospitali binafsi na kudorora kwa huduma katika hospitali za umma ni masuala ambayo yanahitaji usimamizi wa kibunge.

Hata hivyo, inafahamika wazi kwamba wagonjwa wenye hali tete wamehamishiwa katika hospitali za rufaa wengine kutoka hospitali binafsi na wengine kutoka katika hospitali za chini kote nchini kwa ajili ya kupata huduma toka kwa madaktari bingwa na kwa kutumia vifaa tiba vya hali ya juu zaidi; hivyo kuwarudisha walipotolewa au kuwabakiza katika hospitali za chini hata kama wanapaswa kupatiwa rufaa ni kuweka maisha yao rehani. Kwa upande mwingine pamekuwepo na utata kuhusu jaribio la mauaji ya Dr Ulimboka Steven kwa kiwango ambacho uchunguzi unaofanywa na jopo lililoundwa na askari polisi pekee hauwezi kuaminika na hivyo bunge linapaswa kuisimamia serikali kuwezesha uchunguzi huru.

HIVYO kwa kuzingatia sababu nilizozieleza nimeiomba kamati ibatilishe maamuzi hayo yaliyofanyika, kutoa pia muongozo wa kikanuni na pia itoe mapendekezo kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge ili kurekebisha udhaifu wa kuingiliwa visivyo kwa uhuru wa majadiliano bungeni na kuathiri haki, kinga na madaraka ya bunge ya kuisimamia serikali kuhusu maslahi ya watumishi wa afya na hali ya sekta ya afya nchini hata kuhusu masuala yasiyo mahakamani.

Mosi; kutoa idhini kwa mujibu wa kanuni ya 150 (1) ya kutolewa kwa hoja ya kutengua kanuni husika ya 64 (1) (c) kuliwezesha bunge kujadili Taarifa ya Kamati ya Huduma za Jamii. Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa bunge kutengua kanuni muhimu, mathalani, kanuni ya 94 inayolitaka bunge kukaa mwezi Februari kama Kamati ya Mipango kutoa mapendekezo ya mpango wa taifa, ilitenguliwa na matokeo yake ni kuwa serikali iliandaa bajeti ikiwemo ya sekta ya afya na kuwasilisha mwezi Juni bajeti ya serikali isiyozingatia kwa ukamilifu vipaumbele vilivyopendekezwa na wabunge kuhusu sekta ya afya nchini na hivyo kuchochea mgogoro.

Pili, Spika kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni 114 (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge kutaka kamati husika ya bunge kukutana kwa dharura na kuishauri wa haraka serikali kufuta kesi iliyoko mahakama kuu kitengo cha kazi au kutafuta suluhu ya nje ya mahakama ili kulipa fursa bunge kutumia madaraka yake ya kikatiba kujadili na kupitisha maazimio ya kuweza kusuluhisha pandembili za mgogoro badala ya mahakama ambayo mchakato wake utachukua muda mrefu kukamilika huku wananchi wakiendelea kuathirika. Uamuzi wa kurejea mahakamani unapaswa kuwa wa mwisho baada ya hatua zingine kushindikana.

Tatu; Spika kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa kanuni ya 114 (17) na 116 kuitaka Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii kupatiwa na kupitia nyaraka zilizowasilishwa mahakamani, na kuandaa taarifa maalum ya masuala yanayoweza kujadiliwa bungeni bila kuingilia suala lililo mahakamani. Izingatiwe kwamba Serikali imefungua kesi dhidi ya Chama Cha Madaktari (MAT) na haijafungua kesi dhidi ya Jumuiya ya Madaktari na Taasisi zingine katika sekta ya afya; hivyo kufunguliwa kwa kesi hiyo hakuwezi kulizuia bunge kujadili masuala mengine yanayohusu madaktari na sekta ya afya nchini.

Nne; Kanuni ya 53 (2) au 47 (1) za Kanuni za Kudumu za bunge inaweza kutumiwa kwa Waziri husika kwamba suala la namna ambavyo serikali imejipanga kutoa huduma katika hospitali kufuatia mgomo wa madaktari unaoendelea au mbunge yoyote kutoa hoja kuhusu hali kwa sasa ilivyo katika hospitali na sekta ya afya kwa ujumla kufuatia kuendelea kwa mgogoro kati ya serikali na madaktari na masuala hayo yakajadiliwa. Izingatiwe masuala hayo hayahusu mgogoro ulioko mahakamani bali ni ya dharura kwa ajili ya kuepusha madhara zaidi kwa wananchi na nchi kwa ujumla wakati taifa likisubiri taratibu za mahakama kukamilika.

Nimelazimika kukata rufaa juu ya maamuzi hayo kwa kuwa nimetumia njia za kawaida za kiofisi bila kupata majibu yoyote kutoka kwa Spika. Irejewe kwamba tarehe 27 Juni 2012 nilimuandikia barua Spika yenye kumb. OMU/BJMT/015/2012 kumuomba atumie mamlaka yake kwa kurejea Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007) Kanuni 5 (1), 37 (7), 53 (1), 114 (3), 114 (17) na 116 kuruhusu Bunge kujadili hoja ya madai ya madaktari ili kuisimamia Serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupitisha maazimio ya kuwezesha suluhu ya mgogoro unaoendelea.

Izingatiwe kwamba tarehe 30 Juni 2012 niliandika barua ya pili yenye kumb. Na. OMU/BJMT/015/2012 kumuomba Spika atumie mamlaka yake kuliwezesha bunge kujadili hali ya huduma katika hospitali za umma nchini na jaribio la kutaka kuuwawa kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Dk. Ulimboka Steven ili kutumia madaraka yake kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ya katiba ya nchi kuisimamia serikali kuokoa uhai wa wananchi wagonjwa na kuishauri serikali kushughulikia chanzo cha mgogoro.

Nimeomba Spika ataarifiwe kwa mujibu wa kanuni ya 5 (4) na kuitisha kikao cha dharura cha kamati ya kanuni kwa mujibu wa kanuni ya 5 (5) ya kanuni za Kudumu za Bunge na kulijulisha bunge kuhusu uamuzi utakaotolewa. Ni muhimu nguvu zielekezwe katika kushughulia chanzo cha mgogoro wa serikali na madaktari na wananchi kuhusu sekta ya afya ambacho bajeti finyu inayotengwa na serikali na kiasi kidogo cha fedha kinachotolewa katika sekta hii nyeti, na hivyo kushindwa kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya wakiwemo madaktari kwa upande mmoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kwa upande mwingine.

Hatua ya serikali kukimbilia mahakamani na kutumia kivuli cha mahakama kukwepa kushughulikia madai ya msingi ya madaktari ni kuendelea kushughulikia matokeo na hivyo kuendeleza migogoro ambao hata kama ukiwa ni wa chini kwa chini una athari katika huduma za afya. Wenu katika kuwawakilisha wananchi,

John Mnyika (Mb)
 
Leo ni bajeti ya Wizara ya Afya, je masuala haya yataruhusiwa kujadiliwa au kwa mara nyingine tena serikali itasingizia yako mahakamani?

serayamajimbo
 
Back
Top Bottom