Juzi niliweka taarifa za mtoto Ian Bahati Emmanuel wa Tarakea, aliyepotezana na baba yake mwezi Oktoba 2025 baada ya kuachwa kwenye daladala. Kwa mujibu wa Ian, baba yake alisafiri naye kutokea Tarakea kwa bibi yake kwenda Dar kabla ya kupotezana.
Wenye daladala walimpeleka kituo cha Polisi Oysterbay ambapo alifunguliwa jalada la taarifa nambari OYB//RB/2025. Polisi walimkabidhi Ustawi wa Jamii Kinondoni ambao walimtunza katika nyumba salama kwa zaidi ya miezi 6. Jitihada za kutafuta ndugu zake zilifanyika kwa kutangaza kwenye TV, Radio na vyombo vingine vya habari bila mafanikio.
Sasa habari njema ni kwamba baba mzazi wa Ian amepatikana ndani ya masaa 24 tu tangu tulipoweka taarifa kwenye ukurasa huu. Ikumbukwe kwa zaidi ya miezi 6 vyombo vikubwa vya habari vilitangaza lakini hakuna ndugu aliyepatikana. Tunamshukuru Mungu kupitia ukurasa huu mtoto kaungana na ndugu zake ndani ya masaa 24 tu.
Baba anakiri kumchukua mtoto Tarakea, kwa nia ya kumleta Dar kwa mama yake. Inadaiwa mama alimuacha Ian kwa baba yake akiwa na mwaka mmoja na miezi mitano tu. Baba akampeleka kwa bibi Tarakea kulelewa.
Mwaka jana Oktoba akamchukua mtoto na kuja naye Dar kwa lengo la kumkabidhi kwa mama yake. Lakini wakiwa kwenye daladala ya Tegeta kabla hajaonana na mama yake, mtoto akapotea.
Baba alihangaika kumtafuta bila mafanikio. Alitoa taarifa kituo cha Polisi Madale na akaacha picha ya mtoto. Amekuwa akienda kituoni mara kwa mara kuulizia kama amepatikana bila mafanikio. Hatimaye baada ya miezi 6 amemuona mwanae.
#MyTake:
Kwanza nawashukuru sana wote waliosaidia mtoto Ian kuungana na ndugu zake. Shukrani kwa Idara ya Ustawi wa Jamii Kinondoni, dereva na konda wa daladala, wananchi waliosambaza taarifa na zaidi shukrani kwa Mungu wa mbinguni aliyewezesha yote kufanyika kwa ajili ya utukufu wake.
Pili, nashauri Polisi wawe na mfumo unaosomana. Baba alipotelewa na mtoto akatoa taarifa Polisi Madale, na wenye daladala wakaokota mtoto wakatoa taarifa Polisi Oysterbay, lakini ndani ya miezi 6 Polisi Madale hawajui kama mtoto anayetafutwa ameripotiwa Polisi Oysterbay. It’s weird.
Yaani Polisi Madale wanatafuta mtoto, na Polisi Oysterbay wanamtafuta baba wa mtoto huyohuyo. Jeshi moja, mkoa mmoja, wilaya moja, lakini mifumo haisomani. Yaani Polisi Madale hawajui kama mtoto anayetafutwa ameripotiwa Polisi Oysterbay, na Polisi Oysterbay hawajui kama baba anayetafutwa ameripoti Polisi Madale. Aisee hii ni huzuni.
Nashauri serikali badala ya kuwekeza nguvu nyingi kutafuta “umbea mtandaoni” waongeze rasilimali kwa jeshi la Polisi kulisaidia lijiendeshe kiteknolojia. Polisi waache kuandika RB kwenye vikaratasi na kutunza kwenye counter book.
Kuwe na mfumo wa online ambao mtu akiingiza RB number inasoma tukio ni la wapi, limetokea lini na linamhusu nani. Kama ambavyo ukiingiza namba ya gari kwenye mfumo wa TIRA inakupa taarifa zote za gari.
Tuna vijana wengi na wazuri wa IT wanaoweza kufanya kazi hiyo, lakini wapo mtaani hawana ajira. Wapeni kazi jeshi letu lijiendeshe kisasa. Punguzeni resources mlizowekeza kutafuta umbea mtandaoni, mfanye mambo ya maana. Bata, Wahed.!