Tamthiliya

Tamthiliya

Mstahiki Mea

JF-Expert Member
Joined
Jul 13, 2018
Posts
6,027
Reaction score
11,045
Onyesho la Kwanza
CHRISTINA MSALABANI



Na, E. Mashele (2019)

Nyumbani

( Nyumbani kwa kina Christina, nje kidogo mwa nyumba yao katika shamba lao dogo, wanaonekana wanawake wawili wakilima na majembe kwa kutifua ardhi kavu yenye udongo mweusi. Mwanga ni angavu kila kitu kinaonekana, kwa mbali wanaonekana mijusi wawili wakikimbizana kutokea nyuma ya wanawake hawa. Mara wanageuka na kuanza kuwaangalia kila mmoja kwa wakati wake lakini mama Christina haangalii sana. Jukwaa halitakiwi kupambwa sana).

Mama Christina :
( Anapiga jembe moja chini, linadunda kwa ugumu wa ardhi. Anapaka mikono yake mate kisha anaifikicha. Anasafisha koo na kutema kohozi lenye vumbivumbi, kuku waliokuwa jirani wanalidonoa. Anawapiga kwa udongo wanakimbia). Mwanangu Christina, familia yetu hatujajaliwa utajiri, utajiri wetu ni hiki kishamba na hako kajumba alikojenga baba yako hatuna kitu kingine. (Anatema mate angani mara tatu kisha anaendelea) Hivyo, mwanangu soma kwa bidii ili uje ututoe katika umaskini huu, mimi na wadogo zako.


Christina : ( Anapiga jembe chini lakini halifiki udongoni, anafikicha macho kutokana na vumbi kiasi lililotua kwenye kope zake, anatoa vumbi kiasi machoni) Ndiyo mama najua Mungu atanisaidia ili nifaulu mitihani niliyokwisha kufanya, natumaini nitafaulu vizuri na kuendelea na kidato cha tano na sita hadi chuo kikuu, najua tutafaidi mama.


Mama Christina: ( Kwa sauti ya kichovu na mkwaruzo kiasi kutokana na vumbi) Mwanangu usisahau pia kumuomba Mungu kwa kila ukifanyacho. Unajua mwanangu watu wanakuonea wivu sana sijui ukifanikiwa kuwa daktari watasemaje! Lakini pia mwanangu usisahau ile kinga tuliyoleta toka kwa Babu. Hakikisha unakuwa nayo muda wote.


Christina : (Jua bado kali sana, kachoka sana safari hii, kakaa chini udongoni) Mama nimekusikia yote uliyoniambia, tumuombe Mungu tu tutafanikiwa.
( Wote hawalimi tena, adhana inasikika kwa mbali, jua linazidi kusogea chini mara anaingia jirani kutokea nyuma yao upande wa kushoto wa jukwaa. Anaonekana amebeba jambo zito maana anapiga hatua ndefundefu na mdomo ukimchezacheza) .


Jirani : ( Kwa sauti kali ) Jamani wenyewe…


Mama Christina: ( Kwa hamaki) Karibu! Karibu jirani karibu ( mahali ni palepale ni kama jukwaa halipaswi kubadilishwa vitambaa vya mwanzo) Mwenzangu ni jambo la kheri kweli maana sio kwa haraka hizo.

Jirani : ( Huku akikaa katika jiwe karibu na Christina) Sio kheri jirani yangu mumeo huyu Pembe kashindikana kawa kama pwaguzi kakutwa katika banda la kuku wa mzee Faru na wamempeleka kwa Mwenyekiti muda huuhuu.


Mama Christina : ( Muda huo amesimama anakaza vizuri kilemba chake kichwani, anasonya kwanguvu) Huyu mwanaume sasa afe tu, heri shari kamili kuliko nusu shari, amemaliza kuiba vimiambili vyangu sasa amehamia kwa majirani acha wamtoe roho.


Jirani: ( Huku akisimama na yeye, jua linafifia kiasi, katika jukwaa taa kadhaa zinaweza kuzimwa lakini sio zote) Mimi ni hayo tu, ngoja niwahi hapa kwa Mwenyekiti au tunaweza kuambatana pamoja tukasikilize.
( Wote wanaondoka katika eneo lile, mama Christina anaambatana na Jirani, Christina anasogea nyumbani. Kabla hawajafika mbali mama Christina na Jirani wanaonekana wamesimama).


Jirani : (Kwa msisitizo huku akimwangalia mama Christina) Sasa huyu mumeo bwana Pembe amezidi, nasikia wanangu wanasema juzi kuwa wamemuona na mfuko wa maharagwe anapeleka pale kwa Cheupe kule kilabuni.


Mama Christina : ( Kwa hasira lakini anaongea kwa upole) Sasa nitafanyaje ndugu yangu mwanaume keshakuwa hivi!
Jirani: Vumilia, vumilia mama Christina.


Mama Christina : Jirani wahenga walisema mvumilivu hula mbivu lakini sioni hizo mbivu mpaka sasa, mateso, mateso tu kila kukicha.


Jirani : ( Anaguna) Mmh!
Mama Christina: (Kimya).
( Wote wanaendelea na safari hadi kwa Mwenyekiti, wanakuta watu wamekusanyika, wengi ni akina mama; wanaumekadhaa waliokuwepo ni walevi hata Mwenyekiti naye amelewa kiasi).


Mwenyekiti: ( Huku akiingiza kidole katika matundu ya pua yake na kufikicha... Sauti ya redio inasikika kutoka nyumba ya Mwenyekiti lakini kwa mbali, watu wote wamekaa kimya kumsikiliza kuhusu hukumu ya bwana Pembe )

Mimi ndiye Pilato (anacheka, vicheko vinazidi na kila mtu anacheka).
( Mara redio inaongezwa sauti ghafla inakuwa ni kelele, mara taarifa inasikika) Aliyekuwa mbunge wa jimbo lenu amejiuzulu na kujiunga na chama kingine ili kuleta maendeleo…(watu wanatega masikio kisha minong’ono inasikika taa zinafifia kila mmoja anaondoka katika jukwaa, taa zizimwe kwa pamoja.

( Nyumbani kwa kina Christina, taa chache zinawaka katika jukwaa na taa ya kurunzi ipo juu ya mkebe wa unga nyakati za usiku. Kuni zimekolea, moto mkali unawakana maji yapo karibu kuchemka. Panya kadhaa wanakimbizana huku na huko mara darini mara wapande na miimo ya mlango. Kelele za vyura zinasikika kwa mbali na kelele za mtoto anayelia zitapamba onyesho.Wanaonekana watu wawili wamekaa huku wanatazamana, mwanamke na binti yake).

Christina : ( Huku akimeza funda la mate) Mama japo kuchaguliwa kuendelea na masomo ninapata wasiwasi mkubwa sana.

Mama Christina : ( Akivuta muda kidogo na kichwani anaonekana kama amebaki mzigo mzito wa mawazo ) Wasiwasi wa nini mwanangu?


Christina : ( Kwa huruma na sauti ya upole) Ada mama!

Mama Christina : Mwanangu kama unavyojua hali yenyewe ndio hii: kula kwetu shida, kulala kwetu shida, kila kitu shida mwanangu ( anaongeza ) isitoshe huyu baba yako ni kama amefariki tu! Yeye kila kitu kwake sawa, yeye na pombe kama chura na maji pooo!! ( anatema mate mazito chini yanaanguka kwenye mguu wa Christina, Christina anahisi joto la mate ya mama yake kwenye mguu wake lakini hakuna anayejali).

Christina : ( Machozi yakimlengalenga kama mtu anayekata kitunguu) Sasa mama itakuwaje? Wewe ndio tegemeo langu.

Mama Christina: ( Huku akimeza funda la mate) Usijali mwanangu kila kitu kitaenda sawa nitakopa hata kwenye kikundi chetu, lazima usome mwanangu.


Christina : (Kwa moyo uliojaa matumaini na tabasamu hafifu) Nitafurahi sana mama endapo tutafanikiwa katika hili ( mama naye anatabasamu ingawa bado anahisi uchungu moyoni. Sufuria ya ugali nayo imbioni kuchemka, shetani anawapitia wanaendelea kupika maongezi yanawapaa, kelele za vyura zinazidi nje siku inapita).


Hadhira wanasikika wakiimba wimbo
_Wimbo
Mama ni jasiri, wema umekirihi
Wana hawasitiri, maisha wakafurahi
Usiku mchana wanafikiri namna ya kuwastahi
Ujasiri jasiri asilani
Maneno yako ya bwana bila hata mshahara
Wana wawaondolea papara, ukawafungulia baraka
Wana wakawa na stara, wakaondokana na uchwara
Ujasiri jasiri asilani
Nyumba waitunza, usiku na mchana
Mawazo yakakatiza, kala wana na bwana
Maneno yakuumiza ya wako mtwana
Ujasiri jasiri asilani
(Taa zinafifia polepole)
*******************************************************_
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom