Tasnifu za njano5: Kikwete ni rais wetu, wapinzani na watanzania kila mpanda upepo huvuna tufani.

Dotto C. Rangimoto

JF-Expert Member
Nov 22, 2012
1,985
1,282
Pamoja na mafanikio mengi ya rais Kikwete tangu aingie madarakani hususani katika ujenzi wa barabara na miundombinu mingine lakini bado hayo mafanikio si lolote mbele ya kushindwa kwake kutekeleza ilani ya chama cha mapinduzi na ile kauli mbiu yake ya "MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA". Tukijaribu kupima kufaulu na kufeli kwa rais Kikwete katika mizani ya "utendaji", kwa vyovyote vile "kufeli" kutakuinua upande wa kufaulu kwa urahisi zaidi.

Si lengo ya makala haya kuzungumzia kufaulu na kufeli kwa rais Kikwete, na kwa hivyo makala haya hayatabeba ushahidi wa kisayansi wenye kuonesha bila shaka yoyote kuwa rais Kikwete amefeli. Lengo ya makala haya nikuzungumizia japo kwa ufupi unafiki wa watanzania na wanasiasa kila wanapomtazama rais Kikwete na kufeli kwake kama rais. Pamoja na hayo, panapo salama nitakuja kuzungumzia "kufeli" na "kufaulu" kwa rais kikwete.


Tunafanya makosa sana kumlaumu rais kwa kufeli kwake kukata kiu za wananchi wengi, naam, tunamlaumu kwa kukata kiu za watu wachache wenye kipato au marafiki zake. Kitendo hichi kimepelekea athari za kukua kwa uchumi na kupungua kwa umaskini wa kipato kubaki kwenye makalablasha ya serikalini tu, lakini mtanzania wa Kinyope, Mkanyageni, Kiboje, Mpui, Kinesi, Sanya juu, Lusitu, nk bado hata sasa hawajapatwa na athari hizo za kwenye makalablasha. Kiukweli wananchi wengi tunaishi kwenye lindi la umaskini.

Tunafanya makosa sana kwa kumlaumu rais Kikwete kwa yote yasoridhisha ayafanyayo kama rais. Yawezekana mwaka 2005 tulikuwa hatujamtambua vizuri na alikuwa hodari kwa kutoa tabasamu lenye kuashiria upendo, uadilifu, huruma, na uwajibikaji kwa umma. Mara baada ya kushinda kwa kishindo, lile tabasamu lilileta tafsiri ya mwanamume jamali mwenye hulka ya kulaza ukope ili kulaghai mabanati. Mwenye kulaghai akifanikiwa hajui kurai, JESHI LA POLIS halisemi urongo.

Tunafanya makosa sana kumlaumu rais Kikwete hasahasa katika ngwe yake hii ya pili. Hivi sisi si ndio wenye jukumu la kuwapa watu dhamana ya kuongoza nchi kwa niaba yetu sote? Hivi rais Kikwete hakufeli katika ngwe yake ya kwanza? Kama alifeli ilikuwaje tukalainika hata tumkabidhi mioyo yetu kisa katulazia ukope kwa uhodari zaidi kuliko alivyofanya 2005? Au kujiangusha kwake jukwaani ndio kukapelekea tumuonee huruma? Kura za huruma? "kura za huruma" na "kura za kutisha" tukikubalina tuzitambue katika katiba ijayo maana kura hizi ni mtaji kwa wanasiasa mufilis.

Tunafanya makosa sana kumlaumu rais Kikwete kwa madudu ayafanyao ikulu ikiwa sisi kama umma ndio tuliompa mamlaka ya yeye kuwa pale ikulu na kufanya yote kwa niaba yetu sote. Sisi ndio tuliompa Kikwete mamlaka hayo aidha kwa kumpigia kura ya "ndio" au kutokupiga kura kabisa au kwa kuharibu kura. Wale wote ambao hawakupiga kura kwa makusudi wamechangia ushindi wa Kikwete, endapo tu kama waliongozwa na chuki yao dhidi ya CCM au Kukata kwao tamaa ndio msingi wa hatua yao ile ya kususia kupiga kura.

Sasa kama mtu mara baada kuweka alama ya "vema" chini ya picha ya Dr.Slaa au Prof Lipumba akaitoboa picha ya Kikwete kwenye macho, hapo hivi tutegemee nini? Kama mtu anazila kwenda kupiga kura kisa tu uchaguzi uliopita mgombea aliyempigia kura hakushinda. Mwingine anasema kura yangu moja haiwezi kuumpa au kumnyima mgombea ushindi, mwingine anasema mgombea yeyote atakayeshinda sawa hivyo hakwenda kupiga kura. Watu hawahawa ndio wanaoilaumu serikali kwa kushindwa kuihudumia jamii ipasavyo.

Wanasiasa wa upinzani wanakosea sana kumlaumu Kikwete kwa ayafanyao Ikulu, ni bora wanasiasa hawa wavishukie vitendo vyao ambavyo havina tija kwa vyama vyao na kwa umma ujumla. Hivi kwanini wanamlaumu Kikwete badala ya kuvilaumu vitendo vyao ambavyo tangu mfumo wa vyama vingi uanze vimeshindwa kuwapatia uhalali wa kuunda serikali na hata kuwaunganisha kama wapinzani.


Ni vema wapinzani wasiishie tu kumlaumu Kikwete na ufisadi wake anaoufanya ikulu, ingekuwa lawama dhidi ya serikali ni mtaji mzuri wa kwenda ikulu basi Kikwete asingeshinda urais kwa awamu zote mbili, kwani jina lake lipo katika orodha ya mafisadi papa, katu hakuna mwenye ubavu wa kumtenganisha Kikwete na ufisadi wa BOT na kubwa zaidi ufisadi wake ulitangazwa hadharani pale Mwembeyanga. Nasema hivyo kwasababu, pamoja na nyimbo zao za ufisadi lakini bado watanzania wakamchagua Kikwete kwa mara ya pili. Nasema wasiishie kuimba "ufisadi" tu, bali ni vema watazame pia na hali ya mambo katika vyama vyao kutokana na sababu zifuatazo.


KWANZA: WANASIASA WA UPINZANI WANA MASHABIKI WENGI KUZIDI VYAMA VYAO.
Vyama hivi vipo tu Dar es salaam na vingine vipo kwenye briefcase tu lakini havipo kwa watanzania. Hata vile ambavyo vinaamini kuwa sasa vipo katika maeneo mengi ya nchi yetu kama vile CHADEMA, kiukweli huko vina mashabiki wa viongozi wa vyama hivyo na si mashabiki wa vyama hivyo. Mfano Zanzibar kuna mashabiki Seif Sharifu na si mashabiki CUF, na Mbeya kuna mashabiki wa Sugu na si mashabiki CHADEMA. Sasa kama chama hakina hata mashabiki ndio kitakuwa na wanachama?

Kuwa na kadi ya chama fulani au kuwa katika orodha ya wanachama wa chama fulani hakumaanishi wewe ni mwanachama wa chama hicho bali kunathibitisha wewe ni mwachama wa chama hicho. "Kumaanisha" mahala pake moyoni, uthibitisho mahala pake machoni. Mtu anaweza kuwa na kadi zaidi ya moja na kila kadi itamthibitishia uanachama wakati zile zingine akizificha mfukoni. Leo anaweza kuwa CUF kwa kuficha kadi ya CCM na CHADEMA, na kesho anaweza kuwa CHADEMA kwa kuficha kadi ya CUF na CCM. Mtu aliyewilaya shauri ya kuwa mwanachama wa "kumaanisha" hawezi kuwa na mzigo wa "kadi hai". Atakuwa na kadi hai moja tu, na zingine kama anazo zitakuwa ni "kadi mfu".

Viongozi wa vyama upinzani wafanye jitihada za kuhakikisha mashabiki wao wanakuwa mashabiki wa vyama vyao tayari kwa kuwafanya wanakuwa wanachama wa vyama vyao wa "kumaanisha". Mashabiki wa Sugu pale Mbeya sasa wageuzwe wawe mashabiki wa CHADEMA na baadae wawe na uanachama wa "kumaanisha" na si uanachama wa kadi. Wakati viongozi hawa wakipambana na ufisadi kwa kumuoneshea kidole rais Kikwete lazima pia wawafundishe mashabiki wao falsafa, itikadi na sera za vyama vyao juu ya mambo yanayomgusa mpiga kura mojakwamoja. Nasema wakome kuishambulia tu serikali, mfano kwa CHADEMA, huu ni muda wa kuwageuza mashabiki wa Zitto na Dr.Slaa wawe mashabiki wa CHADEMA na hatimaye wawe wanachama wa chama hicho.


PILI: SASA TUNATAKA MABADILIKO NA SI UKOMBOZI, DHANA YA KUJITOLEA ISIPOTOSHWE.
Kwa vyovyote vile katibu mkuu wa CHADEMA Dr.Slaa ameshagundua kuwa CHADEMA haina wanachama na mashabiki wengi bali ina mashabiki wengi wa Dr.Slaa, Mbowe, Zitto, Mnyika, Sugu, Lema na viongozi wengine wa CHADEMA wenye ushawishi mkubwa. Kwa kuligundua hili ndio maana Dr.Slaa anampango wa kuhakikisha CHADEMA inafika kila kijiji na kila mtaa kwa kufungua matawi ya CHADEMA huko. Kila tawi litakuwa na misingi isiyopungua mitano na kila msingi utakuwa na wanachama wasiopungua 30. Hii ina maanisha kila mtaa na kijiji utakuwa na wanachama wasiopungua 150.

Misingi na Matawi haya yakianzishwa juu ya mwamba wa uanachama wa "kumaanisha" basi hiyo misingi na matawi yatakuwa mali ya CHADEMA, lakini ya kianzishwa chini ya ushabiki na nguvu ya ushawishi wa kiongozi fulani basi hiyo misingi na matawi yatakuwa mali ya CHADEMA kinadharia tu, lakini kiukweli hiyo misingi na matawi itakuwa mali ya kiongozi mwenye mashabiki waliounda misingi na matawi hayo. Kama matawi na misingi anayojigamba Dr.Slaa itafunguliwa nchi nzima itafunguliwa chini ya mwamba wa ushabiki basi sitashangaa kuja kusikia jiwe la tawi fulani limepakwa rangi za CUF au CCM au NCCR mara baada ya wanachama wa tawi zima kuamia chama cha rangi husika kisa tu yule wanayemshabikia kaamia chama hicho.

Kazi ya kuwafanya mashabiki wa watu fulani wanakuwa mashabiki wa chama ni kazi ya makatibu wa wilaya na majimbo. Makatibu hawa ndio wawe na wajibu kuanzisha, kujenga na kuyasimamia matawi na misingi. Viongozi wa makao makuu na wabunge wawe wazinduzi tu wa haya matawi na misingi. Makatibu katika kujenga wahakikishe kila mwanachama anakuwa na japo kivuli cha katiba ya chama na wawafundishe falsafa na itikadi ya chama. Ofisi ya wilaya ndio ipange proglamu ya kuendesha mafunzo katika matawi.

Makatibu wa Jimbo na Wilaya watashindwa kufanya hayo kwa ufanisi kama wakiendelea kuwa watumishi wa kujitolea. Lazima vyama vya upinzani viwekeze kwa kuwalipa japo posho za kujikimu makatibu wa wilaya na jimbo. Waaondoe ile dhana ya kujitolea kwa lengo la kudai ‘UKOMBOZI", sasa hivi watanzania tunataka "MABADILIKO" na si "UKOMBOZI". Chama chenye nia ya kutaka kuleta mabadiliko lazima kiingie gharama kwa kuwaajiri watendaji wataalamu na watendaji wa kisiasa, chama kisipoingia gharama kwa watendaji hawa, kitapa hasara zifuatazo.

A/Mosi, makatibu ndio injini ya chama. Kitendo cha makatibu hawa kutolipwa mshahara au posho ya kujikimu kinapelekea watumie muda mwingi kuhemelea familia zao badala ya kufanya kazi za chama. Hizi ofisi wakati mwingine zinafanya kazi kipindi cha uchaguzi tu. Badala ya kumlaumu Kikwete kuwa ni fisadi ni bora viongozi hawa watafute namna ya kuwekeza kwa kuwalipa japo posho za kujikimu makatibu hawa.

B/Pili, makatibu wa kujitolea ni rahisi kurubuniwa hata wakihujumu chama. Wagombea bandia wa udiwani na ubunge ni matokeo ya kurubuniwa kwa viongozi wa jimbo na wilaya. Mgombea kujitoa kwenye uchaguzi ni kiashiria cha wagombea bandia ambao wapo ili kukikosesha chama husika mgombea. Pamoja na kwamba hata kiongozi mwenye mshahara huweza kurubuniwa, lakini ukweli uko wazi kuwa kiongozi asiye na mshahara ni rahisi sana kurubuniwa.

*Vyama hivi visiishie kuishambulia serikali tu, bali pia viwekeze katika kuimarisha vyama vyao, kuwekeza katika siasa ni pamoja na kuwalipa watendaji mishahara na posho.


TATU: HUU NI MUDA WA KUTENGENEZA KURA.
Kama nilivyosema uko juu kuwa makombora ya wapinzani dhidi ya CCM tija yake ni ndogo sana na ndio maana kila uchao kasi ya nguvu ya CCM inapungua kidogo sana, na kwa upunguaji huo ni vigumu kutabiri kuwa uchaguzi ujao chama cha upinzani kitashinda. Hivyo wapinzani wasiishie kutangaza ufisadi unaofanywa na CCM tu, bali ni lazima pia watengeneze kura halali za ushindi.

Watanzania wengi hawajui thamani ya kura, umuhimu wa kupiga kura, na umuhimu kulinda kura. Watu wanajiandikisha ili wapate kitambulisho na si kwa lengo la kupiga kura, ndio maana watu waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2010 walikuwa milioni 20, na waliojitokeza kupiga kura ni milioni 8. Zaidi ya asilimia 50 hawakujitokeza kupiga kura. Vyama vya upinzani vikome kuishambulia tu serikali, badala yake vifanye hivyo huku vikiwekeza ipasavyo katika kutoa elimu ya uraia kwa hawa watu asilimia 50 ili uchaguzi ujao wajitokeze na wawe silaha ya maangamizi dhidi ya CCM.

Wakati watendaji wa chama wakiwafundisha wanachama wao falsafa na itikadi za vyama vyao hata wawe wanachama wa "kumaanisha", pia watumie fursa hiyo kuwapatia na elimu ya uraia. Wasiishie kufundishwa mambo ya vyama vyao lakini pia wafundishwe umuhimu wa kujiandikisha kupiga kura, umuhimu wa kupiga kura, thamani ya kura na umuhimu wa kulinda kura. Hili likifanikiwa, hata mtu akipewa khanga au kofia hatohadaika, kinyume chake tutakuwa tunawalaumu wagawa bahasha, lakini wenyewe lawama zetu wamezipa sifa za kelele za mlango ambazo siku zote hazimzuii mwenye nyumba kuota njozi za mafuraha.

NNE: UBINAFSI WA VYAMA VYA UPINZANI NA UTITIRI WA VYAMA VYA SIASA.
Kwa ubinafsi wa vyama vya siasa na utitiri wa vyama vya siasa katu CCM haiwezi kutoka ikulu. Nadhani kuwa na vyama utitiri si jambo baya, jambo baya ni vyama hivi kushindwa kuonganisha nguvu zao na kusimamisha mgombea mmoja wa nafasi ya urais. Kila uchaguzi vyama hivi huwa vinagawana kura na kumuachia CCM kura nyingi. Kuelekea uchaguzi mkuu, vyama hivi visiishie kuishambulia serikali tu, bali pia vitafute namna ya kutupatia mgombea mmoja wa urais. Kinyume chake tutaendelea kupanda "upepo" na "tufani" litabaki kuwa vuno kwetu.


HITIMISHO:
Tunakosea sana kumlaumu Kikwete kwa madudu ayafanyayo Ikulu, ikiwa sisi kama umma tumehusika katika kufanikisha ndoto za Kikwete. Vyama vya upinzani vinaongozwa na ubinafsi, havina mpango wa kuongeza wanachama au havitekelezi mipango ilivyojiwekea ya kuongeza wanachama, vinaridhika na mashabiki wengi ambao wengi wao ni washabiki wa watu na si mashabiki wa chama na mbaya zaidi wananchi nao hawajui thamani ya kupiga kura.

Wizi wa kura, sheria mbovu za uchaguzi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola ni visingizio tu vya wanasiasa walionyimwa ridhaa ya kuongoza nchi, na katu havimfanyi Kikwete kupoteza uhalali wa kuvaa joho la urais. Kikwete bado ataendelea kuwa rais, na ni jukumu letu kushirikiana naye ili kuhakikisha anamaliza kipindi chake hichi kilichobaki kwa usalama. Kwa yanayoendelea kutokea sasa nchini, hususani machafuko na vurugu ni kiashiria tosha kuwa rais yetu anahitaji msaada.


Aghalabu mfalme juha hupatikana katika kaumu za majahili. Rais asiyewajibika na asiye na uadilifu ni zao la wapigakura waliokosa uadilifu na wasiojua wajibu wao wa kuwachagua kiongozi bora. Hivi ikiwa tumepanda "upepo" iweje tughairi kuvuna "tufani"? Hili ni letu wala si la jirani zetu, naam, tumerikoroga shuruti tulinywe. Pamoja na hayo, kuanza alifu kwa ujiti si ujinga, bali ni werevu wa kutoa kisiki kilichotukwaa jana.

Nahitimisha kwa kusema, "TUJENGE UMMA WENYE ADILI SASA"

Njano5.

0784845394.
 
Tutamkumbuka kwa kutuachia udini na umasikini kwa kuongezeka pengo kati ya walionacho na wasionacho,pia jitihada zake za kuwawezesha mafisadi kuwatengenezea Upenyo kiulaini kwa cover ya vyeo vyake fake,pia tutamkumbuka kwa kuanzisha clinic za supression na elimination za kuwang'oa vinara wa watetea haki meno na kucha bila hata ganzi(ligunicane)
Pia tutamkumbuka kwa staili yake ya kumtumia mwanae kujilimbikizia mali

Sent from my BlackBerry 9300 using JamiiForums
 
Tutamkumbuka kwa kutuachia udini na umasikini kwa kuongezeka pengo kati ya walionacho na wasionacho,pia jitihada zake za kuwawezesha mafisadi kuwatengenezea Upenyo kiulaini kwa cover ya vyeo vyake fake,pia tutamkumbuka kwa kuanzisha clinic za supression na elimination za kuwang'oa vinara wa watetea haki meno na kucha bila hata ganzi(ligunicane)
Pia tutamkumbuka kwa staili yake ya kumtumia mwanae kujilimbikizia mali

Sent from my BlackBerry 9300 using JamiiForums

uko sahihi kabisa.
 
Siasa za Tanzania zimejaa porojo nyingi na kwa ujumla zimedumaa na kukosa mwelekeo. Haihitaji elimu kubwa sana kutambua kuwa siasa imekuwa ndiyo kamba ya kuyanyonga mafanikio yetu. Hili liko katika maeneno mengi sana ambayo bila shaka mkuu Njano5 umejitahidi kuyaelezea kiunagaubaga.

Katika yote uiyoeleza umesahau kukumbusha matatizo mawili makubwa katika siasa zetu ambayo ni mosi; siasa kugeuzwa ujasiriamali na pili siasa kutekwa nyara na dola.

Kimsingi,tatizo la siasa kugeuzwa ujasiriamali limechukua nafasi kubwa sana iwe kwa chama tawala au vyama vya upinzani. Wakati wananchi wakiweka matumaini makubwa ktk kuifanya siasa kuwa dira ya maendeleo yao, wanasiasa wameifanya siasa eneo la machumio ya fedha na ulaji huku wakiwatimulia vumbi la njaa, mateso, jasho na damu wananchi mafukara. Ukitaka kulifahamu hili kwa kina chunguza miradi mikubwa na vitega uchumi vinavyofunguliwa nchini utayapata majina ya wanasiasa nyuma yake, fuatilia uharamia, ufisadi, uvunaji wa pembe za ndovu, biashara za madawa ya kulevya nk. majina ya wanasiasa wamo na wengine wamekuwa wakitajwa waziwazi bila hatua zozote kuchukuliwa.

Wapinzani katika hili japo mianya yao ya kula imezibwa baadhi yao wamegeuka wapiga dili kutoka kwa watawala na mashirika ya umma au hata wawekezaji wa kigeni. Wamekuwa ni wa kutishia nyau ili wavute mikwanja kutoka kwa watuhumiwa mbalimbali (na usisahau kutoka wahisani kutoka nje-rejea utitiri wa vyama vya siasa vya briefcase na events driven). Wamekuwa wakizibwa midomo kwa vipande vya fedha ili kufumbia uharamia dhidi ya rasilimali na stahiki za umma.Wanasiasa wachache wa upinzani ambao bado wana mioyo ya kupambana wameishia kujinyonga wenyewe mifukoni na kuteseka katika kuwafikia wapiga kura ingawa katika mazingira magumu na yaliyo katikati ya miiba ya mateso na wanasiasa wengi wanaochuma fedha kifisadi na kuwa matajiri. Hapa ndipo tatizo la pili huanzia.

Siasa kutekwa nyara na dola;Hili limeelezwa sana na wachambuzi huru wa siasa za Tanzania ingawa kwa kuangaza jinsi vyombo vya dola vinavyolalia waziwazi upande wa chama tawala. Lakini kuna upande wa pili mchungu zaidi,baadhi ya vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani ni sehemu ya mkono wa dola hiyohiyo inayokandamiza upinzani. It is a two way of destructing the opposition internally and externally. Ni wazi wanasiasa wachache wa upinzani wanao onesha kuwa na udhati katika mapinduzi wamejikuta katikati ya msitu uliojaa mateso na usaliti mkubwa.
 
Last edited by a moderator:
^^
Rais alikuwa sahihi ktk ahadi yake, kuna WATANZANIA na kuna WANANCHI,
Iwapo amewainua watanzania ni sawa,lakini kwa wananchi heri Mkapa alileta uwiano wa maisha
^^
 
Umenena vyema,lakini naomba ufahamu kuwa neno ukombozi kwa wanyonge wa nchi hii kupitia chadema linatokana na vitendo vya udhalimu na kikatili vya utawala uliopo mamlakani na kwa udhalimu huu wa chama cha mapinduzi lazima tuuite ukombozi wa pili kupitia chadema.

Pia naomba uelewe kuwa watanzania wengi ni waelewa zaidi kuliko unavyodhani!
Kinachosubiliwa ni kuboresha daftari la wapiga kura tu,hapo ndipo wewe na c.c.yem mtakapojua kuwa hakuna mwana zitto,mwana mbowe ,mwana slaa.
Bali kuna wanachadema tu na watamchagu raisi wao mpedwa wamtakae naye ni dk.slaa.

Na pia udhaifu wa jei kei lazima usemwe bila woga kwani mahali ambapo amelifikisha taifa hilini pabaya na panatisha.


"chadema ni mpango wa mungu"
 
Safi sana kinyume na matarajio yangu; sasa sijui baada ya utitiri wa vyama vya siasa utajiunga na ADC?

Hoja

1. Mhula wa pili JK hakushinda kutokana na kura za wananchi. Kwa takwimu sahihi alishinda kwa 10% Kwa hiyo sishangai anachokifanya Ikulu.

2. Aliyemchulia fomu yake ya kugombea urais na kuitembeza nchi nzima ni mwanae Rizwan Kikwete; haimkini anatekeleza ilani ya familia badala ya ilani ya CCM. Na ilani hiyo ni kujinufaisha yeye, familia yake na marafiki zake.

3, Nakubaliana na wewe hastahiri kulaumiwa kwa sababu hata hiyo 10% ya kura za halali walipiga kura wakiwa wanaelewa au hawaelewi kuwa tatizo si JK bali ni mfumo wetu mbovu wa Kidikteta. Na zile kura 51% ni maafa na majanga yanaonyesha udhaifu wa mfumo mzima kwa kukataza kuhoji kura za wizi.

4. Upinzani wanalaumika na wanastahili kupongezwa maana wanacheza uwanja unaonyumbulika na magoli yanayonyumbulika na kusogezwa na "wenye dola"

Ni kweli uliyoyaona kuhusu ushabiki wa watu badala ya chama; na ni kweli jitihada zinazofanywa na baadhi ya wapinzani hususan CHADEMA hazijapimwa kwa kipimo sahihi bali kwa matokeo ya kishabiki. Hapa kwenye vipimo (vya tathmini) kwangu mimi ndipo pananipa shida kwa sababu

i. Hakuna utamaduni wa kujipima katika hatua 5, tunajipima kwa ushabiki

2. Serikali haijawahi kujipima kwa lo lote kiuhalisia bali kwa sifa zisizopimika kama mabarabara ya fadhili na mikopo ambayo mipango yake ni shinikizo toka nje

3. Tathmini ni taaluma ina vigezo vya kitaalamu, mimi na wewe ni shahidi kuwa elimu yetu toka chini kabisa hadi juu kabisa haitoi wasomi bora bali bora wasomi wasiokidhi mahitaji ya elimu yao kwa jamii.

4. Siasa zinazoendeshwa kwa sasa ni za mdomoni, ni nzuri kwa sababu tunajifunza kwa tabu, matatizo na kwa kushuhudia; elimu hii ya tabu na matatizo na ushuhuda ina tabia ya kudumu.

Nashukuru kwa uchambuzi wako ila na wewe hujatoa mkakati wako wa kuwafikia walengwa wale kwenye msingi
 
Siasa za Tanzania zimejaa porojo nyingi na kwa ujumla zimedumaa na kukosa mwelekeo. Haihitaji elimu kubwa sana kutambua kuwa siasa imekuwa ndiyo kamba ya kuyanyonga mafanikio yetu. Hili liko katika maeneno mengi sana ambayo bila shaka mkuu Njano5 umejitahidi kuyaelezea kiunagaubaga.

Katika yote uiyoeleza umesahau kukumbusha matatizo mawili makubwa katika siasa zetu ambayo ni mosi; siasa kugeuzwa ujasiriamali na pili siasa kutekwa nyara na dola.

Kimsingi,tatizo la siasa kugeuzwa ujasiriamali limechukua nafasi kubwa sana iwe kwa chama tawala au vyama vya upinzani. Wakati wananchi wakiweka matumaini makubwa ktk kuifanya siasa kuwa dira ya maendeleo yao, wanasiasa wameifanya siasa eneo la machumio ya fedha na ulaji huku wakiwatimulia vumbi la njaa, mateso, jasho na damu wananchi mafukara. Ukitaka kulifahamu hili kwa kina chunguza miradi mikubwa na vitega uchumi vinavyofunguliwa nchini utayapata majina ya wanasiasa nyuma yake, fuatilia uharamia, ufisadi, uvunaji wa pembe za ndovu, biashara za madawa ya kulevya nk. majina ya wanasiasa wamo na wengine wamekuwa wakitajwa waziwazi bila hatua zozote kuchukuliwa.

Wapinzani katika hili japo mianya yao ya kula imezibwa baadhi yao wamegeuka wapiga dili kutoka kwa watawala na mashirika ya umma au hata wawekezaji wa kigeni. Wamekuwa ni wa kutishia nyau ili wavute mikwanja kutoka kwa watuhumiwa mbalimbali (na usisahau kutoka wahisani kutoka nje-rejea utitiri wa vyama vya siasa vya briefcase na events driven). Wamekuwa wakizibwa midomo kwa vipande vya fedha ili kufumbia uharamia dhidi ya rasilimali na stahiki za umma.Wanasiasa wachache wa upinzani ambao bado wana mioyo ya kupambana wameishia kujinyonga wenyewe mifukoni na kuteseka katika kuwafikia wapiga kura ingawa katika mazingira magumu na yaliyo katikati ya miiba ya mateso na wanasiasa wengi wanaochuma fedha kifisadi na kuwa matajiri. Hapa ndipo tatizo la pili huanzia.

Siasa kutekwa nyara na dola;Hili limeelezwa sana na wachambuzi huru wa siasa za Tanzania ingawa kwa kuangaza jinsi vyombo vya dola vinavyolalia waziwazi upande wa chama tawala. Lakini kuna upande wa pili mchungu zaidi,baadhi ya vyama vya siasa na wanasiasa wa upinzani ni sehemu ya mkono wa dola hiyohiyo inayokandamiza upinzani. It is a two way of destructing the opposition internally and externally. Ni wazi wanasiasa wachache wa upinzani wanao onesha kuwa na udhati katika mapinduzi wamejikuta katikati ya msitu uliojaa mateso na usaliti mkubwa.

mkuu uko sahihi kabisa,,, vyombo vya dola kujiingiza kwenye siasa si kosa, bali vyombo vya dola kujiingiza kwenye ushabiki au uanachama wa chini ya pazia kwa vyama vya siasa ndio kosa lenyewe. Nafikiri na kwa vyovyote vile bulikusudia tabia ya vyombo vya dola kushabikia vyama vya siasa. Hii ni hatari, na kiukweli TISS na jeshi la polisi ni vibaraka wa CCM.

Pamoja na hayo,,ukweli unabaki pale pale, nguvu ya umma haiwezi kushindwa na polis au TISS,,,.mfano Misri na Tunisia...tukifanikiwa kuvijenga vyama vyetu na tukienda na hoja zenye kuwagusa wananchi moja kwa moja,,2015 CCM inashindwa asubuhi na mapema.
 
Back
Top Bottom