Spika Sitta na 'ufyatukaji' wake! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Spika Sitta na 'ufyatukaji' wake!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Teamo, Feb 19, 2009.

 1. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #1
  Feb 19, 2009
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  RAIA MWEMA
  Februari 18, 2009
  Johnson Mbwambo  NILIPATA kuandika huko nyuma kwamba nchi yetu hivi sasa inapitia kipindi kigumu mno chenye majaribu ya kila aina. Nilisema kwamba ili kuweza kukivuka kipindi hiki ambacho pandora box limefunguka, tunahitaji kuwa na viongozi wenye hekima, ujasiri na uvumilivu.

  Nilisema kwamba bila hekima, ujasiri na uvumilivu kutoka kwa viongozi wetu, taifa litapoteza dira kabisa na kuwa sawa na ndege ya abiria inayopita anga lenye mawingu mazito; huku ikiwa kwenye auto-pilot.

  Tumefika mahali ambapo Watanzania wengi wamekatishwa tamaa na watawala. Tumefika mahali wafanyabiashara na wanasiasa maarufu wanaanzisha magazeti ya kushambuliana kuhusu masuala yao ya ndoa, ngono na uchafu mwingine!

  Tumefika mahali DC mzima wa wilaya ya Bukoba Vijijini anakiri (tena bila woga) kwamba aliamrisha walimu wacharazwe viboko na koplo kwa sababu ya kuchelewa kazini!

  Tumefika mahali ambapo hata watawala wenyewe kwa wenyewe hawaelewani; huku baadhi wakijenga ujasiri wa kuwanyooshea wenzao vidole kwamba wao ndiyo chanzo cha wananchi kupoteza imani kwa watawala wote. Na kwa sababu hiyo, malumbano ya wakubwa si haba. Hakika pandora box limefunguka!

  Katika mazingira kama hayo, haishangazi atokeapo kiongozi mmoja kuishiwa uvumilivu na kutoa kauli ambazo wakati mwingine hazipendezi sana kutolewa na mtu wa wadhifa wake. Na hivyo ndivyo nilivyoziona kauli zilizotolewa wiki iliyopita na Spika wetu, Samwel Sitta kwenye kikao cha Bunge kilichomalizika, Jumatano iliyopita, mjini Dodoma.

  Namfahamu Sitta si tu kama spika wa bunge letu, lakini pia kama mzee wa kanisa wa usharika ambao mimi pia nasali – KKKT Kinondoni. Namjua kwamba ni mzee mwenye busara, hekima na uvumilivu.

  Hata hivyo, kwa kauli zake za wiki iliyopita alizozitoa bungeni, Dodoma, napata hofu kwamba yaelekea naye anaishiwa na uvumilivu au labda niseme naye ameanza kukata tamaa kama sisi.

  Nazungumzia kauli zake mbili alizozitoa, lakini labda nianze na maneno mawili – potelea mbali, aliyoyatamka ndani ya bunge wakati akitoa kauli yake ya kujibu malalamiko ya Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan kwamba Bunge limekuwa likiingilia uhuru wa Mahakama.

  Nakubaliana na Spika Sitta kwamba malalamiko yaliyotolewa na Jaji Mkuu hayawezi kunyamaziwa na Bunge kwa kuwa suala hilo ni la kikatiba. Lakini pia nakubaliana na haki ya Jaji Mkuu kulalamika mbele ya Rais kwamba Bunge linaingilia kazi za mahakama.

  Nisichokubaliana nacho, au labda nisema kilichonishangaza, ni matumizi ya Spika ya maneno “potelea mbali”. Alisema hivi: “Hapa, watasema pia naingilia Mahakama, lakini potelea mbali.”

  Maneno potelea mbali, kama alivyoyatumia yeye, yanaashiria mtu aliyeishiwa uvumilivu wa kurekebishwa tatizo lililopo kwa utaratibu wa kawaida; na hivyo anaamua kutoa dukuduku lake bila kujali yatakayofuata! Potelea mbali, kwa namna alivyoyatumia yeye, yanafanana na maneno ya Kiingereza come what may!

  Sasa kwa kuchagua kutumia maneno hayo, Spika Sitta ametia doa hoja yake nzuri kwamba Bunge haliwezi kukaa kimya likikosolewa na mhimili mwingine wa utawala, na wala haliwezi kukaa kimya likiona mhimili mwingine hauheshimu maslahi ya umma (ya walio wengi).

  Kwa kutumia maneno hayo ya liwalo naliwe, Spika Sitta ameweka taswira ya mpambano – confrontational (dhidi ya Jaji Mkuu Augustino Ramadhan?) , na nahisi ni kwa sababu ya kuishiwa uvumilivu.

  Sasa sidhani kwamba katika kipindi hiki kigumu, baada ya pandora box kufunguka, tunahitaji spika ambaye anaishiwa uvumilivu haraka kiasi cha kusema potelea mbali (liwalo naliwe). Nadhani tunahitaji spika mtulivu, asiye na jazba, anayepima hoja na anayetumia busara kutafuta maslahi ya umma yanaangukia wapi katika pande mbili zinazokinzana.

  Lakini zaidi ya yote tunahitaji spika mvumilivu; maana spika akiishiwa haraka uvumilivu, iweje kwa sie raia wa kawaida? Kwa ufupi, lugha ya potelea mbali (come what may) si lugha tunayoitarajia itumiwe na spika.

  Tukiyaweka maneno yake hayo mawili pembeni, bado pia kuna mengine yasiyopendeza aliyoyatamka ndani ya bunge siku ya pili yake wakati akieleza kukerwa kwake na uandishi wa baadhi ya magazeti nchini.

  Alisema hivi:“Nafikiri sheria ya magazeti haiwezi kushindwa kushughulikia hili. Kama kawaida yangu nafyatuka tu. Sasa kama hii ndiyo hulka yangu utafanyaje? Hii ndiyo kawaida yangu, na wakati mwingine ni vizuri katika taifa kuwepo na watu kama mimi wanaofyatuka ili mambo yaende mbele.

  Sitaki kuzungumzia hoja kwamba kushambulia magazeti hayo bungeni kunaweza nako kutafsiriwa kuwa ni kuuingilia mhimili wa nne (fourth estate); lakini niseme tu kwamba maneno aliyoyachagua Spika Sitta kuwasilisha malalamiko yake hayo, nayo yameniacha hoi.

  Spika Sitta anasema: “kama kawaida yangu nafyatuka tu.” Hivi kweli katika kipindi hiki kigumu ambapo nchi inatikisika kutokana na kukithiri kwa ufisadi na kutelekezwa kwa maadili ya uongozi, tunahitaji Spika anayefyatuka tu?

  Ninavyojua mimi, mtu anayefyatuka tu si mtu mwenye busara wala hekima. Hivi kweli katika kipindi hiki kigumu tunahitaji spika ambaye anafyatuka tu? Mimi naamini tunahitaji spika mtulivu, spika mwenye hekima zaidi, ujasiri zaidi na mvumilivu zaidi!

  Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba pamoja na kuwa maudhui ya alichozungumza ni mazuri, lakini halikuwa jambo zuri kwa yeye kuwatangazia Watanzania wote (na kuingia katika hansard za Bunge) kwamba ni kawaida yake kufyatuka. Sidhani kwamba ufyatukaji ni moja ya sifa za kiongozi bora.

  Hata hivyo, nisisitize tena hapa kwamba tuna spika jasiri na anayekerwa kweli kweli na umasikini wa Watanzania. Tuna spika anayekerwa na kukithiri kwa ufisadi nchini.Tuna spika anayekerwa kweli kweli na kukwama kwa nchi yetu ki-maendeleo.

  Tuna spika ambaye amesimama kidete kuibana serikali kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya Bunge juu ya masuala yanayougusa umma kuliko spika mwingine yeyote tuliyewahi kuwa naye katika historia ya nchi yetu.

  Na ndiyo maana ninataka kuamini kwamba kwa kutumia maneno aliyoyatumia wakati alipotaka kuonyesha hisia zake hizo bungeni, wiki iliyopita, ni kughafilika tu, na si dalili za kukata tamaa na kuishiwa uvumilivu. Spika Sitta ni mtu wa mwisho tunayetarajia kukata tamaa na kuishiwa na uvumilivu!

  Nimalizie tafakuri yangu kama nilivyoianza. Pandora box limefunguka. Tunapitia kipindi kigumu. Ufisadi umetamalaki nchini. Kuna kukata tamaa, na kwenye kukata tamaa kuna kuishiwa na uvumilivu. Tuombe tu Mungu kwamba wanaotuongoza wasiwe ndiyo wa kwanza kuishiwa uvumilivu na kuanza kuwa confrontational.

  Tafakari.
   
  Last edited: Feb 19, 2009
 2. Piemu Esquire

  Piemu Esquire Member

  #2
  Feb 19, 2009
  Joined: Nov 17, 2008
  Messages: 64
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hakika tafakari hii inataka muda wa kutosha kuichambua,Kwanza kumjua Sitta mwenyewe,Pili kumjua Sitta kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Tatu kumjua Sitta kama Kiongozi wa watu(hapa wewe umesema unamjua kama mzee wa Kanisa huko Kinondoni mnakosali pamoja).

  Samwel Sitta ni mtu aliyewahi kushika nyadhifa nyingi Serikalini kuanzia awamu ya Kwanza,Ya pili ,Ya Tatu na sasa ya Nne.Tulitegemea nini kwa mtu kama huyu mwenye uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa Serikali.Sitta ni mwanasheria kwa taaluma,Nijuavyo mimi wale ndo kaka zetu wasomi !Sasa basi maneno yake mbele ya umma wa Watanzania yana twasira gani kimaadili?Anataka kutuambia yeye ndiye kiranja wa kakawasomi wote?

  Samwel Sitta anajua fika kuwa mihimili mikuu ya Serikali ni pamoja na Bunge na Mahakama.Leo akiwa Spika tena Kakamsomi iweje hadharani ajitokeze kukemea mahakama kama imeingilia Bunge?
  Mambo mengi ndani ya mijadala ya Bunge Mh.Spika amejaribu kuyachukulia kwa style yake mwenyewe.Ni pamoja na kujitangaza kwa majina yasiyo na sifa zake mwenyewe "Standard and Speed".Hata mara nyingine amekuwa akijaribu kutumia msimamo wake mwenyewe kama kigezo cha kuwaweka chini wale ambao hafungamani nao kwa namna moja au nyingine,Iwe Serikalini au Bungeni.Kuna tabia siyokuwa ya kimaadili kwa kiongozi huyu ambayo tunaamini kuwa ataifikisha nchi pahala pasipo kwa vijembe na kejeli zake mara kwa mara kwa viongozi wenzake.
  Hata wakati mwingine wanazuoni wamekuwa wakimtizama kwa jicho la kutaka kuingia kwenye kinyang'anyiro cha Ukuu wa nchi miaka ijayo.Lakini kwa jinsi hii nasi wananchi tunapata wasi wasi kama kweli Uzooefu wake unamaanisha busara au mazoea tuu.Je hao ndiyo viongozi tunaowataka katika karne hii.Si ni busara kuwapumzisha kuliko kuchochea migogoro kwa style ya kuuma na kuupuliza?
   
 3. N

  Nyauba JF-Expert Member

  #3
  Feb 19, 2009
  Joined: Jul 10, 2008
  Messages: 1,098
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 135
  Mzee sitta ana matatizo kwani kwa hisia zangu juu yake ni kwamba bado ana matamanio ya ukuu wa taifa hili.
  amekuwa na jeuri mbaya sana hasa baada ya kuwa kiongozi wa BUNGE. anaonyesha jeuri baada ya kuupima utawala uliopo na kugundua mapungufu makubwa waliyo nayo.

  ila unafiki bado unamgarimu kwani mtandao ndo pia walimfikisha hapo alipo sasa.
  anajenga mazingira gani kwa vijana tunamwona kama kiongozi wa kuiga kwa kutoa lugha za iana hii kwa jamii.

  mh zitto alipotoa hoja ya buzwagi alimkandamiza, slaa na epa alimkebehi lakini kwa sasa anajaribu kujirudi kwa kasi kuwapenda na kuwaunga mkono moyoni.

  ana agenda zake na ana kundi nyuma yake. yetu macho kwani vurugu zaom huenda tukafaidika kwa mabadiliko ya kimtazamo ni kiungozi.
   
 4. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #4
  Feb 19, 2009
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 104
  Trophy Points: 145
  Na ile kashfa yake vp?
  Ya kutumia mali za bunge hawala zake sijui iliishia wapi?
   
 5. Ayayoru

  Ayayoru Senior Member

  #5
  Feb 19, 2009
  Joined: Feb 17, 2009
  Messages: 113
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 33
  Kweli mkuu Sitta ni ndumilakuwili anauma na kupuliza bt ajue kua mwisho wa ubaya ni aibu hayo anayoyafanya leo kwa kutumia madaraka alopewa yanamwisho wake.......time will come
   
 6. Shaycas

  Shaycas JF-Expert Member

  #6
  Feb 19, 2009
  Joined: Feb 13, 2009
  Messages: 899
  Likes Received: 34
  Trophy Points: 45
  Sitta anajua anachokifanya ila jazba ilimpanda baada ya jaji mkuu kulalamika kwa RAIS.Ingawa si busara lakini ni BORA ASEME TUMJUE kuliko kujifanya mnafiki.
  Sitta ameendesha BUNGE kwa ubabe mkubwa dhidi ya SERIKALI hadi kufanikiwa kuundwa kamati ya BUNGE KUCHUNGUZA ZABUNI iliyopewa RICHMOND pia mnaweza kuona ALIVYO MZUIA MAKAMU WAKE ASIENDESHE MJADALA WA RICHMOND,Hii ni kwa sababu YULE MAMA ANAIBEBA SANA CCM ANAPOKALIA KILE KITI.
   
 7. Teamo

  Teamo JF-Expert Member

  #7
  Feb 19, 2009
  Joined: Jan 9, 2009
  Messages: 12,286
  Likes Received: 51
  Trophy Points: 145
  Shycas UMENENA!
   
Loading...