The Richest Man In Africa: Kila Utajiri Una ukafiri nyuma yake
SEHEMU YA TATU
Kwa wasomaji wa makala zangu naamini watakuwa si wageni kwa mtindo wangu wa uandishi ninaopendelea mara kadhaa kwa kuianza simulizi kuanzia mwishoni au katikati na kisha kuchambua mwanzo wa sakata zima na hiki ndicho nakusudia hasa kukifanya katika makala hii.
Katika sehemu zilizopita nilieleza namna ya mazingira ambayo Mzee Kabila aliuwawa na pia nimegusia kiduchu kuhusu washirika wa mauaji hayo.
Lakini pasipo kutoka nje ya mstari na kusahau lengo, makala hii si mahususi hasa kuchambua historia au mgogoro wa Congo bali ni utetezi wangu juu ya hoja ambayo najaribu kuijenga kuhusu mtu ambaye ni tajiri zaidi barani afrika lakini kamwe huwezi kukuona akitajwa katika majarida ya kuorodhesha matajiri kama Forbes na Forbes Africa. Kama ambavyo nilianza kujenga hoja yangu juu ya ushawishi alionao katika ukanda huu wa nchi za maziwa makuu na namna ambavyo ana uwezo wa kuratibu matumizi ya rasilimali katika nchi hizi ndivyo hivi ambavyo nitaendelea na makala hii kwa kuangalia ushaiwhi huo na chimbuko lake.
Sasa basi katika sehemu hii nataka nichambue kwa kina mno (mno hasa) chimbuko la uhusika wa "Paul" kwa kile ambacho kilitokea Congo kuanzia mauaji ya Patrice Lumumba, Kung'olewa kwa Mobutu, kuuwawa kwa Mzee Kabila na hiki ambacho kinaendelea sasa nchini Congo. Naomba ufuatane nami kwa makini sana nikichambua uhusika wake kule Congo na itakuwa rahisi zaidi tukianza kuchambua alionao kwenye nchi nyingine za Afrika mashariki na namna ambavyo anaratibu matumizi ya rasilimali.
Sasa basi….
Kuelewa kinachoendelea hivi sasa Congo pamoja na mfululizo wa vifo vya viongozi wa juu mara tu baada ya baada ya kupata uhuru, karata nzuri ya kuelewa namna ambavyo Paul alifanikiwa kwa umahiri kujipenyeza na kuimarisha ushawishi wake nchini humo.
Ni kwamba, baada ya kupata uhuru na kisha muda mchache baadae nchi ya Congo kuingia kwenye machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na mparaganyiko kwenye jeshi kufuatia kuuwawa kwa Patrice Lumumba kuliibuka vikundi kadhaa vya wapiganaji nchini Congo. Kipindi hiki ninachokiongelea hasa ni mwanzoni mwa mwaka 1964 kipindi ambacho Cyrille Adoula alikuwa ndiye anaongoza nchi ya Congo. Cyrille Adoula alikuwa ni kiongozi dhaifu mno ambaye hakukubalika kwa ukubwa ndani ya Congo kwa wananchi na hata kwa wanasiasa wenzake. Huko mbeleni nitafanya rejea na kugusia hili kwa undani pamoja na kifo cha Lumumba na kuibuka kwa Mobutu.
Mparaganyiko wa kijeshi ulisababisha kuibuka kwa vikundi karibia vinne vya wapiganaji msituni lakini vyote vikiongozwa na umoja uliojiuta NLC (National Liberation Council). Kuna bwana aitwa Gaston Sumaliot alikuwa anaongoza vuguvugu hili kutokea kaslazini mashariki mwa Congo huku moja ya Maluteni wake Bw. Laurent Kabila akiongoza vuguvugu hili kutokea mashariki mwa Congo. Wakati huo huo moja ya maswahiba wakubwa wa Lumumba aliyeitwa Christopher Gbenye na kikundi chake cha wapiganaji walikuwa wanashikilia eneo kubwa pia la Congo kwa msaada mkubwa wa Urusi na Uchina.
Mwezi July mwaka huo 1994 Moise Thsombe alifanikiwa kuingia madarakani kwa kumuondoa Cyrille Adoula na baada tu ya kushika madaraka alianza kutafuta msaada wa kijeshi kwa Marekani, Ubelgiji na kwa makaburu wa Afrika Kusini kitendo ambacho hakikuwafurahisha wazalendo wengi wa Kiafrika.
Ikumbukwe kwamba Marekani wana maslahi makubwa mno nchini Congo kabla hata ya Uhuru wa Congo hasa kutokana na ulukuki wa rasilimali zilizopi nchini humo. Kama ambavyo tutaona hapo baadae kinagaubaga kabisa shirika la ujasusi la Marekani, CIA walihusika moja kwa moja katika mauaju wa Patrice Lumumba kwa mikono ya kina Sese seko Mobuttu.
Kwa hiyo kitendo cha Moise Tshombe kuomba msaada wa kijeshi kwa jumuiya ya kimataifa yalikuwa ni mazingira sawia kabisa ambayo Marekani yaliwavutia.
Rais wa Marekani wa kipindi kile Bw. Lyndon Johnson alimtuma Bw. Averell Harriman ambaye alikuwa ni waziri wa biashara kipindi hicho kwenda nchini Congo katikati ya mwaka 1964. Ilitumiwa 'cover' ya waziri huyo kutembelea nchi ya Congo akiwa na msafara wa 'Wafanyabiashara' wa Kimarekani kana kwamba wameenda kuangalia fursa za uwekezaji nchini humo. Lajini ajabu ni kwamba katika msafara ule alikuwemo moja ya sura ambazo watu wengi hawakuifahamu sana kipindi kile, Bw. Cyrus Vance ambaye alikuwa ni naibu Waziri wa ulinzi wa Marekani (baadae alikuja kuwa Waziri wa Mambo ya Nje).
Dhumuni hasa la safari ile ilikiwa ni kufanya tathimini ya hali halisi ya Congo ili kujua hatua stahiki za kijeshi ambazo Marekani wanaweza kuzifanya.
Safari ile ilizaa matunda mzuri kwani mwezi September mwaka huo 1964 Ubelgiji ilituma kikosi chake kusaidia jeshi la serikali ya Moise Tshombe. Pia makaburu wa Afrika Kusini pamoja na wapiganaji kutoka Rhodesia waliwasili ndani ya Congo katika kipindi hicho hicho. Mwezi November mshirika wa Karibu wa Marekani, Uingereza naye alituma wanajeshi wake nchini Congo. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba vikosi vyote hivi viliingizwa Congo kwa ndege za jeshi la Marekani. Lengo kuu la wanajeshi hawa na vikosi hivi vilivyoingia Congo ilikuwa ni kudhibiti nakutokomeza vikundi vya 'waasi' walioko msituni.
Ni dhahiri kabisa kwamba Marekani alikuwa anajaribu kuficha mkono wake juu ya uhusika wa uingizaji wanajeshi nchini Congo hasa kutokana na aibu kubwa ambaye walikuwa wametoka kuipata nchini Cuba kwenye mapambano ya 'Bay of Pigs' ambayo Marekani na vibaraka wake aliowapandikiza walitandikwa kwa aibu na kuzua mzozo wa kimataifa kati ya nchi za kibepari na zile za mlengo wa kijamaa zikiongozwa na Urusi na Cuba.
Ikumbukwe kwamba katika miaka ile ya sitini vuguvugu la nchi za Afrika kupata Uhuru lilikuwa limeshika kasi, kwa hiyo kitendo cha nchi za Ulaya kuingiza vikosi vya kijeshi Congo kilionekana kana kwamba Wakoloni waliotimuliwa walikuwa wanarejea upya. Viongozi wote wa Afrika walipinga kitendo hicho lakini kiongozi mwenyewe wa Congo kipindi hicho Moise Tshombe aliwakumbatia mabeberu.
Mwaka huo huo 1964 mwezi Desemba kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa, mwanamapinduzi Che Guevara alitoa hotuba kali akilaani juu ya hujuma na uzandiki unaofanywa na mataifa ya magharibi kwenye nchi za Ulimwengu wa tatu na akatoa mfano hai nchi ya Congo. Hotuba ile ni moja ya hotuba za kukumbukwa zaidi mpaka leo hii. Guevara alipinga vikali kitendo hicho ambacho alikiita cha uvamizi wa ardhi huru. Moja ya kauli yake ya kukumbukwa zaidi kwenye hotuba yake ni ile ambayo alisema kuingizwa kwa wanajeshi wa kimagharibi nchini Congo ni njama (conspiracy) ya mataifa yenye nguvu ya kimagharibi kujitwalia tena afrika akitoa mfano wa taarifa ya intelijensia akidai kwamba kwa mfano wapiganaji wa kibelgiji walipakiwa kwenye ndege za jeshi la marekani ambazo ziliruka kutoka kwenye viwanja vya ndege vya kijeshi vya Uingereza (Belgian paratroopers, carried by US planes, took off from British Bases).
Kama tujuavyo kwamba Guevara hakuwa mtu wa utani wala maneno matupu. Guevara ni moja ya wanamapinduzi mahiri zaidi kuwahi kutokea tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Baada ya mkutano ule wa Umoja wa Mataifa Che Guevara kwa kushauriana na Fidel Castro alianza Ziara Barani Afrika kwa nia ya kuratibu mbinu za namna ya kukomboa mataifa hayo ya Afrika. Ziara ya Guevara ilianzia Algeria, kisha akaenda Mali, kisha Congo-Brazaville, kisha Senegali, kisha Ghana, kisha Misri na ziara hii alihitimisha moja ya sehemu ambayo alikusudia zaidi, TANZANIA… naam sio Congo bali Tanzania japo dhumuni lake lilikuwa ni Congo. Alikuja Tanzania kwa sababy moja kubwa, Rais wa Tanzania kipindi hicho, Mwalimu Julius K. Nyerere alikuwa amekusudia kumkutanisha Guevara na kijana wa kikongo mwenye kikundi chake cha msituni na mwenye nia hasa ya kuikomboa Congo. Mwalimu Nyerere alikuwa anataka kumkutanisha Guevara na Laurent Kabila.
Itaendelea…
Habib - 0718 096 811
To Infinity and Beyond