Donatila
JF-Expert Member
- Oct 23, 2014
- 7,563
- 21,665
Tanzania inatarajia kuanza kuzalisha umeme wa jotoardhi zaidi ya megawati 20 ifikapo mwaka 2018 mradi utakaopunguza gharama za nishati hiyo nchini.
Kiwango cha nishati hiyo kitakachozalishwa kutoka miradi minne inayoendelea kufanyiwa kazi kwa sasa, kinatarajiwa kuongezeka mpaka megawati 200 ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Jotoardhi nchini (TGDC), Mhandisi Boniface Njombe aliwaeleza wajumbe wa mkutano wa wataalamu wa jotoardhi jana kuwa, mbali na mpango huo wa muda mfupi, wamejiwekea malengo ya kuzalisha zaidi ya megawati 200 ndani ya miaka tisa ijayo.
“Hii ni nishati salama na rafiki wa mazingira,” alieleza bosi huyo wa TGDC ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco).
Mpaka sasa miradi inayoendelea kufanyiwa kazi ikiwa kwenye hatua mbalimbali ni Ngozi na Mbaka iliyopo mkoani Mbeya, Kisaki wa Morogoro, Mlima Meru na Ziwa Natron kwenye Mlima Lengai.
Alisema, TGDC inashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira (UNEP) kufanya mapitio ya jotoardhi, kuendeleza na kuchakata nishati hiyo kabla haijaanza kutumika.
Akifungua mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo alisema Tanzania ina hazina ya takriban megawati 5,000 ya nguvu za kuzalisha nishati hiyo na kwamba ipo karibuni kuanza kuitumia.
Alisema mpango wa Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na utafikiwa endapo kutakuwa na nishati ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani na viwandani.