Malalamiko Muungano
Alisema kila upande wa Muungano una malalamiko mengi kuhusu muundo na kwamba tume hiyo imeorodhesha malalamiko 10 kwa upande wa Zanzibar na manane kwa upande wa Tanzania Bara.
Alisema kwa upande wa Zanzibar, malalamiko matatu makubwa ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano ambalo linaisaidia zaidi Tanganyika kuliko Zanzibar na kuifanya Tanganyika kuwa Tanzania.
Pili, mambo ya Muungano kuongezeka na kuathiri madaraka na kuishusha hadhi Zanzibar na tatu ni kumuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema kwa Tanzania Bara, malalamiko makubwa ni Zanzibar kuwa nchi huru yenye bendera yake, wimbo wa taifa, serikali yake na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake. Katiba ya Jamhuri inasema Tanzania ni nchi moja lakini Katiba ya Zanzibar inasema ni nchi mbili.
Pili, Zanzibar imebadili Katiba yake na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano, kuelekeza sheria za Muungano zinazopitishwa na Bunge la Muungano zipelekwe kwanza kwenye Baraza la Wawakilishi kabla ya kutumika.
Tatu, wananchi wa Tanzania bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar, wakati wenzao wana haki hiyo Tanzania bara.
Muundo wa Muungano
Alisema katika kuchambua malalamiko ya Zanzibar, Tume imebaini kuwa muundo wa Muungano wa Serikali mbili umeifanya Serikali ya Muungano kushughulikia zaidi mambo ya Tanzania bara, hasa maendeleo na uchumi.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977, Serikali ya Muungano ina mamlaka ya kusimamia mambo ya Muungano na yasiyo na muungano kwa upande wa bara... "Kwa msingi huo, Serikali ya Muungano inashughulikia sana kilimo, elimu, afya, maji, nishati na madini, ujenzi, uchukuzi, maliasili na utalii na mengine ya Tanzania bara yasiyo ya Muungano."
Alisema kutokana na hali hiyo, Tume haikuwa na njia nyingine kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka ya kutosha juu ya mambo ya maendeleo na uchumi kwa upande wa Zanzibar na kwamba hata utafutaji wa rasilimali zaidi ni kwa ajili ya Tanzania bara kuliko Zanzibar.
Alisema Zanzibar inafanya mipango yake ya maendeleo, kwamba ili ipate rasilimali, kama mikopo na misaada, ni lazima ipitie Serikali ya Muungano jambo ambalo utekelezaji wake umesababisha matatizo mengi.
"Njia pekee ambayo ingeiwezesha Zanzibar kufaidi shughuli za Serikali ya Muungano wa maendeleo ya Zanzibar ni mambo yote kuwa chini ya Muungano kwa maana ya kuwa na Serikali moja, lakini hilo likifanyika kuna hofu ya Zanzibar kumezwa," alisema.
Alisema tume hiyo imefanya uchambuzi wa mambo 22 ya Muungano ili kubaini kama yanaingilia hadhi ya uhuru wa Zanzibar na kubaini kuwa siyo yote yanayotekelezeka. Mengi yamebadilishwa bila kubadili Katiba au kwa makubaliano ya pande mbili.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kodi, bandari, viwanda, usafiri na usafirishaji wa anga, utafiti, posta na simu, uraia, takwimu, mafuta na gesi na Mahakama ya Rufaa.
"Kama Katiba ya Zanzibar ikibaki kutakuwa na nchi mbili; zikiwa nchi mbili haitawezekana nchi moja iwe na hadhi na uhuru na nchi nyingine isiwe na hadhi na uhuru, kwa tathmini yetu, tunaona ukarabati huu ni mgumu. Serikali tatu ndiyo suluhisho," alisema.