Kwenye hoja moja nimetoa mfano wa jeuri za kisomi tulizonazo Watanzania kwa wenzetu ambao ama hawajasoma au hawafanyi kazi za "hadhi".
Kuna jamaa watatu ambao nawafahamu ambao wanafanya (walifanya) kazi McDonald na Payless shoes.
Hawa jamaa, walianza kazi kama watu wa kawaida na wakaendelea mpaka kuwa store manager.
Sasa majigambo yakawa jamaa wame-losti, kisa wanafanya kazi McDonald na Payless, wti kazi hazina hadhi.
Walikuwa wanatoa kashfa wakasahau kuwa wenzao kufikia hatua ya kuwa store manager, wamejifunza mengi, iwe ni book keeping, stock taking, administration, marketing, sales and sales goals/quota, human resource; interview, scheduling, vendor relationship na payments of bills and other expenses!
Sasa sisi tunafikiri kuwa tukishapata vyeti, basi tuko tayari kuwa mameneja na mawaziri kwa kuwa tumehenyeka vyuoni!
Ndio maana ninapozungumzia elite class, ni hata wale ambao ni waalimu wa vyuo na wataalamu wetu. Kama wangekuwa ni makini, basi wasingeendelea kuitegemea Serikali au kuirushia Serikali makombora kuwa Wasomi wa Tanzania hawasikilizwi.
Je wameshindwa nini kuingia katika sekta binafsi au taasisi na kufany akazi ambazo kipimo cha kuelimika kwao itakuwa ni matunda ya kazi zao na si vyeti?
Mtu anakwenda somea Kilimo SUA, akimaliza miaka yake ya chuo na shahada zake, anataka apewe dawati pale Wizara ya Kilimo au kwenye Shirika la Kilimo. Je mbona asiende kwenye vijiji au kijijini kwao akafundishe Wajomba, Shangazi na majirani mbinu bora za kilimo?
Kwa nini tutegemee kusukumwa na Serikali au tupewe imla na Serikali ni jinsi gani tufanye kazi?
Kama mtaalamu huyu angekwenda kijijini, akatumia utaalamu wake kwa kumuonyesha mkulima jinsi gani ya kuongeza mavuno yake kwa kutumia ardhi ile ile au muda mdogo na mfupi na hivyo mkulima huyu kuwa na ziada, basi mafanikio ya mkulima huyu na wenzake, yangeekezwa na sifa kupewa mtaalamu huyu.
Mwaka 2004, nilikuwa Dar na nikawa navinjari kule Gongo la Mboto, nikasimama kwenye kibanda cha jamaa mmoja muuza matunda na mboga. Tukaanza kusogoa nikaanza kumuuliza je kwa siku anaingiza pesa kiasi gani na ni mara ngapi kwa siki anakwenda shimoni (Kariakoo) kununua bidhaa za kujazia kwenye kibanda/genge chake?
Akaniambia anakwenda Shimoni kila siku na mapato yake kwa siku si makubwa sana. Nikamuuliza je ni asilimia ngapi ya anachonunua kila siku kinauzika, akaniambia ni takriban asilimia35%. Nikamuuliza kama anauza theluthi tuu, kwa nini kesho yake anakwenda nunua kwa wingi ule ule wa siku iliyopita na si kuhakisha kuwa ananunua fidia ya alichokiuza, akaniambia hajui kwa nini.
Pale nje ya kibanda chake, kulikuwa na takataka kibao za matunda yaliyooza na jamaa walikuwa jirani wakicheza bao walikuwa wakilalamika kuhusu harufu na nzi. Nikamuuliza tena, ni wapi anapotupa takataka, akaniambia hana shimo bali huzitupa hapo pembeni.
Nikaamua kukaa chini kwa dakika ishirini, kumfundisha pamoja na jirani zake ni vipi wanaweza kujineemesha kwa kufanya biashara kwa ushindani na umahiri.
Nikawapigisha darasa kuwa si lazima wanunue ujazo ule ule wa bidhaa kila siku, bali wanaweza kuongezea kujazia kila baada ya siku tatu na zile bidhaa zilizokaa zaidi ya siku mbili wapunguze bei ili ziuzike na zisioze.
Zaidi nikawaambia inabidi ama wawe na pipa la takataka au watafute mahali wachimbe shimo wawe wanamwaga takataka na kupaweka pale kijiweni pakiwa safi, waweke magudulia ya maji na hata kwenye meza ya watu kubangaiza wanaweza kuweka ubao wa drafti na karata.
Nikamuuliza kama anaweka fedha benki, akasema hapana, nikamshuri inabidi aanze kuweka fedha benki ili aweze kutunza mahesabu yake vizuri na kwa usalama.
Nikarudi tena kupima maendeleo baada ya wiki kama mbili, jamaa akaniambia mambo mdundo, ndipo akaniuliza nakaa wapi na imekuwaje nilienda kumfundisha yeye na wenzake jinsi gani ya kufanya biashara kwa ubora.
Sikumwambia ninapokaa, ila nilimwambia kuwa nia yangu ni kumsaidia hata kama si kwa pesa au mimi kulipwa kwa kutoa ushauri, bali ni kumuona yeye akipiga hatua katika biashara yake!