Wizara ya Maji
Govt Institution
- Oct 2, 2024
- 33
- 20
Bwawa la Farkwa ni mradi wa maji wa kimkakati ulioibuka kama mkombozi wa huduma ya maji kwa wakazi wa Jiji la Dodoma na maeneo jirani. Ni Safari na matunda yake yanaonekana wazi kwa furaha na tabasamu za wananchi.
Dodoma, ikiwa makao makuu ya serikali, imekuwa ikikua kwa kasi katika idadi ya watu na shughuli za kiuchumi. Hali hii iliongeza mahitaji ya maji safi na salama. Kupitia bwawa hili, tatizo hilo linaenda kuondoshwa.
Ni safari yenye maono makubwa, safari yenye mwanzo mchungu lakini mwisho wake umejaa neema na tabasamu lukuki miongoni mwa wananchi wa jiji la Dodoma pamoja na viunga vyake na maeneo jirani.
Kwa miaka michache iliyopita hadi leo jiji la Dodoma linaongezeka kwa idadi ya watu na kazi mbalimbali za kiuchumi hivyo kuhitaji huduma muhimu ya maji zaidi kukidhi mahitaji na kuondokana na na mgao ambao unatumika ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila kukicha.
Kwa uchache, Ujenzi wa Bwawa la Farkwa Dodoma unatarajiwa kuleta faida kubwa za kiuchumi, ikiwemo uzalishaji wa maji lita milioni 128 kwa siku, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, na kuchochea ukuaji wa viwanda na biashara. Serikali imewekeza katika mradi huo kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).