TAFAKURI: Ni "Diaspora" Gani Serikali ya Magufuli Inawataka na Kuwapenda?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,476
39,995
upload_2017-8-15_13-30-6.jpeg
Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya hoja ninazozisikia mara nyingi tangu Rais Magufuli achaguliwe kuwa Rais mwaka 2015 ni kuwa hapendi Watanzania walio nchi za nje na kuwa ana uhasama wa wazi na Watanzania wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje. Kwamba, yeye au watu wake wa karibu wanaona kuwa Watanzania hawa wanataka “kote kote”; kwamba wanataka kuishi na kufanikiwa nchi za nje na wakati huo huo wanataka wachukuliwe kama Watanzania wengine wakiwa na haki zote.

Mara kwa mara viongozi wa Serikali (kuanzia Rais hadi wabunge) wanapoenda nje ya nchi hufanya jitihada ya kukutana na “Watanzania” wanaoishi nchi hizo. Huu si utaratibu mgeni na umekuwepo kwa muda mrefu. Mara kwa mara tunaona picha za viongozi hao wakikutana na kuzungumza na Watanzania hao na kusikiliza maswali yao mbalimbali na kujibu hoja zao mbalimbali. Kundi hili la Watanzania wanaoishi nchi za nje wanaitwa kama “diaspora”.

Neno hili “diaspora” lina asili ya neno la Kigiriki la “diaspeirein” lenye maana ya “kutawanya, kusambaza”. Neno hili kwa maana yake ya kwanza kabisa lilikuwa linatumiwa kuelezea Wayahudi waliotawanyika nje ya Israeli kufuatia uhamisho wa Babeli. Miaka ya karibuni hivi neno hili limekuwa likitumiwa kuelezea watu wote au jamii ya watu ambao wametawanyika sehemu mbalimbali nje ya nchi zao za asili. Hivyo, watu weusi waliotawanyika nje ya Bara la Afrika wanaweza kuitwa “diaspora” na Wahindi waliotawanyika nje ya India wanaweza kuelezewa hivyo hivyo.

Hata hivyo, neno hili lilipotumiwa kwa Wahayudi lilikuwa hasa linamaanisha watu waliopelekwa uhamishoni, waliolazimishwa kutoka katika nchi yao na kutawanyika duniani. Wayahudi hawa hawakuondoka Palestina ya kale kwa hiari yao bali waliondoka kwa kulazimishwa wakati mababu zao walipochukuliwa utumwa Babeli. Kwa Waafrika mfano sahihi wa watu walio kwenye dayaspora ni wale wote waliochukuliwa utumwa na uzao wao. Kwa muda mrefu wale wahamiaji wengine ambao wanaenda nje kwa hiari na kuamua kuishi huko kwa hiari walikuwa wanajulikana kama ‘wahamiaji” au “wahamiaji wa kigeni” (alien immigrants). Wahamiaji hawa wengi bado wana mawasiliano na mahusiano na nchi zao za asili.

Hata hivyo, sasa hivi neno hili ‘diaspora’ linajumuisha makundi yote mawili; yale yanayotokana na masalia ya utumwa (kama Wamarekani Weusi) na wale wahamiaji weusi. Hata hivyo, katika kundi hili la pili tunaweza kuligawa katika makundi mengine mawili – kundi la wahamiaji ambao bado wana uraia wa Tanzania na wahamiaji ambao wamechukua Uraia wa nchi hizo nyingine na hivyo hawana uraia wa Tanzania tena.

Hapa ndipo msingi wa swali langu upo; je serikali yetu inataka kuhusiana na ‘diaspora’ wapi hasa? Je, ni wale ambao wako katika nchi za kigeni lakini bado wana uraia wa Tanzania tu au inajumuisha na wale ambao wana asili ya Tanzania lakini wameshachukua uraia wa kigeni?

Jibu la swali hili ni rahisi; kwa kuangalia serikali inavyoshughulika na makundi haya mawili ni wazi kuwa Serikali haina sera, utaratibu au mfumo wowote unaowatambua kwa namna, njia, mpango, utaratibu au mwelekeo wowote wa kufuatilia mambo yanayowahusu Watanzania walioacha uraia wa Tanzania na kuwa raia wa nchi nyingine.

Mwaka jana Waziri wa Ardhi William Lukuvi (pichani) akitekeleza maamuzi na msimako wa Serikali ya Rais Magufuli alitangaza umma kuwa Watanzania diaspora (walio na uraia wa nchi nyingine) hawastahili kumiliki ardhi Tanzania hata kama ardhi hizo walizipata wakiwa Watanzania (kabla ya kuchukua uraia wa nchi nyingine). Lukuvi alinukuliwa kusema “Mtu akishaukana uraia wa Tanzania hana haki tena kama raia wa Tanzania, hivyo atamiliki ardhi kama mwekezaji na siyo raia, ardhi itabaki kuwa ya Watanzania tu, tutawasaka wale wote ambao wanamiliki ardhi kinyume na sheria za nchi”.

Kuna Kongamano linapangwa kufanyika huko Zanzibar ambalo linawahusu “Diaspora” (Watanzania wanaoishi nje ya nchi) Augusti 23, 24. Ni wazi kuwa wanaowataka siyo watu wenye asili ya Tanzania ambao wanaishi nje ya nchi, bali wale Watanzania (wenye uraia wa Tanzania bado). Kama hili ni kweli, ni muhimu sana kwa Serikali kuwa muwazi – waseme wanaowataka ni WALE WENYE URAIA WA TANZANIA TU. Kwa sababu kwa wale wengine ambao wana asili ya Tanzania, hata kama wana familia, ndugu, jamaa huko lakini wana uraia wa nje, hawa SIYO WENZETU ( kwa msimamo wa serikali).

Lakini pia watu wenye asili ya Tanzania ambao wana uraia wa nchi nyingine, hata kama wanamapenzi kiasi gani na Tanzania ni wakati na wao waanze kufikiria maslahi yao zaidi na ya watoto wao. Kwanini watu hawa wanajitahidi kusaidia nchi ambayo “siyo yao” na wanajitahidi kupeleka misaada huko wakati serikali ina uhasama nao? Sina tatizo mtu akiamua kumtumia hela kidogo ndugu yake au ndugu zake kuwasaidia maana hiyo ni damu yake, lakini kwanini mtu ahangaike na mambo mengine wakati angeweza kufanya mambo hayo Uganda, Congo, Kenya au Uganda au nchi nyingine yeyote? Kwanini mtu mwenye asili ya Tanzania atake kuwekeza Tanzania wakati angeweza kuwekeza nchi nyingine ambapo angeweza kupata faida zaidi na labda biashara yake ingekuwa na usalama zaidi?

Jambo hili limeanza kuwa na matokeo; nimeshakutana na baadhi ya ndugu zetu wenye asili ya Tanzania ambao wameanza kuachana na mawazo ya kuwekeza nyumbani na badala yake wanafikiria kuwekeza na kujiwekeza zaidi katika nchi zao hizi mpya. Hili si jambo geni kwani jamii nyingine za kigeni (kama hapa Marekani) zimejijenga katika nchi hii na kuzidi kufanikiwa.

Lakini jambo hili linaendana pia na mfumo wa serikali ambapo imejenga utaratibu wa kumvua mtu uraia wa nchi yake hata kama mtu huyo hajaukana uraia huo kwa hiari yake. Lukuvi alisema “mtu akishaukana uraia”; ukweli ni kuwa wengi wa ndugu zetu hawa hawajaukana uraia wao; wamenyang’anywa uraia huo kibabe. Mtu anapoukana uraia anaukana kwa sababu fulani na anaulizwa kuwa anaukana uraia huo; mfumo wetu umetengeneza utaratibu tu kuwa mtu anaukana uraia kwa sababu tu amechukua uraia wa nchi nyingine. Marekani kwa mfano, haijali kabisa mtu anauchukua uraia wa nchi gani, kwa kadiri ya kwamba hajasimama mahakamani kuukana uraia wa Marekani basi Marekani inautambua uraia wake kwanza. Kama mtu hajaamua kuukana uraia wa Tanzania kwanini Tanzania imnyang’anye uraia wake hasa kama bado ana mapenzi na utii kwa Tanzania?

Nitalizungumzia hili wakati mwingine lakini itoshe kusema tu kuwa Serikali inahitaji kukaa chini na kuja na sera yenye mantiki inayohusiana na watoto wa Watanzania waliotawanyika pote duniani. Ni maslahi na ni jema zaidi kuendelea kuwa na ushirikiano rasmi na watoto hao hata kama wamechukua uraia wa nchi nyingine. Hii haina maana mtu hawezi kuukana uraia wa Tanzania. Lakini tuweke utaratibu ambapo unampa mtu haki hiyo bila kumlamisha mwingine kupoteza uraia wa Tanzania. Uraia wa Tanzania usifutwe au kuondolewa isipokuwa kwa mtu kwa hiari yake kukana mahakamani. Usiondolewe kwa ndoa au kwa mtu kuchukua uraia wa nchi nyingine. Tuutukuze uraia wetu na kuufanya uwe vigumu kuufuta.

Lakini kama serikali imeamua kuendelea na mfumo huu kandamizi na kama bado imeamua kuona kuwa Watanzania walio na uraia wa nchi nyingine si “Watanzania tena” basi kuanzia sasa serikali inapopanga masuala ya kuzungumza na “diaspora” iweke wazi na bayana kuwa inataka kukutana na WALE TU ambao hawana uraia wa nchi nyingine. Viongozi wanapokuja nje na wanataka kukutana na watu wenye asili ya Tanzania waseme mapema kuwa wanataka kukutana na watu wenye uraia wa Tanzania na wahakikishe kuwa wanaokuja wanaangalia paspoti zao ili wageni (hata kama wana asili ya Tanzania) wasiingie kwenye mikutano hiyo. Kama hawawezi kumiliki ardhi kwa sababu ni wageni, mawazo yao ya nini?

Lakini pia nina wito wa uchokozi; jumuiya za Watanzania zilizoko nje ya nchi japo wenyewe kwa wenyewe hatuulizani nani ni “raia na nani si raia” wakati umefika na sisi tulio katika diaspora kuwa na msimamo wa pamoja; viongozi wanapokuja na kutaka kukutana nasi tuwaulize kama wanataka kukutana na wale wenye uraia wa Tanzania tu au hata wasio na uraia huo hata kama ni wenye asili ya Tanzania? Wakisema “wenye uraia tu” TUSIKUBALI KUKUTANA NAO. Tukikubali tutakuwa tumekubali wao watutenganishe!

Diaspora ni watu wamoja, ni wakati sasa wa kuonesha umoja na nguvu yetu kama wamoja hadi pale Serikali itapokuja na sera yenye mantiki ambayo itaheshimu utu wetu kama Watanzania na watu wenye asili ya Tanzania. India kwa mfano, inautaratibu wa “Raia wa India walio Ng’ambo” yaani Oversea Citizens of India (OCI). Huu ni utaratibu wao walioubuni kwani India kama Tanzania hairuhusu Uraia wa nchi mbili.

Lakini je sisi kama taifa tumeshindwa kubuni kitu chetu wenyewe na kuhakikisha kuwa jamii yetu walioko nyumbani, waliko kwenye jirani za Kiafrika na walio katika nchi za mbali nao wanaheshimiwa na kuthaminiwa kama raia wengine wa Tanzania?

Au tuulize tena ni ‘diaspora’ gani ambao Serikali inawataka na kuwajali na iko tayari kufanya nao kazi kwa manufaa ya Tanzania? Binafsi ni muumini wa Uraia wa Tanzania Kwanza. Ni muumini wa dhana ya uraia ya Mwalimu Nyerere ambayo uraia msingi wake ni utii kwa nchi yetu. Kama mtu hajaondoa utii na mapenzi kwa Tanzania hakuna sababu ya msingi ya kumnyang’anya uraia wake kama vile tulimpa kama zawadi wakati alizaliwa nao!
(ZAMAMPYA.COM)
 
Wanavua citizenship tu lakini nationality iko palepale, nationality haivuliwi na mtu wala serikali, the place of birth na waliokuza ndo inauunguruma zaidi.

Wekeza kwenu hata kama serikali haikutambui, kutokukutambua hakuna maana wewe siyo mtanzania ni mambo ya wakati tu. Atakuja mwelewa zaidi wa mambo haya na atayerekebisha vyema na tena ni hiki kizazi cha hawa wahenga tu kitapita ndani ya miaka 10.

Nunua ardhi kwa jina la mama yako dada yako unless wewe siyo mtanzania kwelikweli.

Diasapora wengi ambao hawana uraia wa nchi husika wengi wao 99% hawana hela. Utaipataje hela ugenini bila kuwa na uraia wa nchi husika, labda muuza madawa. Serikali hawaelewi bado yawapasa waelimishwe.
 
Mimi ni diaspora na nilikuja 1997 mwezi kama huu baada tu ya kumaliza Form six.

Tatizo kubwa tulilo nalo kama Watanzania hatujaribu kuwaelewa watu au vitu kwa undani kabla ya kujifanya tunajua vitu bila kuwa na data au uzoefu wowote. Watanzania wengi ikiwa pamoja na Magufuli, VP na waziri mkuu hawajui maisha ya diaspora zaidi ya kusikia maneno kwa watu.

Pili ni kwamba Diaspora wanachukuliwa kama wawekezaji kuliko kuchukuliwa kama wenzetu! mara nyingi ukiongelea diaspora watu watakimbilia kukuliza wana faida gani kama vile hawa sio watu ni bank hata serikali inawaongelea hawa watu kama vile ni mtaji! tujiulize mwanakijiji anaye kijijini mbona watu hawaulizi je anaifanyia nini nchi yake na mchango wake kwa nchi?.

Ukiacha Membe, hakuna kiongozi wa serikali aliyewahi kuelezea maisha ya diaspora na kuelewa vizuri, hawajui je ni kwanini mtu anachukua uraia wa nchi nyingine kama kwenye anapenda nchi yake badala yake Watu wengi wamekuwa wakiweka sababu bila kuuliza.

Mimi naona badala ya kujifanya tunajua tuanze polepole na kuwauliza Watanzania ambao wengi tulikuja 1990's-2000's;
Je, ni kwanini umechukua uraia au una mpango huo?
Je, uliishi vipi kwa miaka 15-20 hapo ulipo?
Je, una changamoto gani?
Je, unafikiri tufanye nini twende mbele kama nchi?
Je, Tanzania weakness yetu ni nini?
Je, kwa upande wako umeona nini tofauti?
Je, unaweza kuasaidia vipi nchi? na
Je, kama Tanzania tukusaidieje ili uweze kuwekeza nyumbani?
 
Wanavua citizenship tu lakini nationality iko palepale, nationality haivuliwi na mtu wala serikali, the place of birth na waliokuza ndo inauunguruma zaidi. Wekeza kwenu hata kama serikali haikutambui, kutokukutambua hakuna maana wewe siyo mtanzania ni mambo ya wakati tu. Atakuja mwelewa zaidi wa mambo haya na atayerekebisha vyema na tena ni hiki kizazi cha hawa wahenga tu kitapita ndani ya miaka 10.
Nunua ardhi kwa jina la mama yako dada yako unless wewe siyo mtanzania kwelikweli.

Diasapora wengi ambao hawana uraia wa nchi husika wengi wao 99% hawana hela. Utaipataje hela ugenini bila kuwa na uraia wa nchi husika, labda muuza madawa. Serikali hawaelewi bado yawapasa waelimishwe.

Lakini sidhani kama serikali ya Tanzania inauliza kuhusu "utaifa".
 
Pili ni kwamba Diaspora wanachukuliwa kama wawekezaji kuliko kuchukuliwa kama wenzetu! mara nyingi ukiongelea diaspora watu watakimbilia kukuliza wana faida gani kama vile hawa sio watu ni bank hata serikali inawaongelea hawa watu kama vile ni mtaji! tujiulize mwanakijiji anaye kijijini mbona watu hawaulizi je anaifanyia nini nchi yake na mchango wake kwa nchi?.

Umesema mambo muhimu sana na ninaamini ndio shida iliyopo. Kwa mfano, wengi wanaopinga hili la uraia wa nchi mbili mara nyingi wanafikiria interms ya mtu aliyeko kwenye nchi zilizoendelea (Ulaya huko Japan, Marekani n.k) lakini hawamfikirii Mtanzania aliyeko Malawi, Rwanda, Congo, Kenya n.k Na ni kweli mara nyingi watu wanazungumzia suala hili kwa mitazamo ya kiuchumi zaidi na hata sisi wenyewe mara nyingi tumekuwa tukipigia hoja hii kwa misingi ya manufaa ya kiuchumi ambayo tunaweza kuwa nayo. Binafsi naamini kwa dhati kabisa kuwa hili ni suala la haki za kiraia zaidi na haki ya mtu zaidi. Bila kujali manufaa ya kiuchumi ya mtu huyo.
 
Wanavua citizenship tu lakini nationality iko palepale, nationality haivuliwi na mtu wala serikali, the place of birth na waliokuza ndo inauunguruma zaidi. Wekeza kwenu hata kama serikali haikutambui, kutokukutambua hakuna maana wewe siyo mtanzania ni mambo ya wakati tu. Atakuja mwelewa zaidi wa mambo haya na atayerekebisha vyema na tena ni hiki kizazi cha hawa wahenga tu kitapita ndani ya miaka 10.
Nunua ardhi kwa jina la mama yako dada yako unless wewe siyo mtanzania kwelikweli.

Diasapora wengi ambao hawana uraia wa nchi husika wengi wao 99% hawana hela. Utaipataje hela ugenini bila kuwa na uraia wa nchi husika, labda muuza madawa. Serikali hawaelewi bado yawapasa waelimishwe.
Umeanza vizuri ila umemaliza kihuni..suala la kuwa na pesa halihusiani na passport yako bali mikakati yako tu ikiwa sokoni
 
Busara ni kusikiliza kwanza kabla ya kuongea na ku assume kila kitu
Viongozi wengi hawafahamu kwanini mtu anachukua uraia, wanaofahamu ni wachache sana. Watanzia wengi roho mbaya na colonial mentality ndiyo force behind inayo drive yote haya.
Lakini sidhani kama serikali ya Tanzania inauliza kuhusu "utaifa".

Tatizo namba moja la watanzania wenda akiwemo Rais hawajui tofauti ya Utaifa(Nationality) na uraia wa kisiasa(kumiliki passport-citizenship).
Wanashindwa kabisa kuelewa kwa sababu yoyote taifa husika linaweza revoke uraia wa kisiasa. Ila Utaifa hua hautoki wala haunyanganywi.
Tatizo namba mbili, ni colonial mentality iliyojikita ndani ya watanzania na viongozi wengi kwa ujumla. Maana wengi wanafikiri huko uliko kuna ka mti kakuchuma fwedha eti mwekezaji ama unafaida gani watakuuliza, hiyo ni pure colonial mentality. Sasa utapata je pesa huko uliko bila kuwa na uraia wa huko ili uje uwekeze? wanataka uwe muuzaji wa madawa ya kulevya??
 
Cha kujiuliza Diaspora ni team Tanzania? kama jibu ndiyo basi tupange kama team kusaidia taifa badala ya kutumia muda mrefu sana kuangalia maisha ya mtu mmoja mmoja na kuweka sera kwa mawazo na fikra ambazo sio za nchi? Tuache uivu na kujua Mafanikio ni kila mahali na Mungu hata kupa kwa hate bali kwa love
 
Unajua kwa kuanzia tu na kama kweli serikali ingekuwa ina nia njema na uelewa ingefanya kitu simple sana. Tunajua wanaogopa Wanzazibari kurudi kwa wingi ..... sasa kuna simple solution kwa hilo.

Tanzania ingetoa Permanent Residence kwa mtu yeyote aliyezaliwa Tanzania na kwasababu yeyeote kuchukua uraia wa nchi nyingine.

Hii ingepunguza sana matattizo ya kifamilia yanayotokana na uraia pacha, hao diaspora wasingeweza kupiga kura lakini wangepata haki muhimu za kiraia na wenzetu wa Kenya hawana ujinga wa kuchukua uraia wa watu kama sisi lakini tumeshindwa hata hii simple Permannet Residence
 
:DSerikali Ya Viwanda :p
Fungueni Viwanda Huko Huko Atawatambua Haraka Sana :cool:
 
Hatuwahitaji tuacheni tuendelee kujenga Tanzania yetu. Mijitu imejakalia kuweka.majungu tu kwenye mitandao hamna chochote mnachochangia kwa uchumi wetu. Endeleeni kusaidia kujenga uchumi wa wenzenu. Tuacheni tuendelee kulima dengu na mihogo,, mdogo mdogo tutajikomboa tu.
 
Hatuwahitaji tuacheni tuendelee kujenga Tanzania yetu. Mijitu imejakalia kuweka.majungu tu kwenye mitandao hamna chochote mnachochangia kwa uchumi wetu. Endeleeni kusaidia kujenga uchumi wa wenzenu. Tuacheni tuendelee kulima dengu na mihogo,, mdogo mdogo tutajikomboa tu.

Hii ni colonial mentality. Ngoja nikwambia kitu, uraia ni moja ya human rights kama zingine. Mfano kwa sheria hii maana yake inakukataza indirectly kuoa ama kuolewa na mtu wa wa Taifa jingine, ya kwamba kwa kufanya hivyo mmoja wenu lazima akane kwao. Hii ni violation of human rights.
 
Mawazo yangu yapo kisiasa zaidi, Mtanisamehe. Na sidhani kama nakosea kufikiria mambo kisiasa kwani kwa Tanzania siasa ndiyo huamua maisha yetu.

Mimi naona serikali ipo sawa kabisa, Diaspora siyo privileged group ambalo linafaa sana kusikilizwa, huwa hawana uhalisia wa maisha hasa yanayoendelea huku, yes mara nyingine huja na mawazo mbadala ila 90% ni opportunists.., wamekaa kaa kimtego, matapeli..., Ona Dr. Slaa naye ni diaspora baada ya kulikoroga, Ona anachokifanya Mange Kimambi, Ona anachokifanya Mzee Mwanakijiji . ni aina fulani ya watu wanaofanya kazi kwa maslahi flani, binafsi. hawaendi na uhalisia wa nini kinaendelea field.

Tuanze kuukosoa utaratibu wote wa serikali iliyopo, hatuwezi kujadili mada za maslahi binafsi. Uzuri kwenye kila familia lazima mmojawapo ataisoma namba kwa namna moja au nyingine awamu hii, zamu yako ikifika usilalamike sana, kunywa maji tu.

Serikali yetu haijazoea kusikiliza mawazo ya makundi mbali mbali, ingawa awamu hii hili limezidi. angalau awamu zilizopita walikuwa wanapiga nao picha nakuwapenyezea fursa flani flani..,

sheria nyingi zinapitishwa bila kushirikisha makundi muhimu, serikali inajiamulia mambo ipendavyo...,

Vyuo vikuu vya hapa ni muhimu zaidi kuliko hao wahamiaji haramu.

Pesa za kuhongwa zikiisha mje tulime biringanya tujenge nchi. Ndo uzalendo wenyewe
 
Back
Top Bottom