Simulizi ya mtu mrefu kutoka Chato hadi Marekani

Etwege

JF-Expert Member
Jul 4, 2018
5,738
15,211
The giant Julius mwenye urefu wa futi 7 na nchi 5 aliyezaliwa wilayani Chato miaka 26 iliyopita ametajwa kuwa ndiye binadamu mrefu zaidi nchini Tanzania kwa sasa.
The giant Julius amesimulia changamoto anazokutana nazo pia na alivyoanza kucheza buskatball mchezo uliomuwezesha kwenda jimbo la Seattle nchini Marekani.

========

Dar es Salaam. Inashangaza! Lakini sio mshangao pekee, inavutia kumtazama binadamu mwenye urefu usio wa kawaida.

Wakati binadamu wa kawaida akikadiriwa kuwa na urefu wa futi 5 hadi 5.5, hali ni tofauti kwa Julius Charles, mwenye urefu wa futi 7 na inchi 5.

Julius (26) kwa sasa huenda akawa ndiye binadamu mrefu zaidi Tanzania, ukiachana na rekodi ambayo alikuwa akiishikilia mchezaji wa kikapu maarufu wa Kitanzania, Hasheem Thabiti ambaye ana urefu wa futi saba na inchi tatu.

Tumeandika awali kuwa anavutia, basi ni hivi; Julius mbali na kimo hicho kirefu, viganja vya mikono na shingo yake vyote vina urefu usio wa kawaida. Anataka kufanana na twiga kwa mvuto wa shingo yake.

Lakini Julius bado ana sifa nyingine za ziada. Ukimkaribia unakutana na binadamu mwenye misuli mikononi iliyotuna mishipa yake.

Unajua analazimika kuvaa viatu vya ukubwa gani? Julius kwanza anavaa viatu saizi 18, sawa na namba 56 na hulazimika kuviagiza nje ya nchi!

Historia yake
Mama mzazi wa Julius, Rachel Joram anasema: “Nilimzaa Oktoba 28, 1995 mjini Chato akiwa na uzito wa kilo tisa. Ilikuwa ni ajabu lakini walisema hata marehemu babu yake ‘Mgini’ ambaye alikuwa mrefu sana pia alizaliwa na uzito mkubwa.”

Akizungumza na Mwananchi jana, kijana huyo maarufu kwa jina la ‘The Giant Julius’, alisema amezoea hali ya watu kumshangaa na kumuona kama ni kitu cha ajabu.

“Watu walionizunguka hawajanizoea na kiukweli sizoeleki, kwa upande wangu hainipi shida, namshukuru Mungu hivi nilivyo ni mapenzi yake.

“Walionizoea ni familia yangu ambao nakaa nao, wengine marafiki ninaokutana nao hawajanizoea. Kuna nyakati nikipita Kariakoo, Mbagala au kokote kule, kuna ile hali ya kuonekana tofauti na watu wengine, kwani wananishangaa,” alisema Julius, ambaye kwa sasa ana uzito wa kilo 120.

Hata hivyo, alisema licha ya urefu alionao, kwake anaifurahia hali hiyo. “Nafurahia kwa sababu ni mapenzi ya Mungu, kwangu mimi wanaonishangaa nawachukulia ni mashabiki wangu,’’ alisema.

Maisha yake
Akizungumzia maisha yake, Julius alisema mbali ya kuzaliwa Chato, alikulia jijini Mwanza, alikosoma elimu ya msingi na alipohitimu darasa la saba, baba yake alifariki dunia na huo ndio ukawa mwisho wa kusomeshwa na familia.

Alikaa nyumbani miaka mitatu mpaka alipopata mfadhili wa kumsomesha elimu ya sekondari .

Alimpata mfadhili huyo baada ya kuvutiwa na kipaji chake cha uchezaji wa mpira wa kikapu.

“Nilipozaliwa nilikuwa wa ajabu na wenzangu walinishangaa sana, uzuri nilikuwa mpole mno. Nilikuwa napata tabu kwa watoto wenzangu wananicheka, wananipiga na kunikejeli kutokana na umbo langu.

“Hata hivyo nilikuwa mrefu kiasi, lakini nilianza kukua kwa kasi, nikiwa na miaka 13 watu walikuwa wananiambia unakua sana, unakwenda wapi? Nilikuwa nachukulia kawaida,” alisema.

Julius alisema tangu utoto wake hajawahi kwenda hospitalini kuangalia afya yake.

“Sijawahi kupelekwa hospitali kuangaliwa afya, haijawahi kutokea...” alisisitiza.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kurithi umbo kubwa kutoka kwa mmoja wa wanafamilia wake, alisema kwa maelezo ya wazazi wake, babu yake mzaa baba ambaye hata hivyo hakuwahi kumuona, naye alikuwa mrefu sana.

Fursa

Wakati umbo lake likiwavutia wengi kumtazama, Julius alisema ameichukua hali hiyo kama fursa.

“Jambo la watu kunishangaa mwanzo liliniwia ugumu sana, kwani wengine walinikimbia. Wapo waliowahi kupoteza fahamu, nakumbuka ni watu wanne. Zamani ilikuwa inaniumiza, siku zinavyokwenda naizoea, watu wakikimbia nabaki nacheka tu.”

Kwa sababu baadhi ya watu hutaka kupiga naye picha, jambo analoliona kama kumpotezea muda, baadhi ya nyakati anasema huwatoza fedha.

“Wapo wanaonilipa 2,000 mpaka 50,000, inategemea na hali ya mtu.”

Anasema kwa hali yake, alilazimika kutafuta kazi ya kuwa balozi wa kampuni, shughuli anayosema inamsukuma kimaisha.

‘‘Baadhi ya kampuni zimenitumia, wanajua kazi yangu na ninafanya shughuli zangu vizuri sana, wateja wanakuja na ninanufaika,” alisema.

Masomo
Licha ya nafasi aliyonayo sasa, Julius alisema amesoma kwa shida kwa sababu alilelewa katika familia ya kimaskini.

Alisema hali hiyo ilitokana na baadhi ya ndugu zake wakubwa kuwa masomoni, jambo lililosababisha asubiri kwanza uchumi wa familia utengemae.

Hata hivyo, baadaye alifanikiwa kuanza safari yake ya kusoma na kufikia ngazi ya chuo, elimu ambayo hata hivyo bado hajaimaliza.

“Mpaka nakuja kusoma ni juhudi zangu binafsi, hakuna ndugu wala yeyote aliyenilipia ada, baada ya kuona nakua na umbo langu kubwa nikajiingiza mchezo wa basketball (mpira wa kikapu). Huko kuna mwandishi siku moja alinifanyia mahojiano nikapata ufadhili wa masomo katika shule ya Lord Baden Memorial School, nikasoma mpaka kidato cha nne,” alisema.

Alisema akiwa shule alishiriki mchezo huo na kuchezea timu ya shule iitwayo Scorpion na kushiriki katika mashindano ya Umiseta kuanzia mwaka 2012 mpaka 2014 na mengine yaitwayo Feasa yaliyokuwa yakifanyika Dar es Salaam.

“Sijawahi kuchezea klabu za Tanzania, kwani mfano ligi ya RBA ya Dar ile ni ligi kubwa na wachezaji ni wakubwa, ilinibidi niwe na nauli sababu sijaajiriwa na kipindi hicho sikuwa na fedha hivyo nilishindwa kujiunga.

“Nyakati hizo zote nilikuwa nacheza mitaani kama sehemu ya mazoezi kujiweka fiti, nilikuwa nafuatilia ufadhili na nilibahatika mwaka 2018 nikakaribishwa chuo kimoja kipo Marekani jimbo la Seattle, lakini nilishindwa kujiunga kutokana na kukosa fedha za nauli,” alisimulia.

Julius alisema alilipiwa malazi, chakula na mahitaji mengine ikiwemo viza, lakini ilimchukua miezi sita kupata nauli kiasi cha Sh5 milioni na hivyo alijikuta amekaa Marekani kwa miezi sita pekee.

“Nilirudi nchini mwishoni mwa mwaka 2019 na hapo wakati najindaa nipate viza nyingine ili niendelee na ule ufadhili, corona ikaingia hivyo nilishindwa kurudi Marekani ijapokuwa nafasi yangu bado ipo na ninaendelea na mawasiliano nao,” alisema.

Mbali na mpira wa kikapu, Julius alisema amejikita pia katika uigizaji ambao anaendelea nao kwa sasa, akifanya kazi chini ya wasanii wawili nguli wa filamu, akiwemo Gabo Zigamba.

Changamoto za maisha
Julius alisema: “Mungu anavyokuumba kwa tofauti ana maana yake; kila kitu kwangu ni changamoto kuanzia nguo, kitanda, godoro usafiri na viatu.

“Nalazimika baadhi ya vitu kuagiza nje, mfano mavazi yapo lakini si mengi kama ya wengine. Viatu navaa namba 18 sawa na namba 56.”

Alisema changamoto kubwa kwake awali ilikuwa ni kitanda mpaka pale alipopata uwezo na kwenda kuchonga kitanda cha saizi yake.

“Ilikuwa nikilala lazima nikunje miguu, naumia! Nikaamua kwenda Keko pale walinitengenezea kitanda cha saizi yangu futi 7 kwa 6 nikilala natosha kabisa na upande wa godoro niliweka oda kiwandani nikapata,” alisema.

Akizungumzia nyumba anayoishi, Julius alisema bado hajajenga ila anapata matukio mengi ya kujigonga kichwa anapoingia kwenye nyumba nyingi zenye milango mifupi.

Kuhusu marafiki na uhusiano, alisema ana marafiki wengi wa rika lake na waliomzidi, japo bado anapambana na changamoto katika masuala ya uhusiano wa kimapenzi.

“Niliwahi kuwa kwenye uhusiano na watu wanne lakini kutokana na changamoto ya maisha nipo katika kutengeneza maisha yangu kwanza. Uhusiano bila hela hauendi, nitafikiria kuoa hapo baadaye,” alisema.

Alipoulizwa sababu ya kufikia maamuzi hayo alisema:

“Ni changamoto ninazokutana nazo. Namna nilivyo wanawake ninaokuwa nao tunashindana kwa ajili ya wivu, ninaishi kila siku kuwaaminisha kwamba wanawake ninaoongozona nao ni marafiki tu, kwa sababu hiyo ya wivu, nikaamua kukaa pembeni.

Uimara wa afya

Kutokana na hali yake, Julius alisema tangu akiwa na umri wa miaka 18 amewahi kuugua mara moja malaria na homa ya matumbo pekee.

Aidha, miaka saba iliyopita alipima wingi wa damu tangu wakati huo hajafuatilia kujua afya yake.

“Tangu nimeanza kujitambua nikiwa na miaka 18 mpaka sasa, sijawahi kuumwa hadi nikalazwa hospitali. Sina maumivu yoyote ninayoyasikia mwilini na hata katika kutembea sihisi uzito wowote; nipo kawaida kama vile mtu mwembamba anavyohisi. Ukiniona natembea taratibu nimetaka kutembea hivyo,” alisema.

Urefu kwa mujibu wa wataalamu
Daktari bingwa wa mifupa kutoka Taasisi ya Mifupa MOI, Kennedy Nchimbi alisema mtu kuwa mrefu siyo tatizo, ni maumbile tu na kwamba ni sawa na mtu kuwa mfupi sana.

“Wengi wanakuwa warefu kutokana na vichocheo, yaani homoni ambayo ina mambo mengi, lakini wengine wanakuwa hivyo na hawapati shida yoyote ingawaje wengine wanapata shinikizo la damu, kisukari, uvimbe kwenye ubongo na matatizo mengineyo, alisema na kuongeza: “Kwa mfano kuna mwingine ukimwangalia unajua huyu anaweza kuwa na shida fulani lakini ukimpima ndiyo unafahamu. Hivyo ni vema kufanya vipimo mapema ili kama ana shida yoyote anaitambua mapema na kufanya matibabu.”

Vyakula
kilo na chapati nane vikiambatana na matunda mengi mchanganyiko.

Mchana kwake ni ugali wa dona na kitoweo cha samaki au dagaa, chakula anachosema ndicho kimemkuza.

“Usiku siku zote ule chakula cha kutosha, sisi Wasukuma tumezoea kupika ugali mzito, lakini mara nyingi nakula wali robo tatu au kila moja unatosha nakula peke yangu,” alisema.

Licha ya hayo, alitaja changamoto kubwa anayokumbana nayo kuwa ni usafiri.

Kutokana na umbo lake, Julius anasema hawezi kutumia usafiri wa pikipiki na hata kwenye daladala humuwia ugumu kutokana na urefu alionao na mpangilio wa viti hauendani na hata akisimama, bado hulazimika kujipinda.
 
Sasa mbona kama jamaa yupo Tanzania na sio Marekani?
 
Jamaa nimemcheki kwenye video moja mtandaoni . Ni mrefu Ile hataaaari. Ngoja tupakue tu insert humu soon.
 
Back
Top Bottom