Simulizi ya kweli: Niliolewa na Jini bila kutarajia

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,443
Ilikuwa kwenye mida ya saa mbili usiku wakati tumekaaa kwaajili ya chakula cha usiku.
Wakati nakula simu yangu ikaita kuangalia mpigaji ni mpenzi wangu Sam ila nikashindwa kunyanyuka kwenda kupokea kwani mama alikuwa ananiangalia sana ikabidi nibonyeze kitufye cha kimya (silence).

Mama kumbe alisikia wakati inaita akauliza,

"Nani anakupigia wakati wa kula?"

"Hakuna mtu mama, ni alarm tu"

"Unadhani sijasikia wakati inaita? Umeanza uongo eeh!!"

"Hapana mama ni Sam"

"Nilijua tu, anakupigia wakati wa kula amekununulia hiyo simu? Anaijua bei yake?"

Ikabidi nikae kimya, mama yangu alikuwa anamchukia sana Sam. Hakupenda kabisa mahusiano ya mimi na Sam ingawa tulipendana sana.

Tulipomaliza kula tulikuwa tumekaa sebleni, nikatamani kuinuka kwenda chumbani nikazungumze kidogo na Sam na kumwambia kuwa muda aliokuwa anapiga nilikuwa nakula.

Nikawa nainuka, mama akaanza kuongea kabla hata sijaanza kutembea.

"Unaenda wapi Sabrina?"

"Naenda chumbani mara moja mama"

"Kuongea na simu eeh!! Amekupa nini huyo Sam jamani? Yani unashindwa kukaa hapa kuzungumza na mama yako na chakula kitulie, wewe macho juu juu kukimbilia ndani kuongea na Sam. Amekuwa mzazi wako huyo? Sipendi hiyo tabia, haya kaa tuzungumze ya maana hapa"

Ikabidi nikae ila mawazo yangu yote yalikuwa ni kwa Sam tu hata maneno ambayo mama alizungumza sikumuelewa hata kidogo, nikaona anapiga kelele tu.

Nadhani pale aliyekuwa anamsikiliza ni dada yangu Penina tu maana ndio waliokuwa wakijibishana. Mama akaniomba simu yangu na kupigia ndugu zake, akaongea wee hadi muda wa maongezi ulipokata ndio akanirudishia. Nikabakiwa na ujumbe mfupi tu bila ya muda wa maongezi.

Mama aliponyanyuka nami nikanyanyuka kuelekea chumbani, kisha nikamtumia ujumbe mfupi Sam kuwa anipigia. Naye hakusita kunipigia ila alinipa lawama mwanzo mwisho.

"Sabrina una dharau sana, yani simu yangu hupokei. Nangoja kidogo kupiga namba inatumika yani kuna watu unawaona wanathamani sana kushinda mimi. Poa tu Sabrina"

"Jamani Sam mpenzi wangu, tafadhari nisamehe"

"Umefanya makusudi wewe, poa tu mi nalala saivi"

Halafu akakata simu, nikajisikia vibaya sana ikabidi nimtumie ujumbe wa kumuomba msamaha ila Sam hakupiga wala kujibu ujumbe wangu.

Sikuweza kumwambia Sam kama mama yangu anamchukia kwani nilijua wazi kuwa akijua tu lazima atajisikha vibaya ukizingatia kwao mama yake ananipenda sana mimi.

Asubuhi na mapema nikapata ujumbe toka kwa Sam.

"Yani wewe Sabrina una dharau sana, sijui kwavile umejua nakupenda sana. Yani umeshindwa hata kunipigia simu upooze mawazo yangu umekazana na ujumbe tu!! Najua muda wote wa maongezi umemaliza kwa watu wako ila poa tu. Mimi nitaendelea kukupenda Sabrina"

Nikaamua kuamka na kwenda kununua vocha ili nipate kuzungumza na Sam.

Ila maduka yalikuwa bado hayajafunguliwa, nikaamua kuanza kufanya kazi mbalimbali za pale nyumbani ili niwahi kumaliza na niweze kwenda kwa Sam kwani nililuwa nimemkumbuka na pia nilitaka nikamweleweshe ya jana.

Baada ya kazi nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea rafiki yangu Suzy, mama hakuwa na pingamizi akaniruhusu niende nami nikaenda moja kwa moja kwa Sam ila sikumkuta na mlango wake ulikuwa na kufuri.

Ikabidi niende duka la karibu kununua vocha kisha nikampigia ila hakupokea nikajua tu kisirani kimempanda.

Nikaamua kuondoka na kwenda kweli kwa kina Suzy ili badae nipate kurudi tena kumuangalia.

Nilikaa sana kwa kina Suzy ila sikumueleza Suzy jambo lolote lile kuhusu Sam, badae nikaaga na kwenda tena kwa Sam nikawa namngoja kuwa pengine ameenda kazini ila ilikuwa ni mwisho wa wiki ndiomana nilijiamini na kwenda.

Nilimngoja sana Sam bila ya kutokea, nilikata tamaa na moyo kuniuma sana kuwa kwanini Sam amenifanyia vile kwa kosa dogo kiasi kile.

Nikajaribu kuwauliza na majirani ambao walisema kuwa Sam ameondoka asubuhi sana, nikajiuliza kuwa labda ameenda kwao ila kwanini asipokee simu? Nikaona kuwa Sam ananifanyia kusudi, hisia mbaya zikanitawala kuwa Sam atakuwa kwa mwanamke mwingine tu hapo roho ikaniuma sana.

Muda ulizidi kwenda, ikabidi nirudi nyumbani.

Nilifika nyumbani kwenye mida ya saa tatu usiku, nikamkuta mama na dada wakifanya maongezi ya hapa na pale.

Nikawasalimia na kwenda kuoga kisha kula chakula.

Dada akaanza kuzungumza,
"Halafu wewe Sabrina, kupenda kwako huko kutembea usiku usiku ipo siku utakumbana na majini huko njiani"

Nikashtuka sana na kumuuliza dada,
"Majini? Una maana gani dada?"

"Usiku ni mida ya majini, yakikukumba huko usituletee balaa hapa"

"Kwani majini yakoje?"

"Ukikutana nayo lazima nywele zisisimke, halafu ni marefu sana mara nyingine huwezi ona mwisho wa urefu wao"

"Mbona unanitisha dada?"

"Sikutishi ila huo ndio ukweli, unatakiwa kuwa makini sana. Majini hayana masikhara, likikuvaa ndio limekuvaa utakula nalo, kulala nalo na kuamka nalo bila ya kutarajia"

Nikaanza kuingiwa na uoga, mama nae akaanza kuchangia hoja zake.

"Unakumbuka kule makaburini wakati wanamzika yule dada mwenye mashetani kilichotokea?"

Dada akajibu,

"Ndio nakumbuka mama, yani majini hayataki mchezo"

Ikabidi niulize tena,

"Kwani majini yanafanana na kitu gani"

"Majini yanatisha mdogo wangu usiombe ukutane nayo njiani unaweza usilale siku mbili unaweweseka tu."

"Inamaana yanaweza kutokea wakati mtu amelala?"

"Ndio, unaweza ukashangaa umelala na jini pembeni yako"

Niliogopa sana na kuwaza kwanini nimesikiliza habari za majini usiku.

Mama akaongezea kitu kingine ambacho kilifanya niende chumbani kumtafuta Sam.

"Ila leo umenifurahisha kitu kimoja, kwenda kweli kwa Suzy maana huyo Sam wako amekuwa hapa siku nzima kukungoja"

Nikagundua kuwa, wakati mimi namngoja Sam kule kwake kumbe na yeye alikuwa kwetu kuningoja ila kwanini hakutaka kupokea simu yangu.

Nikaenda zangu chumbani kwa lengo la kumpigia tena Sam simu.

Ila nikasita kwani nikaona Sam nae ananifanyia kusudi, kama kweli alikuwa kwetu kuningoja kitu gani kimemfanya asipokee simu yangu. Mara dada akaniita na kufanya yale mawazo yangu juu ya Sam yakatike.

"Vipi Sabrina ndio unataka kulala muda huu?"

"Ndio dada, nataka kulala"

"Njoo mara moja, kuna kitu nataka unisaidie huku chumbani kwangu"

Nikatoka na kufatana na dada hadi chumbani kwake.

"Kuna kitu kinanichanganya hapa kwenye computer yangu, naomba uniondolee hii picha"

Mimi nikaitazama ile picha, ilikuwa ni ya mwanaume mzuri sana. Nikamuuliza dada kuwa kwanini anataka kuifuta,

"Kwanini uifute dada? Mbona picha yenyewe ni nzuri?"

"Hata sielewi nimeidownload vipi hiyo picha hadi imekaa hapo, nitolee bhana mipicha mingine inaweza kuwa ya majini"

"Mbona unapenda sana story za majini dada?"

"Yapo na ndiomana nayaongelea, usishangae siku ukitokewa na jini"

"Basi yaishe, mi sitaki tena hizo habari nisije kushindwa kulala bure"

Nikafanya ninachojua kuifuta ile picha kisha nikamuaga dada usiku mwema na kuondoka.

Nikarudi chumbani na kuendelea kuwaza kuhusu Sam wangu. Wakati nikiwaza juu ya Sam, wazo la majini likanijia tena kichwani nikajikuta naanza kuogopa chumbani halafu ile picha ambayo dada aliniomba kuwa nimsaidie kufuta ikawa inatembea kichwani mwangu.

Niliona chumba kimekuwa kikubwa sana, nilipokaa kitandani nilihisi kama vile kuna mtu pembeni yangu nikaanza kuogopa zaidi huku nikijilaumu kuwa kwanini nimesikiliza stori za kutisha muda wa kulala. Nikachukua tena simu na kuamua kumpigia Sam ili kujiliwaza kidogo ila kabla sijapiga nikapitiwa na usingizi.

Mwanaume mzuri sana na mtanashati alikuwa mbele yangu, asili yake kama mwarabu hivi au muhindi. Alikuwa anatabasamu na kusogea taratibu kuja mahali ambako mimi nipo. Nilikuwa namwangalia kwa jicho la mshangao tu. Alipofika karibu yangu, akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 02

Akanivuta mkono kisha akatoa kitu cha ajabu kilichofanya nishtuke.

Nikajikuta jasho jingi likinitoka pale kitandani, nikawa najiuliza kuwa ni ndoto ya aina gani na inamaanisha kitu gani? Je huyo mwanaume mzuri sana kushinda Sam wangu ni nani?

Hapo ndio nikakumbuka kuwa natakiwa kumpigia Sam simu.

Nikaangalia simu yangu na kuichukua kisha nikaibonyeza, nikakuta simu ambazo hazijapokelewa kumi (10 missed call), kuangalia zote ni kutoka kwa Sam na ujumbe mfupi tano (5 messages).

Kila ujumbe ulikuwa ni wa lawama tu kutoka kwa Sam, nikaona haya majanga sasa.
Nikabonyeza simu na kuanza kupiga nikasikia,
"Salio lako halitoshi kupiga simu, tafadhari ongeza........."

Nikaishusha ile simu na kuikata, kuangalia kweli nimebakiwa na sifuri nikaanza kujiuliza kuwa nimeitumiaje ndipo nikakumbuka kuwa nilinunua salio na kusahau kujiunga na huduma za bure na wakati narudi nyumbani nilimpigia Suzy na kuongea nae sana tu nikijua nimejiunga kumbe sikujiunga, vocha yangu yote ya elfu mbili imekwenda bure bure bila hata ya faida sikujua cha kufanya kwa wakati huo.

Nikatamani niende chumbani kwa mama nikachukue simu yake na kuhamishia salio lake kwangu kama ana salio. Nikainuka pale kitandani na kusogelea mlango kisha nikafungua, wazo la stori za majini likanijia tena kichwani na kujikuta nikiubamiza ule mlango kwa kuufunga na kurudi tena kitandani, nikajiuliza kuwa kwanini ile stori ya majini imenikaa sana kichwani mwangu? Nikaanza tena kufikiria ile ndoto kuwa ilikuwa na maana gani kwangu.

Sikuweza kulala tena kwa uoga na pia bado nilikuwa na mawazo juu ya Sam.

Asubuhi yake, mimi ndio nilikuwa wa kwanza tena kuamka, nikafanya usafi na kazi za hapa na pale nyumbani huku nikingoja pakuche vizuri nikanunue vocha ya kuweza kumpigia Sam.
Nilipomaliza usafi nilirudi tena chumbani, nikajilaza kitandani na usingizi ukanichukua hapohapo.

Yule mkaka mtanashati akaanza kunionyesha mali zake, zilikuwa nyingi sana. Kumbe yule mkaka alikuwa tajiri, akanionyesha magari ya aina nne halafu akaniambia kuwa nichague moja liwe langu naye atanipa lotelote, nikawa natabasamu kwani magari yalikuwa mazuri sana na ndoto zangu siku zote ni kuwa na gari ila gafla nikakumbuka kuwa nina Sam wangu ambaye hawezi kunipa vyote vile ila anaweza kunipa mapenzi ya dhati, nikajikuta nikishtuka na kupiga kelele.

"Saaaaaaaaaammmmmm....."

Mama akaja chumbani na kusema.

"Wee Sabrina wewe, usiniletee uchuro nyumbani kwangu. Yani wewe kuamka tu na kumtaja Sam! Amekuwa Mungu huyo Sam?"

"Hapana mama, ila nimeota vibaya"

Jasho nalo lilikuwa lanitoka.

"Umeota vibaya kivipi? Umeota Sam anachinjwa au?"

"Hapana mama."

"Haya inuka hapo, kuna mboga ya kukata kata huku"

Nikainuka tena pale kitandani na kumfata mama jikoni, kisha kukiendea kisu na kukata kata ile mboga.
Mawazo yalikuwa ni juu ya ile ndoto na yale magari, kisha nikakumbuka tena kuwa nilitakiwa kununua vocha na kumpigia Sam.

Nilikata mboga haraka haraka na kuibandika jikoni kisha nikajitanda vizuri ili niende dukani kwanza.
Kabla sijatoka mama akauliza,

"Unaenda wapi Sabrina?"

"Naenda dukani mama."

"Kufanya nini?"

"Kununua vocha mama"

"Ili umpigie Sam eeh!! Sijui huyo mwanaume amekupa nini mwanangu unakuwa kama chizi"
Sikutaka kumsikiliza zaidi kwani nilijua kuwa lazima atanizuia tu.

Nilinunua vocha na kurudi nyumbani. Nikamkuta mama sebleni,
"Huna adabu mwanangu Sabrina, yani umeona vocha ya maana kuliko maneno yangu? Vocha ambayo pesa nakupa mimi!!"

Nilibaki kumuangalia tu mama na maneno yake kwani nilijua yote sababu hataki niwasiliane na Sam.
"Haya lete hiyo vocha haraka"

Nilimpa ile vocha mama kwa shingo upande kwani moyo uliniuma sana, nikatamani hata kuwa na maisha ya kwangu. Nikatamani kutoa machozi mbele yake ila nikajizuia kwa kufumba macho ili mama asinione mzembe, ingawa na kujizuia kule bado machozi yalipenya na kudondoka mashavuni mwangu.
"Kaone kalivyo kajinga, eti kanamlilia mwanaume. Hebu niondolee uchizi wako mbele yangu haraka"

Nikaondoka na kukimbilia chumbani, huko nililia nitakavyo katika kupooza uchungu wangu. Nilipotazama tena simu nikaona ujumbe wa Sam tena wa kutosha, sikuweza kujibu hata jumbe moja kwa kukosa vocha. Nikajikuta nikiulaumu mtandao ninaotumia pia kwa kushindwa kutuma tafadhari nipigie. Nilizidi kutokwa na machozi tu mule ndani.

Wakati nalia nikasikia mtu akigonga mlango wa chumba changu, nikashtuka na kujiuliza ni nani maana dada na mama hawanaga hodi, huwa wanaingia tu chumbani.

Nikamuitikia kuwa aingie ndani, huku nikimaliza kujikausha machozi yangu. Kumbe alikuwa ni rafiki yangu mpenzi Lucy, nilifurahi kumuona nikainuka pale kitandani na kumkumbatia, nikamkaribisha vizuri sana.

Kumbe Lucy naye alishangazwa na hali aliyonikuta nayo,
"Nimekungoja sana hapo sebleni kwenu ndipo mama yako aliposema nikufate chumbani eti umechukia sababu ya mwanaume. Mmh! Mwanaume gani tena huyo Sabrina?"

Nikamueleza kwa kifupi kuhusu Sam kwani Lucy alikuwa hajui chochote kuhusu Sam.
"Inamaana kushindwa kuwasiliana nae ndio kunakuliza jamani shoga yangu? Chukua basi simu yangu uwasiliane nae maana ina muda wa kutosha"

Nikachukua simu ya Lucy na kumpigia simu ambapo alishangaa kuona namba ngeni.
"Mbona namba mpya hii, ni ya nani?"

"Ni ya rafiki yangu mmoja anaitwa Lucy ila wewe humjui, ipo siku utamjua"
Wakati nazungumza na Sam, Lucy nae akaniomba simu ili amsalimie shemeji yake huyo, nami nikamkabidhi.

Baada ya salamu tukazungumza na Sam kisha tukapatana tena na kusameheana kwa yote yaliyopita halafu Sam akanitumia vocha ili niache kumpigia kwa namba mpya.

Kilichobaki ilikuwa ni stori na vicheko baina yangu na Lucy.

"Mmh shemeji ana sauti ya kuvutia huyo, yaonyesha atakuwa handsome sana"

"Mmh Lucy ushaanza maneno yako, hukui wewe?"

"Kwani nikimsifia shem wangu kuna ubaya Sabrina?"

"Hakuna ubaya"

"Ila ningependa kumfahamu zaidi, natumaini ipo siku utanikutanisha nae"

Niliongea mengi sana na Lucy ila alikazana sana kumsifia Sam hadi akawa ananipa mashaka ila sikuyatilia maanani sana.

Lucy alipoaga, nilimsindikiza akaondoka.

Jioni ilipoingia kama kawaida ya siku hizi za karibuni, wakaanza tena stori zao za majini na aliyeanzisha alikuwa ni dada yangu Penina.

"Jamani Posta kuna mambo, yani mtu niliyepishana nae ni dhahiri kabisa alikuwa jini maana nywele zote zilinisimama"

Mama nae akadakia,
"Ulikuwa hujui mwanangu? Yani Posta na Kariakoo hakuwezi kukosa majini kule, unadhani unaopishana nao huko wote ni watu basi! Nusu yao ni majini"

Nikaanza kuogopa tena kwa yale maneno na hata sikujua kwanini mimi yaliniogopesha wakati wao walioyaongea hawakuogopa.

"Hivi jamani, kwanini ikifika usiku ndio mnaanza hizo stori za majini? Hakuna stori zingine?"

Dada akaanza kunicheka kuwa kwanini naogopa wakati ni kitu cha kawaida tu.
"Sasa wewe Sabrina unaogopa nini? Unadhani yatakutokea?"

"Naogopa tu jamani"

Mara mama akanitisha,
"Haya, huyo nyuma yako"

Nilipiga kelele na kurukaruka, huku wote wakiwa wananicheka.
"Hutakiwi kuogopa mwanangu, haya ni mambo ya kawaida na wengi yanawapata ndiomana tunayaongelea. Na ukitaka kutokuogopa kitu basi wewe kizoee"

"Ndio kuzoea majini mama?"

"Hapana si kuzoea majini, ila stori hizi uzione kama kawaida na hautapata shida tena"

Wakaendelea kusimuliana mambo ya watu wanaofufuka na majini.
Ikabidi nimuulize dada kuhusu ile picha aliyoniomba niifute jana yake.

"Dada, nakumbuka uliniambia kuwa majini ni mabaya na sura zao zina tisha. Mbona yule mkaka mzuri ulisema tufute picha yake kuwa huenda akawa jini?"

"Nilikuwa najisemea tu ila hata hivyo majini yanamtindo wa kubadilika kama kinyonga"
Mama akaingilia mazungumzo yetu.

"Kumbe na wewe Sabrina unawajua wakaka wazuri? Mbona ukampenda Sam basi?" Dada akanisaidia kujibu,"Ila Sam sio mbaya jamani mama, humpendi tu sababu ya kipato ila usisingizie uzuri"

Nikawaacha na kwenda chumbani kwangu. Nikaenda kuoga kisha kujiandaa kulala. Usiku wa leo ulikuwa na uoga kiasi kwangu na furaha pia kwani vocha nilikuwa nayo na Sam nilishapatana naye.

Nilipokuwa tu kitandani nikampigia Sam simu ili kupotezea yale mawazo ya stori ambazo mama na dada walikuwa wakisimuliana. Niliongea sana na Sam kwenye simu hadi saa saba usiku kisha nikapitiwa na usingizi huku simu ikiwa sikioni.

Nilikuwa ufukweni (beach) na Sam tukifurahia upepo na kuchezea maji. Sam alivaa nguo nyeupe na mimi nilivaa gauni la pinki, tulifanya mambo mengi sana ambayo wapendanao huwa wanafanya.

Tukaanza mchezo wa kufunikana macho kwa nyuma na wakati huo Sam alikuwa nyuma yangu na mikono yake imepita juu ya mabega yangu kisha viganja vyake vilifunika macho yangu, akaanza kunitembeza na kunipeleka nisipopajua.

Kufika mbele akaniuliza,
"Nikufumbue macho nisikufumbue?"

Nami nikamjibu kwa sauti ya taratibu tena ile ya kudeka,
"Nifumbue bwana"

Basi Sam akaachia vile viganja vya mikono yake nami nikapata kuona kilichopo mbele yangu, nikamuona yule mkaka wa kwenye ndoto akiwa mbele yangu na alivaa nguo nyeupe tupu kuanzia kiatu, suruali hadi shati.

Nikajikuta nikitetemeka ila yeye alikuwa akitabasamu, nikaangalia nyuma yangu kama yupo Sam ila hakuwepo na sikujua ameelekea wapi, nikaanza kukimbia huku yule mkaka akinifata nyuma alipokaribia kunishika nikashtuka kumbe nilikuwa naota.

Jasho jingi lilinitoka, kutazama nje kulikuwa kumekucha kabisa yani kama sio saa mbili basi ni saa tatu.
Kabla sijafanya chochote, simu yangu ikawa inaita kuangalia ni Sam anapiga basi nikaipokea, baada ya salamu nikamsikia.

"Uwahi kujiandaa mpenzi ili badae twende beach, sawa Sabrina. Halafu uvae lile gauni lako la pinki"
Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 03

Niliendelea kuweka ile simu sikioni bila ya kujua cha kujibu.

Upande wa pili nao ulishangazwa na kimya changu na kuuliza,
"Vipi mpenzi mbona kimya? Hujanielewa au?"

Nikajikaza kumjibu kwa sauti ya upole,
"Ndio sijakuelewa"

"Nimekwambia kuwa uwahi kujiandaa kwaajili ya ile safari yetu ya beach na uvae gauni lako lile la pinki. Bado hujaelewa?"

Nikaishusha ile simu taratibu, sauti ya mama ikanishtua ambapo alifungua mlango bila ya hodi kama kawaida yake na kuanza kuongea.

"Yani mtoto wa kike ndio unaamka saa nne hii, halafu kitu cha kwanza ni kukumbuka hilo pepo lako chafu la simu"

Nikajikuta nikiiachia ile simu kwani nilishangaa kuwa muda ule ni saa nne sema kwa bahati ilikuwa ni kwenye kitanda ndio ikaangukia hapo.

"Mbona umetoa macho tu hata hunijibu wakati simu umeongea nayo?"
"Jamani mama hata salamu? Shikamoo."

"Haina umuhimu saa nne hii, kazi zote umeniachia mamako kama vile sikuzaa jamani!! Haya inuka hapo kitandani uje huku"

Halafu akatoka, nikamshangaa mama kuongea vile wakati si kawaida yangu kulala sana mpaka kupitiliza kiasi kile. Na hata kama nikilala vile basi ni kwamba kuna muda niliamka na kufanya kazi kisha kurudi tena kulala ila siku hiyo nilipitiliza hadi kujishtukia.

Nikajitoa chumbani na kwenda jikoni kumuomba mama msamaha kwa kuchelewa kuamka.

"Unaona kama nakukera mwanangu ila mimi nakufundisha hata utakapoolewa uwahi kuamka, hakuna mwanaume anayependa kuishi na mke mvivu. Yani hadi saa nne mwanamke hajaamka, hajafanya usafi wala kuandaa chai. Nakwambia kwa mtindo huo mwanaume lazima akuache, mwanamke mwingine anamuachia kazi zote msichana wa kazi hadi kazi za mumewe, mwisho wa siku mume anachukua msichana wa kazi badili ya mke. Nakufundisha kazi mwanangu, sijui kama unanielewa!"

"Nakuelewa vizuri sana mama yangu"

"Itabidi nikupe darasa kabisa na kama ukilifata basi kuachika usahau kabisa na kama huyo mume akikuacha basi atakuwa na hila ya kwapa kunuka bila kidonda"

Kwakweli mama yangu alikuwa ni muongeaji sana hadi kipindi wakati baba yupo alikuwa anamuita mama kasuku na tulikuwa tunacheka sana.

"Sasa mama utanipa lini hilo darasa? Nipe leo basi"

"Kwani unataka kuolewa? Hebu nitolee uchuro wako mie nionekane nina uchu sana wa mahari yako."
"Kwani mama mi sifai kuolewa?"

"Nikuoze kwa kale kajamaa kale!! Katanipa nini mimi? Hebu nenda kwanza kaoge huko"
Nikajiinukia kwa unyonge na kwenda kuoga.

Niliporudi chumbani nilikuta simu yangu inaita na mpigaji alikuwa ni Sam, nikaipokea ile simu.
"Mbona unadharau hivyo Sabrina? Kweli wewe wa kutokuijibu simu yangu jamani!"

"Nisamehe mpenzi wangu"

"Ndio unachoweza kusema hicho, unakumbuka tulichopanga usiku wakati tunaongea kwenye simu?"

"Nimesahau Sam"

"Nakata simu halafu nakupa dakika kumi uwe umekumbuka, nitakupigia tena kunipa jibu"

Halafu Sam akaikata ile simu, nikajikuta nikianza kurudisha mawazo ya nyuma kichwani mwangu.
Nikakumbuka kuwa niliongea na Sam hadi usiku sana ila sikukumbuka tumeongelea kitu gani, mara kumbu kumbu za ndoto zikanijia hadi pale ambapo Sam aliponipigia simu ni hapo nilipojituliza akili na kujiuliza kuwa kuna mahusiano gani ya yule mwanaume wa kwenye ndoto zangu na Sam? Na kwanini Sam aniambie nivae gauni la pinki ambalo limetokea kwenye ndoto zangu?

Wakati natafakari hayo simu yangu ikaanza kuita, nilipoona kuwa ni Sam nikajua tu kuwa anayataka majibu yake. Nikapokea ile simu,

"Haya niambie ulichokumbuka"

"Kwakweli tuliyoyaongea usiku sikumbuki kabisa ila ninachokumbuka ni tulichoongea asubuhi"
"Ok, hiyo asubuhi nilisemaje?"

"Ulisema kuwa niwahi kujiandaa ili twende beach na nivae gauni langu la pinki"

Sawa sawa, kumbe kumbe kumbukumbu unayo. Sasa kwanini hukumbuki vya usiku? Na je ushajiandaa kwa safari?"

"Bado sijajiandaa"

"Kwanini unanifanyia hivyo Sabrina jamani? Unajua mambo mangapi nimeacha kwaajili yako? Mbona unadharau kiasi hicho?"

"Hapana Sam"

"Kwanini Hapana?"

"Kwanini uchague gauni la pinki? Na mbona umenishtukiza na hiyo safari wakati siku zote huwa nakwambia kwamba uniambie mapema? Unanionea tu Sam na yote sababu unapenda ubabe"

"Naomba uelewe Sabrina, kwanza kabisa hii safari si ya kushtukiza. Jana usiku tumejadili wote kwenye simu kuwa leo twende beach, halafu kuhusu swala la nguo ulilianzisha mwenyewe jana na ukasema kuwa mimi nivae shati nyeupe na ukaniuliza kuwa mimi ningependelea wewe uvae nguo ipi, wakati nakujibu ulikuwa umepitiwa na usingizi ndiomana nikakupigia muda ule kukuambia kuwa nimependelea uvae gauni la pinki. Haya kosa langu ni nini hapo?? Je tutaenda huko beach?" Nilibaki kimya nikijishangaa kuwa usiku nilikuwa nikijadili na Sam kitu cha namna ile, Sam alingoja jibu hadi akaamua kukata simu.

Nilitafakari mara mbili mbili na kujiuliza sana kuwa au sikuota chochote sema ni maruweruwe tu, ila kumbukumbu zinaniambia kuwa mambo yale nimeyaona kwenye ndoto kwahiyo sikuwa na jinsi zaidi ya kukataa ile safari.

Sam aliponipigia tena nikamwambia kuwa sitaenda basi aliongea maneno mengi ya hasira. Kwakweli Sam alichukizwa sana na maamuzi yangu ila nilifanya vile ili kuepusha kutokea kama kilichotokea kwenye ndoto.

Mama akaja kunifata tena chumbani na kunikuta nikiongea na simu huku nikimbembeleza Sam aweze kunielewa.

"Simu hizo simu mwanangu, sijui hata zinakusaidia nini? Toka useme unaenda kuoga hadi sasa jamani? Hujala wala hujafanya chochote cha maana. Kwakweli nakuhurumia mwanangu, haya njoo tule chakula tayari mamako nishapika na kukuandalia malkia wa nyumba hii"

Mama akatoka, kwakweli nilijisikia vibaya ila ikabidi nitoke kumfata mama pale mezani ili asiseme tena.

Wakati tunakula, sauti ya Sam ikawa inajirudia kichwani mwangu kuwa kwanini nimemkatalia ile safari.
Sauti ile ikarudia mara kwa mara hadi nikajikuta nagonga meza na kusema,
"Aaaaaaaarggghhhhhhh........"

Kumbe nilipiga kelele mi nilijua kuwa nimejisemea chini chini, mama akashtuka na kuniangalia kwa jicho kali, "Wee mwana wee umeanza kuwehuka?"

Nilibaki kumkodolea tu macho mama bila ya kusema chochote.

"Mamako nimepika chakula kizuri na kitamu ili malkia wa humu ndani ule ufurahi sasa unaniletea uchizi mezani. Unatatizo gani jamani mwanangu mzuri Sabrina?"

Nilitamani kumueleza mama ila nikajua kuwa kwa vyovyote vile lazima atazidi kumchukia Sam, ikabidi nimwambie kuwa sina tatizo. Ila kile chakula nilikuwa nakitazama tu na kuchezesha kijiko, mama alimaliza kula na kuniacha mwenyewe pale mezani. Badae nikaenda kukifunika jikoni, kisha nikarudi sebleni na kuweka picha za ngumi kwenye video na kuanza kuangalia.

Nikasikia simu yangu inaita, nikaenda kuichukua nikakuta ni Lucy ananipigia nikaenda kuongea nayo sebleni.

"Jamani Sabrina! Yani shem anakuomba mtoke out unamkatalia jamani! Kwani unafanya nini hapo kwenu?"

"Kwani wewe nani kakwambia?"

"Nimewasiliana na shem kaniambia, kwakweli ulichofanya sio kizuri shoga yangu."

"Fanya yako mengine hayakuhusu"
Halafu nikaikata ile simu hata nikajishangaa kwa kumchukia hadi Lucy.

Niliangalia Video ile ila bado haikunoga, moyo wangu ulikuwa unavutika kuwa ufukweni tu mambo mengine yote kwangu niliona kama ni kujisumbua tu.

Mama alikaa na mimi na tukaangalia wote ila bado haikunoga, hadi dada anarudi alinikuta palepale sebleni na sielewi chochote. Mara gafla kichwa kikaanza kuniuma, nikamwambia mama akaenda kuniletea dawa nikanywa kisha akaniambia kuwa nikapumzike kwanza ilikuwa kama mida ya saa kumi na mbili jioni.

Nilipofika tu kitandani usingizi ukanichukua hapohapo na kama kawaida ndoto za maruweruwe zikanianza tena. Nilikuwa mahali nimesimama na mbele yangu amesimama Sam huku akinilalamikia kuwa kwanini nimekaa kwenda nae.

"Najua Sabrina hunipendi ndiomana umekataa kutoka na mimi."
Na mimi nikamjibu,
"Hapana Sam nakupenda tena sana tu"

"Sabrina hunipendi, ila kuna mvulana mzuri na mtanashati wa kwenye ndoto zako ndio unayempenda. Najua yeye anaweza kukupa gari, nyumba na chochote cha gharama utakacho ila mimi sina uwezo huo Sabrina ndiomana hunipendi"

"Si kweli Sam nakupenda wewe"

"Ungenipenda mimi usingekataa kwenda beach na mimi Sabrina, usingekataa kutoka na mimi"
pembezoni mwa mazungumzo yetu akatokea yule kaka wa kwenye ndoto huku akitabasamu.

Nikashtuka gafla na kusema,
"Nakupenda sana Sam"

Kisha nikainuka pale kitandani, nikatoa gauni langu la pinki tena bila hata ya kufikiria mara mbili, nikavaa na viatu navyo nikavaa.

Kisha Nikatoka chumbani na kupita sebleni hakukuwa na mtu yeyote yule, wote walikuwa wameshalala kumbe ilikuwa ni usiku sana ila sikujali, nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 04


Nikaenda kufungua milango ili nitoke nje niende huko ufukweni. Nilikazana kufungua mlango wa nje bila ya kujari chochote na nikafanikiwa kutoka nje kumbe mama alisikia wakati nafungua milango, akatoka chumbani kuja kuangalia akaniona nikikazana kuongoza njia.

Mama hakujali kama alitoka na khanga moja ila alinikimbilia na kunishika mkono huku akianza kunirudisha nyumbani kwa nguvu ambapo nilikuwa nagoma.

"Jamani Sabrina mwanangu unaenda wapi?"

"Niache mama, naenda beach."

"Beach usiku huu mwanangu!! Nakuomba turudi nyumbani"

Nilikuwa nagoma kurudi, mama aliendelea kunivuta na dada Penina akaja kumsaidia mama ila kwavile nilipofika hapakuwa mbali sana na nyumba yetu, mama na dada walifanikiwa kunivuta na kunirudisha tena ndani kisha dada akafunga milango halafu mama akanipeleka sebleni na kunikalisha kwenye kochi.

"Mwanangu Sabrina jamani umechanganyikiwa?"

Nikawa namuangalia tu mama tena kwa macho ya hasira, dada naye akadakia.
"Hiyo beach ya usiku huu ukakutane na nani jamani mdogo wangu?"

Hapo sasa, usiku huu akutane na nani? Mbona unataka kutuletea majini wee mtoto, hujui kuwa ndio mida yao hii? Tena huko baharini ndio nyumbani kwao"

Wakati mama akisema hayo mimi nilijiinamia na kuanza kulia bila sababu tena nililia sana.
"Nadhani fahamu bado hazijamrudia huyu"

"Hivi kwani ilikuwaje mama?"

"Nadhani kaamshwa na zile ndoto za usiku za kutembeza watu, si unazijua zile ndoto. Mtu anaamka na kwenda asipopajua na wengi hupotelea huko, jamani mwanangu kidonda cha babako hapa bado hakijapona halafu wewe unataka kunipatia kidonda kingine. Nitakuwa mgeni wa nani mimi jamani!!"

Mama aliongea kwa uchungu hadi nikaacha kulia na kumtazama usoni.

Mama alikuwa ananiangalia kwa sura ya huruma na upole sana.

Kisha akainuka na kwenda kuchukua maji na kuninawisha uso, kisha akaniinua na kunipeleka dirishani, akafunua pazia na kuniambia.

"Angalia giza la nje mwanangu, ni giza totoro na je unajua ni muda gani saizi?"
Nikatikisa kichwa kwa kukataa kuwa sijui.

"Ni saa nane usiku mwanangu, mbona unataka kuniletea makubwa wewe!"

Tulirudi na kukaa tena kwenye kochi huku akili yangu ikianza kama kuwa sawa hivi.
"Itabidi niwe nalala na funguo siku hizi naona mwanangu Sabrina ameanza kupatwa na vitu vya ajabu, maana mchana ameshindwa kula na usiku huu anataka kutoka bila taarifa mmh sijui ni mambo gani haya?"

Dada akashauri kuwa turudi kulala na mengine tuyazungumze kesho.

Basi mama akanipeleka chumbani kwangu na kuhakikisha nimepanda kitandani ndio akatoka na kwenda chumbani kwake.

Sikuweza kulala kabisa wala kujielewa, nilikuwa najishangaa tu. Kila nikiwaza nakosa jibu kabisa, yule mkaka mtanashati alishaichanganya akili yangu na sikujua kwanini alipenda kunifata kwenye ndoto zangu.

Kulipokucha, mama alikuwa wa kwanza kuja chumbani kwangu kuniangalia na kuniuliza kuwa nimeamkaje, ila nilikuwa mzima wa afya na nilikuwa Sabrina wa kawaida na siku zote.Nilitoka na kuanza kufanya usafi ili mama atambue kwamba ninajielewa na wala hakuna tatizo tena kwangu.

Baada ya zile kazi mama akaanza kuzungumza na mimi kuhusu ndoto.

"Sikia nikwambie mwanangu, ndoto ni muunganiko wa mambo yote uliyoyafanya siku nzima, usiku ndio yanageuka na kuwa ndoto. Au mara nyingine ni mawazo unayoyawaza ndio hugeuka na kuwa ndoto"
Nikajifikiria inamaana mimi naota vitu ninavyoviwaza au.

Nikaamua kumuuliza mama,
"Inamaana mtu akiota ndoto ya kitu ambacho hajawahi fanya wala kuwaza inakuwa ni ndoto ya aina gani?"

"Mwanangu ndoto zingine hazitabiriki kabisa ila unachotakiwa kufanya ni kumuomba Mungu sana. Lakini mara nyingi ndoto huwa katika mtindo huo niliokueleza, kama vile wewe ulivyoamka usiku na kutaka kwenda beach inaonyesha hicho ni kitu ambacho ulikiongelea kabla"

Nikawa kimya kutafakari kauli ya mama kama ina ukweli wowote ndani yake.

Siku hii sikujishughulisha na simu kabisa nilikaa na kutafakari maisha yangu tu.

Ila ilipofika jioni nilichukua simu yangu kuangalia kama kuna mtu yeyote aliyenitafuta, nikaona hakuna ujumbe wala simu ambayo haikupokelewa.

Nikajiuliza kuwa inamaana Sam amechukia kiasi kwamba ameshindwa kunitumia hata ujumbe! Nikaamua kumtumia mimi mjumbe mfupi wa kumsalimia na ilionyesha kuwa umepokelewa ila hakukuwa na majibu kabisa, nikashangaa sana kwani tabia ya Sam imebadilika.

Kwa kawaida Sam hata nimkosee vipi hawezi kukaa kimya kunijibu hata salamu tu, nikaona lazima kuna tatizo hapa.

Muda huo nilikuwa chumbani na nikamsikia mama kapata ugeni wa rafiki yake pale sebleni, baada ya muda kidogo mama akaniita.

"Sabrina mwanangu, hebu njoo na huku uchangamshe akili"
Ikabidi nitoke nikakae pale sebleni na kumkuta mama Salome ambaye ni rafiki sana wa mama, nikamsalimia na kukaa. Yule mama akaendelea kuzungumza mazungumzo ambayo alikuwa anaongea na mama, ila mimi ndio nikawa mfano katika mazungumzo yake.

"Basi mtu mwenyewe yupo kama Sabrina, yani mwili wake hivyo hivyo. Akapandisha yale majini na kuanza kuropoka mambo ya pale"

Nikajikuta nikichukizwa na zile stori kwani sikupenda kusikiliza stori za majini karibia na usiku sababu zilinitisha wakati wa kulala, nikajaribu kuingizia mambo mengine kama vile kuwaulizia wakina Salome ila yule mama hakuacha kuelezea ile habari yake.

"Yani hali ilikuwa mbaya, kwakweli majini si ya kuchezea mama Penina"

"Sasa mkafanyeje?"

"Mwenzangu, si akataka tumtafutie marashi...."

Sikutaka hata kusikiliza zaidi, nikainuka na kurudi chumbani hadi pale niliposikia kuwa yule mama kaondoka.

Dada Penina aliporudi alikuja moja kwa moja chumbani kwangu.
"Kwani una tatizo gani mdogo wangu?"

Nilitamani kumueleza kuhusu zile ndoto ila nikasita.

"Sina tatizo dada"

"Basi njoo nikuonyeshe kitu"

Nikafatana na dada hadi chumbani kwake.

Akafungua mkoba wake na kunitolea maua mazuri sana na mdori mdogo mzuri,
"Umeona huyu mdori mdogo wangu na haya maua?"

Nikaitikia kwa kichwa.
"Kuna mtu kazini amenipa kama zawadi ila mimi nimeamua kukuletea wewe mdogo wangu, usiwe na mawazo sana. Unaweza kuweka hivi vitu mezani kwako na ukavifurahia"

Kisha nikaenda nae hadi chumbani kwangu, akanipangia yale maua na yule mdori kwenye meza ya pale chumbani kwangu.
"Umeona ilivyopendeza?"

Nikaitikia kwa tabasamu na kumshukuru dada kisha nikamkumbatia.
"Usijari mdogo wangu, sipendi kukuona na mawazo muda wote. Wewe bado mdogo, usijikomaze kwa mawazo. Ukiwa na tatizo lolote niambie hata kama litamuhusu Sam, mi kama dada yako nitakupa ushauri mzuri"

Nikafurahi ila wazo la kuwa Sam hajajibu ujumbe wangu likanijia kichwani na kujikuta nikinyong'onyea kiasi na kumuuliza dada.

"Hivi kwa mfano umemtumia message mtu unayempenda halafu hajakujibu utajielewaje?"

"Kwa haraka haraka unaweza kuhisi amekudharau au kuna kitu bora anafanya kuliko wewe ila ukweli ni kwamba simu haina vocha au imeharibika au ujumbe hajauona, usipende kumfikiria mtu kinyume. Sawa?"
Niliitikia kwa kichwa ila maneno yake yalinipa faraja kiasi.

Usiku wa leo baada ya kula, dada aliweka picha ya ngumi na kunitaka tuangalie wote. Tuliangalia hadi saa tano usiku kisha kuamua kwenda kulala.

Nikiwa kitandani, niliyatafakari sana yale maneno ya dada kuhusu kutokujibiwa ujumbe wangu hadi muda ule. Nikamtumia ujumbe tena na tena Sam ila bado sikujibiwa.

Niliendelea kuhisi kuwa Sam amenifanyia kusudi kwa kutokunijibu nikajisemea kuwa lazima kesho yake niende kwa Sam ili nikamuhoji.

Niliwaza na kupitiwa na usingizi pale kitandani.

Leo katika ndoto, nilimuona dada yangu akiwa kazini kwake kisha akatokea yule mkaka mtanashati wa kwenye ndoto zangu na kumkabidhi zawadi, dada alitabasamu na kuifungua yalikuwa maua na mdori kisha yule mkaka akanitazama mimi kwenye ndoto na kutabasamu.

Nikashtuka pale kitandani na jambo la kwanza lilikuwa ni kuangalia vile vitu alivyonipa dada, ile kupiga jicho kwa mdori nikamuona akitabasamu.

Niliogopa sana, nikajifunika shuka gubigubi ila bado nilimuona mdori yule akitabasamu.

Niliogopa hata kunyanyuka pale kitandani na kupiga makelele pia nilishindwa, nilijikuta nikiwa vile hadi kunakucha na palipokucha jambo la kwanza nilikimbilia chumbani kwa mama. Mama naye akashtuka na kuniuliza,

"Kwani kuna nini mwanangu?"

"Hata sijui"

"Na mbona umekimbia sasa? Si bure umeshaanza kuwehuka wewe."

"Hapana mama"

Sikutoka chumbani kwake hadi na yeye alipotoka, dada Penina alikuwa ameshaenda kazini.

Niliporudi tena chumbani kwangu hali ilikuwa shwari na yule mdoli alikuwa kawaida kabisa ila nikaamua kukusanya yale maua na yule mdoli na kuvirudisha chumbani kwa dada, kisha nikarudi na kukipanga chumba changu upya.

Mchana wa siku hiyo nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea Lucy, mama hakupinga akaniruhusu kwani alimuona Lucy nae aliponitembelea.

Safari yangu ilikuwa moja kwa moja hadi nyumbani kwa Sam, sikumkuta ila nikaamua kumngoja na hakukawia sana akawa amerudi kwenye mida ya jioni hivi.

Tukaingia ndani na kuanza mazungumzo, nilimlalamikia kwanini hajibu meseji zangu akadai kuwa hajapata ujumbe wangu hata mmoja na kusema kila alipojaribu kunipigia alikuwa hanipati hewani.

"Yani hapa nilikuwa nafikiria Sabrina kuwa nimekukosea nini hadi kufikia hatua ya kunizimia simu? Wakati kama safari ya beach ulikataa mwenyewe"

Kwakweli sikumuamini Sam kama kweli alikuwa hanipati hewani wakati simu yangu ipo hewani muda wote na sikumuamini kama kweli meseji zangu hazikufika kwake wakati kwangu zilionyesha kuwa zimefika.

Nikamnyang'anya simu yake ili kuhakikisha kama kweli na moja kwa moja nikaenda kwenye ujumbe unaotumwa kwake (inbox), kuangalia kama kweli ujumbe wangu hata mmoja haukufika.

Kwakweli wakati naangalia nikapatwa na presha kabisa kuona ujumbe uliotumwa na Lucy ukiwa umeongozana kwenye simu ya Sam, tena kila ujumbe niliosoma ulikuwa ni mzito sana.

Nilimuangalia Sam kwa jicho kali sana,
"Ndio nini hiki Sam?"

"Kwani nini?"

Nikampa ile simu yake aangalie mwenyewe.

"Angalia upuuzi unaochat na Lucy"

"Jamani! Lucy si rafiki yako na umenitambulisha mwenyewe?"

"Sasa kama rafiki yangu ndio uchat nae message za namna hiyo?"

"Kwanza unanipa lawama za bure Sabrina na unapandisha jazba bure tu. Tulia kwanza nikueleze"
"Hakuna cha kunieleza Sam, ujumbe wa humo umeshajitosheleza. Sam wewe una tamaa sana yani hadi kwa rafiki zangu loh!"

Nikainuka na sikutaka maelezo yoyote ya ziada na kuanza kuondoka kwani nilipandwa na hasira za ajabu.
Sam akawa ananirudisha ila sikutaka kumsikiliza wala nini ndio kwanza niliongeza mwendo.

Sam alinifatilia hadi alichoka na giza lilikuwa limeshatanda, akaomba kunisindikiza nyumbani nikamkatalia sikutaka tena kumsikiliza Sam ikabidi aniage kwa lazima huku natembea haraka haraka akasema kuwa kesho atakuja nyumbani ili tuweze kuzungumza vizuri.

Sikumsikiliza chochote na niliendelea na safari, nilifika kwenye njia flani na haikuwa na mtu yeyote, nikasikia nyuma yangu mtu akiita,
"Sabrina"

Nikapatwa uoga hadi nikashindwa kugeuka kwani sauti ilikuwa ya kiume ila sio ya Sam.

Wakati natembea haraka haraka nikahisi kama huyo mtu ananikimbilia kwa nyuma, nami nikaanza kukimbia. Nikasikia tena sauti,

"Usinikimbie Sabrina, usiogope."

Nikazidi kupatwa na uoga kwani yule mtu alishafika nyuma yangu.

Mara akanishika bega, uoga ukazidi kunijaa kwani mikono yake ilikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.

Itaendelea​
 
SEHEMU YA 05

Uoga ukazidi kunijaa kwani mkono wake ulikuwa na ubaridi uliopenya mwilini mwangu.
Nilishindwa kugeuza shingo yangu kumtazama kwani nilijua wazi atakuwa ni yule jamaa wa kwenye ndoto zangu, jamani kwenye matatizo acheni kabisa kwani gafla nilitoa mbio hata nadhani ingekuwa ni mashindano basi lazima mimi ningekuwa mshindi.

Mbio nilizokimbia haikuwahi kutokea maishani mwangu, nilikuwa nimechanganyikiwa kabisa na kujikuta gafla nishafika kituo cha madaladala huku nikihema juu juu.

Ikatokea daladala mbele yangu na kuisimamisha, iliposimama nikapanda na kukaa kwenye siti. Nikajiinamia chini, sikujielewa kabisa na sikuelewa chochote.

Nilipokaribia na kituo cha nyumbani nikatoa nauli na kumwambia konda ashushe, gari iliposimama nikashuka na kuanza kuondoka mara konda wa daladala akanishika bega na kusema,
"Umesahau chenji yako Sabrina"

Nilihisi kupagawa kwani mkono wa yule konda ulikuwa na ubaridi kama wa yule mtu aliyenishika bega njiani, na je yule konda amejuaje jina langu? Nilihisi kuchanganyikiwa, nilipogeuka kumuangalia yule konda nikamuona akitabasamu kama yule mdoli.

Hapo nilihisi kuwa chizi jamani kwani nilianza kukimbia huku nikipiga makelele ya kuomba msaada, nilikimbia na kituo cha kwanza ilikuwa ni nyumbani kwetu. Nilifika mlangoni na kuanguka na kupoteza fahamu kabisa.

Nilipozinduka nilikuwa mikononi mwa mama, kichwa changu kilikuwa kwenye mapaja yake. Kumtazama usoni alikuwa amejawa na machozi huku dada akiwa pembeni na mama Salome.

Niliinuka ili niweze kukaa, mama akanisaidia kufanya hivyo kisha wakanipa maji niweze kunywa.
Baada ya kutulia, mama akaanza kuniuliza.

"Umepatwa na nini mwanangu? Unajua umenitisha!"

"Mmh hata sijui nimepatwa na nini mama ila viungo vyangu vyote vinauma"
Mama akaniambia kuwa ilibidi wamuite mama Salome ili kunipatia huduma ya kwanza kwani yeye alikuwa ni nesi mzoefu. Na ndiye aliyewapa moyo kuwa nitaamka tu.

Siku hiyo nililala chumbani kwa mama kwani mama alitaka kuangalia hali yangu inaendeleaje kwanza.
Kabla ya kulala nilienda kumuuliza dada maswali mawili matatu wakati anatizama video.

"Eti dada kwa mfano ukahisi mpenzi wako amekusaliti, je kuna haja ya kusikiliza maelezo yake?"

"Sikia mdogo wangu, unapomuhisi mpenzi wako vibaya au unapoona kitu kibaya toka kwake hutakiwi kufanya hasira. Unachotakiwa kufanya ni mambo matatu, kwanza kabisa muulize mpenzi wako kuhusiana na kile unachohisi, kusikia au kuona, pili sikiliza maelezo yake hata kama anakudanganya na tatu kaa chini kutafakari na kuyapima maelezo hayo. Usipende kuchukua maamuzi ya gafla kwani yatakuumiza wewe na umpendae"

Ushauri wa dada ukaniingia na kunikaa sawa, kisha nikaenda kulala huko kwa mama kwani mama alikuwa ameshalala muda huo.

Kesho yake nilikuwa na hali ya kawaida kabisa na kuanza kuongea na kucheka na mama.
"Ila wewe mwanangu ni wa ajabu, sijui ulifukuzwa na wezi jana. Yani umekuja na mbio na kuangukia mlangoni, pochi yako ndogo mkononi na simu ndani ya pochi mmh mi nilijua umevitupa"

Kwanza na mimi nilicheka kwani nikikumbuka jinsi nilivyokimbia halafu bila kutupa ile pochi ni kitu cha ajabu sana.

"Mambo mengine ni maajabu tu mama yangu"

"Ila nini kilikukimbiza haswaa?"

"Kuna mtu alinitisha pale stendi, ndiye aliyefanya hadi nianze kukimbia."

"Una vituko wewe, ulinitisha sana ujue"

Niliongea mambo mengi ya hapa na pale na mama.

Mchana wa siku hiyo Sam alifika nyumbani na kumkuta mama, kiukweli mama yangu alikuwa hampendi Sam ila Sam anapofika na kuniulizia mama lazima ataniita ila atanipa muda wa kuzungumza nae.

Mama akanifata ndani,
"Sabrina, kijamaa chako kipo hapo nje kinakuulizia. Sasa sio ndio unachukua muda wote kuzungumza nae, ongea nae kidogo arudi kwao. Sawa?"

"Sawa mama"

Aliposema tu kijamaa nilijua moja kwa moja anamzungumzia Sam.

Nikatamani kukataa kwenda kuzungumza nae kwa yale ya jana ila pia nilitaka kujua anajipya gani la kujitetea kwani nilifata ushauri ambao dada alinipa.

Nikatoa viti viwili na kukaa nje na Sam, na yeye alikuja kutimiza ile azma yake ya jana kuwa angekuja leo nyumbani kwetu na ndio alikuwa amekuja.

Nilikuwa najiandaa kusikiliza maneno ambayo Sam angeongea kujitetea, hata hivyo nilijua lazima atakachoongea kitakuwa cha uongo tu.

"Sam, hivi unajua jinsi gani nakupenda? Na je unajua ni jinsi gani nimeumizwa na huo uchafu wa kwenye simu yako?"

"Naelewa mpenzi ila unatakiwa kunisikiliza kwanza ili nikwambie ilivyokuwa, na unachofikiria juu yangu si kweli"

"Haya, ongea huo ukweli"

"Siku ile uliyowasiliana nami kwa kutumia ile simu ya rafiki yako, badae alinitafuta na kusema kuwa ananisalimia. Nilishamsahau ila alipojitambulisha ndio nikagundua kuwa ni rafiki yako wa mchana.

Kesho yake akanipigia simu asubuhi na kunisalimia, kisha akauliza kuwa nina mipango gani siku hiyo. Nikamwambia kuwa nimepanga kwenda beach na wewe, akaniambia ni vizuri kisha akapongeza kwa hilo.
Badae akaniuliza kama tumeshaenda huko beach, nikamwambia kuwa wewe umekataa ndio akasema kwamba atajaribu kuzungumza na wewe."

"Kwahiyo zile message alikuwa akikufariji kwavile mimi nimekataa?"

"Bado sijamaliza maelezo mpenzi"

"Haya, malizia basi"

"Badae akanipigia simu na kusema kuwa wewe unaonekana kuna kitu umechukizwa na mimi, hivyo akaniambia kuwa anao ujumbe wa kutosha wa mapenzi unaoweza kukufariji wewe, ndio akaanza kunitumia zile message kuwa niziangalie nikiona inayovutia nikutumie wewe. Ila mi sikuwa nachat nae na wala sikumuomba hizo message"

"Kwahiyo ulitaka mimi nifarijike kwa maneno ya mwanamke mwenzangu? Ulishindwa vipi kumzuia asikutumie? Nadhani ulizipenda ndiomana hukuziondoa kwenye simu yako."

"Si kweli Sabrina, yule ni rafiki yako. Mimi siwezi kukusaliti na kuwa na rafiki yako au kuwa na msichana mwingine, wewe ndiye nikupendae"

"Kweli nimeamini kuwa wanaume ni waongo, yani Sam message inasema nimekumiss sana baby na mwishoni anamalizia na busu mmwaaaaaah halafu unataka kuniambia ni mimi tu unipendaye?"

"Nielewe Sabrina nilichokwambia ni ukweli mtupu, au basi niambie cha kufanya ili upate kuniamini tena. Nakupenda Sabrina"

"Ngoja nifikirie kwanza maelezo uliyonipa kama yana ukweli wowote, ila nisingependa kuona ukiwasiliana tena na Lucy. Nadhani tumeelewana"

Sam alionyesha kujutia sana kile kitendo cha mimi kukuta jumbe za Lucy kwenye simu yake ila ndio hivyo maji yakimwagika hayazoleki.

Nikaagana pale na Sam akaondoka zake tena si kwa kawaida yetu ya kusindikizana, nilimwacha aondoke mwenyewe kama alivyokuja.

Mama akanishangaa kuwa mbona sijamsindikiza Sam.

"Kheee malkia leo umemuacha mfalme wako kaondoka mwenyewe!! Kulikoni??"

"Hakuna kitu mama"

"Mmmh hakuna kitu kweli? Ila kama mmeachana basi ashukuriwe Mungu"

Akainua na mikono juu kuonyesha shukrani hadi nikajisikia kucheka.

"Kwanini mama humpendi Sam?"

"Sio type yako, haendani na wewe kabisa. Wewe mwanangu unatakiwa kupata mwanaume wa ukweli, mwenye kazi ya maana na pesa zake halafu msomi ila sio hao vidampa kama huyo Sam"

"Ila mama mapenzi sio pesa"

"Usibishane na watu tuliotangulia kuliona jua, je utapenda kuona watoto wako wakipata shida au raha?"

"Napenda wanangu wafurahi"

"Basi fata ushauri wangu, olewa na mtu anayejielewa utaona faida yake"
Anavyoongea mama kama vile Sam nae hajielewi wakati Sam ni mwanaume anayejielewa na kujitambua pia.

Dada aliporudi, aliniita chumbani kwake na sikujua ameniitia kitu gani.

Kumbe aliniita kuhusiana na vile vitu ambavyo nilirudisha chumbani kwake.

"Mbona umerudisha maua na mdoli ambaye nilikupa? Nilitaka kukuuliza jana sema ndiovile hukuwa na hali nzuri"
"Me sivitaki tu dada ndiomana nimekurudishia"

"Hadi mdoli Sabrina! Inamaana siku hizi hupendi tena wadoli?"

"Mi sijisikii kuwa navyo tu dada"

"Basi hakuna tatizo vitakaa humu chumbani kwangu"

Sikuweza kumwambia dada ukweli kama yule mdoli alikuwa akitabasamu.

Tulipokaa sebleni dada akamwambia mama kuwa aliniletea zawadi ya mdoli na maua ila nimevirudisha nakudai kuwa sivitaki.

"Ukiona hivyo ujue amekua, maswala ya madoli hayo ni mambo ya kitoto tu. Angekuwa kijijini Sabrina usikute angekuwa na watoto hata watatu sasa hivi"

Dada na mama wakawa wanacheka,
"Nimemshangaa sana leo kukataa mdoli kweli amekua mdogo wangu, eti Sabrina au ndio Sam anataka kukuoa?"

"Atakaemuozesha kwa huyo Sam ni nani? Labda nife ndio aolewe nae"

Kwakweli kauli za mama juu ya Sam hazikuwa nzuri kabisa, ila leo hawakuzungumzia zile stori zao za kutisha angalau nyumba ikawa na amani.

Hata mi mwenyewe, Leo nilikuwa na amani na kwenda kulala chumbani kwangu, kwanza kabisa nilizungumza na Sam kwenye simu kisha nikalala kwa amani kabisa.

Nikawaona Sam na Lucy wakiwa kwenye penzi zito huku mimi roho ya wivu ikiniuma, waliendelea na mapenzi yao na mwisho wa siku wakafunga ndoa.

Nilishtuka sana na jasho jingi likanitoka, yani Sam ananiongopea? Kumbe kweli ana mahusiano na rafiki yangu Lucy hadi watafikia hatua ya kuoana, roho iliniuma sana.

Wakati nawaza hayo, usingizi ukanichukua tena.

Yule mkaka mtanashati akanionyesha nyvmba nzuri sana na kusema kuwa itakuwa mali yangu endapo nitakubali kuwa na yeye, akanyoosha mkono wake ili niambatane nae lakini mimi nilikataa, akawa anafanyakazi ya kunisogelea huku akitabasamu na mimi nikazidi kusogea nyuma, nikafika mahali nikawa nimekwama, kuangalia nyuma kulikuwa na shimo refu lenye wadudu wengi na mbele yangu ni yule mkaka aninisogelea, nilipotaka kuanguka kwenye lile shimo nikashtuka na jasho liliendelea kunitoka tena jingi kushinda la mwanzo. Nikajiuliza kuwa hii ndoto inamaana gani nikakosa jibu.

Nikabanwa na haja ndogo na kuinuka pale kitandani ili niende chooni.
Choo chetu kilikuwa ndani, ila nilipokaribia mlango wa choo nilasikia kama mtu anacheka nikajiuliza ni nani usiku ule wakati mama na dada walikuwa wamelala.

Kufika kwenye mlango wa choo nikamkuta yule mdoli akiwa mlangoni na uso wake ulitazama kwangu huku ukitabasamu, nikaanza kuogopa nikatamani kupiga kelele ila nilishindwa nikaamua kukimbilia chumbani huku nahema juu juu kwani ni mambo ya ajabu ambayo sikuyatarajia kabisa. Nikabamiza mlango kwa uoga.

Nikiwa chumbani kwangu nikaanza kujilaumu kuwa kwanini sikwenda chumbani kwa mama moja kwa moja ila niliogopa kutoka tena.

Nikakaa kitandani kwa uoga, gafla nikashikwa na kitu mgongoni ile kugeuka na kuangalia ni yule mdoli wa chumbani kwa dada, alikuwa akitabasamu kama yule mkaka wa ndotoni.

Hali ilikuwa mbaya zaidi pale nilipotazama mezani na kumuona tena yule mdoli na yale maua.
Hofu ikanitanda, uoga ukajaa nikainuka pale kitandani ili nikafungue mlango nikimbilie chumbani kwa mama.

Nilipoufikia mlango, yule mdoli nae alikuwa mlangoni akitabasamu halafu kwa mbali nilisikia mtu akiita jina langu.

Itaendelea kesho.....!!!
 
SEHEMU YA 06


Yule mdoli nae alikuwa mlangoni akitabasamu halafu kwa mbali nilisikia mtu akiita jina langu.
Nilizidi kuchanganyikiwa, nikaamua kupiga kelele kwa nguvu na kwa bahati muda huo sauti ilitoka.

"Mamaaaaaaaaaaaa..............."

Mama na dada walikuja mbio chumbani kwangu.
Walivyofungua mlango wangu, nilichoropoka na kukimbilia sebleni wakanifata na kuniuliza. Nilikuwa natetemeka sana.

"Kuna nini mwanangu? Kuna nini jamani??"

Mama na dada walikuwa wananishangaa, kwani jasho na machozi vilikuwa vyanitoka.

"Mdoli mama mdoli"

Niliamua kusema kilichonisumbua.

"Mdoli kafanyaje?"

"Ananitisha mama kila mahali namuona halafu anatabasamu"

"Yuko wapi sasa huyo mdoli?"

Nikaamua kuongozana nao chumbani ili nikawaonyeshe.

Kuangalia pale mlangoni hayupo, kitandani hayupo, ndipo nikatazama mezani na kumkuta ametulia kabisa kama mdoli wa kawaida.

Nikawa namuonyesha dada,
"Si umemuona yule mdoli, kafikaje pale wakati alikuwa chumbani kwako?"

Dada yangu akacheka sana hadi mama akamuuliza anachochekea.

"Kweli Sabrina ni muoga jamani loh!!"

"Sema basi unachochekea Penina?"

"Mama, yule mdoli kweli Sabrina alikuja na kumrudisha kwangu kuwa hamtaki. Me nikahisi labda kuna kitu kachukia ndomana kamrudisha yule mdoli. Kwa nimjuavyo Sabrina anapenda sana wadoli, sasa mimi nimemfanyia surplise alipokuwa amelala nikamrudisha yule mdoli na kumuweka pale mezani ili akiamka amkute na kufurahia"

Nilimshangaa sana dada, ataniwekeaje kitu ambacho nilishakikataa!
"Ila mimi simtaki huyo mdoli, jana nilishakukatalia dada."

"Penina mwanangu ulichofanya si kizuri, Sabrina mwenyewe ana maruweruwe siku hizi. Akikataa kitu usimuwekee tena, haya mtoe huyo mdoli wako."

Ikabidi dada amtoe yule mdoli, na mimi nikaendelea kuwaeleza.

"Hata hivyo wakati naenda chooni nilisikia mtu anacheka na mlangoni mwa choo ndio akatokea huyo mdoli akitabasamu"

"Maruweruwe hayo mwanangu"

"Hata hivyo niliyekuwa nacheka ni mimi, nilikuwa naongea na simu si unaju kumekucha tayari! Nilikuwa najiandaa kuoga niende kazini"

Nilishangaa sana kwani muda niliodhania mimi kuwa ni usiku wa manane kumbe ilikuwa ni alfajiri, maneno ya mama kuwa nina maruweruwe nikaona huenda yakawa ni kweli ila bado sikuwa na imani na yule mdoli.

Mchana wake wakati tumekaa na mama ikabidi aniulize,
"Hivi ni kweli ulikuwa unatishwa na yule mdoli mwanangu?"

"Ndio mama, tena amenitisha sana tu"

"Kwahiyo unaamuaje maana dadako hayupo saizi tunauwezo wa kufanya chochote"

"Itakuwa vyema kama tukimchoma moto"

"Basi sawa mwanangu"

Mama akanituma nikamchukue yule mdoli ili tumchome moto lakini nilikataa kumfata, hivyo mama akaenda kumchukua mwenyewe.

Akaniita tumchome moto, akammwagia mafuta ya taa na kumuwasha moto.

Wakati yule mdoli anaungua ikatokea harufu kama vile kuna nyama inachomwa hata mama akashangaa.

"Mbona mdoli mwenyewe ana harufu kama ya kiumbe hai?"

"Ndio uone maajabu hayo mama, mi nikisema mnaona ni maruweruwe"

"Itabidi dadako akija nimuulize alipomtoa huyo mdoli"

Wakati tunajadiliana na yule mdoli akizidi kuungua, ikanyesha mvua iliyotuondoa mahali pale kufika ndani ikakatika.

Tukarudi tena kuangalia mdoli alivyoungua, tukakuta vinaungua vitu kama vya plastiki plastiki hivi. Wala haikuonekana dalili ya mdoli, mama akasema labda mdoli alishaungua wote.

"Na hiyo plastiki inayoungua je?"

"Labda wapita njia wameweka"

Nikacheka kweli kwa makisio ya mama.

Tukarudi ndani na kukaa, mara dada akawa amerudi hata tukamshangaa jinsi alivyowahi kurudi siku hiyo.
Ikabidi mama amuulize kuwa mbona amewahi sana.

"Mbona umewahi kurudi leo?"

"Majanga mama"

Halafu akaenda chumbani kwake kuweka mkoba, kisha akarudi tena sebleni na kuniuliza.

"Kheee Sabrina umemchukua tena yule mdoli?"

Kabla sijamjibu, mama akamuuliza tena.

"Niambie Penina, majanga gani hayo?"

"Mwenzangu, (akanigeukia mimi) unakumbuka kuwa nilikwambia kuna kijana kazini kanipa zawadi ndio nikakuletea wewe yale maua na yule mdoli?"

Nikaitikia kwa kichwa huku nikiwa na hamu ya kujua kuwa huyo kijana kafanya nini, kumbe mama nae alikuwa na shauku ya kujua, akauliza haraka haraka,

"Kafanyaje?"

"Kanifata ofisini kuwa ana shida na mimi, akaniombea ruhusa kwa bosi basi nikaondoka nae. Akaniambia kitu ambacho kimenivutia sana na kufanya nifatane nae, nia yetu ilikuwa ni kuja huku nyumbani kumfata yule mdoli. Tukapanda daladala, sijui hata tumechanganyana nae vipi. Yani mi nikashuka kumbe nimemuacha kwenye gari amesinzia, namuangalia chini hayupo na gari imeondoka. Nikajaribu kupanda gari jingine hadi mwisho, nikakuta lile basi lipo kupakia abiria wengine nilipomuuliza konda akasema kuwa yule kijana alivyoshtuka akashuka njiani hata sielewi amepotelea wapi kijana wa watu jamani mweeeh! Hana namba yangu ya simu na hapa hapajui. Ndio nikaamua kurudi nyumbani tu"

"Sasa yeye alikuwa anataka nini haswaaa"

"Mama, yule mdoli kumbe alikuwa wa bosi wake, yeye hakujua. Sasa amegundua kuwa yule mdoli nyuma kwake kule kwenye zipu kuna..... (kisha akanigeukia na kusema), hebu kamlete yule mdoli Sabrina nije kumuangalia mwenyewe"

Mimi na mama tukabaki tunatazamana kwani mdoli tulishamchoma.

Dada alipoona simjibu kitu, akainuka na kwenda chumbani kwangu akapekua na kurudi.

"Umemuweka wapi yule mdoli Sabrina?"

Ikabidi mama aulize tena,
"Kwani ana nini huyo mdoli Penina?"

"Amewekwa pesa kule kwenye zipu mama, tena ni dola za kimarekani nyingi tu."

"Unasema kweli Penina?"

"Ndio mama, mmemuweka wapi sasa?"

Mama akajibu kwa unyonge,

"Tumemchoma"

Dada akawa kama vile mtu ambaye hajasikia vizuri,

"Mmemfanyaje mama?"

Ikabidi mama amueleze dada kuwa mimi na yeye tulikaa na kutafakari kuwa yule mdoli achomwe moto.
Dada alichukia sana, akaenda pale nje kuangalia kisha akarudi chumbani kwake kwa hasira.

Jioni ya leo nilikaa na mama tu sebleni kwani dada alikuwa na hasira na sisi.

Mama akaanza kuniuliza,
"Hivi na sisi tuliingiwa na nini mwanangu hadi kuchoma mdoli asiyetuhusu?"

"Ila mama, yule mdoli alikuwa ananitisha bhana"

"Tungemchunguza kwanza kabla ya kuamua kumchoma, kwakweli tulichukua maamuzi ya haraka sana"

"Ila ishatokea mama haifai kupeana lawama"

"Tumeteketeza pesa mwanangu mmh!"

Hapo nikajua tu kwa tamaa ya mama yangu lazima ashikwe uchungu juu ya hiyo pesa aliyoisikia.

Usiku sikutaka kulala chumbani kwangu, ikabidi nikalale kwa mama ingawa kulikuwa kwa masharti kwani nikilala nae hataki nishike simu kuipokea wala kujibu ujumbe wa aina yoyote ile, ilibidi nikubaliane na vyote tu.

Sam nae akaanza kunipigia simu, nilitamani kupokea ila nilimuhofia mama kuwa atachukia sana nikipokea simu, tena ukizingatia ni ya Sam kijana ambaye hampendi.

Niliiacha iite hadi kukatika sema ilikuwa ikiita kimya kimya, sikutaka kuizima kwani nilijua kuwa nikiizima nitamchukiza Sam ambaye alipiga na kupiga na kupiga bila kupokelewa.

Nikatamani kurudi chumbani kwangu ili niwe huru ila uoga ulinisumbua, nilikaa na mawazo na kupitiwa na usingizi.

Nilishtuka gafla nikiwa na kiu ile kupitiliza, kwavile mama huweka maji mezani mule chumbani kwake kwaajili ya kunywa akishtuka nami nikainuka na kumimina maji kwenye kikombe ili ninywe.

Wakati na kunywa nikahisi kama kuna mtu ameshikilia ile bilauli na kunisukumia maji yote kinywani hadi nikapaliwa, na kuanza kukohoa. Nilikohoa sana hadi mama akaamka hadi na damu zikawa zinanitoka mdomoni, mama akashangaa sana ikabidi anipatie huduma ya kwanza nayo ni kuniweka sehemu yenye hewa zaidi na kuniwashia feni inipepee.

Nilipotulia akaniuliza nini tatizo, nikamueleza mama kuwa nimepaliwa wakati wa kunywa maji na tukarudi kulala.

Nikamuomba mama asizime taa ya mule chumbani kwani kila akizima nilikuwa naona kama kuna mtu anafungua ule mlango wa mama na kuingia.

Ikabidi mama asizime ile taa na kuniona mwanae kuwa nimeanza kuchanganyikiwa, nililala nimemkumbatia mama hadi kunakucha.

Kwakweli kwangu mchana ulikuwa bora kushinda usiku kwani usiku vioja vinakuwa vingi sana.

Kulipokucha mama akaanza kunilalamikia kwa kumlaza na mwanga wakati yeye kazoea kuzima taa.

"Na leo ukalale chumbani kwako, hayo maswala ya kufanya taa ikeshe chumbani kwangu sitaki. Wewe umekuwa mtu wa maruweruwe tu siku hizi hata sijui una nini jamani? Uoga wako umetukosesha mahela toka kwa mdoli."

"Najua tu hilo la mdoli utakuwa unajilaumu siku zote ila sikuwa na la kufanya kwajinsi alivyokuwa akinitisha"

"Unamaajabu sana mwanangu, eti mdoli anatabasamu loh! Na mimi bila hata ya kufikiria mara mbili, eti tumchome mwanangu. Hii ndio haraka haraka haina baraka"

"Basi yaishe mama"

Nilibaki kujisemea kuwa laiti kama yangekuwa yanawatokea kama ambavyo yananitokea mimi labda wangeelewa.

Badae niliwasiliana na Sam ambaye alikuwa amechukizwa sana na kitendo changu cha kupotezea simu zake.

Mchana wake nilitembelewa na rafiki yangu Suzy, nilifurahi sana na kuongea nae mambo mengi kama rafiki.

Nikamueleza Suzy kuhusiana na alichonifanyia Lucy kwa Sam na jinsi Sam alivyonipa maelekezo ya ilivyokuwa.

"Kwahiyo sasa wewe umeamuaje?"

"Kwakweli nilichukizwa sana, nilitamani hata kuachana na Sam kwa usaliti wake"

"Sikia shoga yangu, usithubutu kuachana na Sam kwaajili ya Lucy. Yani Lucy ni gubegube hana mfano, kazi yake ni kuiba mabwana za watu yani hana lolote nakwambia. Usimuachie Lucy"

"Kama wao wamependana je itakuwaje?"

"Hakuna cha kupendana hapo, Lucy namjua vizuri. Usimuachie bwanako, atamuiba kweli. Unamchezea Lucy eeh! Hana masikhara yule mtoto wa pwani"

"Unanitisha sasa Suzy"

"Usiogope, unatakiwa kuwa ngangari. Pigania penzi lako, usikubali mpita njia akakuharibia safari yako."
Maneno ya Suzy yalinitia moyo kwakweli na kujikuta nikipata nguvu mpya juu ya Sam.

Jioni yake Suzy akaaga na nikaamua kumsindikiza stendi ili akapande daladala la kurudi kwao.

Tukasimama pale stendi na kuendelea na maongezi yetu huku tukingoja daladala na kulikuwa na watu wengine pale nao wakingoja usafiri.

Ikaja basi na kusimama mbele yetu, ikashusha abiria kisha Suzy akapanda basi lile na tukaagana. Kwakweli sikumuangalia hata kidogo yule abiria aliyeshuka.

Baada ya lile basi kuondoka, kuja kutahamaki nilibaki mwenyewe pale kituoni hadi nikashangaa wakati mwanzoni walikuwepo watu wengi tu, nikageuka ili nianze safari ya kurudi nyumbani.

Wakati nageuka, nikashangaa kushikwa mkono na mkaka, ule mkono wake ulikuwa na ubaridi sana uliopenya hadi moyoni mwangu, kisha akasema,

"Habari yako Sabrina"

Nilikuwa nikitetemeka, kuinua macho na kumtazama ni yule mkaka wa ndotoni.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 07

Nilikuwa nikitetemeka, kuinua macho na kumtazama ni yule mkaka wa ndotoni.
Nilizidi kutetemeka kwani ubaridi uliotembea mwilini mwangu ulikuwa mkubwa sana.

Akaendelea kunishikiria mkono na kuzungumza,
"Mbona waniogopa sana Sabrina? Mimi sitishi, nipo kawaida kama wengine. Nahitaji kukusaidia."
Sikujibu chochote na kuzidi kutetemeka, akaendelea kuongea.

"Tambua kwamba, huwezi kunikwepa kamwe. Ipo siku utaingia kwenye himaya yangu."
Kizunguzungu cha gafla kikanishika na kuanguka.

Nilipozinduka nilikuwa nyumbani kwenye kochi, nimezungukwa na mama, dada na majirani zetu wawili. Sikuelewa nini kilitokea hadi mimi kuwa pale, ilibidi niwaulize kwani nini kimetokea ukizingatia wote walikuwa wananipa pole nilivyozinduka.

Dada ndiye aliyenijibu swali nililouliza,
"Nimekukuta stendi pale, wakati nashuka kwenye daladala ulikuwa unatetemeka sana na badae ukaanguka. Ndio nikakuwahi pale na watu wengine walikuwepo stendi pale wakasaidiana nami kukuleta nyumbani. Pole sana mdogo wangu."

Nikawa najiuliza, inamaana dada hakumuona yule mkaka niliyesimama nae? Nikawa na maswali mengi kichwani. Mama akasema nipumzike kwanza na wale majirani wakaaga na kuondoka.

Mama alikuwa karibu sana na mimi.

"Saivi uache safari za jioni mwanangu, nadhani una tatizo wewe"

"Sio unadhani mama, huyu Sabrina atakuwa na tatizo tu"

Mama akaniangalia kwa makini sana,
"Hebu niambie mwanangu, nini tatizo?"

"Hata sielewi mama ila kuna mtu huwa ananitokeaga ndotoni, sasa huyo mtu......"

Nikapaliwa na mate na kuanza kukohoa sana, nilikohoa hadi damu ikabidi mama aanze kunipatia huduma ya kwanza.

Dada akaja na kutoa ushauri,
"Au Sabrina atakuwa na malaria inayopanda kichwani?"

"Eti eeh!"

"Inawezekana mama, angalia mambo anayofanya kama ni ya kawaida"

Nikashindwa kumuelewa dada, kupaliwa na mate kunahusiana nini na malaria inayopanda kichwani? Labda kwavile mi sikuwa daktari. Wakakubaliana kuwa kesho yake nipelekwe hospitali kwenda kupima hayo malaria.

Usiku nililala tena na mama, nikamuomba asizime taa wakati tumelala kumbe mama alivizia muda ambao usingizi umenipitia haswaa na kuzima ile taa.

Nikashtuka kwenye usingizi, na kumuona mtu amesimama kwenye mlango wa mama nikapiga kelele iliyomuamsha hadi mama.

"Ma.....mamaaaaaaaaaa.........."

Kitu cha kwanza kabisa ni mama kuniuliza kuwa kuna nini, nami nikajibu kwa hofu.
"Kuna mtu mlangoni mama"

Huku nimeziba sura yangu kwenye mwili wa mama.

Mara taa ya chumbani kwa mama ikawashwa, hapo ndipo uoga ulizidi kunikamata kwani nilijua kwa vyovyote vile atakuwa ni yule mtu wa ajabu kwani sikumuona mama akiinuka na kwenda kuwasha taa ila taa iliwashwa nikajua leo lazima mama ataelewa kwanini mimi naonekana kama chizi. Nikaamua kuropoka,

"Si unaona amewasha na taa"

Mara kikasikika kicheko, kusikilizia ni sauti ya dada aliyekuwa akicheka sana hadi anagongagonga mguu chini, akaanza kuongea.

"Kheee malimwengu haya humu ndani, tumeanza kuogopana wenyewe kwa wenyewe!!"
Mama akamuuliza dada,

"Na wewe vipi mapema hii wakati ni mwisho wa wiki? Unaenda kazini na leo?"

"Hapana mama, leo Fatuma kaniomba nimsindikize mahali na inatakiwa tuwahi asubuhi sana. Hivi nimekuja kukudamsha uje kufunga mlango, namshangaa huyo chizi wako anapiga kelele"

Akacheka tena, mama nae akajibu.

"Uliyoyasema jana ni kweli, nadhani Sabrina ana malaria iliyopanda kichwani. Nilitaka leo umpeleke hospitali kumbe na wewe una safari zako loh! Basi tutakuja kuongea vizuri ukirudi."

Kwakweli hata sikuelewa elewa, nilijiuliza maswali mengi sana kuwa kuna kitu dada anakijua ila anaficha. Au la anatumiwa, hata kama mimi muoga ila nakataa kabisa kama aliyesimama pale mlangoni mwanzoni alikuwa ni dada. Nikabaki kama nimepigwa bumbuwazi.

Nilibaki nyumbani na mama aliyekuwa anasisitiza kuwa natakiwa kwenda hospitali ila hakutaka niende mwenyewe.

Nilikuwa nikiongea nae huku akiniuliza maswali ya kupima akili yangu.

"Ila mama, mi dada Penina simuelewi siku hizi sijui na yeye ana matatizo gani?"

"Mwenye matatizo ni wewe Sabrina, yani wewe ukapimwe kabisa hiyo akili yako. Nina uhakika utakuwa na matatizo kichwani."

"Sio matatizo mama, kuna mambo ya ajabu huwa yananitokea ndiomana nakuwa hivi"

"Hayo mambo ya ajabu ni yapi mbona huwa huyataji? Au ile kusema mdoli anakuchekea sijui kila mahali ukienda unamkuta, mara tukilala kama mtu anafungua mlango. Ndio hayo mambo ya ajabu? Mbona wenzako hayatutokei sasa, utakuwa na matatizo wewe sio bure."

"Ila kama huko hospitali mi sitaki kupelekwa na dada Penina"

"Sawa hakuna tatizo, nitampigia simu hata kaka yako Deo aje akuchukue akupeleke"

"Hapo sawa"

Mimi sikuwa mgonjwa kama wanavyonifikiria, tatizo lao hawataki kunisikiliza na kunielewa. Aliposema habari za kumpigia kaka Deo simu nikaona itakuwa afadhari pengine yeye ataelewa nitakapomwambia kinachonisumbua.

Mchana wa siku hiyo, mimi na mama tulikaa nje ambako tulitandika mkeka. Tukashangaa kumuona dada akirudi muda huo maana na yeye kwa kawaida yake kama hajaenda kazini na ametoka tu kwa safari binafsi basi kurudi kwake ni usiku ila siku hiyo alirudi mchana.

Akafika na kumsalimia mama kisha akakaa kwenye mkeka, akaniomba nimpelekee mkoba wake ndani basi nikauchukua na kumpelekea chumbani kwake. Nikauweka ule mkoba, kuangalia mezani namuona yule mdoli tuliyemchoma moto na yale maua, nilitetemeka sana.

Nikakimbilia nje huku nikihema juu juu na kupiga kelele, mama na dada wakaniuliza kuna nini.
"Yule mdoli tuliyemchoma mama yupo chumbani kwa dada"

Ikabidi mama na dada wainuke na kufatana nami hadi chumbani kwa dada, ni kweli mezani walimkuta mdoli ila sio kama yule.

"Umeamini mama kama mwanao malaria imepanda kichwani??"

"Kweli kabisa mwanangu anaumwa, hebu Penina nenda nae hospitali"

"Hata bila ya kupumzika jamani mama?"

"Mpeleke kwanza utakuja kupumzika ukirudi, mdogo wako ana matatizo huyu, atawehuka bure hapa"
Mimi nikawa nawasikiliza tu wanavyonijadiliana kuhusu mimi kama vile mtoto mdogo wakati ni mtu mzima hadi nayajua mapenzi ni nini.

Ikabidi dada anipeleke hospitali, tukaondoka nyumbani na kufanya safari ya kwenda huko hospitali. Njiani akakutana na rafiki yake wa kiume na kuanza kuzungumza nae kisha akamwambia kama tunaenda hospitali, yule rafiki akasema tupitie kwanza baa tupate mbili tatu halafu hospitali atatupeleka kwenye zahanati ya rafiki yake na huko tutaenda kutibiwa bure. Kwajinsi dada yangu anavyopenda vitu vya bure akafurahi sana na kukubali, basi tukapitia hapo baa ili wazungumze.

Mimi sikuwa mnywaji wa bia kwahiyo niliagiza soda tu ila dada yangu alikuwa ni mnywaji wa haswaa ila zile bia za bure ndio anazozipendelea sana.

Yule mkaka akaagiza na nyama ya mbuzi aliyekaushwa ambayo ikawa inaliwa na kushushia na vinywaji.

Mara akaja mkaka mwingine ambapo yule rafiki wa dada alimtambulisha yule kaka kama rafiki yake, maongezi yakaendelea. Kila nikimtazama yule kaka mwingine aliyekuja sura yake inabadilika inakuwa ya yule mkaka wa ndotoni, nikajikuta napiga kelele na kuishtua baa nzima kisha nikaanguka.

Kuja kushtuka nilikuwa hospitali kitandani nikipimwa pimwa kuwa nina tatizo gani, dada akaniambia kuwa nilipoanguka ikabidi waniwaishe hospital.

"Mmh! Sijui una degedege siku hizi mdogo wangu!"

Nilimuangalia sana dada hata sikuelewa urafiki wake na watu wa ajabu ajabu kiasi kile ameanza lini. Nikahudumiwa kisha nikapewa dawa, daktari akasema kuwa sina tatizo ila nanaanguka sababu ya mshtuko tu ambao hakujua unasababishwa na nini.

Tukaanza safari ya kurudi nyumbani. Dada akaanza kunipa masharti yake njiani,

"Tukifika nyumbani usimwambie mama kama tulipitia bar, sawa?"

"Sawa sitamwambia"

"Basi nitakupa zawadi ya yule mdoli mwingine mdogo wangu."

"Hapana, sitaki zawadi yoyote"

Dada alinishangaa mimi kukataa zawadi.

Kurudi nyumbani, jambo la kwanza mama kuliulizia ni kuwa daktari kasemaje kuhusiana na hali yangu. Dada akamjibu kuwa daktari amesema kuwa sina ugonjwa wowote.

"Sasa ni kitu gani kina msumbua huyu Sabrina?"

"Amepewa dada atumie halafu tutaangalia hali yake inaendeleaje, ikizidi tutaenda nae tena"

Mama akanigeukia kuniuliza tena,

"Hivi siku ile hadi umepaliwa ulitaka kusema nini?"

"Sio siku ile mama, ni jana tu hapo."

"Haya nieleze basi"

Nikataka kumueleza mama, mara kichwa cha gafla kikaanza kuniuma yani kichwa kiliuma kama vile mtu anagonga na nyundo.

Ikabidi mama anipe dawa kisha akaniambia nipumzike, nililala palepale sebleni kwenye kochi.

Akatokea yule kaka, leo alikuwa na sura ya upole kabisa huku akiongea.
"Nihurumie Sabrina, naomba unikubalie. Nitakupa chochote utakacho kwenye ulimwengu huu na nitakupeleka popote utakapo, naomba unikubalie"

Nikawa natikisa kichwa kwa ishara ya kukataa, yule mkaka aliendelea kuongea.

"Nina vingi vya kukupa ambavyo mwanadamu wa kawaida hawezi kukupatia"

Wazo likanijia kuwa huyu lazima ni jini na ndiomana kajitoa kwenye kundi la binadamu wa kawaida. Nikamuuliza,

"Kumbe wewe ni jini?"

"Mimi ni malaika Sabrina"

Akawa ananisogelea ili anishike huku akinyoosha mkono wake, wazo la Sam likanijia nikakumbuka kuwa nampenda sana Sam wangu, yote hayo yalikuwa yakitembea ndotoni.

Yule mtu akasisitiza nimkubalie, nikaona kama amekuja kwenye maisha ya kawaida na kunishika kisha kunisukuma sukuma kama mtu anayeniamsha, nikashtuka gafla na kupiga kelele kwa nguvu,
"Sitakiiiiiii............."

Kumbe mama ndiye aliyekuwa akiniamsha kuwa ninywe dawa na niende chumbani kulala, jasho lilikuwa linanitoka jingi sana.

Nikanywa dawa na kuelekea moja kwa moja chumbani kwangu kulala nadhani hata mama alishangaa kwa mimi kwenda kulala mwenyewe chumbani kwangu, hata sijui ilikuwaje ila nilijikuta uoga umepotea.

Kulipokucha nilijishangaa sana kulala mwenyewe tena chumbani kwangu wakati nimekuwa nikipaogopa kwa siku hizi za karibuni.

Wazo likanijia kuwa natakiwa kumwambia Sam ukweli ili tujue la kufanya, pengine Sam anaweza kunisaidia kwa majanga haya. Nikachukua simu na kumpigia Sam kuwa badae nitakuwa kwake, nikaona njia rahisi ya kuruhusiwa kutoka pale nyumbani ni kujifanya nimepona na kufanya kazi zote za nyumbani.

Basi nikaamka, nikasafisha nyumba, vyombo na kila kitu. Nikafagia uwanja na kuweka kila kitu sawa, nikabandika na mboga ya mchana kwani chai nilishaiandaa.

Mama na dada walipoamka walishangaa sana, hadi mama akasema.

"Naona Sabrina umepona mwanangu, umerudia kuwa mtoto mzuri tena"

Mchana wake nikamuaga mama kuwa naenda kumtembelea Suzy ila nitawahi kurudi.

"Suzy si alikuwa hapa juzi tu?"

"Ndio mama ila nimemkumbuka tu"

Mama aliniruhusu kwani aliamini kuwa nimeshapona.

Safari yangu ilikuwa ni moja kwa moja kwa Sam na lengo la safari yangu ni kumwambia Sam ukweli ili ajaribu kutafuta njia ya kunisidia.

Mwanzoni niliogopa kumwambia ukweli kwa kuhofia kwamba huenda Sam atajisikia vibaya na kuhisi kuna mtu mwingine nampenda, kwahiyo tangia nijue kuwa yule mkaka si binadamu wa kawaida ndio nimeamua kumueleza Sam aweze kunisaidia kwa njia yoyote ile.

Nilimkuta Sam ndani na nikakaa nae kitandani ili niweze kumweleza kuhusiana na mambo yanayonitokea.
Nikaanza kumweleza Sam,

"Unajua mwenzio kuna mambo ya ajabu sana yananitokea siku hizi!!"

"Mambo gani hayo?"

Kwavile nilikuwa naongea huku nimejilaza kitandani, nikajikuta usingizi umenichukua palepale kabla hata sijasema chochote.

Katika ndoto, niliona mimi na Sam tuko mule chumbani tukiongea mara kuna mtu akagonga mlango tena anagonga kwa nguvu sana, Sam akainuka kwenda kufungua.

Yule mtu akaingia moja kwa moja, kumwangalia ni yule mkaka wa ndotoni akaja kunishika mkono na kunivuta kuwa niende nae.

Sam hakuweza kupambana nae kwahiyo akaniachia niende.

Nikashtuka gafla na kusema kwa nguvu "Siendi popote" hadi Sam akanishangaa.

"Una nini Sabrina?"

"Hata sijui"

Mara mlango wa Sam ukaanza kugongwa kwa nguvu sana hadi tukashtuka.

Itaendelea​
 
SEHEMU YA 08


Mara mlango wa Sam ukaanza kugongwa kwa nguvu sana hadi tukashtuka.
Sam akainuka na kutaka kwenda kufungua, nikamshikilia mkono kumzuia kuwa asiende.
"Mbona unanizuia Sabrina?"
"Usiende kufungua Sam"
"Kwanini? Kwani unamjua mgongaji wewe?"
Nikatikisa kichwa kwa kukataa kuwa simjui.
"Kama humjui kwanini hutaki niende kumfungulia?"
Nikawa namuangalia tu Sam bila ya kusema chochote huku jasho jingi likinitoka.
"Wewe Sabrina nadhani una matatizo wewe sio bure, niachie basi nikamfungulie"
"Muulize kwanza ni nani ndio nitakuachia"
Nilizidi kumshikilia Sam, akauliza kuwa anayegonga ni nani ila mgongaji hakujitaja jina na kuzidi kugonga tu. Mi nikazidi kuogopa na kumuangalia Sam,
"Si unaona hataji jina lake? Huyo si mwanadamu wa kawaida Sam"
"Unamaana gani?"
"Nimeota vibaya Sam na simuamini mgongaji"
"Acha mambo ya ajabu Sabrina, hakuna chochote kibaya. Acha tu nikamfungulie"
Nilizidi kumkataza Sam ila hakunisikia hata kidogo, akainuka na kwenda kufungua mlango ambapo nilijiziba sura ili nisiweze kushuhudia kinachotokea.

Mlango ulipofunguliwa tu, yule mgongaji aliingia moja kwa moja tena kwa mbwembwe na kelele nyingi.
"Surpliiiiiseeeeeeee..........."
Akaja na kunikumbatia, nikatoa mkono machoni alikuwa ni Lucy.
Nikashangaa sana, Lucy amefata nini kwa Sam na je amepajuaje? Sikuwa na furaha kabisa na kuwauliza.
"Mbona sielewi?"
Sam nae akajibu,
"Hata mi mwenyewe sielewi, ngoja Lucy atufafanulie mwenyewe"
Nikamuangalia Lucy kwa jicho kali sana.
"Umefata nini hapa Lucy? Nani amekuelekeza huku?"
"Punguza hasira mumy nikwambie"
"Haya niambie, nahitaji kueleweshwa"
"Kuna siku nilimuuliza Sam anapoishi nae akanielekeza, kwavile mitaa hii naijua wala haikunipa tabu kupafahamu hapa na nilimwambia kuwa ipo siku nitamtembelea. Leo asubuhi nilipozungumza nae akaniambia kuwa wewe unakuja kwake na mimi nimeona leo kuwa siku bora ya kuwasurplise"
Kwakweli maelezo ya Lucy sikuyapenda na wala tabia ya Lucy sikuipenda pia.
Rafiki gani huyu? Utafanyaje surplise kwa mpenzi wa mwenzio anakuhusu? Marafiki kama hawa ndio huusika kuharibu mahusiano ya watu.
Akaanza kufungua mzigo wake kuwa amebeba na keki na vinywaji ili tufurahie pamoja, sikujisikia kula chochote kile alichobeba Lucy hadi Sam akaniuliza.
"Mbona hivyo Sabrina wangu jamani? Punguza kisirani mama, mimi ni wako tu. Njoo tule pamoja"
Ingawa alinilainisha kwa maneno ila moyo wangu bado ulisita kula vitu alivyobeba Lucy.
"Sijisikii kula mpenzi, tumbo langu limejaa sana"
Sikutaka Sam aendelee kuniona kuwa nina kisirani, ila kula sikujaribu hata kidogo licha ya Sam kunilazimisha sana.
Sam na Lucy waliendelea kufurahia, maneno ya Lucy yakawa yananichefua.
"Susa mama sie twalaaa"
Yani nilitamani nimponde Lucy na hata Sam nae sijui alikuwaje kwani hakuweza kabisa kumfokea Lucy.

Baada ya kukata ile keki na kula kisha kunywa vile vinywaji, Lucy akaomba tufungulie mziki ili acheze.
Sam akainuka na kufungulia mziki, Lucy akawa anacheza huku akijibidua na kujishebedua, roho ilizidi kuniuma.
Sam akaniambia niinuke ili tucheze wote nikagoma, mara nikamsikia Lucy akisema.
"Kama hataki kucheza njoo ucheze nami Sam, nipo single hapa uuuhuuu"
Huku akizungusha kiuno chake, hasira zikanikamata na kuinuka, kwakweli uzalendo ulinishinda jamani. Nikaenda kuzima ule mziki, Lucy akawa wa kwanza kuuliza.
"Mbona umezima mziki Sabrina?"
"Tafadhari Lucy naomba tuheshimiane"
"Kwani kosa langu nini?"
"Kukutambulisha shemeji yako isiwe sababu ya wewe kujitawala kiasi hiko, unatamani kucheza mziki nenda disko kwanza hakuna aliyekuita hapa. Kama vipi jiondokee tu."
Sam akaingilia kati yale mazungumzo, nadhani na yeye alinogewa na kiuno cha Lucy jinsi kilivyokuwa kinazunguka.
"Punguza hasira Sabrina, sijaona kosa lolote alilofanya Lucy. Amekuja kutuchangamsha tu hapa."
"Unajua usinichanganye Sam! Kwanza wewe na Lucy mmejuana vipi kwa sura mpaka Lucy kuingia moja kwa moja ndani?"
"Sabrina mpenzi, Lucy nimemjua kupitia wewe na leo ndio mara yangu ya kwanza kumuona. Punguza hasira mama"
Hasira nilizokuwa nazo zilikuwa ni za hali ya juu na niliona Sam akinidanganya tu, kisha akamgeukia Lucy.
"Usijali shem, ipo siku tutapanga twende huko disko"
Lucy akawa amesimama tu kutuangalia, nikaona Sam nae ananizingua nikainuka na kubeba mkoba wangu ili niondoke mimi halafu yeye aendelee kufurahi na Lucy wake.

Kabla sijafungua mlango, Sam alikuja na kunizuia kuwa nisitoke.
Kisha Lucy akatoka mule ndani, Sam akaendelea kunishikilia mkono.
"Tafadhali Sabrina, usifanye hasira kama za siku ile nakuomba"
"Sam, niache niende"
"Siwezi kukuacha uende mwenyewe Sabrina, leo nitakupeleka mimi hadi nyumbani kwenu"
Lucy alikuwa ametoka ila amesimama palepale nje bila ya kwenda popote, ikabidi nimwangalie Lucy na kumwambia.
"Si uondoke, unachongoja hapo kitu gani?"
Lucy akatabasamu kisha akaondoka, nikabaki mimi na Sam sasa.
Sam aliendelea kunibembeleza kuwa nitulie, nami nikatulia kwa muda na kumwambia kuwa nataka kurudi nyumbani. Akaniomba kuwa niingie tena ndani ili na yeye ajiandae tutoke, nikarudi mule ndani kwa Sam.
Mezani nikaona pochi ya Lucy, eti Lucy alisahau ile pochi yake ndogo nikajua hayo ni majaribu tu na Lucy amefanya kusudi kuacha pochi ili aweze kurudi tena. Nikachukua simu na kumpigia, nikamwambia kuwa amesahau pochi yake ndogo akasema kuwa ameshafika mbali na atakuja kuichukua siku nyingine eti hawezi kurudi tena muda huo wakati ameondoka pale muda sio mrefu, nilichukia sana kwani Lucy anajiamulia tu kama mahali ni pake.
Nikamuangalia Sam na kumwambia,
"Kwahiyo hiyo pochi ndio itakuja kukuunganisha tena na Lucy?"
"Hapana Sabrina, unanifikiria vibaya tu."
Wazo lingine likanijia kuwa niichukue mimi ile pochi na kwenda nayo ili Lucy aikute kwetu ila moyo wangu ukasita, kwahiyo sikuichukua tena.

Niliondoka na Sam pale nyumbani kwake akinisindikiza nyumbani, njiani tulikuwa kama mabubu kwani sikutaka kuzungumza nae kabisa ingawa kuna muda alikuwa akijiongelesha mwenyewe tu bila ya kujibiwa. Mawazo yangu yalikuwa ni kwa Lucy jinsi alivyokuwa akikatika mbele ya Sam, tukapanda daladala ila sikukaa nae siti moja nilikaa na mkaka mwingine kabisa aliyeanza kuniongelesha kwa kunisifia.
"Una sura nzuri dada, nimevumilia nimeona nikwambie ukweli tu"
Na mimi nikacheka, ambapo nikampa upenyo wa kuongea maneno mengi zaidi.
"Mmh! Tabasamu lako limegusa hadi moyo wangu Sabrina"
Nikashtuka sana na kumuangalia kwa makini,
"Umejuaje jina langu?"
"Aaah! Samahani, ulipokuwa chini nilimsikia jamaa yako akikuita Sabrina kuwa mpande hili gari"
Hapo kidogo nikapumua ingawa sikuwa na uhakika kama kweli Sam aliniita jina pale chini, yule mkaka akaendelea kujiongelesha.
"Naitwa Carlos na nimefurahi sana kufahamiana na wewe Sabrina, je naweza pata mawasiliano yako?"
Nikamuangalia Sam aliyekuwa amesimama kwakuwa yeye hakupata siti, macho yangu yakagongana na macho ya Sam akanikonyeza na kutabasamu nami nikainama chini kwa aibu.
Yule mkaka akaniongelesha tena,
"Naomba namba yako ya simu Sabrina"
Nikampa jibu la haraka hata bila ya kufikiri mara mbili,
"Sina simu"
"Sawa bhana Sabrina, milima haikutani lakini binadamu hukutana"
Tukafika kituoni na kushuka.

Sam akanisindikiza hadi nyumbani mlangoni kabisa, alihakikisha nimeingia ndani ndipo akaondoka.
Nilimkuta dada akijilalamisha ndani,
"Sijui mkaka wa watu akitokea tena kunidai yule mdoli wake nitafanyaje?"
"Hakuna la kufanya Penina, maji yakimwagika hayazoleki. Ukimuona mwambie ukweli tu huenda akaelewa"
Nikawasalimia pale na kwenda chumbani kwangu.
Baada ya kuoga na kula nilikaa nao pale sebleni ambapo baada ya muda wakainuka na kwenda kulala kwani ilikuwa ni usiku.
Nilikaa nikiwasiliana na Sam kwa njia ya ujumbe mfupi ila kichwani ilikuwa inanijia sura ya Carlos mkaka niliyekutana nae kwenye daladala.
Mara nikasikia kama vile kuna watu pale sebleni wakizungumza ila sielewi maneno yao wala wao hawaonekani. Nikaamua kwenda chumbani kwa uoga.

Nilipokuwa chumbani nikampigia simu Sam ili nijiliwaze kwanza.
Ila simu ya Sam ilikuwa inatumika, nikimtumia ujumbe anajibu ila simu yake ukipiga inatumika. Nikapatwa na wazo kuwa Sam anaongea na Lucy tu, nikajaribu kumpigia Lucy nae namba yake ilikuwa inatumika kwakweli nikaona Lucy anataka kuninyang'anya tonge mdomoni kabisa yani.
Nikawaza sana na usingizi kunichukua.

Nikamuona yule mkaka wa ndotoni akimkabidhi Lucy ile keki na juisi, halafu akaniangalia na kusema.
"Umekataa kabisa hata kuonja zawadi niliyokufungia Sabrina? Kila zawadi yangu huitaki ila najua kuwa ipo siku utakayopokea zawadi yangu kwa moyo mweupe na kuitumia, na hapo utakuwa wangu milele"
Akawa anatabasamu.
Nikashtuka gafla na jina la kwanza kunitoka mdomoni ni,
"Carlos"
Nikakaa ni kujiuliza kuwa kuna mahusiano gani na Carlos kijana niliyekutana nae kwenye daladala na huyu mwanaume wa ndoto zangu? Nikajiuliza maswali mengi na kukosa majibu, na je Lucy yeye anahusika vipi na huyu mkaka wa ndotoni.
Maneno ya yule mkaka kwenye daladala yalikuwa yakitembea akilini mwangu kuwa milima haikutani lakini binadamu hukutana.
Nilitamani nitoke chumbani ila zile sauti za sebleni zilinitisha.
Mara nikahisi kama vile kuna mtu anatembea tembea karibu na mlango wangu, uoga ulinishika nikajifunika sana shuka na kupitiwa na usingizi hadi kuna kucha.

Kesho yake sikutaka kupoteza muda, nilimpigia simu Suzy ili nipate kumueleza mambo aliyonitenda Lucy.
Nikiwa namngoja Suzy aje, nilimfata dada Penina na kumuuliza maswali yangu baadhi.
"Eti dada, mwanamke anayeweza kucheza sana mziki ndio anapata mchumba kiurahisi?"
Dada akacheka sana,
"Ingekuwa hivyo basi wale wanenguaji wa kwenye bendi wote wangekuwa wameshaolewa. Kucheza muziki sio kumridhisha mume, zipo njia za kumfanya mwanaume afurahi kuwa na wewe."
"Njia zipi hizo?"
"Maswali mengine kamuulize mamako huko anatamani kweli kuulizwa maswali hayo."
Mama akasikia na kuuliza,
"Maswali gani tena?"
"Mwanao anataka kujua njia za kumridhisha mume"
Halafu akacheka, mama akaniita.
"Sabrina mwanangu mbona unapenda kuharakia mambo? Muda ukifika utaambiwa yote."
"Ila mama sidhani kama kuna ubaya nikijua hata kidogo."
"Ameshaanza kukuchanganya huyo Sam mwanangu, maana wewe hata husikii unachoambiwa. Nitakufundisha siku ukija kumtambulisha mwanaume mwingine tofauti na Sam hapa nyumbani kwangu"
Ikabidi nitulie kumngoja Suzy afike nyumbani.

Suzy alipofika nikamsimulia jinsi Lucy alivyofanya nyumbani kwa Sam na vile alivyoacha pochi yake.
"Shoga yangu, ukicheka na nyani utavuna mabua. Nilishakwambia kama Lucy si mtu mzuri ila wewe unamchekea tu, shauri yako"
"Sasa nifanye nini jamani Suzy?"
"Kwanza umekosea sana kuiacha pochi ya Lucy nyumbani kwa Sam, hujui kama unampa nafasi ya kujitawala? Bora ungeondoka nayo mwenyewe"
Hapo hapo nikaona kuwa itakuwa ni vyema kama tukifata ile pochi kwa Sam kabla Lucy hajaenda ili nimpigie simu na kumwambia kuwa aifate nyumbani kwetu.

Suzy akanisaidia kuaga kwa mama ila hatukusema kama tunaenda kwa Sam.
Safari ikawa moja kwa moja kwa Sam, na ile kufika tu, kwa mbali nikamuona mtu kama Lucy akitoka mule ndani kwa Sam huku jasho likimtoka.
Nikamuacha Suzy akiwa kaduwaa pale nje nami nikakimbilia chumbani kwa Sam ili kumuona Sam ana hali gani.
Nikamkuta Sam amelala kitandani ila akiwa hajitambui kabisa, ikabidi nimuite Suzy ili aje kusaidiana nami mule ndani na tujue Sam kapatwa na tatizo gani.
Ila hakuingia Suzy kama nilivyotarajia, bali aliingia mkaka. Kumuangalia ni yule Carlos wa kwenye daladala.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 09

Ila hakuingia Suzy kama nilivyotarajia, bali aliingia mkaka. Kumuangalia ni yule Carlos wa kwenye daladala.

Nikashtuka sana na kuanza kutetemeka kwa uoga, nikainuka na kujibanza ukutani kama vile nauomba ukuta ufunguke nitoke nje mara Suzy akaingia nyuma yake na kusema.

"Nimeona mkaka huyo anapita, kwajinsi ulivyoniita kwa nguvu nikajua lazima kuna matatizo ndio nikamuomba atusaidie. Mbona umejibanza ukutani sasa?"

Nikawa kama mtu aliyetoka ndotoni, nikamuangalia yule kaka ambaye alikuwa akiniangalia na mimi.

"Wewe si Carlos wewe?"

"Ndio mimi ni Carlos kwani kuna tatizo?"

"Hapana, si tulikutana kwenye daladala jana?"

"Ndio tulikutana Sabrina, hata hivyo milima haikutani binadamu hukutana. Tumsaidie mwenzetu kwanza."

Akainama na kumnyanyua Sam, ila bado sikupenda kusaidiwa na yule Carlos ingawa tulifatana nae hadi kwenye gari ambayo ilikuwa kama inatungoja sisi.

Sam akawekwa kiti cha nyuma ambapo nilikaa nae halafu Suzy na yule mkaka walikaa siti za mbele, gari ikaanza kuondoka huku yule mkaka akidai kuwa tunaenda hospitali.

Kufika njiani, Sam akazinduka ambapo alidai kuwa kichwa kinamuuma sana na hata hakuweza kuongea zaidi. Yule mkaka akasimamisha gari na kusema kuwa tumnunulie dawa ya kutuliza maumivu ya kichwa kwanza kabla ya kufika hospitali, kwakweli hata sikujua alikuwa na lengo la kutupeleka hospitali gani.

Gari ikasimama karibu na duka la madawa, Suzy akashuka na kununua dawa na maji kisha tukampa Sam anywe. Alipokunywa tu akasema kuwa amepona na kichwa hakimuumi tena na akachangamka sana kupita maelezo huwezi hata kusema kuwa alianguka, yule mkaka akageuka na kutuuliza.

"Kuna haja ya kwenda hospitali tena?"

Sam akajibu tena kwa uchangamfu wa hali ya juu,
"Hakuna haja, kama aliyekuwa anapelekwa hospitali ni mimi basi hakuna haja maana nimeshapona kabisa"

Nikamuangalia Sam kwa makini.
"Usiseme haina haja Sam, tumekukuta na hali mbaya sana unatakiwa ukapime. Kwani nini kilikupata?"

"Hata sijui kilichonipata."

"Kama hujui basi inabidi twende hospitali ili tujue nini tatizo."

"Haina haja bhana"

Nikaona kama nachezewa mchezo tu hapa yani Sam tuliyemkuta hoi hajitambui kabisa eti saa hizi anakataa kwenda hospitali, nikajua lazima kuna kitu kimejificha. Swali jingine likanijia kuwa yule Lucy aliyekuwa anatoka chumbani kwa Sam muda ule huku akitokwa na jasho alikuwa ametoka kufanya nini.

"Na Lucy alivyotoka chumbani kwao, mlikuwa mnafanya nini au alikufanya nini?"

Sam akajifanya kushangaa,

"Lucy!! Sijamuona Lucy ndani kwangu mimi"

"Eti Suzy hukumuona yule mdada aliyetoka kwenye chumba cha Sam?"

"Mmh! Sikumuona mtu kwakweli ila nilishangaa kukuona wewe ukikimbilia lile eneo la tukio"

Hapa ndipo walipozidi kunichanganya jamani, baada ya Sam kukataa kwenda hospitali yule mkaka aligeuza gari na kuturudisha kwa Sam.

"Jamani, nadhani huu ndio mwanzo mzuri wa kufahamiana. Mimi naitwa Carlos na nyie wenzangu nimewasikia majina yenu mkiitana, kuwa huyu Suzy na huyu Sam na Sabrina. Naona S zimetawala hapo"

Sam akacheka na kumwambia Carlos,

"Hata wewe ni mwenzetu, naona una S mwishoni mwa jina lako"

Wakafurahi wote kasoro mimi niliyekuwa na mawazo bado.

Tukaingia ndani wote na wala yule Carlos hakuondoka, bado nikaendelea kujiuliza yani huyu mkaka kutoa msaada ndio anazamia moja kwa moja! Inamaana hana mambo ya kufanya?

Nadhani alicheza na mawazo yangu na kuamua kuaga, kisha akamuomba Sam namba ya simu alipopatiwa akaondoka.

Nikaangalia kwenye meza ya Sam na kuona kuwa pochi ya Lucy bado ipo, nikamwambia Suzy.

"Pochi yenyewe ya Lucy hiyo hapo"

"Mpigie simu aje kuifata hata wakati tupo wote, na ilete tuione"

Nikampigia Lucy simu aje na wala hakupinga, alisema kuwa anakuja na mimi nikamngoja kwa hamu ili nimuone atakavyokuwa.

Nikachukua ile pochi ya Lucy na kumkabidhi Suzy aiangalie kama alivyohitaji.

Suzy alishika ile pochi na kulala usingizi wa ajabu huku ile pochi ikiwa mkononi, alilala na kukoroma kabisa hadi mimi na Sam tukawa tunamcheka jinsi alivyokuwa akikoroma.

Mara mlango ukagongwa, nami nikaenda kufungua. Aliingia Lucy akiwa na nguo zile zile nilizomuona nazo awali, nikawa namuangalia kwa makini ambapo aliingia moja kwa moja ndani.

"Pochi yenyewe iko wapi?"

Nilishindwa kumjibu kwani nilikuwa nikimshangaa bado, Sam akamuonyesha kuwa ipo mikononi kwa Suzy, hapo Lucy akainama na kuibeba ile pochi.

"Mimi hata sio mkaaji jamani, tutaonana siku nyingine"

Akatoka na kuondoka, ni hapo Suzy nae akaamka.
"Mmh! Usingizi wa ajabu huu sijui hata umetokea wapi jamani. Hebu tuondoke Sabrina"

Kwakweli bado nilikuwa nachanganywa na vitu kichwani jamani kuhusu Lucy. Suzy akainuka na kunikazania kuwa tuondoke, ikabidi tumuage Sam ambaye aliamua kutusindikiza.

Kufika kituoni, tukaona gari ikisimama na akashuka Carlos kisha akatufata na kuomba kutupa lifti. Sam akakubali kwani alimuona Carlos kuwa mtu mwema, kisha mimi na Suzy tukapanda ile gari. Nikamuomba huyo Carlos anipeleke mimi kwanza kisha Suzy afatie.

Suzy nae akahamaki kwa mshangao,

"Kheee! Kwanini asitangulie kunipeleka mimi halafu wewe ufatie?"

"Mi naona itakuwa vyema akianzia kwetu."

Carlos akacheka kwa yale mabishano yetu.

"Mbona mnaniogopa jamani? Mimi sio chinja chinja bhana, muwe huru tu."

Nikajifikiria na kuendelea kusisitiza kuwa nipelekwe mimi kwanza, mwisho wa siku akakubali.

Ile kufika kwetu gari ikasimama, wakati nashuka tu Suzy nae akashuka akidai kuwa hawezi kuongozana na mtu asiyemfahamu halafu peke yake ila Carlos aliendelea kusisitiza kuwa ampeleke tu. Mara dada yangu Penina alikuwa anatoka ndani na kutukuta pale nje tukibishana, akauliza na tukamwambia tunachobishaniana.

Dada Penina akamuangalia Suzy na kumwambia,
"Suzy, hebu panda twende wote hata mi nimefurahi kujipatia lifti hapa nje."
Ikabidi Suzy arudi tena ndani ya gari na dada na kuondoka.

Nikiwa ndani tumekaa na mama baada ya kula chakula na kufanya mambo mengine, mama akaanza kunilalamikia kuhusu dada.

"Siku hizi Penina amebadilika sana sijui hata ana matatizo gani na yeye."

"Kwani naye anawehuka kama mimi?"

"Hapana ila ananiletea marafiki wa ajabu sana, leo alikuja na rafiki yake mmoja hivi yani ile kumuona tu hadi nywele zimenisisimka. Nikamuuliza Penina kama yule ni mtu wa kawaida kweli, akadai ndiye aliyempa zawadi ya mdoli eti hakuamini kama mdoli alichomwa ndio alikuja kuhakikisha"

Dada Penina nae akawa amerudi na alifikia moja kwa moja kwenye maongezi yetu.
"Unajua mama hata mi mwenyewe nimepatwa na mashaka na yule kijana, macho yake yapo juu juu halafu sina hata mawasiliano nae"

"Ulimkutia wapi sasa hadi kuja nae hapa nyumbani?"

"Nilimkuta stendi ndiyo kumueleza na kuja nae hapa, mmh unavyosema sio wa kawaida hadi unanitisha mama."

"Mnajiokotea tu marafiki wanangu, huenda akawa ni jini? Loh! Kutuletea majini hapa nyumbani wa nini?"

"Mmeshaanza na stori zenu za majini tena! Mngejua ambavyo sizipendi hata msingeendelea."

Mama na dada wakacheka na kunitania kuwa mimi ni muoga tu.

Wakati wa kulala sikuweza kuendelea kukaa pale sebleni kwani mambo mengi yalitawala kichwa changu, nikaenda chumbani kwangu na kuona kama chumba changu kimekuwa kikubwa sana halafu mara nyingine nilihisi kama vile kuna uwepo wa mtu chumbani mule.

Hofu ilikuwa imenijaa moyoni nikaamua kumpigia Sam simu ambapo niliongea nae na kujilidhisha kuwa yu salama huku nikitafuta usingizi bila kujenga mawazo kichwani mwangu, kisha nikalala.

Nikaona nipo kwa Sam, nikiwa na Suzy pale nje kama tulivyokuwa mchana na kumuona mtu akitoka chumbani kwa Sam ila hakuwa Lucy kama ambavyo nilimuona mchana bali alikuwa yule kijana wa ndotoni.


Halafu wakati nimempigia Lucy kuwa aje achukue pochi yake, aliyekuja hakuwa Lucy bali ni yuleyule mkaka.

Kumbe na ile pochi haikuwa pochi kama tulivyokuwa tukiiona bali lilikuwa ni jiwe linalowaka sana ndiomana Suzy alipoichukua ila aiangalia akashikwa na usingizi wa ajabu. Yote hayo nilikuwa nayaona
wakati nimelala.

Nikawa mahali pengine, hapo nilikuwa nimekaa chini akatokea yule mkaka wa ndotoni na kusema.
"Asante Sabrina, leo nimefika kwenu."

Nikashtuka gafla kutoka ndotoni, hofu ikazidi kunijaa na uoga kunitawala nikaanza kujiuliza kuwa je huyo mkaka ndio yule ambaye mama alisema kuwa alikuja nyumbani na dada Penina au ni Carlos.

Bado nilikuwa na maswali mengi kichwani, mara nikasikia mtu akicheka mule chumbani kwangu hapo ndipo uoga hunitawala yani kati ya mambo yote usiombee kifanyike kitu ambacho hukioni kwa macho ya kawaida eti unasikia sauti tu ila ubaya zaidi ni kumuona afanyaye kama si binadamu wa kawaida unaweza ukazirai.

Kile kicheko kiliniogopesha sana, mara gafla kikatulia nikaamua kuchukua simu na kumpigia Sam ambapo niliongea nae hadi kunakucha ili kujiridhisha na uoga wangu.

Kesho yake jambo la kwanza likawa ni kumpigia Lucy simu ili niweze kujibiwa maswali yangu. Ila simu haikupokelewa, nikaendelea na kazi zangu na badae Lucy akanipigia nami nikaanza kumuuliza alichokuwa anafanya kwa Sam jana ni kitu gani, Lucy akashangaa sana na kukataa kuwa jana hakuja kwa Sam.

"Acha uongo Lucy, nimekuona kwa macho yangu."

"Si kweli Sabrina, mara ya mwisho kuja kwa Sam ni siku ile uliyonifukuza. Tangia hapo sijafika tena kwa huyo Sam wako."

"Na ile pochi uliyoisahau siku ile si ndio uliifata jana Lucy?"

"Hapana, mi sijafika huko jana. Hata hivyo siku ile sikusahau kitu chochote huko sasa ningekuja kufata nini? Na pia nisamehe kwa siku ile, nilighafirika tu shoga yangu."

Nilikata simu na kuanza kujiuliza maswali kuwa inamaana ndoto niliyoota usiku ni ya kweli, vipi sasa ile ndoto niliyoota kwa Sam? Mbona alikuja Lucy siku hiyo na amekubali kuwa alikuja ila ya jana anakataa inamaana yule mkaka alijigeuza na kuwa Lucy? Hapo hofu ikanitawala na hata sikujua cha kufanya kwa muda huo. Nikatamani kumueleza mama ila maelezo yakawa yanagoma hata sikujua ni kwanini.

Jioni yake nilipigiwa simu na Suzy, akaanza kunieleza kuhusu Carlos.

"Yule mkaka alitaka namba zako jana ila nimemnyima"

"Vizuri sana, najua Sam nae hawezi kumpa namba zangu. Vipi dada Penina jana mlimuacha wapi?"

"Alishukia njiani, ila mimi nina mashaka na yule Carlos"

"Mashaka gani hayo?"

"Ngoja nimchunguze kwanza, nikipata jibu nitakwambia"

Mara nikamsikia dada yangu kama akipiga kelele hivi za kuniita, nikaacha kuongea na simu na kumkimbilia ili kujua kuwa nini tatizo.

"Mambo ya ajabu mdogo wangu."

"Yapi hayo?"

"Angalia mwenyewe"

Ilikuwa ni kwenye kompyuta yake kuna picha kama ile niliyomtolea mwanzo, akaniomba nimtolee tena.

Nikawa najaribu kuitoa, mara ikawa na sura ya yule mkaka wa ndotoni nikajikuta nikiacha na kukimbilia sebleni.

Nikawa kama vile sijielewi kwa kile kinachotokea, nikasikia simu yangu inaita nikaenda kuichukua, kuangalia namba mpya nikaipokea.

"Mambo vipi Sabrina?"

"Nani mwenzangu?"
"Carlos anaongea hapa."

Nikapatwa na mshtuko kuwa ameitoa wapi namba yangu. Nikiwa nawaza hilo, mara macho yangu yakatizama ukutani nikaona imebandikwa picha ya yule mkaka wa ndotoni.

Itaendelea
 
SEHEMU YA 10


Nikapatwa na mshtuko kuwa ameitoa wapi namba yangu. Nikiwa nawaza hilo, mara macho yangu yakatizama ukutani nikaona imebandikwa picha ya yule mkaka wa ndotoni.

Uoga ukatawala moyo wangu na kuanza kutetemeka, sikuweza tena kuendelea kuongea na ile simu.
Hofu ilizidi pale nilipoona kuwa ile picha ina tabasamu, uoga ulijaa zaidi nikaanza kupiga kelele na kuangusha simu yangu maana nilikuwa nimesimama basi ikaanguka hadi chini.

Mama aliyekuwa jikoni akakimbilia chumbani kwangu kujua kuna nini,
"Picha mama"

"Picha imefanyaje?"

Nikamuonyesha pale nilipoiona ile picha ila haikuwepo tena.
"Inamaana uchizi wako umekurudia?"

Dada nae akaja chumbani,
"Mbona makelele Sabrina?"

Nikawa kimya, mama akanishika mkono na kunivutia sebleni ili kunipa moyo na kunipunguza uoga.
"Kwani unaizungumzia picha gani Sabrina?"

Dada nae akadakia,
"Tena Sabrina asante kwa kunitolea ile picha maana ilikuwa inanikera kweli yani"
Nikawa nashangaa kuwa nimeitoaje wakati ilinishinda kuitoa.

"Inamaana ile picha imetoka? Ila mi sijaitoa kwakweli"

"Sasa nani ameitoa?"

Bado nilikuwa natetemeka kwa uoga, nikakumbuka kuwa simu yangu ilianguka. Nikamuomba dada anisindikize chumbani kwangu nikaichukue ile simu, nikakuta kila kitu kipo kivyake. Nikaiokoto na kuviunganisha, kujaribu kuwasha ikawa haiwaki dada akaniambia.

"Ishaharibika hiyo teyari, hakuna mawasiliano tena pole sana"

Roho iliniuma kweli kwa kuharibikiwa na ile simu ambayo nilikuwa naipenda.

Tukawa tumekaa sebleni, nikamuomba mama kuwa nitalala nae siku hiyo na muda wa kulala ulipofika nilienda kulala kwa mama.

Wakati tumelala nikamsikia mtu akiniita kwa sauti ya chini chini.

"Sabrina, Sabrina"

Nikashtuka usingizini, nikasikia tena akiniita, hapo uoga ukanishika. Nikamsogelea mama na kumkumbatia, nikahisi mtu akinishika mgongoni huku akiendelea kuniita, uoga ulinitawala kwani nilishindwa hata kujigeuza, nilikazana kumkumbatia mama kwa nguvu na sikumuachia kabisa, ndipo mama nae akashtuka.

"Kwani kuna nini Sabrina?"

Huku nikitetemeka kujibu,

"Kuna mtu mama"

Mama akainuka na kwenda kuwasha taa.

"Angalia sasa, yuko wapi huyo mtu? Hukupona wewe."

"Mama, alikuwa ananiita kabisa."

"Akuite nani usiku huu mwanangu? Mchawi? Maana wachawi ndio wanamchezo wa kuita watu usiku."

"Labda ni wachawi kweli mama, maana nilikuwa nahisi kuguswa mgongoni."

"Labda mzimu wa babako umekuja kututembelea leo"
Kauli ya mama ikanipa uoga zaidi, hata sijui kwanini yeye hakuogopa kuongea kauli kama zile usiku. Akataka kwenda kuzima taa tena, nikamshikilia kuwa asizime taa.

"Unaogopa nini Sabrina? Mbona mimi siogopi kitu?"

"Wewe mkubwa mama"

Akacheka, na kurudi kulala ila sikuweza kulala hadi panakucha. Nilikuwa naona bora mchana kuliko usiku. Kulipokucha kama kawaida dada aliondoka mapema sana kwenda kazini, mimi na mama tukabaki nyumbani. Nikamvizia mama alipokuwa jikoni, nikaenda kuchukua simu yake ili kumjulisha Sam kuwa simu yangu imepata matatizo.

"Sasa itakuwaje Sabrina?"

"Ngoja nipeleke kwa fundi ila sina hela sasa sijui itakuwaje!"

"Ipeleke tu halafu utaniambia gharama za matengenezo nami nitakuletea hiyo pesa Sabrina, usipende kulalamika kitu ambacho mimi nina uwezo nacho"

"Sawa nimekuelewa."

Mama akaanza kuniita kwa nguvu.

Nikaweka simu yake na kumfata jikoni.

"Muda wote nakuita hauitiki au ndio ulikuwa unazungumza na mzimu wa babako"
Ikawa mara ya pili kumsikia mama kuhusu mzimu wa baba ikabidi nimuulize vizuri kuwa ana maana gani.
"Kwani mizimu huijui mwanangu?"

"Mi sijui mizimu mama"

"Mizimu ni viumbe ambavyo vipo tokea enzi za mababu na mababu, ni vigumu sana kumtendea jambo baya mtu mwenye mizimu kwani mara nyingi sana mizimu ile humuepusha nalo au humwambia kabla hajatendewa"

"Sasa mbona unasema mzimu wa baba? Inamaana baba kawa mzimu?"

"Mtu anapokufa huwa hawezi kurudi tena duniani ila kinachoweza kuzunguka na mzimu wa mtu huyo ambao huvaa sura ya muhusika."

"Inamaana kama huo mzimu wa baba utakuwa na tabia za baba?"

"Mzimu ule ulikuwepo na baba yenu enzi za uhai wake, kwahiyo unaporudi kwenu unakuwa kama yeye kwa kuwalinda watoto wake."

"Mmh mama hata sikuelewi, mizimu haitishi kweli?"

"Mizimu inatisha kweli mwanangu. Ipo hivi, kama mtu akimuua mtu asiye na mizimu basi haitampa shida sana ila akiua mtu mwenye mizimu atajuta maisha yake yote kwani itamtokea mara kwa mara na kumtesa."

"Kheee mama!! Na utajuaje kama huyu mtu ana mizimu au la? Mi naogopa sana"

"Usiogope mwanangu, kwenu kuna mizimu sana ipo siku nitakueleza vizuri zaidi. Baba yenu wakati wa uhai wake alikuwa akioteshwa na kuona mambo mengi sana yatakayotokea au kama yaliyotokea yametokea kwa sababu ipi. Ipo siku nitakwambia vizuri tufanye kazi kwanza."

Habari hii ya mizimu iliniingia sana akilini na kujikuta nikitamani kujua zaidi na zaidi, kama mizimu inatisha mbona mama anaitaja bila hofu na hata haogopi chochote? Nilitamani kujua mengi zaidi kuhusu hili jambo.

Baada ya kazi zote, alirudi dada Penina na leo tena aliwahi kurudi na kuanza malalamiko yake ya majini.

"Yani leo mama ndio live bila chenga tumekula chakula na majini"

"Ulikuwa na nani, halafu mmejuaje?"

"Nilikuwa na Fatuma mama, yani tumeagiza chakula kingi hilo ila hata hatujashiba. Fatuma akasema hatujasali ndomana hatujashiba, eti bila kusali majini yanakuja na kufakamia chakula."

"Na nyie mmezidi uroho, ila hizo ni imani tu. Ndio mkumbuke kusali kabla ya kula, maneno kidogo tu yatakusaidieni na kuwaepusha na vitu vibaya."

"Ndio, Fatuma kaniambia kuwa nikiona shida kufanya sala ndefu basi niseme Bismillah tu inatosha"
Mama akacheka sana,

"Wavivu utawajua tu"

Dada akainuka na kwenda kubadili nguo na mimi nikaendelea kutafakari kuwa kuna mambo mengi hapa, kwanza mizimu na pili majini kwakweli hali sio nzuri.

Usiku kama kawaida ilikuwa ni mtihani kwangu, leo mama akaniambia nilale mwenyewe na nisiwe na uoga wowote kwali ameshaniombea tayari. Nikamuomba dada tuangalie picha ya ngumi kwanza, ilivyoisha nikaingia chumbani kwangu na kulala kwani sikuwa na simu tena ya kuweza kuwasiliana na Sam.

Niliacha taa inawaka na kujifunika shuka gubigubi, usingizi haukukawia kunichukua. Nilikuwa mahali kwenye nyasi nyingi nimekaa, huku nikisikia sauti ya mtu akizungumza na mimi.

"Sabrina, Sabrina. Wewe ni binti wa kipekee sana, unatakiwa uishi maisha ya kimalkia mwanadamu wa kawaida hawezi kufanya wewe uishi kama unavyotakiwa kuishi"

Nikashtuka toka usingizini, sauti nyingine ikaniambia kuwa nichungulie dirishani.

Nikasikia sauti ya paka nje, nikajua sauti inayoniambia nichungulie inataka nimfukuze yule paka.

Nikainuka na kufunua pazia la kwenye dirisha kwa uoga, nikamuona yule mkaka wa ndotoni amesimama karibu na dirisha halafu macho yake yanawaka kama taa.

Nikafunika lile pazia kwa uoga, nilihisi kutetemeka. Sauti nyingine ikasikika,
"Unaogopa nini Sabrina? Huyo ndio mumeo."

Nilizidi kutetemeka kwa uoga, nilitamani hata nibadilishiwe mazingira. Wakati natetemeka, upepo ukaanza kuvuma chumbani kwangu kama vile niko nje, nilikuwa nimejikunyata kabisa mara nikasikia sauti ya paka tena,

"Nyau.... Nyaaau.... Nyaaau.... Nyaaau"

Kama vile yule paka ameingia ndani, nikazidi kutetemeka kwa uoga na gafla taa ikazimwa, halafu sauti ya yule paka akilia ikatawala chumba changu chote kwa hapo sikujua kilichoendelea tena jamani kwani nilizimia.


Niliona tu kumekucha na mama akiwa chumbani kwangu.

"Leo tena yamekupata yanayokupataga mwanangu?"

"Mama leo ndio makubwa zaidi, nilizimiwa hadi taa"

Mama akacheka sana kama kawaida yake,

"Nani akuzimie taa mwanangu? Uoga wako tu, umeme ulikatika leo"

Kwakweli chumba changu niliona kichungu wala maneno ya mama sikuyaelewa. Mchana nikatoka nyumbani na kumpelekea fundi simu ile simu yangu kwani jana yake sikupata muda.

Niliporudi nyumbani nikabambana na maswali ya mama kuwa nimetoka wapi, nikamwambia kuwa nimetoka kwa fundi simu.

"Amekwambia sh. Ngapi?"

"Amesema ni elfu ishirini, simu ile imevunjika kioo cha ndani na nini sijui gharama yake ndio elfu ishirini"

"Unayo hiyo hela au unamtegemea yule pangu pakavu tia mchuzi wako akupe?"

"Mmh! Ndio nani huyo mama?"

"Si huyo Sam wako ambaye akijikuna anatoka unga, labda akakope. Na mimi ndio usifikirie kabisa kama nitakupa hiyo pesa"

"Mmh! Mama nawe unamdharau sana Sam"

"Nisimdharau ananisaidia nini hapa zaidi ya kero na karaha tu"

Nikaona kuzidi kuongea na mama kuhusu Sam ni kujiumiza mwenyewe ikabidi niwe kimya tu.

Badae nikamvizia mama na kuchukua simu yake kumpigia Sam kwani fundi alitaka na pesa ya kianzio kwanza ambayo sikuwa nayo kwa wakati.

Nikaongea na Sam na kumueleza kuhusu zile gharama,
"Sijui kama unaweza kuniamini Sabrina"

"Kukuamini kitu gani?"

"Bosi alinipa pesa za ofisi nikarudi nazo hapa nyumbani ili nipeleke benki, nimeenda kuoga ile kurudi sijakuta sh. Kumi yani kwa kifupi nimeibiwa wakati mlango niliufunga hata sijui cha kufanya, nimechanganyikiwa hapa. Halafu......."

Mama akanikuta nikiongea na simu yake akanipokonya na kuikata.

"Simu yangu ni muhimu kuongea na watu muhimu sio hao wachuja nafaka kama huyo Sam wako"
Nikatamani mama anipe simu ili nimuulize vizuri Sam kitu ambacho kimemsibu, ila sikuweza kwavile sikuwa na simu tena na wazo la kuikomboa simu yangu kwa fundi likapotea.

Nilikuwa ndani nimetulia, mama akaniambia kuwa nje kuna mgeni wangu amekuja kuniulizia. Nikatoka nje kwenda kumuangalia ni nani.

Nikamkuta ni Carlos akiwa amesimama, nikasalimiana nae na maswali mawili matatu kisha akasema kuwa ameniletea zawadi, akafungua gari lake na kunitolea.

Kuangalia zawadi yenyewe ni simu, ikabidi nimuulize kuwa mbona kaniletea simu.

"Kwavile simu yako ilianguka na kuharibika nimeona ni vyema kukuletea nyingine."

Nilishtuka na kujiuliza amejuaje kama simu yangu ilianguka? Wakati hata Sam sikumwambia kama imeanguka zaidi ya kusema imeharibika tu?

Wasiwasi ukanijaa juu ya Carlos, nikataka nikimbilie ndani kwa mama. Nilipogeuka ili kuondoka tu akanishika mkono na mkono wake ulikuwa wa baridi sana.

Itaendelea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom