CCM yashindwa kufungua kampeni zake Tarime
WAKATI baadhi ya vyama vya upinzani vikiwa vimeshaanza kampeni za kuwania kiti cha ubunge cha jimbo la Tarime, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kuzindua kampeni zake kwenye Kata ya Tarime Mjini kutokana na kifo cha kada wake, Gidioni Nyamhanga.
Ingawa CCM ilishindwa kuzindua kampeni zake jana, mgogoro na tuhuma nzito wanazotupiana viongozi wa kambi ya upinzani, hasa kitendo cha Mchungaji Christopher Mtikila, kumshambulia mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wengine, zinaonekana kukifagilia njia chama hicho tawala kuweza kutwaa jimbo hilo.
CCM ambayo jana ilipanga kuzindua kampeni kwenye Kata ya Tarime Mjini, ilishindwa kutokana na kuungana na maelfu ya wakazi wa eneo hilo kushiriki mazishi ya kada huyo ambaye pia aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha.
Nyamhanga, ambaye ni kada mwandamizi wa CCM, alifariki jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu. Miongoni mwa waliojitokeza ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.
Kampeni za CCM kata ya Tarime mjini na ubunge zitaendelea hapo kesho, katika kata ya Pemba katika vijiji vya Nyabisaga, Pemba na Nyabitocho huku uzinduzi wa viongozi wa kitaifa ukitarajiwa kufanyika Septemba 21, ambao utafanywa na Makamu Mwenyekiti Pius Msekwa.
Wakati kampeni hizo zikiendelea, tuhuma miongoni mwa viongozi wa upinzani na uamuzi wa kila chama kutaka kusimamisha mgombea, zinaonekana kuisafisha njia ya kutwaa kiti hicho ambacho kilishikiliwa Chadema, kabla ya kifo cha Marehemu Chacha Wangwe.
Wakati Mbowe akiwa Mwanza juzi, pasipo kumtaja Mtikila, alishutumu baadhi ya vyama visivyo makini kutumiwa na CCM, Mtikila amejibu mapigo akisema kuwa kama Mbowe na wenzake wamekashifiwa wakaenda mahakamani.
Kwa msisitizo, Mtikila jana alipoulizwa kwamba anatumiwa na CCM kuvuruga upinzani, alisema hiyo si hoja bali hoja ya msingi katika taarifa yake ya mwishoni mwa wiki ni kifo cha Wangwe, ambacho vigogo wa Chadema wakiongozwa na Mbowe wanahusika.
Hata hivyo, Chadema imekwisha zitolea ufafanuzi tuhuma hizo kikisema kwamba hakuna kiongozi wake aliyehusika na kifo hicho, huku Katibu Mkuu Dk Wilbrod Slaa, akitaka iundwe tume ya uchunguzi.
Akizungumzia onyo la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, kwamba atakichukulia hatua chama hicho iwapo kilitumika kuendesha siasa za kuchafuana, Mtikila alisema msajili huyo hana uwezo huo.
Tendwa alinukuliwa akionya kwamba, atapitia taarifa ya Mtikila kuona kama DP ilihusika kukichafua Chadema na pia akahoji kutuhumiwa watu.
Mvutano huo umeifanya Chadema kushutumu vyama vingine kwamba, vinatumiwa na CCM kukihujumu huku vyama vingine navyo wakiwemo wanasiasa kama Mtikila, wakitoa tuhuma nzito kwa Chadema.