[h=4]1.3 Chimbuko la Historia ya CCM[/h] Pamoja na kwamba Chama Cha Mapinduzi kuwa kilizaliwa rasmi tarehe 5 Februari, 1977, chimbuko lake linaanzia miaka mingi kabla, sambamba na historia ya uhai wa taifa la Tanzania. Mizizi ya historia ya CCM imo ndani ya harakati za kukataa ukoloni na usultani, zilizofanywa na wananchi wa Tanzania. Wahenga wetu kwa pamoja tangu enzi, walionyesha wazi kukataa kwao kutawaliwa. Historia ya Tanzania inao utajiri wa mifano mingi ya harakati hizo japokuwa zilijengwa katika misingi ya ukoo na ujirani, katika wilaya na mikoa mbalimbali hata kabla ya kuundwa kwa vyama vya TANU na ASP.
Wananchi hao waliotutangulia walikataa kunyonywa, kupuuzwa, kubaguliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na kugawanywa katika misingi ya rangi, kabila, dini, jinsia, nk. Utu na uhuru wao ulikuwa na thamani kubwa sana. Hivyo waliamua kupambana dhidi ya udhalimu huo. Baadhi ya mifano ya jitihada za mapambano ya awali ni Vita ya Majimaji huko Umatumbi na maeneo ya kusini, Mbiru huko Upare, Waluguru, Wameru, Wahehe na mengineyo huko Unguja, Pemba, Kanda ya Ziwa na katika jamii za wafugaji. Ari, utashi, uzalendo na dhamira ya kweli ya kutaka kujitawala vilivyojidhihirisha katika harakati hizo, viliotesha mizizi iliyoshikilia uhai wa vyama vya TANU na ASP.