SEHEMU YA 33:
Fenicha zilizokuwa hapo sebuleni zilihitaji sana kufanyiwa ukarabati. Nilimshangaa sana Mustafa kumiliki gari zuri na kupanga katika nyumba nzuri lakini ameshindwa hata kumnunulia mama yake fenicha mpya. Wanaume wengine wa ajabu sana.
SASA ENDELEA…
Sasa mmepanga kuoana lini?” mama mkwe akaniuliza.
“Hatujapanga siku, nimemleta kwanza muonane mjuane,” Mustafa akamjibu.
“Tumeshaonana, tumeshajuana na tutajuana zaidi, sasa swali linakuja mtaoana lini?”
Mama alikuwa mswahili kweli.
“Ndiyo tuko kwenye mipango,” Mustafa akamjibu.
“Sikiliza Mustafa, wewe ni mwanangu na mimi ni mama yako. Kama umeshapata mchumba ambaye umempenda na yeye amekupenda, nataka muharakishe kuoana. Msiendelee kuishi hivyohivyo ni haramu.”
“Mpaka nimemleta hapa ujue kuwa mambo yamekaribia. Usifikiri kwamba tunaishi hivihivi, tumepanga kuoana na tutaoana.”
“Inshaallah. Na wewe sema inshaallah.” mama mkwe akamwambia mwanaye.
“Inshaallah,” Mustafa akamfuatisha mama yake aliyeonekana kuwa mtu wa dini sana.
“Kila jambo jema linaongozwa na Mungu, lazima useme inshaallah.”
“Inshaallah,” na mimi nikatia mkazo.
“Japokuwa nimekuwa mzee lakini nitafurahi sana kama mtaharakisha kuoana na nawaombea Mungu awe nanyi katika mipango yenu.”
”Twashukuru mama, asante,” nikamwambia.
Mustafa mwenyewe alikuwa akitabasamu tu. Baada ya mazungumzo marefu na mama mkwe tulimuaga.
“Mimi nilijua mtalala hapa,” mama mkwe akauliza.
“Tutalalaje hapa mama, si unajua kazi zetu,” Mustafa akamwambia.
“Kazi zenu zina nini?”
“Yaani tukilala huku kazi zetu zitaharibika.”
“Wewe kila siku ni kazi tu, huna siku unayosema nikalale kwa mama. Kazi mpaka lini mwanangu?”
“Nitatafuta siku mama, nitakuja kulala. Usijali.”
Tukaondoka kurudi Dar. Mustafa alikuwa amefurahi kwa sababu mama yake alikuwa amempa baraka zote za ndoa yetu.
“Sitamuarifu tena, siku tukienda tena ninamwambia tumeshafunga ndoa,” Mustafa akaniambia.
“Kwa hiyo tutaoana peke yetu?”
“Watakuwepo ndugu na jamaa.”
“Lakini usisahau nilivyokwambia.”
“Vipi?”
“Tuoane hivyohivyo kimyakimya, sherehe tutafanya baadaye.”
“Kwa nini hupendi tuchanganye na sherehe pamoja?”
“Tutachelewa kuoana, mambo yatakuwa mengi. Tuoane kwanza halafu ndiyo tupange sherehe.”
“Sawa.”
Ingawa Mustafa alinikubalia, hakuelewa maana yangu hasa ya kutaka tufanye sherehe hizo baadaye na pia kutaka ndoa yetu ifanyike kimyakimya.
Tayari nilikuwa mke wa mtu na sikuwa nimeachika hivyo sikutaka ijulikane kuwa ninaolewa tena, ndiyo sababu nikataka ndoa hiyo ifanyike kimyakimya.
Na pia akili yangu ya kutaka sherehe ifanyike baadaye ni kuwa atakaponioa suala la sherehe nitalipotezea mbali. Hatutaifanya tena kwani sherehe itahusisha watu wengi, huenda wakawepo wanaonijua.
Kutoka siku ile nikawa namuhimiza Mustafa kuhusu suala la ndoa kwa vile Musa alikuwa bado yuko Burundi.
“Unasikia Mustafa, tuharakishe kufunga ndoa kwanza, ndoa haina gharama ni kupanga siku tu. Baada ya hapo ndiyo tutapanga mambo mengine, nilikuw
a nikimwambia Mustafa.
Siku moja Mustafa akanipa nusu ya mahari yangu shilingi milioni moja akaniambia kesho yake ndiyo tutaoana. Nilikwenda kuziweka benki zile pesa.
Kwa vile nyumbani kwangu kulikuwa na mlinzi, katika kipindi hicho nilikuwa nalala kwa Mustafa. Mlinzi nilikuwa nampa posho ndogondogo ili anitunzie siri.
Kwa hiyo ilikuwa rahisi kukamilisha mipango ya ndoa yetu. Ile siku ambayo Mustafa alipanga kunioa nilikwenda saluni asubuhi kutengenezwa nywele na kupambwa kisha nikarudi.
Niliporudi Mustafa akaja na shehe na mashahidi wawili.
Wakaniuliza jina langu. Nilipowaambia wakaniuliza walipo wazazi wangu.
“Wazazi wangu wameshakufa,” nikawajibu.
“Wazazi wako wote wawili wamekufa?” shehe akaniuliza tena ili apate uhakika.
“Baba na mama wameshakufa.”
“Huna ndugu wengine kama vile kaka?”
“Nilizaliwa peke yangu.”
“Sasa walii wako atakuwa nani?”
“Walii ni nani?” nikamuuliza.
“Walii ni baba atakayekutolea idhini nikuozeshe.”
“Nitajitolea idhini mwenyewe.”
“Kwani ulishawahi kuolewa chuo cha kwanza?”
Nikatikisa kichwa haraka.
“Hapana sijawahi kuolewa.”
“Itabidi upate walii. Huwezi kujiidhinisha mwenyewe.”
“Sasa nitampata wapi mimi.”
“Basi mimi nitakuwa walii wako kama utanikubali na pia ndiye nitakayewaozesha. Wewe utakuwa kama mwanangu.”
“Sawa.”
Shehe akamtazama Mustafa.
“Mimi nitakuwa walii wake wa kumsimamia, ndoa ni lazima walii. Halafu mimi nitawaozesha,” akamwambia.
“Sawa,” Mustafa akamjibu.
Baada ya hapo shehe akaniambia kuwa kutoka muda ule ninatakiwa kukaa chumbani kama mwari na nivae nguo za sitara na nijitande mtandio kama biharusi kwani saa chache baadaye atatufungisha ndoa.
Niliambiwa kuwa ndoa hiyo itafungwa msikitini lakini mimi nitabaki nyumbani. Baada ya ndoa ndiyo Mustafa angekuja kunipa mkono.
Ilikuwa kweli. Ilipofika saa mbili usiku ndoa ikafanyika. Nyumbani nilikuwa mimi na ndugu wachache wa Mustafa waliokuwa wakiishi palepale