Tabia ya viongozi wa Serikali kufanana na kambale

Frumence M Kyauke

JF-Expert Member
Aug 30, 2021
630
1,245
TABIA YA VIONGOZI WA SERIKALI:
Wiki iliyopita nilimsikiliza Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akielezea namna wateule wa Rais katika nafasi mbalimbali wanavyopandishiana mabega, nikakumbuka maisha ya kambale ambayo kila mmoja ana sharubu zake.

Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuwa mkali sana katika hili, kwa vile asipodhibiti hali hii ya kila mmoja kuwa ni mkubwa kwa mwenzake, vita hii haitatuacha salama, kazi za kushughulika na maendeleo ya Watanzania hazitafanyika.

Mwisho wa siku Rais Samia na Chama cha Mapinduzi (CCM) wajue kuwa wakiacha misuguano hii iendelee, 2025 Watanzania watapiga kura kwa kuwaangalia wamefanya nini (performance voting) si ahadi kama chama kipya.

Labda kwa faida ya wasomaji wa makala hii, ni vyema nikawapitisha katika kile ambacho Dk Mpango alikisema Jumapili ya Oktoba 24, 2021 Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Siku hiyo alimwapisha Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Pauline Gekul kuwa naibu wake na akamwapisha pia Injinia Kundo Mathew kuwa Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekinolojia ya Habari.

Halikadhalika aliwaapisha Jaji Jacob Mwatebele, Magdalena Rwebangira na Asina Omar kuwa wajumbe au makamishina wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ndipo Dk Mpango alitema nyongo kuwa kuna wateule bado somo halijawaingia.

Dk Mpango alisema inavyoonekana somo la kufanya kazi kama timu na kwa ushirikiano bado halijawaingia baadhi ya mawaziri, makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na manaibu wao, kwani wanapandishiana mabega ofisini.

Nikimnukuu Dk Mpango, alisema: “Hili somo inaonekana halijazama kichwani. Kwa hiyo nipende kuchukua nafasi hii kuwakumbusha tena. Mheshimiwa Rais alishasema hapa, yeye hana hulka ya kuanza kukaripia watu wazima hadharani.

“Lakini aliwaambieni kwamba anapenda zaidi kuzungumza kwa kalamu. Kwa hiyo nawasihi mchukulie maneno haya kama ni onyo kutoka kwa msaidizi mkuu wa mheshimiwa Rais juu ya haya ambayo tunayaona. Mjitahidi sana.

“Ukiwa kiongozi ni muhimu sana uwe mnyenyekevu katika kazi yako. Mmeteuliwa wote mmepewa dhamana na mheshimiwa Rais, huna haja ya kupandisha mabega, yeye anajua kwa nini amewateua mshirikiane.” Mwisho wa kunukuu.

Kauli hii ya Makamu wa Rais si nyepesi hata kidogo, ina tafsiri pana kwamba wapo wateule wa Rais ambao Rais aliwateua kwa dhamira njema ya kuona wanafaa kumsaidia, lakini wao sasa wanahasimiana kwa sababu ya vyeo.

Kuna mambo mengine unajaribu kujiuliza kinachowagombanisha ni nini? Ni madaraka tu? Mbona kila mtu majukumu na mipaka yake imeainishwa? Kama ni waziri si kila mmoja ana mwongozo, au ni mafungu yanaleta shida?

Bahati mbaya sana, kirusi hiki cha kujimwambafai (kujikweza) hakikuanza leo, kwani hata katika awamu ya tano chini ya hayati John Magufuli, kulikuwa na mtifuano mkubwa tu kati ya waziri na Katibu mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hali ilikuwa hivyo hivyo, na sidhani kama imekwisha, labda imepungua tu, kwamba katika baadhi ya mikoa, baadhi ya wakuu wa mikoa walikuwa wakivurugana na wakuu wa wilaya na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri.

Hatuwezi kuendesha nchi hivi, kwamba kila mtu katika ofisi ya umma ana sharubu kama kambale, walioaminiwa na Rais wasimwangushe na wasiwaangushe Watanzania, lakini kubwa zaidi wasituzeeshee Rais wetu.

Rais hawezi kuwateua mumsaidie ili yeye ahangaike na mambo ya kitaifa na kimataifa, nyinyi huku chini ni kuonyeshana umwamba nani ni zaidi, nani ana madaraka zaidi na huu kwa kweli nathubutu kusema ni uzuzu au ulimbukeni.

Nimkumbushe Rais kuwa mwaka 2025 yeye na chama chake watapimwa kwenye sanduku la kura kama uchaguzi utakuwa huru na haki, hivyo hana sababu ya kuwakumbatia watu ambao hawamsaidii kutimiza ilani ya CCM 2020-2025.

Kwa vile Rais kupitia ibara ya 36(1) na (2) ya Katiba ya Tanzania ya 1977, ana mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali, atumie ibara hiyohiyo kuwaondoa wateule wa aina hii.

Nakumbuka katika siku zake za kwanza kwanza tu baada ya kuapishwa, Rais Samia alisema atafanya kazi na yeyote yule bila kujali yuko chama gani ilimradi ni Mtanzania. Ondoa hawa kambale ambao kila mmoja ana sharubu.

images - 2021-10-28T163843.329.jpeg
 
Back
Top Bottom