TCU yamsafisha Waziri Mathayo

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), imemsafisha Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Dk. David Mathayo kwa kutambua vyeti vya elimu yake.

Hatua ya TCU imekuja siku chache baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta kulitangazia Bunge kupokea vyeti vya taaluma vya Dk. Mathayo, kwamba amevipata kutoka vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Aidha, Tanzania Daima Jumatano imeipata nakala ya barua ya Februari 13 mwaka huu kutoka TCU kwenda kwa mwanasiasa huyo ikimtaarifu kutambua shahada zake.

Barua hiyo yenye kumbukumbu namba TCU/A.40/2/VO.56/35 ilikiri kuwa Dk. Mathayo alituma vyeti vyake vya taaluma vinavyoonyesha alipata Shahada ya Kwanza ya Madawa ya Mifugo katika Chuo cha Kilimo cha Morogoro (SUA) mwaka 1997.

Katika barua hiyo, pia inaelezwa kwamba alipata Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Pretoria, nchini Afrika Kusini mwaka 2001.

TCU katika barua hiyo ilikiri pia vyeti vya Dk. Mathayo viliambatanishwa na Shahada ya Uzamivu katika Mifugo aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Free State cha Afrika Kusini mwaka 2003.

“TCU kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu namba 5 (1) (n) cha Sheria ya vyuo vikuu namba saba ya mwaka 2005 inatambua shahada alizotunukiwa Mathayo kama ilivyoidhinishwa hapo juu na kwamba vyuo hivyo vinatambulika,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Wasiwasi wa vyeti vya shahada za baadhi ya vigogo umeibuka hivi karibuni baada ya mwanaharakati Kainerugaba Msemakweli kuandika kitabu kiitwacho ‘Ufisadi wa Elimu’ kinachowataja baadhi ya mawaziri na manaibu wa serikali ya awamu ya nne kuwa wameghushi shahada zao ama wamezipata katika vyuo visivyotambulika.
 
Back
Top Bottom