Siri ya Kuuwawa Zitto - UWONGO

Siri ya Kuuwawa Zitto - UWONGO

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Joined
Mar 2, 2007
Posts
1,562
Reaction score
10,890
Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘SIRI YA KUUWAWA ZITTO YAFICHUKA' na vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini' dk. Slaa atajwa kumtuma Saanane kummaliza'. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa.

Napenda kusema yafuatayo:

Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari sahihi.

Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.

Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.

Nne, Nawashauri viongozi wenzangu wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache. Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.


=============


Thread inayoongelea kilichoandikwa na Mtanzania hii hapa - https://www.jamiiforums.com/jukwaa-...ajwa-kumtuma-ben-saanane-kummaliza-zitto.html
 
asante mtani kwa ufafanuzi na kwa vile hii ni kauli yako mwenyewe basi watatumia wino na karatasi zao kuandika mambo ya maana.
 
Hongera sana mkuu Zitto kwa kuja kulielezea hili. Kuna watu wameeneza hizi propaganda kwa muda mrefu na nia yao si nzuri kwako na kwa chadema. Nadhani ifike wakati hawa watu uwachukulie hatua stahiki ili iwe fundisho na malipo ikwa propaganda za kipumbavu namna hii.
 
Last edited by a moderator:
Karibu kamanda....! Umenena vema kabisa.Tunashukuru kwa ufafanuzi uliotoa.
 
Nimezisikia hizi habari zikishabikiwa na kiredio fulani kama sikosei ni clouds fm wameishabikia hii mada utadhani siyo professionals, as if ni wamama fulani wamekaa kibarazani wanajadiri umbea. Clouds FM inajipotezea sana status yake kushupalia uzushi tena kwa upendeleo, uzushi unaokichafua CCM wanakuwa kimya ila uzushi wa kuichafua CHADEMA utamsikia Geladi Hando, Kibonde na watu wa level hiyo jinsi wanavyo ishupalia kimbea,

Namshukuru Mungu kwa kuniepusha na aibu ya kutumika na wanasiasa.
 
Nimefurahishwa na post yako kwani imewaweka huru watu wengi sana.Pili uongo huu siyo unajenga chuki yako na Dr.Slaa bali jamii nzima itawachukia wale wanaodhaniwa kudhuru wenzao.Asante sana kwa kupeleka ujumbe huo mzito kwa wahusika wanopenda kuwagombanisha watu.

Waandishi wa habari acheni kushabikia ujinga ambao maafa yake ni makubwa kuliko pesa mlizopewa kuandika ujinga huo.Mjue mnaweka maisha ya watu wengine hatarini.
 
Asante sana Zitto nadhani sasa hawa vilaza umewafunga mdomo asante sana, maana wamekalia sana umuandama DR SLAA, na wafanye yao waiache CHADEMA kama ilivyo....
 
Last edited by a moderator:
Ahsante sana Kamanda Zitto!....Siasa za kuchafuana hazIitalikomboa taifa letu! Tunahitaji kufanya siasa za kujenga chama pamoja na taifa kwa ujumla!
hongera pia kwa kumaliza mafunzo!
karbu jukwaan
 
"Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi"
Maneno murua kabisa mwenye kusikia na asikie sasa!
 
Asante Zitto kamwe tusimpe nafasi mtu atugawe. Tunaelekea wakati mujimu sana katika historia ya Taifa letu, nao ni ukombozi wa nchi yetu kwa nguvu ya umma. 2015 Yes.
 
....................Gazeti la Mtanzania ni wazushi na wazandiki na huu ni mwanzo .....chunga sana
 
Vizuri sana Zitto kwa ufafanuzi mzuri.Gazeti la Mtanzania siku hizi limekuwa kama gagulo la kuandika uchochezi,chuki,fitina,majungu na uzandiki dhidi ya Chadema hasa likimuandama Dr Slaa.

Sijui kwanini Hussein Bashe anaruhusu gazeti hili kuandika upuuzi kama huu.

Again Thankyou Zitto you have made my day.
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom