TCB yabuni mbinu kuongeza unywaji wa kahawa nchini

Umkonto

JF-Expert Member
Dec 27, 2018
2,102
3,615
Moshi. Bodi ya kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na wadau pamoja na wataalamu mbalimbali, inakusudia kuanzisha migahawa ya kahawa inayotembea, (Mobile Coffee Shops), lengo likiwa ni kuongeza kiwango cha unywaji wa kahawa nchini kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025.

Migahawa hiyo, ambayo itakuwa na vifaa vya kisasa vya kutengeneza kahawa za aina tofauti ikiwemo Capucchino, Cofee Latte, Americano na Espresso, itawezesha wananchi mbalimbali kufikiwa mahala popote walipo na kufurahia kinywaji hicho, hatua inayodhaniwa kuwa itachochea ukuaji wa soko la kahawa nchini.

Hayo yamebainishwa leo Mei 4,2023 na kaimu Mkurugenzi idara ya uhamasishaji na ubora kutoka TCB, Frank Mlay wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuhusiana na mikakati iliyopo katika kuhakikisha soko la ndani la kahawa linakuwa na kupunguza utegemezi wa soko la nje.

Mlay ambaye ni Afisa ubora na uhamasishaji katika bodi hiyo, amesema zaidi ya silimia 90 ya kahawa inayozalishwa nchini, inategemea soko la nje na mpango uliopo ni kubuni na kutengeneza migahawa inayotembea ambayo itazungusha kahawa kama vile zinavyozungishwa Ice Cream mitaani ili kuamsha ari ya kunywaji wa kinywaji hicho kuanzia ngazi za chini kwenye jamii.

Amesema migahawa hiyo ambayo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2023/2024, itakuwa ya kisasa na yenye mitambo ya kisasa ya kutengeneza kahawa za aina zote na watagawiwa vijana vijana ambao wataitumia kama vyanzo vyao vya mapato.

Aidha amesema mbali na mkakati huo, pia wanakusudia kutoa mafunzo kuwajengea uwezo vijana na kuanzisha migahawa ya kahawa katika vyuo vikuu vyote nchini, hatua ambayo itasaidia kujenga jamii ambayo inapenda kunywa kahawa kuanzia ngazi ya chini.

"Ili kuimarisha soko la Kahawa ndani na nje ya nchi, sisi wenyewe tunapaswa kuanza kuipa thamani kahawa yetu, na katika kufanikisha hili, bodi tumejipanga kuongeza unywaji wa kahawa nchini na kupambana na dhana potofu iliyoko kwenye jamii juu ya matumizi ya kinywaji hicho kwa kutoa elimu"

"Kama tunavyoona baiskeli mbalimbal zinazotembeza ice cream na vitu vingine mtaani, ndivyo tunavyotaka kufanya kwa ajili ya kahawa, lakini pia, tuna mkakati wa kufungua migahawa katika vyuo vikuu vyote nchini, na migahawa hiyo tunategemea itaendeshwa na vijana, hatua ambayo itajenga utamaduni wa kunywa kahawa yetu kuanzia ngazi ya chini,” amesema.

Mtafiti upande wa usambazaji wa Teknolojia na Mafunzo kutoka taasisi ya utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) Dk Jeremiah Magesa amesema unywaji wa kahawa nchini ni mdogo ambapo ni asilimia 7 hadi 10, hivyo kunahitajika kuendelea na uhamasishaji, ili kuinua kiwango hicho.

"Tunaendelea kuhamasisha wananchi na wadau wote kuendelea kunywa kahawa ili kuimarisha soko la ndani la kahawa yetu, na tukifanya hivyo pia tutaondoa changamoto ya kuyumba kwa soko la zao hili".

Mmoja wa vijana ambao wanaendesha Mobile Coffe Shop mkoani Arusha, Aman Mwenera amesema walibuni mgahawa huo unaotembea baada ya kuona kuna uhitaji wa huduma hiyo katika jamii na kwamba wameweza kuwafikia watu katika maeneo mbalimbali.

"Kupitia mgahawa huu unaotembea, tunaweza kuwafikia wanywaji wa kahawa katika maeneo mbalimbali mitaani na hata kwenye sherehe na mikutano na hii inachochea kwa kiasi kikubwa unywaji wa kahawa nchini".

Chanzo: Gazeti la Mwanchi, 04 Mei, 2023
 
Naomba kuelimishwa, kahawa ina faida gani mwilini?

Nimesoma hiyo habari nimeona ni uhamasishaji mwanzo mwisho, na sijaona wakitaja faida za kahawa.

Mimi ni miongoni mwa watu wanaoamini kahawa inasababisha ugonjwa wa moyo na presha, mana miaka ya nyuma nilijaribu kuwa nakunywa kahawa kila siku jioni mapigo ya moyo yakawa yanaenda mbio.
 
Back
Top Bottom