· UCHUNGUZI WA KIMATAIFA UFANYIKE YAWEZEKANA RAIS WA CHINA HAJUI
· MTASIKIA WATU WAMENYONGWA CHINA SABABU SISI HATUCHUKUI HATUA
Mh. Joseph Mbilinyi "Sugu" ameitaka serikali kuchunguza kuhusu tuhuma zilizotolewa na Televisheni ya Al-Jazeera kuhusu sakata linalohusu tuhuma za kuwa ndege ya Rais wa China ilihusika kusafirisha pembe za ndovu kwa kushirikiana na maofisa wa Ikulu. Huku akisisitiza kuwa humu ndani mnasema kuna watu wanaichonganisha serikali na wananchi ila mchawi wa CCM ni CCM yenyewe kwa mambo yanayofanyika kila siku.
Watanzania wa sasa hivi sio wale, wa sasa hivi wanajua kinachoendelea wanaelewa inamaanisha nini wakiona Televisheni ya Al jazeera inapoonyesha kuwa ndege ya Rais wa China pamoja na maofisa wa Ikulu wameshiriki kusafirisha pembe za ndovu. Mbunge huyo amemtaka waziri wa mambo ya nje aache kukurupuka na kutolea majibu kuwa shutuma hizo ni uzushi badala yake wafanye uchunguzi sababu mtu amehojiwa bila kificho anaelezea kwa namna gani wanavyoshirikiana na Wachina katika kusafirisha pembe za ndovu na wanatoa ushahidi wa meno ya ndovu bila kificho.
Sugu akasisitiza kuwa Waziri anasema "Rais wa China kaja alifanya saa ngapi shopping", Mbunge Mbilinyi akahoji yaani inamaanisha Rais wa China aende vinyagoni Mwenge kufanya shopping? Wanasema ile ziara ndiyo imetumika yawezekana ukakuta Rais mwenyewe wa China ajui kuwa ndege yake ilihusika kusafirisha pembe za ndovu mkifanya uchunguzi mtasikia kuna watu wamenyongwa China, sababu sisi hatuwezi kuchukulia hatua watu wetu
kwa mfano mara ya kwanza tulisema kuhusu meli ya Kinana watu wakapiga kelele leo tunaambiwa ndege ya Rais wa China. Ripoti inasema uchunguzi ulifanyika kwa miaka kumi halafu waziri Membe anasimama na kusema kuwa wazungu wameleta uzushi, akasema "kwa nini wazungu wakisema Rais wetu ni kinara wa utawala bora Waziri Membe asemi ni uzushi?" alihoji.
Alitakiwa aje na kusema inatakiwa ufanyike uchunguzi wa Kimataifa tujue ukweli na kama tukigundua Ripoti ni ya uongo, Tanzania kama nchi tuchukue hatua kwa wale waliotuchafua haswa ikichukuliwa taarifa imetolewa na vyombo vikubwa vya habari kama BBC na AL JAZEERA, kufanya mambo ya maendeleo inabidi tushirikishe wananchi na wananchi wanavyokatishwa tamaa na taarifa kama hizi wanashushwa moyo wa kufanya shughuli za maendeleo.