Sikuona ajabu kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuwa kwenye orodha ya majeshi yenye ufanisi mkubwa duniani. Sikuona ajabu kwa sababu Jeshi letu ndiyo pekee katika Afrika kusini mwa jangwa la Sahara lililojitoa, wakitumia silaha duni lakini kwa moyo mkubwa na uzalendo usioelezeka, kupigania ukombozi wa mwafrika aliyedhalilishwa kwa kutawaliwa na wengine kuuzwa kama kanzu na binadamu wenzake. Kwa kifupi JWTZ ni jeshi la ukombozi. Hiyo ni sifa ambayo ipo, bila kujali kama mtu yeyote anaikubali ama anaipuuza, ipo tu!
Nalipongeza Jeshi la Wananchi, naipongeza serikali ya Rais Kikwete kwa mafanikio haya. Rais Kikwete katika uongozi wake amefanya operesheni mbili kubwa ambazo zote zilikuwa na mafanikio. Mafanikio hayo ni ya Rais Kikwete kama Amiri Jeshi Mkuu kwa niaba ya watanzania wote na kwa niaba ya binadamu wote wapenda amani na heshima ya utu. Operseheni ya kwanza ni ile ya mwaka 2008 kumuondoa dikteta Kanali Mohamed Bacar aliyengangania madaraka katika kisiwa cha Anjuan nchini Komoro. Sote pengine tunajua kwamba ndani ya muda mfupi baada ya kuwasili kwa wanajeshi wa Tanzania waliongoza mapambano yale wakishirikiana na Sudan, Kanali Bacar aliikimbia Anjuan ikisemekana alitoroka akivaa baibui. Operesheni ya pili ni ya mwaka 2013 kuwaondoa waasi wa M23 nchini Kongo. Kitendo cha Rais kuamua kukomesha udhalilishaji wa kina mama wa Kongo na mauaji ya watu wasio ni hatia uliofanywa na kikundi cha M23 kilikuwa ni cha kijasiri sana.
Ni matumaini yangu kwamba uongozi wa awamu ya tano utayaendeleza mafanikio hayo kwa kwenda hatua zaidi; kuwekeza katika utafiti. Jeshi linalototegemea mbinu na zana zilizogunduliwa na wengine haliwezi kuwa na uhakika muda wote kumshinda adui. Ingawa sisemi tusiwategemee wengine lakini ni muhimu kuliwezesha jeshi kujitegemea kwa fikra na zana kwa njia ya kufanya utafiti, kubuni na kutengeneza zana zake yenyewe. Nchi zenye nguvu kama Marekeni zimefika hapo kwa sababu ya utafiti. Sasa wamewekeza dola bilioni 100 katika ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Anga kilomita 3500 kutoka duniani kwa ajili ya utafiti wa anga. Hatuwezi kuwa kama wenzetu lakini tutaweza kumuda kuyatawala mazingira yetu vizuri kama tutawekeza katika utafiti.
Nimalizie kwa kusema; tumepata sifa nzuri, lakini tusijaze upepo vichwani tukadhani sisi ni viranja wa kugonga kwenzi kila anayeonekana kuwa na mawazo tofauti na sisi, hapana! Tuendelee katika misingi ile ile ya kupigana inapobidi kulinda heshima ya utu wa mwanadamu, umoja, uhuru na amani. Na tunapolijenga jeshi letu, tulijenge katika lengo hilo. Hongera JWTZ.