Wanajamii wanapaswa kuishi kwa kuheshimiana, kuhurumiana na kusaidiana. Hizi ni nguzo muhimu sana katika jamii yoyote ile anayoishi mwanadamu. Hakuna mtu anayeweza kujidai kwamba, hamuhitajii mtu katika jamii anayoishi. Hata mfagia barabarani, wafanyakazi wa manispaa wanaozoa mavi na taka hawapaswi kudunishwa kwa sababu tu ya kazi yao. kwanza hakuna kazi duni, kazi ni kazi bora iwe ya halali na ambayo inampatia mtu riziki yake na familia yake. Pili kama leo wafanyakazi hao watagoma mjini patakalika kwa taka na uchafu? Hivyo katika jamii moja ya mambo yanayoapswa kulindwa ni suala la kuheshimiana. Kuheshimiana kunajumuisha mtu kuheshimu majirani, kazi zao na hata imani na itikadi zao za kidini. Kujitokeza mtu akautusi Uislamu au Ukristo ni jambo la hatari mno, kwani huko ni kujeruhi hisia za mtu na itikadi yake ambayo yeye anaiamini na anaamini kwamba, ni kupitia dini yake hiyo ndipo anamfikia Mwenyezi Mungu na kumtumikia. Hivyo tuache kutoa kauli za kejeli, dharau na matusi dhidi ya dini za wengine. Huu sio uungwana hata kidogo. Kama ambavyo mtu akaiitusi dini yako (kwa sharti kwamba, uwe kweli una imani nayo na uchungu pia) huwezi kuridhia hata kidogo. Ukitukaniwa mkeo au mwanao unakuja juu kama moto wa kifuu seuze dini yako? Tuwe waungawana jamani. watanzania tunasifika kwa ukarimu, uungwana, kuhurumiana na kuishi kwa amani baina yetu. tuthamini neema hii ya amani tuliyonayo. Tusije kuitumbukiza nchi katika dimbwi la machafuko kwa kauli za matusi kejeli ambazo naona hapa JF zimeongeza mno katika masiku ya hivi karibuni sijui lengo hasa ni nini. Unapotoa kauli za kejeli dhidi ya dini ya mwezio unataka kufikisha ujumbe gani?