Simulizi ya Kijasusi: Hakuna aliye Salama

Simulizi ya Kijasusi: Hakuna aliye Salama

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
34,061
Reaction score
79,423

HAKUNA ALIYE SALAMA

Mtunzi: Robert Heriel

0693322300
Chungu cha 01

Kinu alikuwa ameketi kwenye wheelchair, akitingisha kichwa chake kwa taratibu, udenda ukimtoka mdomoni. Macho yake yalikuwa matupu kwa nje, lakini kwa ndani yakiwa kama rada ya kijeshi. Nyuma yake alikuwa amesimama Moreen, mwanamke aliyefunga kilemba na kuvaa mavazi ya kushangaza—mchanganyiko wa Pamba iliyochanika na blauzi ya rangi ya dhahabu iliyopoteza hadhi ya urembo.

Kazi ya Moreen ilikuwa rahisi: kumzungusha Kinu maeneo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam kila siku, kuanzia Posta, Mnazi Mmoja, kufikia Kariakoo na Upanga. Alifanya kazi hiyo kwa moyo wote. Haikuwa kazi rasmi, wala haikuwa ajira ya kudumu—ilikuwa mpango wa muda mfupi, lakini wenye masharti magumu: Usiulize maswali. Usijue sababu. Usizungumze na mtu yeyote kuhusu kazi hii.

Kwa watu wa mitaani, Kinu hakuwa chochote zaidi ya ombaomba. Suruali yake ya kaki ilikuwa na viraka vitano, fulana yake ilikuwa imechanika kifuani na kufuliwa mara nyingi bila sabuni ya kutosha. Machoni mwao, Kinu alikuwa na utindio wa ubongo, huenda ni usonji. Lakini haikuwa hivyo. Kinu hakuwa mgonjwa. Wala hakuwahi kuumwa akili hata siku moja.

Kinu alikuwa Jasusi. Jasusi wa kiwango cha juu, aliyefanyiwa mafunzo ya hali ya juu huko Bulgaria, India na Ujerumani. Alikuwa katika kazi hatari sana, kazi ambayo ilimlazimu kujivika mwili wa maskini, akili ya mgonjwa, na maisha ya kuhurumiwa na kila mtu.

Na Moreen? Hakuwa jasusi. Wala hakuwa na historia yoyote ya kijeshi. Alikuwa msanii wa make-up maarufu ambaye ofisi yake ipo Mbezi Beach, mtaalamu wa kubadili sura za watu, ama kuwafanya waonekane kama malaika au kama mapepo. Kazi yake hapa ilikuwa moja tu: kumpaka Kinu hadi asitambulike. Au Kwa namna yoyote atakayoagizwa na Kinu, boss mpya.

Siku hiyo Moreen alikuwa amemvalisha Kinu mavazi ya ajabu—suti iliyochakaa, viatu vya plastiki visivyofanana, na kofia ya kaniki. Alihakikisha uso wake umejaa vipodozi vya kuharibu sura, akamwekea kovu bandia shavuni. Kinu alionekana kama mtu aliyepoteza kila kitu duniani.

Lakini macho ya Kinu, licha ya udenda, yalikuwa makini. Aliyaelekeza kwenye kila upande wa barabara, akihifadhi kila harakati, kila sura, kila jengo. Akili yake ilikuwa kama kamera yenye uwezo wa kuzoom, kuscan, na kuhifadhi data kimya kimya.

“Unaona yule kijana mrefu mwenye Kofia nyekundu?” Kinu aliuliza kwa sauti ya chini mithili ya mtu anayegugumia mate, huku Moreen akimsogeza karibu na barabara ya Libya, kuelekea Samora Avenue.

Moreen alimtazama yule kijana harakaharaka. “Ndio, anaonekana kama mteja wa kawaida wa mtaa.”
“Anavaa Kofia nyekundu kila Jumatatu, anasimama eneo lilelile kwa dakika 17, huondoka bila kusema na mtu yeyote,” Kinu alisema. “Hana simu, hana begi, lakini anatoka katika jengo la ‘Eagle Holdings’.”

Moreen alikenua midomo. “Na unafikiri ni nani?”
Kinu aligeuza macho yake kuelekea gari jeupe lililoegeshwa kwa umbali kidogo. Kwenye kioo cha mbele kulikuwa na stika ya shirika lisilojulikana. Ndani kulikuwa na mtu mmoja aliyevaa miwani meusi na fulana ya kijani. Kwa macho ya kawaida hakuwa wa maana. Lakini kwa Kinu, huyo alikuwa link ya kwanza kwenye mlolongo wa hatari.

“Kama nitatoweka, Moreen,” Kinu aliongea kwa sauti ya chini zaidi, “usiende nyumbani. Rudi kwa mama yako Mtwara. Usimwambie mtu chochote. Wala usijaribu kunitafuta.”
Moreen alitetemeka. Hakuwa jasusi, lakini tangu aanze kusaidia kazi hii ya ‘kuigiza’ na Kinu, alishaanza kuhisi joto la dunia ya watu wa vitengo vya siri. Na sasa alihisi kuwa hakuwa tena msanii wa vipodozi tu—amekuwa sehemu ya jambo kubwa, zito, na hatari.
“Lakini…” alisema kwa sauti ya kupasua ukimya, “mbona kila mtu anayetuzunguka huwa hacheki? Kama vile wanajua kitu.”
Kinu alimtazama kwa jicho la upande, akavuta pumzi, kisha akasema kwa sauti ya kitetemeshi;
“Kwa sababu wanajua. Na ndio maana nakuambia, Moreen… Hakuna Aliye Salama.”
/


Moreen alikumbuka siku ya kwanza alipokutana na Kinu.
Ilikuwa jioni ya Jumamosi, studio yake Mbezi Beach ilipokuwa imejaa wateja wa harusi. Mwanamke mmoja aliyekuwa na vipodozi vya dhahabu usoni alikuwa anapigwa picha za harusi, wakati mwingine aliyetoka China alikuwa anafanyiwa “skin blend” kwa uso.
Ndipo mlango ulipofunguliwa kwa taratibu. Mtu mmoja mrefu aliingia akiwa amevaa koti refu jeupe, kofia ya mchirizi na miwani meusi. Alikuwa mgeni wa aina yake. Hakuonekana mwenye haraka, hakuwa na sura ya mtu wa harusi, lakini macho yake yaliongea zaidi ya mdomo.

“Wewe ndiye Moreen?” aliuliza kwa sauti ya chini yenye ukakamavu.
“Ndio,” Moreen alijibu kwa mashaka, “unataka huduma gani?”

“Huduma tofauti. Si make-up ya picha, si ya harusi. Tafadhali. Dakika mbili nje tuzungumze"
Moreen hakubisha, aliaga wateja wake kisha akatoka nje.
"Nataka unitengeneze uso wangu kila siku… ili nisiwe mimi. Na pia nikupe kazi nyingine ya ziada, kuniendesha mtaani kwenye wheelchair. Kazi ya siku 21 tu. Nitalipa pesa nzuri.”

Moreen alicheka kwa kejeli. “Hiyo ni kazi ya maigizo?”

“Hapana,” yule mgeni alisema kwa sauti ya kutisha kidogo. “Ni kazi ya maisha na kifo. Sitaki ajue mtu mwingine. Sitaki picha. Sitaki maswali. Sitaki urafiki. Nataka uigize kuwa dada yangu au msaidizi wangu. Kila siku utapewa shilingi laki moja taslimu—kwa siku. Bila kuchelewa.”

Moreen alinyamaza. Shilingi laki moja kwa siku? Alipiga hesabu za haraka, kwa wiki tatu, maana yake alikuwa anaenda kupata milioni mbili na laki moja. Kiasi hicho hakijawahi kupita mkononi mwake kwa kazi ya mteja mmoja. Hakuwa mjinga wa kukataa pesa, lakini hakuwa pia mjinga wa kukubali bila tahadhari.

“Nataka kujua kama hii ni haramu. Kama ni biashara ya dawa za kulevya au silaha, sitaki kujihusisha,” alisema kwa msimamo.

“Hii ni kazi ya nchi. Lakini hutaambiwa mengi. Ukiuliza sana, nitatafuta mwingine"
Kwa moyo wa nusu nusu, sitaki nataka, Moreen alikubali. Lakini alijua, kazi hii ingegharimu taswira yake ya hadharani. Aliamua kuchukua hatua ya kwanza: kubadili uhusika wake kabisa.

Alienda kwenye duka moja la mitumba kule Mwenge, akanunua nguo za kawaida kabisa, alinunua blauzi zisizo na nembo, viatu vya plastiki vya Tanga. Alijifunza kutembea polepole, kumenyeka na kuongea kwa lafudhi ya mtaani. Kila alipokuwa karibu na jiji, alijifunga kilemba kikubwa na kuvaa miwani meusi. Hakutaka hata mmoja wa wateja wake wa mjini amtambue. Alijua mtu mmoja akimtambua, maneno yangetapakaa Instagram na TikTok kama moto wa nyika.

Kazi ilianza.
Kila siku asubuhi, kabla ya saa mbili, Moreen alikuwa anafika eneo la Kivukoni, akimkuta Kinu tayari keshajipaka udenda bandia, suruali yake ikiwa imepiga magoti, na uso wake ukionekana kama wa mtu aliyevurugikiwa akili. Kazi yake ilikuwa moja tu: kumsukuma, kumpeleka mitaani, na kuhakikisha anaonekana kama mtu wa kupuuzwa.

Moreen alizoea kazi hiyo haraka kuliko alivyotarajia. Lakini kila siku, alipomtazama Kinu, alihisi kama kuna kitu kingine ndani yake, nguvu isiyoelezeka, siri nzito ambayo haijafunuliwa, na hatari inayomnyemelea… hata yeye mwenyewe.

Na ndani ya moyo wake, Moreen alianza kuhisi kitu ambacho hakukitazamia: hofu ya kumpoteza mtu ambaye hakumjua vizuri, lakini alimwamini ajabu.
Na kwa mbali, ndani ya kivuli cha jiji, jua lkiwa limemaliza nusu ya anga kuisaka nusu nyingine, macho ya adui yalimtazama Kinu. Walijua anajua. Walijua anatambua. Na kwao, kulikuwa na amri moja tu:

“Mwondoe kabla hajafika mbali.”
/

Jua lilikuwa kali kiasi cha kuunguza nywele zilizofichwa ndani ya kilemba. Moreen alikuwa amechoka. Siku hiyo walikuwa wamepitia maeneo ya Kisutu na sasa walielekea kwenye mtaa wa India Street, karibu na jengo la zamani la usalama wa taifa.
Kinu alikuwa kimya. Alikuwa kama sanamu. Lakini macho yake yalikuwa bize yanafuatilia kila mtu, kila mwendo, kila mlango unaofunguliwa na kufungwa kwa kasi isiyo ya kawaida.
Moreen alikosea njia kwa sekunde chache tu, akasogelea kona ya jengo la ‘Shanaz Towers’ badala ya kupita nyuma ya Askari Monument kama walivyozoea. Ilikuwa ni kosa dogo lakini kwa Kinu, kosa la aina hiyo lilitosha kuamsha tahadhari ya hali ya juu.
“Geuka nyuma,” aliongea kwa sauti ya chini sana, kama mtu aliyekonda kupita kiasi. “Haraka. Sema unataka ice cream pale barazani.”
Moreen alishangaa lakini hakupinga. Aligeuza wheelchair taratibu, kisha akasema kwa sauti ya kuigiza kama mtoto anayeng’ang’ania pipi, “Ngoja twende pale nipate barafu kidogo, jua kali bwana!”
Wakageuka.
Sekunde chache baadaye, gari aina ya Toyota Alphard nyeusi ilipita kwa kasi isiyo ya kawaida, ikapunguza mwendo mbele yao kisha ikasogea hadi kusimama upande wa pili wa barabara. Mwanaume mmoja wa miraba minne alishuka, akavaa miwani meusi na kujifanya kupokea simu, lakini macho yake yote yalikuwa kwao.

“Yule mwanaume… ni wa tatu leo,” Kinu aling’amua. “Wanajaribu kuthibitisha kitu.”
“Wananiangalia mimi au wewe?” Moreen aliuliza huku akizidi kuvuta kitenge chake kujificha zaidi.
“Wote wawili. Ila tatizo ni kwamba… sasa wameanza kuamini kuwa mimi siyo kichaa.

Kabla Moreen hajajibu, simu ya Kinu—ile aliyokuwa ameificha chini ya blanketi la wheelchair—ilitoa vibrate moja ya haraka. Aliichukua kwa ustadi, akasoma ujumbe mmoja tu:
“DEKA-6 IMESHUKA DSM. KATIKA SAA 48, WATAJUA UPO HAI. TOKA ENEO LA KATI MARA MOJA.”
— Kituo-M

Macho ya Kinu yalibadilika ghafla. Aligeuza uso wake kama mtu asiyeelewa chochote, akakumbatiana na udenda wake kama kawaida. Lakini ndani ya akili yake, alishajua: sasa wanamfuatilia rasmi. Na Deka-6, kundi la wauaji wa kimyakimya ambalo lipo ndani ya nchi. Lakini halijulikani, halipo kisheria lakini lilikuwa na nguvu kuliko sheria.
Hawakuwahi kushindwa kazi waliyopewa.


“Moreen,” alisema taratibu. “Leo tunabadilisha mpango. Hatuendi tena Mtaa wa Azikiwe. Tutapitia uchochoro wa India Street, tutapotelea Gerezani. Kuna mtu nitakutana naye huko kwa dakika tatu. Ukiona mtu yeyote anapiga picha, usikubali, nipiganie kama ndugu yako. Ukiona mtu anatoa simu, zibua makelele. Usidharau mtu yeyote.”
Moreen alitaka kuuliza maswali, lakini alijizuia. Alimwelewa Kinu sasa: kila neno lake huwa lina maana zaidi ya linavyoonekana. Kila maelekezo yalikuwa kama kamba ya kuokoa maisha.
Na alipoanza kumsukuma kuelekea kwenye mtaa wa pembeni, walipishana na mwanamke mmoja aliyekuwa amebeba daftari na glasi ya kahawa. Alipowaona, mwanamke huyo alicheka kidogo kisha akawasha Bluetooth earphone yake.
Hakuna kilichoonekana cha ajabu.
Lakini Kinu alisema taratibu:
Huyo mwanamke si mpita njia. Hii vita ina sura nyingi. Na kumbuka nilivyokwambia, Moreen…
Moreen alijibu taratibu kwa sauti iliyotikiswa na hofu:
Hakuna Aliye Salama…
/


Mtaa wa Gerezani ulikuwa kama kawaida — kelele za wasafirishaji, vibaka waliogeuka wajasiriamali, wanawake waliouza chai kwa vikombe vya plastiki, na wauzaji wa vyakula waliopika kwenye ndoo za rangi ya bluu.
Hakuna mtu aliyekuwa anajua kuwa kati ya machinga hao, waliokuwa wakiuza miwani, soksi na vocha za mitandao, kulikuwa na wawili waliotumwa rasmi na Kituo-M, shirika la siri linalopambana na Deka-6 kimyakimya kwa kutumia jasusi wachache waliobaki waaminifu. Kinu alikuwa mmoja wao aliyebaki huru.

“Simamisha hapa,” Kinu alimwambia Moreen. “Mimi nitashuka. Nivute kidogo blanketi la miguuni, kisha geuza uso wako upande mwingine. Usimuangalie mtu. Usisikilize sauti yoyote itakayoita jina lako.”
Moreen alihisi moyo wake ukidunda kwa kasi. “Una uhakika ni salama?”
“Salama haipo. Lakini nina dakika tatu tu. Nikiwa na zaidi ya hizo, najua wamejua nilipo.”
Akatupa blanketi upande wa kushoto, akajigeuza taratibu kama mtu mwenye kupooza viungo vyote. Alishuka kwa msaada wa mikono yake tu, akasogea polepole kama mzigo wa mateso, hadi akajificha kwenye kivuli cha duka la vifaa vya elektroniki lililokuwa limefungwa.
Macho yake yaliangaza upande wa kushoto. Mwanaume mmoja mwenye t-shirt ya Free Palestine alisimama karibu na begi la plastiki. Kinu alimtambua. Alikuwa Mcharo — jasusi wa zamani, aliyefukuzwa kazini kwa kosa la kuvujisha siri, lakini aliendelea kusaidia nchi kwa kificho.

Kinu alipofika karibu, Mcharo hakumwangalia moja kwa moja. Alizungumza bila kumtazama.
“Wako karibu. Unapoteza muda kwa kila sekunde unayobaki hapa.”
“Unajua nani ananifuata?” Kinu aliuliza.
“Sitaki kujua majina. Nasikia tu minong’ono. Watu waliowekwa juu ya mfumo. Nje ya sheria. Nje ya uhalali. Wanaitwa Deka-6. Lakini hakuna anayejua walipoanzia. Hakuna anayefahamu sura zao. Hata vifo vyao huandikwa kama ajali za kawaida au kupotea ghafla.”

Kinu alipumua polepole. “Nahitaji majina mawili. Moja liwe wa mtu anayepeleka taarifa zao serikalini. La pili, mtu aliyeko karibu yangu. Ambaye naweza kuwa nimemwamini vibaya.”
Mcharo alimpa bahasha ndogo ya plastiki, ndani yake kulikuwa na picha moja ya mtu , alikuwa mwanaume wa makamo, mweupe kiasi, uso wa kirafiki, aliyevaa suti ya kawaida. Hakukuwa na jina, lakini picha hiyo ilikuwa kama bomu kichwani mwa Kinu.
Alitazama kwa sekunde tano tu. Kisha akaificha mfukoni.
“Ni yeye?” Kinu aliuliza kwa sauti ya chini.
“Ndio. Na hajui kuwa tayari tumemwona. Lakini yuko na wewe mara kwa mara. Anauliza sana. Anaonekana kupenda kujua unatembea wapi. Uwe makini. Ana macho mawili tu, lakini macho mengine yako kwenye simu yake.”

“Na yule wa pili?”
“Bahasha ya pili iko ofisini kwangu. Ila siwezi kuifikia tena. Jana usiku niliona watu watatu wamekaa kwenye gari jeupe nje ya mtaa wangu kwa saa mbili. Wala hawakushuka. Watakuwa wameniweka kwenye rada pia"

Kinu alikataa kuonyesha hofu. “Ina maana sasa wameingia hata kwenye familia za watu waliostaafu?”
Mcharo alitabasamu kwa uchungu. “Hakuna aliyestaafu kwa hawa watu. Ukijua jambo moja, tayari wewe si salama. Ukijua mambo mawili , basi umeshahukumiwa kifo. Unachongoja ni siku tu ya utekelezaji.”
Kinu alitaka kuuliza zaidi, lakini akasikia tone la kengele kwenye sikio lake la kushoto. Saa yake ya ndani ilikuwa imetimia , dakika tatu zilikuwa zimepita.

Akaanza kurudi taratibu.

Moreen bado alikuwa amegeuza uso wake. Hakumwangalia. Hakumsalimia. Alikuwa mtiifu kwa kiwango kisichoelezeka.
Lakini alipompandisha Kinu tena kwenye wheelchair, Moreen alisema kwa sauti ya kuongea mwenyewe na upepo;
“Watu wawili walipita hapa. Wote walikuwa na glovu nyeusi. Mmoja aliinua simu, mwingine akatoa sigara bila kuitia mdomoni. Walikuwa wakikuangalia.”
Kinu alijua kilichomaanishwa.

Glovu nyeusi, alama ya wajumbe wa Deka-6. Hawajifichi. Hawana haraka. Wanakufuata hadi uanze kuwa na wasiwasi mwenyewe.
“Leo,” Kinu alisema kwa sauti ya polepole, “tutarudi kwa njia ndefu. Tutapotea kwenye mitaa ya Mchikichini, halafu tutaunganisha hadi Mbagala kwa bajaji. Usilalamike. Usiongee.”
Moreen alimuangalia kwa jicho la mashaka. “Una uhakika tutakuwa salama?”
Kinu alijibu baada ya sekunde chache:
“Hata sielewi tena kama tutakuwa salama. Maana sasa naanza kuamini… hata sisi wenyewe… huenda tumeshatekwa kiakili.”
Wakaondoka.

Mbali kidogo, juu ya jengo la ghorofa moja, kamera ya usalama ya kibinafsi iliwafuata hatua kwa hatua. Mtu mmoja aliyekuwa kwenye chumba cha kuangalia ‘live footage’ alibonyeza kitufe kimoja. Kisha akatuma ujumbe mfupi kwa anwani iliyosajiliwa kwa jina bandia.

Ujumbe ulisomeka:

"Mzee Ameridhia. Muda umeiva. Mchakato uanze kesho. Moreen awe wa kwanza."

Itaendelea..
 
HAKUNA ALIYE SALAMA
Mtunzi, Robert Heriel
+255693322300

Chungu 02

Moreen alikuwa ndani ya bajaji, akiwa na Kinu. Walikuwa wametokea Gerezani kupitia njia za Mchikichini na sasa walikuwa wanakatiza maeneo ya Chang’ombe kuelekea Temeke kwa mzunguko wa tahadhari.
Alikuwa kimya sana, tofauti na siku nyingine. Kinu alihisi kuwa kimya chake kilikuwa na ujumbe mzito. Mara kadhaa alitaka kumwambia atulie, lakini akajizuia. Alijua, mwanamke anayepambana na hofu bila kilio, anahitaji nafasi ya kujiweka sawa. Sio huruma.
Lakini dakika kumi baadaye, walipofika karibu na mtaa wa Mtoni Relini, simu ya Moreen ikalia.
Namba haikuwa imehifadhiwa. Moreen hakuwa anaijua namba hiyo.

Akaitazama. Kisha akampa Kinu Simu.

Kinu aliipokea, akabonyeza speaker, lakini hakusema neno. Kulisikika sauti ya kiume, iliyopoozwa sana, kana kwamba ilikuwa imerekodiwa kabla:
“Hii bajaji uliyopanda ina watu wa tatu waliokuja nayo. Dereva si dereva halisi. Simama baada ya mita 200. Pitia upande wa kushoto kuna nyumba ya udongo yenye namba ya nyeupe, hiyo ni salama kwa dakika saba tu. Moreen, usijesema neno. Kinu, usifanye kosa la kupiga kelele. Sisi ni wengi kuliko unavyodhani.”
Simu ikakatika.
Moreen alipigwa na butwaa. Miguuni alianza kutetemeka. Kinu alichomoa bastola yake ndogo ya mkunjo kutoka ndani ya blanketi, kisha akainama taratibu, kana kwamba ananyoosha mguu wake wa kupooza. Akamwambia Moreen kwa sauti ya chini:
“Pindi nikuambia ‘sasa’, jirushe kutoka kwenye bajaji upande wa kushoto. Ukivunjika, bora upone ukiwa hai kuliko kufika waliko.”
Walikuwa bado ndani ya bajaji, dereva alikuwa anaendesha bila kusema hata neno moja. Hakutazama kioo cha nyuma hata mara moja. Kitendo hicho kilimpa Kinu ujumbe: huyu mtu si dereva wa kawaida. Alikuwa amefundishwa. Huyu ni mtu wa Deka-6.
Bajaji ilipokatiza mbele ya duka moja la mbao lililokuwa limefungwa, Kinu alisema taratibu lakini kwa msisitizo:
Sasa.
Moreen hakuwahi kulazimishwa kuruka kwa dharura kabla ya hapo. Lakini hofu ikamfanya afanye maajabu. Alijirusha nje, akatua vibaya kwenye kiuno chake lakini bado alikuwa anapumua. Kinu alimtazama kwa sekunde mbili, kisha akarusha bastola juu kwa ustadi, ikatua juu ya paa la duka lililokuwa pembeni. Kisha naye akajirusha nje ya bajaji.
Bajaji haikusimama.
Iliendelea mbele kana kwamba hakuna kilichotokea, lakini Moreen alipogeuka nyuma kwa haraka, aliona watu wawili waliosimama karibu na uchochoro wakianza kusogea kwa kasi kuelekea walipoangukia. Walikuwa wamevaa miwani meusi, suruali za kawaida, na mashati meupe.
Hakukuwa na maandishi yoyote, lakini macho yao yaliongea:
“Tumewakosa. Kwa sasa.”

Walikimbia mpaka mtaa kama watano hivi.
Waliingia ndani ya duka lililoonekana kama limefungwa. Kulikuwa na mzee wa makamo aliyekuwa amejifunika blanketi akijifanya mgonjwa. Alipowaona, akawapungia mkono bila kusema. Hilo lilikuwa eneo la siri la Kituo-M kwa watu waliokuwa kwenye hatari ya moja kwa moja. Waliruhusiwa kukaa humo kwa dakika saba tu, kisha wanapaswa kuondoka, kabla kamera za barabarani hazijaripoti maeneo yaliyopoteamo Kwa ghafla.
Wakiwa ndani ya duka hilo, Kinu alipokea taarifa kwenye simu ya mkononi kutoka kwa chanzo cha habari ndani ya redio moja ya mitandaoni.

Taarifa hiyo ilimshtua Moreen zaidi:
"Katibu wa Chama cha Upinzani Wilaya ya Kinondoni, Bw. Amani Makwega, aliyekuwa akiongoza kampeni ya haki ya kujieleza na demokrasia, ametoweka tangu jana usiku. Mara ya mwisho alionekana akihutubia mkutano mdogo maeneo ya Mabibo. Simu zake hazipatikani. Polisi wanasema hawana taarifa.
Moreen alishika kichwa.
“Huyu ndiye aliyenipa foundation yangu mwaka jana. Tulikutanaga studio. Alikuwa na sauti kubwa sana, muda mwingi alikuwa akiongelea haki za wanawake na umuhimu wao katika uchumi.”

Kinu alikunja nyuso. “Na leo, sauti yake imezimwa. Hicho ndicho wanachofanya. Wanaanza na walio mbali. Wakimaliza… wanakufuata wewe.”
Moreen alimtazama kwa jicho la hofu na hasira. “Kwa hiyo… hii vita haiko tu kwa watu wa siasa au polisi wa upelelezi. Hata sisi wasanii, warembo, wapishi, tunaweza kulengwa, kama tukiamua kusema ukweli?”
Kinu alijibu bila kuchelewa:
Ndio maana naendelea kukwambia, Moreen… Hakuna Aliye Salama.
**********
Saa kumi na mbili alfajiri.
Upepo wa bahari ulipuliza kwa sauti ya msonyo wa kilio. Mawimbi yalivuma kwa hasira, yakivurumisha povu kama hasira ya Mungu kwa taifa lililojaa dhuluma. Pwani ya Kigamboni, nyuma ya gati lililoachwa, palionekana kiza kisicho cha kawaida. Palikuwa kimya, kama roho ya bahari ilikuwa imepooza.

Ilipofika saa moja kamili, vijana wawili waliokuwa wameenda kuokota samaki waligundua kitu kisicho cha kawaida.

Mwili.
Mwili wa mwanaume aliyefungwa mikono kwa nyuma kwa waya wa chuma, na mdomo wake kufungwa kwa plasta nyeusi ya viwandani. Kwenye paji la uso wake kulikuwa na alama nyekundu iliyochorwa kwa wino ilikuwa herufi kubwa "D".
Ulikuwa mwili wa Amani Makwega, Katibu wa Chama cha Upinzani Wilaya ya Kinondoni, mwanaharakati mkimya ambaye alikuwa sauti kwa wasio na sauti. Mwanasiasa aliyepigania haki ya kujieleza, uhuru wa mikutano, na uwajibikaji serikalini.

Alikuwa ametoweka kwa siku mbili tu.
Na sasa, alikuwa ameshakufa.
Habari hiyo ilisambaa kama moto wa petrol kwenye karatasi kavu. Saa mbili tu baada ya mwili wake kupatikana, picha zilikuwa tayari zimezagaa kwenye mitandao ya kijamii. Kwenye X (zamani Twitter), watu walitumia ‘hashtag’ #AmaniHakujiua. Wengine waliandika:
“Kifo hiki si kawaida. Hii ni ishara ya vita dhidi ya uhuru wetu!”
“Tunaishi nchi gani sasa? Haki ikidaiwa, damu inamwagika?”
“#HakunaAliyeSalama , Leo ni Makwega, kesho ni wewe.”
Serikali ilikaa kimya kwa saa nane.
Baadaye, Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Dar es Salaam alitoa taarifa isiyozidi mistari mitano:
“Mwili wa Bw. Amani Makwega umeokotwa katika eneo la Kigamboni alfajiri ya leo. Uchunguzi wa awali unaonesha hakukuwa na alama za kupigwa risasi wala majeraha ya moto. Tunasubiri ripoti ya daktari wa uchunguzi wa maiti. Tunaomba wananchi kuwa watulivu na kuepuka kushiriki taarifa zisizothibitishwa.”
Haikusaidia.

Vurugu zilianza mtaa wa Tandale, walipoishi baadhi ya vijana waliomkubali Makwega kama mwalimu wa mabadiliko. Walivamia ofisi ya tawi la chama tawala, wakachoma mabango, wakapiga kelele:


“Mtu hakujiua na kujifunga mikono mwenyewe!”
“Hii si ajali — ni maangamizi!”
Polisi walitanda mitaani. Gari la maji ya kuwasha likazunguka Buguruni hadi Magomeni. Kamera za vyombo vya habari vya binafsi zilifungiwa. Saa kumi alasiri, mtu mmoja alifyatuliwa risasi akijaribu kurusha jiwe kuelekea kwenye ofisi za wilaya.

Moreen alitazama taarifa zote akiwa amejifungia ghorofa ya pili ya nyumba ya kupanga Tabata. Macho yake yalikuwa mekundu kwa hasira na woga.
“Ni kweli… wanaua.” Alimnong’oneza Kinu aliyekuwa akimwangalia bila kuongea.
“Niliwahi kuonana naye… pale Redio Uhuru.” Moreen aliendelea. “Makwega alinifundisha kutumia sauti yangu. Alisema, ‘Sanaa yako ni silaha. Tumia midomo yako kama bunduki ya haki. Pia aliniambia, nawe kutumia sanaa ya makeup kueleza jambo Fulani litakalobadisha jamii”

Kinu alifunga dirisha. Alikuwa kimya, lakini ndani yake alikuwa amejaa hasira. Alimkumbuka Amani Makwega, alikuwa mwanadamu wa kawaida aliyeamua kuwa jasiri kwenye taifa la waoga. Alikuwa mtu wa amani aliyekataa kuwa mtumwa wa mfumo.

“Moreen,” Kinu alisema baada ya kimya kirefu. “Kifo chake ni ujumbe. Ujumbe wa kutisha. Wanatuambia: ‘Tunaweza kukuua hata ukiwa huna bunduki.’”
Moreen alijibu kwa macho ya chuki:

“Basi… waruhusu waniue nikiwa nimekaa kimya ni kitu kimoja. Lakini waniue nikiwa nasema ukweli, nitakuwa nimekufa nikiwa na heshima.
Kinu alimwangalia kwa muda. Halafu akatoa bahasha ndogo yenye picha ile ile aliyopata kutoka kwa Mcharo, picha ya mtu aliye karibu sana naye, ambaye huenda ni sehemu ya Deka-6.
“Kesho nitaenda kukutana na mtu. Ninahitaji uthibitisho wa jina lake. Ukiona kimya au nimechelewa kurudi uipelekee hii kwa mtu aitwaye ‘Mama Lutu’, anayeuza vitabu vya dini pale Oysterbay.”

Moreen alichukua bahasha kwa mkono wa kutetemeka. Akaiweka ndani ya mkoba wake wa urembo.
“Na wewe,” Kinu aliongeza, “usitembee peke yako tena. Na usijaribu kuongea hadharani kuhusu Makwega. Ndio maana amekufa, alijua mengi kuliko alivyotakiwa.”
Moreen alijibu kwa sauti iliyovunjika:
“Labda sasa ndio wakati wa kusema. Maana kimya kimekuwa kaburi letu”
"*
Kwa mbali, kwenye kona ya giza la ofisi moja ya ndani ya mfumo, watu wawili waliokuwa wamevaa suti waliketi kwenye chumba chenye mwanga hafifu. Waliangalia rekodi za kamera za usalama. Wakamwona Kinu, wakamwona Moreen. Wakasikia sauti yao. Walifuta sehemu ya rekodi hiyo kwa kificho. Kisha mmoja akaandika ujumbe:
“Kabla hawajafungua mdomo, wafunglieni kaburi. Mwanzoni mwa wiki ijayo, wapotee wote wawili.”

**
Kesho yake, ujumbe wa maandishi ulionekana kwenye kuta za mtaa wa Mwananyamala:
“Hakuna Aliye Salama. Tuseme au tufe kimya?”


*******

Usiku ulikuwa mzito, lakini mwezi ulikuwa wa kijivu chenye kung'aa. Ulikuwa usiku wa fukwe za Mikocheni, kwenye party iliyovutia watu wa tabaka la juu, wanamuziki mashuhuri, wasanii wa Instagram walioteka likes, wafanyabiashara na wanasiasa waliovaa sura za kijamaa.
Party hiyo haikutangazwa hadharani. Ilikuwa ya mwaliko tu, na Moreen alipokea ujumbe wake kutoka kwa msanii mmoja wa zamani aliyewahi kumpaka make-up miaka miwili iliyopita.
Sun Lu atakuwepo! Atakuwa kwenye Comeback Show yake.” ujumbe ulisomeka.

Lakini Sun Lu hakuweza kufika. Alikuwa ameondoka nchini kimyakimya, akitoroka mikono ya deni, hofu, na aibu. Mkopo wake ulikuwa umeiva.

Na hapo ndipo mpango wa Kinu ukaingia kazini.
Nyumbani kwao Sinza Moreen aliketi mbele ya kioo akiwa tayari kuanza kazi. Kinu alisimama nyuma yake akiwa na picha ya mwanamke wa Kiasia, aliyekuwa akijulikana mitandaoni kama Sun Lu, mwanamuziki aliyewahi kutamba na nyimbo za Bongo-Korea, lakini sauti yake na soko lake vilikwisha mwaka mmoja uliopita. Hakuweza kukimbizana na kasi ya muziki wa Kileo. Amapiano hakuimudu. Singeli hakuthubutu!

Make-up ilianza saa 11 jioni.
Ilipofika saa 1 usiku, Moreen hakuwa tena Moreen. Alikuwa Sun Lu, kwa umbo, ngozi, macho na hata sauti — alikuwa amewekewa clip ya meno iliyobadilisha matamshi yake.
“Umenipaka hadi nimepotea. Siwezi hata kujitambua.” Alisema kwa sauti ya kike ya kisanii, yenye lafudhi ya Kiasia iliyochanganywa na Kiswahili cha mitaani.
“Hivyo hivyo wanavyotakiwa wajisikie. Wanapaswa kukuona… lakini wasikujue.”
Kinu alitoa koti jeusi, akavaa miwani ya nyeusi, na alitembea kama mlinzi wa watu mashuhuri. Alijifanya mpenzi anayemlinda mrembo wake, lakini hakuingia moja kwa moja. Alikaa eneo la nje ya party, karibu na gari lao.

Party ilifanyika kwenye beach ya kifahari iliyoitwa Blue Tides Resort, pembezoni ya Mikocheni, ndani kabisa karibu na maji. Taa zilikuwa za bluu na zambarau, muziki ulicheza taratibu kwa sauti za Afro-Korean. Wageni walikuwa wakijiachia, baadhi wakivuta shisha, wengine wakipiga selfie, na wengine wakijifanya hawajui kinachoendelea.
Moreen alitembea kifua mbele, kama malkia wa usiku, akiwa amevalia gauni la shingo wazi na hereni za dhahabu bandia. Hakusema na mtu. Alionekana maarufu kiasi kwamba watu walimsogelea na kupiga naye picha. Moja ya picha hizo aliituma kwa Kinu kupitia WhatsApp ya siri.
“Yupo. Amevaa suti ya kijivu, ana simu mbili. Anacheka sana lakini macho yake hayawezi kuficha msongo alionao"

Kinu alimtuma ujumbe:
“Fuata muda. Saa 3:15 mkutane naye kwenye kona ya restroom. Mvumishe kuwa una proposal ya collabo. Nitakuwa kwenye mlango wa nyuma. Ukimtoa, unaingia na yeye kwenye gari ya tinted. Ukitangulia, fanya ishara ya vidole viwili kwenye kioo cha gari. Nitafungua mlango.”
**
Wakati huo, mtu aliyekuwa kwenye picha, ambaye jina lake halikutajwa hadi sasa, aliitwa Martin Sanga. Alikuwa mfanyabiashara kijana, lakini Kinu alikuwa na taarifa kwamba Martin ni mmoja wa wasambazaji wa taarifa kutoka Kituo cha Ndani cha Deka-6 — sehemu ya mfumo uliopenyezwa ndani ya Serikali kwa sura ya ushauri wa usalama wa taifa.

Martin alionekana mcheshi, mchangamfu, lakini aliwahi kumtambua Kinu mara moja miaka miwili iliyopita. Ilikuwa lazima mpango huu ufanyike kwa ujanja wa juu. Moreen hakuweza kuonekana kama Moreen, maana alishawahi kuposti picha akiwa na Makwega enzi za harakati. Kosa dogo tu, Martin angeelewa.

Saa 3:15, Moreen alijongea kona ya washroom. Martin alikuwa pale, akiongea na mrembo mmoja wa kimasaki. Alipoona “Sun Lu”, mrembo wa zamani wa mitandaoni, alimsogelea kwa haraka.
“Hakika huu ndio mshangao wa usiku. Unarudi kweli au ni stori za mitandaoni?” aliuliza kwa furaha.
Moreen alitabasamu kwa madoido: “Tunaanzisha collabo mpya. Nafikiri tunaweza kuongea kwa sekunde ishirini tu kabla sijaondoka. Kuna mtu alinituma kukuambia jambo.”
Martin alishtuka.
“Jambo gani?”
“Jambo la kukutoa kwenye kaburi unalojichimbia.”
Martin alitetemeka. “Unaongea nini?”
“Hii sio collabo ya muziki. Ni collabo ya kufichua ukweli.”
Moreen alishika mkono wake kwa nguvu, hakumwachia. Kwa kutumia nguvu za ghafla na mafunzo madogo aliyofundishwa na Kinu siku tatu zilizopita, alimvuta kama mpenzi wa muda, kisha akampeleka upande wa kutokea mlango wa nyuma. Kamera za usalama zilishindwa kuona kwa sababu taa ya pembeni ilizimwa kimaksudi na Kinu dakika mbili kabla.
Martin hakupiga kelele. Alijua kile kinachomsubiri kama angestahimili. Angeweza kuuawa palepale kwenye party kwa shoti ya sumum

Moreen alipofika karibu na gari, akapiga kioo mara mbili. Milango ilifunguliwa haraka. Kinu alishuka upande wa pili, akamsukuma Martin ndani na kumpulizia harufu ya chloroform soft mist. Martin akazimia taratibu.
Gari liliondoka kwa kasi taratibu. Kamera hazikuchukua namba. Kisha likapotelea barabara ya Sam Nujoma.
**
Saa 4 alfajiri, Moreen na Kinu walikuwa wamejificha kwenye nyumba salama eneo la Mabwepande. Martin bado alikuwa hajazinduka. Alikuwa mfungwa wa kwanza waliyeweza kumkamata kutoka ndani ya mfumo wa Deka-6.


Kinu alimwambia Moreen kwa sauti ya polepole:
“Leo hatujaokoa mtu… tumechukua bomu. Iwe litatuokoa, au litatupasua wote. Lakini lina jibu la fumbo la Makwega… lina jina la mwanasiasa anayelinda wauaji na watekaji"
Na Moreen akasema akiwa ameketi sakafuni:
“Leo nimeamini… hatuna muda wa kuishi kwa woga. Kama wapo, basi tuwaonyeshe kuwa tumeamka.”
****

Inaendelea
Kesho mambo yasipokuwa Mengi.
 
---

Hakuna Aliye Salama
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 03

Giza la chumba cha chini ya ardhi lilikuwa zito na kimya, kama kimya cha kaburi. Ukuta wa kushoto ulijengwa kwa matofali mabichi yasiyo na rangi, huku upande wa kulia ukiwa na ndoo moja ya maji na meza ya chuma iliyochakaa. Sakafu ilikuwa baridi, na harufu ya jasho, kutu na damu ya zamani ilikaa hewani kama mzimu usioonekana.

Martin Sanga alikuwa amefungwa mguu mmoja na pingu nzito iliyounganishwa kwenye mnyororo mfupi. Mikono yake ilikuwa huru kiasi, lakini tayari ilikuwa imevimba kwa maumivu ya kuchomwa sindano na mazoezi ya mateso ya kisaikolojia aliyokuwa amepitia usiku mzima.
Kinu alikuwa ameketi kimya upande wa pili wa meza, akiwa amevaa koti lake jeusi na miwani ya giza. Mbele yake kulikuwa na rekoda ya sauti, karatasi yenye picha za watu waliokufa, na bastola ya Walther PPK iliyowekwa juu kwa makusudi.

Moreen alikuwa upande wa pili wa chumba, akiwa amevalia jaketi la ngozi. Alikuwa na karai lenye maji ya baridi na glavu za mazoezi. Alimwangalia Martin kwa mda mrefu, akijaribu kusoma usoni mwake chembe ya uoga — lakini hakukuwa na dalili.
Kinu alitazama saa yake. Ilikuwa saa 2:13 asubuhi. Alikuwa kimya kwa saa mbili sasa, bila kusema neno. Aliamini kimya ni adhabu ya mwanzo, kimya huchanganya.

Hatimaye, alizungumza.
“Martin… una dakika tano. Baada ya hapo, nitakuchoma sindano ya NT-7 kwenye uti wa mgongo. Sindano hiyo hufanya mwili usisikie joto wala baridi, ila ubongo unabaki hai na unahisi maumivu yote kwa kiwango cha juu.”
Martin alicheka. Sio kwa dharau. Bali kama mtu anayecheka maneno ya mtoto mdogo.

“Bwana Kinu… naona hujui niliyopitia. Sijaogopa kifo tangu mwaka 2019.”
Kinu alinyosha mkono wake taratibu, akavuta picha ya Amani Makwega, kisha akaiweka mbele ya Martin.
“Mtu huyu alikufa kwa sababu ya kuamini kuwa yupo upande wa haki. Alikuwa mtaalamu wa sheria. Alikuwa sauti ya watu. Alikufa akikuamini wewe.”
Martin alinyamaza. Macho yake yalibadilika, lakini uso wake haukusaliti moyo wake.
“Makwega… alizidisha. Alitaka mengi kwa wakati mmoja. Alijipeleka mwenyewe.”

“Unamlaumu?” Kinu alitupa swali.
Martin alijibu kwa sauti tulivu:
“Ninawahurumia wote mnaotumia nguvu kuokoa mfumo uliokufa. Mnadhani mtaibadilisha dunia hii kwa kuokoa watu wachache wenye ndoto zisizo na uhalisia.”
Kinu alinyosha mkono na kubonyeza kitufe kwenye rekoda. Sauti ya mtoto mdogo ikasikika ikilia:
“Baba alichukuliwa usiku… Mama alilia hadi akazimia. Polisi hawakusaidia…”
Kisha akaleta picha ya mtoto huyo. “Alikuwa mwana wa Mzambia aliyekuwa mwandishi wa habari. Alikuwa jirani yako. Uliona walivyomchukua baba yake. Uliona walivyomteka.”

Martin alipumua kwa nguvu kidogo.
“Unadhani kuwa ukililia familia ya watu waliopotea, watakupa utakatifu? Sisi tulichagua upande wa utulivu. Kama mtu anapoteza roho ili nchi ipate amani, basi na iwe hivyo.”
Moreen hakuvumilia tena. Alisimama, akamkaribia, akamrushia kijiko cha chuma kikakita mezani, kisha akasema kwa hasira:
“Kama wewe ni binadamu, lazima upate hisia kwa mateso ya wengine. Kama huwezi, basi uko kwenye kiwango cha shetani.”

Martin alimtazama Moreen. “Na wewe ni nani? Ulimwengu huu umejaa wanawake wapuuzi, mmojawapo ni wewe. Kujiingiza kwenye mambo mazito yatakayokugharimu. Muda huu ungekuwa upo Kwa Mumeo.”

Moreen alinyamaza.
Lakini Kinu alisimama. Alitembea taratibu hadi kwenye kona ya chumba. Akachukua karatasi ndogo iliyokuwa kwenye bahasha. Akaisoma taratibu kwa sauti:
“Martin Sanga. Alijiunga na taasisi ya upelelezi akiwa na miaka 22. Akaondolewa kwa misingi ya kutoroka mafunzo ya mwisho. Mwaka 2018, alirejeshwa kwenye mfumo kupitia kampuni binafsi. Iligharamiwa na mfuko wa siri wa usalama wa ndani. Akaanza kazi ya kufuatilia vuguvugu la mabadiliko. Kazi yake kuu: kukusanya sauti, picha, na tabia za watu wanaoonekana kuwa tishio kwa mfumo.”

Martin hakusema.
Kinu aliendelea:
“Tuna majina saba. Wote walikuwa wameonana na wewe siku tatu kabla ya kupotea. Tumejua wewe ni kiungo. Hujaua wewe lakini unawatuma wauaji.”
Martin akainama kidogo, akatabasamu.
“Kwa hiyo… mtaniua? Nitakufa nikiwa na jina langu safi. Sina siri. Sina jibu.”
Kinu alimwangalia kwa sekunde kadhaa. Kisha akasema kwa sauti tulivu:
“Basi tutakutesa hadi jina lako liwe fumbo la hofu kwenye vizazi vyako.”
**

Kwa dakika arobaini zilizofuata, Martin alipewa mateso ya saikolojia. Alisikilizishwa sauti za kilio cha watoto waliopotezwa, akakumbushwa video za vifo vya waandishi wa habari, akaingizwa ndani ya chumba baridi hadi akawa anatetemeka kama mtu mwenye malaria. Aliwekewa taa yenye mionzi myekundu iliyoathiri retina za macho yake.

Lakini hakutoa neno. Hakutaja jina. Hakusema hata "Ndiyo" wala "Hapana".

Mwisho wa mateso hayo, Kinu alikaa pembeni. Alizungumza na Moreen kwa sauti ya chini:
“Mtu huyu anaweza kuwa amepewa dawa ya cognitive lock. Dawa hiyo huua uwezo wa mtu kutamka taarifa fulani. Anaweza kuzungumza jambo jingine lolote, lakini siyo kuhusu Deka-6"
Moreen alimuangalia Martin akiwa amezimia.
“Kwa hiyo tumebaki na nini?” aliuliza kwa masikitiko.

Kinu alijibu:
“Tumebaki na ushahidi kuwa tupo kwenye vita isiyo ya kawaida. Wana silaha zisizo za bunduki. Wanadhibiti hadi ubongo wa wafuasi wao.”
Akatulia kwa muda mfupi.
************

Kulikuwa na harufu ya vitabu vya zamani na kahawa ya arabica ndani ya duka dogo lililojengwa kwa mawe ya kale. Jengo hilo lilikuwa limepakwa rangi ya hudhurungi, huku dirisha moja tu likiwa wazi nusu. Kulikuwa na bango lililosomeka:
“Lutu Book Centre – Vitabu vya Dini, Historia na Majibu ya Roho”

Ndani ya duka, mwanamke wa makamo, mwenye glasi kubwa machoni na vazi refu lililoshonwa kwa vitambaa vya kiafrika, aliketi kwenye kiti cha mbao. Alikuwa Mama Lutu anayejulikana kwa jina la kawaida, lakini mwenye heshima kubwa miongoni mwa waliojua undani wa taifa.
Moreen na Kinu walikuwa mbele yake. Wenye miili iliyojaa uchovu, akili zilizochoka, lakini mioyo iliyojawa na kiu ya ukweli.

Mama Lutu alifungua jalada jekundu, akatazama picha ya Martin Sanga.
“Huyu ni mmoja tu kati ya waelekezaji. Lakini si muamuzi. Si chimbuko.”
Akaangalia moja kwa moja machoni mwa Kinu:
“Kabla sijasema nani anayeongoza mauaji haya, ni lazima muelewe kwa nini wanaua. Kwa nini wanaogopa sauti za raia. Kwa nini mfumo huu una miiba kuliko maua"
Alichukua daftari dogo, kurasa zake zilikuwa zimeandikwa kwa mkono. Kisha akaanza kusoma kwa sauti tulivu lakini inayopenya ndani ya nafsi:

“Uhuru wa kujieleza ni msingi wa taifa lenye akili timamu. Ni njia pekee ya kuikosoa serikali isiyotenda haki, ni silaha ya amani ya kuondoa uongozi wa mabavu. Bila uhuru huo, kila uongo hugeuzwa kuwa sheria, kila uongozi wa kidhalimu hugeuzwa kuwa ‘uzalendo.’”

“Demokrasia sio uchaguzi wa kura tu. Ni uwapo wa majadiliano, usawa wa mawazo, na hofu ya watu wanaotawala kuwa watawajibishwa. Bila demokrasia, taifa hujengwa kwa misuli ya kijeshi, si hoja ya kijamaa.”
“Uwazi ni jicho la wananchi kuona kinachofanyika nyuma ya milango ya viongozi. Ukosefu wa uwazi huzaa ufisadi, ukandamizaji, na unyonyaji wa wazi. Uwazi ni mzazi wa uaminifu.”

“Uwajibikaji huifanya Serikali kuwa ya watu. Viongozi wanapojua wataulizwa kesho, wanatenda leo kwa tahadhari. Taifa lisilo na uwajibikaji, ni taifa linalokumbatia wizi kwa baraka ya sheria.”

Mama Lutu alinyamaza sekunde kadhaa. Kisha akatoa jalada lingine lililokuwa na orodha ya majina.
Kinu alilishika kwa mikono miwili, akaanza kulisoma polepole. Moreen alikuwa kando yake, akitetemeka japo kidogo.
Jalada hilo lilikuwa na kichwa:

“WALIOTOWEKA KWA SABABU YA KUSEMA UKWELI, 66”
Orodha ilikuwa kama ifuatavyo:

1. Amani Makwega – Mwanaharakati, Kinondoni
2. Grace Malongo – Mwandishi wa habari, Mwanza
3. Mbaraka Sanga – Askofu, Iringa
4. Dr. Halifa Mboma – Mhadhiri, chuo kikuu Cha taifa
5. Lilian Jonas – Mwanasheria wa haki za ardhi
6. Joseph Mutalemwa – Mwalimu, Mbeya
7. Tito Mwakalukwa – Blogger, Arusha
8. Mary Sarungi – Mtetezi wa mazingira
9. Ally Abdallah – Mwanasiasa wa upinzani
10. Reuben Kalanga – Mwandishi wa makala ya uchunguzi
11. Jumanne Maghembe – Mfanyakazi wa TANESCO aliyefichua rushwa ya zabuni

Wote hawa walitoweka, wengine walikutwa wakiwa wameuawa, wengine miili yao haikuwahi kupatikana. Wote walihusishwa na kauli, maandiko, au uwasilishaji wa maoni yaliyokosoa serikali au mfumo wa kisiasa.

Moreen alishika mdomo wake kwa mshtuko.
“Ni zaidi ya nilivyofikiri… haya majina si majina ya vita, ni majina ya ndugu, waalimu, viongozi wa familia…”

Mama Lutu alijibu kwa sauti ya ndani:
“Na bado hakuna kesi hata moja iliyokwenda mahakamani. Wakati mwingine hata taarifa ya polisi haikutolewa.”
Kinu alijiegemeza nyuma. “Sasa tupo tayari kujua ni nani aliye nyuma ya haya yote?”

Mama Lutu hakujibu moja kwa moja. Alinyosha mkono wake, akavuta jalada lililojaa karatasi za biashara, mikataba ya kivuli, na vielelezo vya kifedha.

Alisema kwa sauti iliyodhibitiwa:
“Kabla hujajua muuaji, ujue faida yake. Damu hii yote si ya kiitikadi, ni ya biashara.”
Akaendelea:

"Baadhi ya viongozi wakuu nchini wamehodhi biashara kubwa kwa majina ya watu wa familia zao. Kuna kampuni 14 zinazotajwa kuwa ‘binafsi’ lakini hazilipi kodi hata senti moja. Zinajihusisha na:
Uingizaji mafuta (wanauza bila ushindani)
Madini (hasa dhahabu kutoka Geita na Mererani)
Vifaa vya ujenzi vinavyonunuliwa na Serikali
Chakula cha misaada kutoka nje kinachouzwa sokoni
Simu za mkononi zilizo na ‘tracking chip’ maalum
Usafirishaji wa binadamu kupitia bandari ndogo (unaofunikwa kama biashara ya uvuvi)”
“Na mtu yeyote anayejaribu kuweka taarifa hizi hadharani... hutoweka.”

Moreen alijikuta akilia kimyakimya.
“Kwa hiyo… wanaendesha nchi kama duka la familia yao?”
Mama Lutu alitabasamu kwa uchungu. “Na sisi ndio wafanyakazi wa duka. Tunaambiwa tucheke wakati wanatuibia.”
Kinu alijisogeza karibu. “Sasa Mama, ni nani anayewasimamia? Nani mlinzi wao? Ni nani anayeweza kupitisha mauaji 66 bila kutajwa?”

Mama Lutu akajibu kwa sauti ya kushuka:
“Jina moja. Si la kutamka kwa hasira. Bali kwa ushahidi.”
Akatulia. Kisha akavuta picha moja ya mtu aliyejulikana, aliyeheshimiwa, na anayependa kuitwa “Baba mpya wa Taifa .”
“Mtu huyu… si kiongozi tu wa juu. Ni kiongozi wa miili ya kivuli. Alianzisha Deka-6 akiwa Waziri wa Ulinzi, sasa yuko juu zaidi ya sheria.”

Na hapo ndipo hadithi iligeuka kuwa mlipuko wa ukweli.
Kinu alinyamaza.
Moreen alishika moyo wake.
Mama Lutu akaongeza:
“Lakini bado kuna njia ya kuangusha mfumo huu. Lazima mtu kutoka ndani… aende nje. Lazima ujumbe upite mipaka.”
*********
Saa mbili usiku. Mtaa wa Masaki.

Kinu na Moreen walikuwa wameketi ndani ya gari la tinted, wakiwa wamepaki pembezoni mwa duka la kuuza samaki lililofungwa. Kinyume na mwonekano wa gari, ndani kulikuwa na kompyuta ya mkononi, redio za mawasiliano, na bahasha kubwa ya kijani iliyofungwa kwa kamba ya katani. Ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na ushahidi mzito kuliko hata bastola yenye risasi zote 15.

Ilikuwa ni ushahidi wa mauaji, ufisadi, utekaji, ukandamizaji wa demokrasia, na majina ya waliopotea.
“Mwenyewe atakuchukua saa tatu kamili. Usiulize jina lake, usimwangalie usoni kwa sekunde zaidi ya tatu,” Kinu alimwambia Moreen kwa sauti ya chini, akimtazama kwa macho yaliyojaa hofu ya ndani lakini sauti iliyodhibitiwa.
“Na kama akiniuliza mimi ni nani?”
“Sema tu... 'mchwa wa mti mweupe. Atajua.”
Moreen alitikisa kichwa. Akaweka mkoba wake pembeni, akavuta pumzi ndefu.

“Najua unanipa maagizo kama vile huu ni mwisho wa mchezo… lakini naona kama…”
“Moreen,” Kinu alimkatisha kwa sauti ya ukali wa mtu mpole. “nimekuingiza sana kwenye hatari. Ulitakiwa kuwa salama. Umevuka mipaka… sasa nataka urudi Mtwara. Leo usiku huu.”

Moreen alinyamaza.
Baada ya sekunde kumi, alisema kwa sauti ya upole:
“Nikiwa Mtwara, nikisikia umeuawa… nitajiona kama msaliti. Wewe ulikuwa jasusi, mimi nilikuwa mchoraji wa uso. Sasa tumekuwa kitu kimoja. Siwezi kurudi na kuishi kama awali”
Kinu alitabasamu kwa huzuni.
“Kwa sasa rudi. Ukibaki, watanilenga kupitia wewe. Na wewe… huna kinga. Ukifa, ukweli utakufa na wewe. Ukibaki hai, bado tuna nafasi.”
Gari lilifika. Toyota Crown nyeusi. Mtu aliyeshuka hakuwa na sura ya kutisha. Alikuwa mzee wa kawaida, mwenye bastola kwenye kiuno lakini macho ya mtu aliyesoma zaidi ya vitabu elfu tano.

Kinu alimkabidhi bahasha. Akainama taratibu. Hakusema kitu. Mzee huyo akaingia kwenye gari lake, likatoweka.
Usiku ulikuwa kimya, lakini kila nyota mbinguni ilionekana kama kamera inayochunguza mioyo yao.

Siku mbili baadaye…
Moreen alikuwa amefika Mtwara. Alikodisha chumba cha kupanga kando ya mtaa wa Mitengo. Aliamua kurudi kwenye kazi yake ya urembo kimya kimya, huku akitunza kila kumbukumbu ya aliyoyapitia. Alihangaika sana usiku wa kwanza. Alikuwa anaota. Ndoto moja ilimsumbua:

Alimwona Kinu amefungwa kamba kwenye kiti cha chuma, akiteswa kwa maswali, akilia akiita jina lake, akimwambia:
“Rudi… kama bado una sauti…"
Moreen alishtuka. Jasho lilimtiririka. Moyo wake ulipiga kwa kasi.

Wakati huo huo, Dar es Salaam…
Mama Lutu alikuwa ndani ya chumba chake cha nyuma cha duka lake. Alikuwa anasoma barua ya zamani, yenye alama ya NGO ya haki za watoto, "Safe Child Africa". Barua hiyo iliandikwa na rafiki yake wa zamani, Morris, mzungu mwenye sauti kubwa ya mvumo, aliyejulikana kama mwanaharakati wa sauti za watoto, lakini ndani ya pazia, alikuwa jasusi maalum wa Marekani, aliyewahi kufanyia kazi CIA kwa miaka 14.

Katika barua, Morris aliandika:
“Deka-6 ni mfumo uliobuniwa kwa jina la ‘usalama wa taifa’, lakini sasa unatumika kuhifadhi uovu wa watu wachache. Walinikaribisha kwenye vikao vyao wakijua mimi ni mshirika, hawakujua nilikuwa narekodi kila kikao. Kiongozi wao ni mtu mmoja tu aliyeonekana mpole lakini ana maamuzi ya kishetani…”

“Nitaondoka nchini muda si mrefu. Lakini kabla sijaondoka, nitakutumia jalada kupitia mtoto wa kimasai anayefanya kazi bandarini. Jalada hilo lina kila kitu… usilipe gharama ya maisha Yako. Kuna mwanaume wakati ukifika atakuja kulichukua hilo jalada. Kila kitu kitawekwa wazi, Mama Lutu.”

Mama Lutu alifunga barua hiyo kwa mikono inayotetemeka. Alichukua kitabu cha Biblia, akakiweka juu ya jalada hilo.
Alijua sasa… mtu aliye juu kabisa ya mauaji, upotevu, na ufisadi nchini ,jina lake lilikuwa kwenye ukurasa wa mwisho wa jalada la Morris.

Na wakati huo, Kinu alikuwa amefuatwa.
Alitekwa kimyakimya. Hakuonekana tena kwenye namba ya mawasiliano. Mtego uliokuwa umetegwa kwa Moreen ukahamia kwake.
Na taarifa ya mwisho iliyomfikia Moreen, ilikuwa meseji isiyosomwa, ikiwa imeandikwa:
“Wakija… usigeuke. Wakiita, usijibu. Ukisikia kimya changu, tambua ni kelele ya mwisho ya mapambano. Kinu.”

Moreen alishika simu hiyo kwa machozi. Akaamka asubuhi, akafunga pochi yake.
“Lazima nirudi Dar. Sijamaliza mchezo huu.”
Hapo ndipo Moreen anarudi Dar, bila kujua kama anakuja kuokoa au kuzikwa pamoja na kumbukumbu za Kinu.

****

Itaendelea
 
---
Hakuna Aliye Salama
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 4

Chumba kilikuwa kimya, lakini kelele ya “kondoo asiyeonekana” ilisikika ndani ya ubongo wa Kinu , kilio cha mashine ya umeme, sauti ya maji yanayodondoka kutoka kwenye bomba la kutu, na mlio wa bomba la hewa linalopuliza baridi kali kwenye mgongo wake uliokuwa uchi.
Alikuwa uchi wa mnyama, mikono yake ikiwa imefungwa juu ya bomba la chuma, miguu ikiwa imefungwa chini. Alikuwa ameketi kwenye kiti kilicho na vichomaji ndio miiba ya moto vinavyowaka mara kwa mara kwenye makalio yake.

"Jina la Kiongozi… anayeendesha mtandao wa upinzani. Ni nani?” aliulizwa kwa Kiswahili kibovu na mwanaume mwenye sura ya Kimasai, lakini mwenye mwili wa askari wa Kisovieti.
Kinu alimtazama moja kwa moja. Akamtemea mate, yaliyochanganyika na damu.
“Nyie mna nguvu ya kuua miili… si dhamira.”
Alichomwa umeme kwenye shingo.
Giza likafunga macho yake kwa sekunde kadhaa. Aliporudiwa na fahamu, alikuwa ndani ya ndoto ya makaburi, huku Makwega akimwambia:

"Usisahau. Ukweli haudanganywi kwa sindano. Unaishi hata baada ya mtoa sauti kufa.”

Walimtesa kwa masaa tisa.
Aliwekewa redio ikipiga kilio cha watoto waliopotezwa. Aliambiwa Moreen amekamatwa, hakupewa chakula kwa saa 36. Wakamuweka kwenye baridi hadi akakojoa mkojo kwa hofu, lakini moyo wake haukuvunja.

Usiku wa siku ya nne…
Askari mmoja aliyechoka alijisahau, funguo ndogo iliyofunguliwa kamba ya miguu ilibaki juu ya meza. Kinu alijikokota, Kwa kugugumia mpaka akaifikia Ile funguo. Kisha akajifungua. Akamuua yule askari mzembe kimyakimya kwa kisu cha plastiki kilichochongwa kwa brashi ya meno.

Alafu akavaa sare za askari huyo, akatoka taratibu. Aliingia kwenye moja ya magari ya wafanyakazi wa ndani, akajificha chini ya kiti. Alipotoka, alikuwa karibu na barabara ya Azikiwe, katikati ya Jiji.
Alianza kutembea kwa kasi. Lakini hakujua kamera tayari zilikuwa zimemkamata, alionekana

**

Deka-6 walituma watu haraka. Magari matatu aina ya Prado nyeusi, mbwa wawili wa K-9, na helikopta yenye taa ya kutafuta.
Kinu alikimbia. Akakimbia kama mtu asiye na tumaini, lakini aliyeamua kupambana hadi pumzi ya mwisho. Aliingia kwenye daraja la juu karibu na posta, akaruka ukutani, akateleza kwenye lami, akakimbia hadi akafika eneo la barabara ya Sam Nujoma.

Hapo, akaona kalavati la maji machafu, liliofunguka pembeni kwa ajali.
Bila kufikiri, akaingia ndani ya lile kalavati

**
Giza lilikuwa nene. Harufu ya kinyesi cha miaka mitano ilivamia pua yake. Maji yalikuwa yamechanganyika na uchafu wa barabara, takataka, na mikojo ya watu asiowajua.
Alitembea chini kwa magoti akiwa amebusu sakafu ya yenye majitaka yanayonuka Fuu!, akakatwa na chupa zilizovunjika katika kidole gumba.

Mara akasikia mbwa wakiingia!
Walinusa, wakabweka kwa ukali. Mbwa mmoja akamrukia kutoka upande wa kushoto. Kinu akampiga teke, yule mbwa akadondokea upande mwingine , lakini mbwa mwingine akamng’ata mguuni kwenye kiatu lakini meno yake yalipenye mpaka kwenye mguu.

Akapiga kelele ya maumivu. Akasogea haraka, akatambaa ndani zaidi.
Kama hakuwa jasusi, angeshakufa. Kwa mtu wa kawaida asingeweza kutambaa na kujiburuza namna Ile huku mguuni akiwa ameshikiliwa na Mbwa.

Akaona mwangaza mdogo upande wa pili wa kalavati. Akajilazimisha kupitia sehemu yenye uchafu uliolundikana. Hapo akambamiza yule mbwa, yule mbwa akaachia huku akitoa sauti ya maumivu. Alipotoka, alikuwa amejificha nyuma ya vibanda vya walinzi wa parking ya magari makubwa.

Lakini, eneo lote lilikuwa limezingirwa.
Watu wa Deka walikuwa kila kona. Walikuwa na silaha nzito, walivalia mavazi meusi ya usiku, na kila mmoja alikuwa na redio ya mawasiliano.
Kinu alikuwa amechoka. Mguu wake ulikuwa na jeraha. Alijua mwisho wake ulikuwa dakika moja tu mbele…

**
Lakini kabla risasi haijarushwa, alisikia honi ya gari ikipigwa mara tatu. Muuu-muuu-muuu...
Gari ya Nissan Murano ya rangi ya dhahabu iliingia kwa kasi. Ilikuwa ikiwasha taa kubwa. Mlango wa abiria ukafunguka kwa kishindo.
“INGIA!” ilisikika sauti ya Moreen.
Mama Lutu alikuwa dereva.

Kinu aliruka kama simba ateaye mwisho wa maisha yake. Alikimbia kwa kujikokota, risasi ikapiga sakafu karibu na goti lake.
Akadondoka, lakini Moreen akashuka, akamvuta kwa nguvu zote.
Akamwingiza ndani. Mama Lutu akagonga gia ya R, akakanyaga mafuta kama mtu aliyewahi kuwa dereva wa mashindano ya magari. Murano ikalia kwa kishindo huku Moshi mwingi ukitoka, ikakata kona, ikapiga drift, na ikatoweka kuelekea maeneo ya Mbagala kupitia njia ya Chuo Kikuu cha Ardhi.

Watu wa Deka walipigwa butwaa. Helikopta ilikuwa juu lakini haikuweza kuchukua picha sahihi, kwa sababu Moreen alikuwa ameweka kinga ya kamera kwenye paa la Murano.

**
Ndani ya gari…
Kinu alilia. Sio kwa maumivu tu, bali kwa mshangao.
“Moreen… uliambiwa urudi. Kwa nini…?”
Moreen alimtazama, machozi yakimtoka.
“Nilijua... lazima uokolewe. Hata kama ingegharimu maisha yangu.”

Mama Lutu akasema taratibu:
“Tuna dakika 11 kabla hawajafunga njia zote. Tutumie mdomo kusema ukweli , tukifika tunapoelekea, tutafungua faili la majibu.”

Na hapo ndipo Murano ilikatisha kwenye uwanja wa magari makubwa, ikapita njia ya chini kwa chini iliyokuwa imeandaliwa kwa dharura.
Safari ya mwisho ilikuwa inaanza ama kuelekea kwenye mwisho wa Deka-6, au mwisho wa maisha yao.
*******
Kulikuwa na ukimya wa aina ya pekee katika maeneo ya pembezoni mwa Mji wa Kisarawe, mita mia kadhaa kutoka barabara kuu, katika ardhi tambarare iliyojaa majani mabichi yaliyokuwa yakielekeana na upepo wa asubuhi. Ranchi hiyo ilikuwa na ng’ombe takriban mia tano waliokuwa wakilishwa kwa mpangilio wengine wakinywa maji chini ya kivuli cha miti ya miembe iliyopandwa kwa ustadi wa mpangilio wa kijeshi.

Kwa nje, lilikuwa tu shamba la mifugo, lakini ndani ya moyo wa ardhi hiyo, palikuwa maficho yenye Siri nzito, nyumba ya mbao na kuta nene, mfumo wa kamera za usalama zenye jicho la infrared, na mashimo madogo ya ulinzi yaliyofukiwa kimkakati. Hapa ndipo alipokuwepo Andrew Kamage, mtu aliyekuwa akitajwa kwa sauti ya chini kama "chemchem ya dhamira".

Moreen alikuwa ndani ya jeep pamoja na Kinu na Mama Lutu. Gari lilipofika langoni, mlango wa mbao uliyochorwa maandishi ya Kimasai ukafunguka polepole, na ndani kulionekana mwanamume mrefu, mwenye mvi nyingi kichwani, si zile za uzee wa udhaifu, bali zile za hekima iliyoishi milimani na mabondeni. Macho yake yalikuwa yakitazama mbali hata akiwa karibu, na miwani yake ya glasi ya uwazi ilionekana kama dirisha la kutazama nafsi.

Alikuwa Andrew Kamage.

Alivalia shati la kitani la kijivu, suruali ya kaki, na buti laini za ngozi. Alipoona gari likisimama, alitembea kwa hatua ndefu na thabiti, kama mtu asiye na haraka, lakini mwenye hakika ya alipo.
“Karibuni nyote,” alisema kwa sauti ya upole iliyokuwa na msisitizo wa ndani, sauti iliyokuwa na mvumo wa maamuzi.

Walishuka wote. Moreen alimwangalia mzee huyo kana kwamba alikuwa anaona taswira ya busara iliyokuwa imepotea duniani. Mama Lutu alitabasamu polepole, hakusema neno, lakini macho yake yalizungumza lugha ya udadisi.

Walikaa kwenye ukumbi mdogo wa nje, uliojengwa kwa mbao zilizopakwa mafuta ya mti. Kulikuwa na meza ya duara, juu yake kulikuwa na chai ya tangawizi , na mandazi ya muhogo yaliyokaushwa juani.

Andrew alianza kwa utulivu:
“Upo wakati wa kupambana kwa silaha, na upo wakati wa kupambana kwa dhamira. Nyinyi mmepitia hatua zote mbili. Leo tumefika mahali ambapo historia huandika mstari wake kwa jasho la watu wachache.”
Akamwangalia Kinu moja kwa moja, kisha akasema:
“Tuna ushahidi, tuna picha, tuna sauti, lakini bado hatuna jambo moja, mzizi wa mfumo. Deka-6 si kundi, ni mfumo uliojificha ndani ya serikali, ndani ya makanisa, ndani ya kampuni, ndani ya mioyo ya walafi.”
Akatulia. Upepo ukavuma, ng’ombe mmoja akalia kwa mbali.

“Nchi hii haikushindwa kwa sababu ya ujinga wa wananchi, bali kwa sababu ya utulivu wa wenye Haki. Waliokaa kimya walipolipuliwa. Waliovaa tai nyeusi walipoiba mabilioni ya kodi waadilifu walikaa kimya. Walioua watu kwa sababu tu waliandika ‘Serikali imekosea. Wapenda Maisha wakaziba midomo"

Moreen alishika kikombe chake bila kunywa.
Andrew akaendelea:

“Kiongozi wa Deka-6 si mgeni katika macho ya umma. Hutabasamu kwenye televisheni, huvaa suti za Kifaransa, hujulikana kwa majina ya heshima. Lakini ndani yake, kuna moto wa tamaa ambao hautapoa mpaka akamate kila chembe ya mamlaka.”
Kinu alisogea mbele. “Ni nani huyo?”

Andrew alimtazama, akapumua kwa muda.
“Ukiona mti unaangusha kivuli kizuri, usiukate, utapoteza kivuli na mvua. Utumie muda kufukua mizizi yake. Mti huu… ni mkubwa. Na ukiuangusha vibaya, utawaponda wengi walioko chini.”

Mama Lutu alikunywa chai yake kimya. Lakini moyoni, alikuwa anajua jina hilo. Alishawahi kusikia sauti hiyo, nyuma ya simu iliyotumwa usiku wa manane. Lakini aliamua kukaa kimya. Kwa sasa, muda haukuwa wa majina ulikuwa wa ushahidi. Pia mafaili aliyopewa na Morris yalikuwa na jina hilo.

Andrew alisimama, akatazama upande wa machweo.
“Mnatakiwa kwenda mikoa mitatu: Tabora, Singida, na Dodoma. Kila mkoa una mtu mmoja ambaye aliwahi kufanya kazi ya ndani ya mfumo wa Deka, lakini alikataa. Walijificha, sasa wako tayari kutoa ushahidi. Ukipatikana, tutavunja mfumo huu kama ukuta wa tope mbele ya mvua ya masika”

Akamalizia kwa sauti yenye kina:
“Hii si vita ya bunduki. Ni vita ya kumbukumbu. Kila picha, kila jina, kila sauti, ni risasi dhidi ya uovu. Mkiwa hai, historia itawakumbuka. Mkifa, dhamira itawaombea.”

Giza lilianza kuingia. Kinu akamwangalia Moreen, akamshika mkono. Mama Lutu alisimama, akasema:
“Tuna kazi ya kuanza usiku huu. Historia itatutazama kama mashujaa"

Na hapo, mlango wa nyumba ya mbao ulifungwa kwa sauti ya utulivu. Ndani ya giza lililokuwa likishuka chini ya uso wa nchi, matumaini yalikuwa kama mshumaa dhaifu, lakini hayazimiki.
******

Barabara ilikuwa kimya, isipokuwa kwa kelele ya injini ya Murano iliyokuwa ikinguruma mngurumo wa ukombozi. Waliingia Tabora, jua lilikuwa linazama, likiacha mawingu mekundu yaliyofunika paa kama majivu ya vita vilivyopita.

Kinu, Moreen, na Mama Lutu walikuwa kimya. Kila mmoja alikuwa akifukuzia kumbukumbu zake. Lakini lengo lao lilikuwa moja, kumtafuta Bakari Kando, aliyewahi kuwa mtaalamu wa mawasiliano ndani ya mfumo wa Deka-6.
Kwa mujibu wa rekodi za serikali, Bakari alifariki kwa ajali ya moto, akiwa ndani ya nyumba ya kupanga maeneo ya Ilemela, Mwanza. Jeneza lililojaa mabaki ya mwili wake lilipelekwa Gairo, Morogoro, alikozikwa kwa heshima ya kitaifa. Waziri mmoja alihudhuria mazishi yake.

Lakini ukweli ulikuwa tofauti.
Bakari alijichoma katika nyumba yake mwenyewe kwa ustadi wa kisanii, akahakikisha mwili wa mnyama aliyekuwa amekufa siku mbili kabla unachomwa hadi kuwa majivu. Kisha akatorokea Tabora kwa jina jipya: Mzee Gadi, fundi wa redio mzee, mkimya, mwenye uoni hafifu, aliyeishi chini ya kivuli cha mti wa mkuyu.

Kinu aliingia eneo hilo kwa kutumia njia ya kuzunguka mtaa, akisindikizwa na Moreen aliyekuwa amevalia baibui na miwani ya macho ya jua, akionekana kama mfanyabiashara wa mkaa.
Walipofika, Mzee huyo aliwatazama, akacheka kwa sauti ya ndani.
“Nilijua mtakuja. Siri haina kaburi la kweli.”
Walikaa nyuma ya nyumba yake, kwenye sebule ya wazi. Hapo ndipo Bakari aliyekuwa ameigiza kifo chake alitoa USB drive iliyofichwa ndani ya spika ya redio.
“Huu ni mzigo wa damu. Ukianguka mikononi mwao, mnaweza kuitwa magaidi.”
Ndani ya kifaa hicho kulikuwa na:
Majina 38 ya watu waliopotezwa.
Mawasiliano ya barua pepe ya maafisa wa serikali waliotoa maagizo ya utekwaji.

Mpango wa kifedha wa mfuko wa siri wa Deka-6, uliojengwa kwa fedha kutoka China, kupitia kampuni ya kivuli ya kusambaza vifaa vya ujenzi.
Bakari alisema kwa sauti iliyobeba huzuni:
“Watu waliokufa kwa ukimya… ndio mashujaa. Kaburi langu lina majani Gairo, lakini moyo wangu upo hapa, unapowaka moto"
Kabla hajaagana nao, aliwapatia simu ya mkononi ya zamani, yenye ujumbe mmoja tu:

“Ukiona jina la Rais likitaja Amani, tafuta damu.”
Kutoka hapo, safari iliwaelekeza Singida.
Walikutana na Helida Majura, karani kipofu wa zamani wa Shirika la SUMP.
Alikuwa ameishi maisha ya kujificha, akitumia mbinu za ndani kuandika taarifa za wizi wa mabilioni ya fedha kwenye zabuni za chakula cha msaada zilizoishia kwenye maghala ya watu binafsi.

Aliwapa karatasi ya plastiki iliyohifadhi barua za kielektroniki.
“Waliwatesa waliokosa kula huku wakicheka mezani, wakila nyama ya msaada. Niliiona orodha. Nikaiandika upya, nikaificha. Niliamua kupoteza macho yangu, kuliko kuona tena unafiki huu.”
Moreen alilia kimyakimya. Hili halikuwa tena suala la ushahidi tu, lilikuwa mwitikio wa uanadamu.

Walipofika Dodoma, walimtafuta Padri Silvano Kidevu.
Alikuwa mrefu, mwenye uso wa utulivu wa kiroho. Aliishi nje ya mji, karibu na shamba la zabibu, akiwa na vijana waliokuwa wakijifunza kilimo.
Kanisani kwake, alifungua sanduku la mbao lililokuwa na faili muhimu za maungamo ya watu waliokiri kusaidia Deka, wakiwemo maofisa waliotekeleza mauaji.

Faili moja lilikuwa la mtumishi wa juu serikalini, aliyehusika moja kwa moja na mpango wa kuwamaliza wanaharakati wa mikutano ya haki ya kiraia Dodoma. Jina lake lilikuwa limefutwa kwa wino mweusi, lakini tarehe na saa ya kikao hicho zilionekana wazi.

Kinu alishikwa na hasira.
“Huyu ni nani? Nataka kumjua.”
Padri alinyamaza, akasema:
“Wengine hubeba msalaba wa kifo, wengine hubeba mzigo wa Siri, Usikate mti bila kujua mizizi yake. Ndio njia ya kujimaliza kwa hasira.”
Wakiwa wanarejea kwenye maficho ya Andrew Kamage, walijua wameshakusanya kila ushahidi muhimu.
Walimkuta akiwa kwenye eneo la wazi, akipika chai kwa kuni.

Alipowaona, alitabasamu kwa namna ya kiongozi wa kizazi kipya.
“Sasa… tuna kila tunachohitaji. Ukweli una miguu yake. Lakini bado hatujaangalia nyuma ya mlango. Kiongozi wa Deka ameshaarifiwa.”
Akatulia, akawatazama wote watatu.
“Amemtuma mtu wa mwisho. Kivuli kinachotembea. Hawataki tena kuchelewa.”
Kinu akauliza, “Ni nani huyu?”
Andrew alijibu kwa sauti ya chini:
“Anaitwa Mung’ong’o. Hana sauti. Hana huruma. Haachi alama yoyote. Ameshaua watu 21, wote waliojua jina la mtu mmoja, Kiongozi wa Deka.

Mama Lutu alishikilia kitenge chake kwa nguvu.
Na hapo taa za eneo hilo zikawaka miale ya hudhurungi. Kamera moja ilionyesha mtu anasogea kwenye lango la shamba.
Kinu alisimama. Moreen alishika bastola yake. Mama Lutu akavuta msalaba mdogo wa shingoni.

Vita ilianza rasmi. Si ya risasi tu, bali ya ushahidi dhidi ya uovu.
*********

Itaendelea
 
Hakuna Aliye Salama
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 05.

Tunarudi kidogo kisha tunaendelea....

Usiku wa kurudi kutoka Dodoma ulionekana kuwa tulivu, ulikuwa umebeba mwanga wa tahadhari uliokuwa hauonekani kwa macho ya kawaida. Kinu, Moreen, na Mama Lutu walipofika kwenye ranchi ya Andrew Kamage pembezoni mwa Dar es Salaam, hawakujua kwamba wameshikwa mkia na kivuli kilichokuwa kikiwasogelea taratibu. Kamera za usalama barabarani zilionesha kila gari lililoingia na kutoka, lakini hazikufanikiwa kuliona gari lao. lakini kamera haziwezi kunusa usaliti, wala kusikia sauti ya moyo wa msaliti anayepita nyuma ya migongo ya wenzake.

Walifika usiku wa saa sita, wakamkuta Andrew Kamage akiwa hamjalala akiwasubiri. wakasalimiana na Andrew ambaye alikuwa amesubiri huku akiwa anasoma kitabu chenye jalada lilolochakaa. akiwa kwenye sebule yake. Alipowaona, alisimama taratibu na kusema kwa sauti ya mzee mwenye hekima, "Karibuni tena. Sasa, tuna kazi ya kuiweka historia katika mstari mpya."

Hawakukaa muda mrefu. Uchovu wa safari ya Tabora, Singida, hadi Dodoma ulikuwa mkubwa, lakini mzigo wa ushahidi waliokuwa nao uliwapa nguvu ya matumaini.

Kinu aliingia moja kwa moja kwenye chumba cha mawasiliano. Moreen alienda kulala katika nyumba ndogo ya wageni iliyo upande wa mashariki mwa ranchi, huku Mama Lutu akiwa amepumzika kwenye chumba kilichokuwa jirani na nyumba ya Andrew. Kulikuwa na utulivu. Ndiyo, kimya kilikuwa kingi mno...

Asubuhi yake haikuwa ya kawaida.
Moreen alikuwa ametoka nje kuchukua mkate kutoka kwenye gari. Kinu alikuwa bado anachambua USB walizopewa, huku Mama Lutu akichemsha chai ya rangi jikoni. Andrew alikuwa katika vyumba vya wafanyakazi akikagua mashine za kuchakata chakula cha mifugo.

Lakini ghalfa muda mfupi baadaye, Moreen alikimbia kwa kasi, macho yake yakiwa na mshangao wa hofu.
"Dereva! Dereva wetu wa usiku... yupo chini ya mti! Amepigwa risasi!"
Kinu aliruka kama mshale. Mama Lutu alishika rosari yake kwa nguvu. Walitoka wote, wakikimbilia eneo la mti mkubwa wa mjohoro palipoegeshwa trekta.

Ndipo walipomwona.
Mwili wa dereva wa shamba, kijana wa miaka ishirini na nne, ukiwa umelala chali, damu ikiwa imeganda kwenye kifua chake, mdomo wake ukiwa wazi kama mtu aliyeshangaa kwa sekunde za mwisho kabla ya Risasi moja. Moja tu , iliyopigwa kwa umakini wa kijeshi, moja kwa moja kwenye kifua chake na kuupasua moyo wake.

Andrew alitokea nyuma yao. Hakusema neno. Aliketi chini ya kisiki, akaangalia mwili kwa muda mrefu kama mtu aliyesikia habari ya msiba.

"Hii... si risasi ya wizi. Hii ni risasi yenye ujumbe," alisema kwa sauti ya kutafakari.

Kinu alitazama eneo lote. Hakukuwa na alama za mapambano Wala Hapakuwa na nyayo. Hakuna ganda la risasi. Hakuna sauti yoyote ambayo mtu angeweza kusema ilisikika usiku. Kamera za ulinzi zilionyesha taswira za kawaida tu lakini dakika tatu baada ya tukio. Kipindi hicho kamera zilionekana kukatika ghafla kisha kuendelea.

Moreen alijikuta akitetemeka akiwa mwenye hofu nyingi "Huyu mtu... alitoka wapi? Na amejuaje tuko hapa?"
Andrew alinyamaza. Alitazama dirisha la jengo la wafanyakazi lililokuwa upande wa mashariki. Akasema kwa sauti ya chini:
"Ni Mung'ong'o... haachi kivuli. Ni wa aina yake. Hatumii mlango wa mbele, wala lango la nyuma. Huingia kupitia mwanya wa hofu ulioachwa wazi."
Mama Lutu alishika mdomo wake kwa kutakabari. Akasema, "Inawezekana alituona wakati tukirudi kutoka Dodoma. Labda tulikuwa tumewekewa kifaa kwenye gari bila kujua. Au... kuna mtu aliyekuwa anatufuatilia pasipo sisi kujua"

Kinu aliinama chini, akakagua mfuko wa dereva. Hakukuwa na kitu, isipokuwa kipande cha karatasi kidogo, chenye maandishi ya mkono, maandishi ya wino wa buluu"
"Mnafuatiliwa. Kila hatua yenu tumeihesabu. Hakuna atakayeweza kutoa. Tunasubiri amri tuu kuwamaliza."
Andrew alikuwa amenyamaza, lakini macho yake yalionyesha kuwa hakuwa ameshangaa.
"Au... ni simu. Labda walimfuatilia mmoja wenu kutoka Dodoma. Au labda... msaliti yupo katikati yetu."

Maneno hayo yaligonga mioyo yao kama bomu la baridi.
Kinu akasimama.

"Lazima tujue. Lazima tujue chanzo. Hatuwezi kusonga mbele bila kuelewa ni nani anatuangalia nyuma ya kioo. Nani Msaliti katikati yetu" Kinu aliongea akimtazama Moja baada ya mwingine huku akijaribu kusoma mioyo Yao kupitia macho Yao.

Moreen alitikisa kichwa, sauti yake ikitetemeka:
"Huyu si mtu wa kawaida. Hii inaweza kuwa ngumu na hatari kwetu. Mung'ong'o anaweza kuwa hatari lakini nani aliyefuta kumbukumbu za kamera. Andrew anasema chumba Cha kamera ni Moja ya vyumba vyenye ulinzi mkali sio rahisi kuingia Kwa mwili Wala kudukua mfumo wa Kamera."

Andrew akajibu kwa sauti ya kina:
"Mung'ong'o amelelewa kwa chuki. Aliondolewa sauti akiwa na miaka saba, ili asitoe siri. Amejifunza kuua kama wanyama wa porini wanavyojifunza kuwindana usiku. Aliwahi kuingia nyumba yenye walinzi sita na wote walikufa kimya, kabla hawajawasha taa. Hakuna aliyewahi kumsikia akikanyaga ardhi. Lakini jambo Moja la kutisha ni kuwa, Mung'ong'o hawezi kufanya shughuli zake bila Mtu wa Siri, Msaliti"

Kimya kilitanda.
Mama Lutu akavuta kiti. Akasema polepole:
"Kama kweli ni yeye... basi hii siyo tena vita ipo mlangoni kabisa"
Andrew alitazama mbali, kwenye kilima cha tatu, palipojengwa mnara wa zamani wa mawasiliano. Akasema:
"Lazima tuhamie. Tutumie 'Plan G'. Tutumie mifumo ya kuficha nyayo. Tutawasiliana kupitia ishara. Na msirudie mahali popote mara mbili."
Alipoondoka, Moreen alichuchumaa mbele ya kaburi la kijana wa shamba. Ambaye tayari walikuwa wameshamzika. Akavuta pumzi.

"Alikufa kwa kuwa tulikuja hapa.. kama tusingekuja huenda angelikuwa hai. na bado hatujaanza kupigana na Deka. Wangapi watakufa, wangapi watasalimika"

Kinu alisimama nyuma yake. Akasema:
"Tutamlipia kwa ushahidi. Na kama ni mmoja wetu aliyesababisha, tutaijua sura ya msaliti hivi karibuni. Msaliti lazima ajulikane. Ole wake "
Na hapo, kamera ya mbali ilionesha mtu mmoja, amevaa koti jeusi, akisimama kwenye jiwe la kichuguu upande wa pili wa shamba, akiwa amefuta nyayo zake kwa matawi ya mti.

Mtu yule aliyekuwa ameficha sura yake Kwa barakoa, akiwa amevaa koti la ngozi jeusi, kapero kichwani. Akaruka uzio kisha akachomoa simu yake ndogo na kufanya mawasiliano Kwa kuiweka masikioni. Ni kama aklikuwa akiwasiliana na mtu Fulani ambaye alikuwa akimjulisha kilichotokea.
Kisha akaondoka, video ya Kamera ilikatika, Andrew alienda kwenye mnara kurekebisha mtambo ya kurudisha video zilizokuwa zimefutwa.

Lakini swali lilikuwa nani aloyefuta video?
Pili Mung'ong'o alijuaje maficho ya Andrew Kamage aliyekaribisha Kinu, Moreen na Mama Lutu?.....

******"*""
Usiku ulianza kushuka taratibu juu ya anga la Dar es Salaam. Anga lilikuwa bubu, kimya kama vile mawingu yenyewe yalikuwa yakitafakari juu ya maafa yaliyotokea. Kwenye ranchi ya Andrew Kamage, hewa ilikuwa nzito, na kila mmoja alitembea kwa tahadhari ya ndani kana kwamba ardhi yenyewe ilikuwa ikisikiliza mioyo Yao.

Kinu alikuwa amekaa ndani ya chumba cha mawasiliano akiwa amevaa headphones, akirekodi na kuchambua mawimbi ya redio ya kijeshi. Mfumo wao wa mawasiliano ulikuwa umevamiwa kwa muda mfupi, muda uliotosha kwa mtu kujua walipo na kufuta ushahidi.

Wakati huohuo, Moreen yeye alikuwa kwenye chumba cha chini kabisa, akipitia orodha ya watu waliowahi kuwa karibu na Andrew Kamage , madereva, wasaidizi wa shamba, walinzi wa zamani, hata wauzaji wa chakula walioingia kwa njia ya tenda.

Lakini majibu ya hakika hayakupatikana kwao.
Katika giza la saa mbili usiku, Andrew Kamage alitoka nje ya jumba lake. Alikuwa amevalia kanzu ya rangi ya udongo, na alikuwa ameshikilia kijitabu, Alimkuta Kinu nje akiwa ameketi kwenye kiti cha mbao, macho yake yakilitazama giza.

"Tumepitia majina mia moja hamsini. Hakuna hata mmoja anayeshukiwa," alisema Kinu kwa sauti ya kukata tamaa.
Andrew aliketi. Akavuta pumzi ndefu. "Wakati mwingine, usaliti hauji kutoka nje. Unatokea pale tunapopumzika zaidi ya tulipotakiwa kupumzika."

Moreen alitoka nje muda huo, akiwa na faili la picha na namba za simu. "Huyu hapa, mfanyakazi wa zamani wa mawasiliano. Aliacha kazi miezi mitatu iliyopita bila sababu. Tena alikuwa wa mwisho kufanyia kazi katika mfumo wa CCTV."

Kinu alichukua lile faili. Jina lilikuwa: James Matari. Alikuwa kijana mwenye akili nyingi, lakini hakuwa na historia ya uhalifu. Kinu akaamua afuatilie zaidi kesho yake.

Lakini ndani ya chumba cha Mama Lutu, mlango ulifungwa kimyakimya. Ndani ya pochi yake ya nguo, simu ndogo ya zamani yenye batani zinazowaka mwanga wa njano iliwaka kimyakimya. Akafunua pochi, akaichomoa na kuandika ujumbe mfupi:

“Hakuna aliyeshuku. Wanaelekeza uchunguzi kwa James. Endeleeni na hatua inayofuata. – M.L”
Kisha akafuta ujumbe huo mara moja, na kuiweka tena simu hiyo chini ya godoro lake. Kisha akavuta pumzi ndefu na kurejea kulala.

Siku iliyofuata, Andrew aliwapeleka Kinu na Moreen kwenye sehemu ya chini ya ardhi, iliyojengwa kama handaki la dharura. Humo kulikuwa na kompyuta za kisasa, mifumo ya kijasusi, ramani za nchi, picha za satelaiti na orodha ya watu waliopotea au kuuawa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Kinu aliangalia orodha hiyo. Ilikuwa ndefu, majina 66. Watu waliopinga mfumo, waliokosoa hadharani, waliowahi kuandika, kupaza sauti, kuongoza maandamano, au hata wale waliotuma ujumbe mfupi tu mitandaoni kuhusu haki za binadamu, uwajibikaji au uhuru wa kutoa maoni.

Wote walipotea.

Moreen alipiga picha ya orodha hiyo. Alikuwa kimya muda mrefu kabla ya kusema:
"Kama kila mmoja anapotea... Na watu wote hawa sasa hawapo.. sisi tuko mbali kiasi gani na orodha hii?"
Kinu alimwangalia kwa macho yaliyokosa jibu. Andrew Kamage alipiga hatua mbili mbele, akasema kwa sauti yenye mzizi wa matumaini:

"Tofauti yenu ni kwamba mnayo nafasi ya kuchagua, kupotea au kupambana kwa nguvu ya kweli. Wale waliotangulia walikosa msaada. Sasa kuna mfumo mpya. Na ndani ya mfumo huu... tupo wachache, lakini wenye Nia na dhamira ya kweli"

Kinu aliangalia saa yake. Ilikuwa saa tano kasoro dakika tano. Akasimama na kugeuka kwa Andrew. "Na Mung’ong’o? Vipi kuhusu kivuli chake?"

Andrew akatabasamu kwa huzuni. "Kivuli hakiwezi kufutwa kwa mwanga tu. Lazima ujue ilipo mizizi yake. Na kwa taarifa nilizonazo — Mung'ong'o hana mizizi ya kawaida. Amelelewa katika nyumba za kubwa isiyo na usajili, Na anayeweza kumtoa ni sisi, lakini tumtoe panya aliyepo ndani ya nyumba yetu"

Kimya kilirudi tena.
Moreen alishika begi lake. "Tutaanza na James kesho. Lakini sidhani kama yeye ndiye mhalifu halisi. Kuna mtu anayecheza mchezo wa pili nyuma ya pazia. Na anatutazama. Kila hatua."
Kinu akasema kwa sauti ndogo: "Kama msaliti yupo... atajifunua mwenyewe. Tuna kazi ya kufanikisha. Ushahidi lazima uwafikie wanaostahili."

Nje ya handaki, upepo ulianza kuvuma. Mbali kule juu ya miti ya miembe, ndege mmoja aliruka kwa hofu. Na chini ya kitanda cha Mama Lutu, simu ndogo iliwaka tena, ikiwa imepokea ujumbe mmoja tu:
“Hakikisha wanaenda Dodoma kesho. Tutaweka mpango mzito kule. – DEKA”
Mama Lutu aliiangalia kwa sekunde kadhaa, kisha akaizima. Akatazama kioo kilichokuwa ukutani.

Sura yake ilionekana thabiti, lakini macho yake hayakusema ukweli.
******

Siku ya kuondoka kwenda Dodoma ilianza kwa ukimya uliosheheni miguno ya upepo na nyimbo za ndege waliokuwa wakihama miti kutoka mti mmoja kwenda mwingine. Jua lilipochomoza kwa tabu, lilitoa Nuru hafifu yenye woga kama mtoto anayekaribia nyumba ya baba mkali. Anga lilifunikwa na ukungu mwembamba, ukungu uliobeba hisia za kitu kinachokaribia lakini hakionekani.

Andrew Kamage aliwasindikiza Kinu na Moreen hadi lango kuu la ranchi, akiwa amesimama katikati ya miale ya jua ya mapema ambayo ilimmulika uso wake wa mvi kama tai aliyechoka na vita lakini bado ana jicho la kutoboa moyo wa adui.

Mama Lutu alitokea akiwa na koti la kijivu, lililokuwa limefunika vizuri mkoba wake mdogo. Alikuwa mtulivu, akitabasamu kwa unyoofu wa mwanamke wa Kizaramo mwenye historia ya mafunzo ya ualimu na mapishi. Hakuna aliyeweza kusoma ndani ya moyo wake… isipokuwa Mungu peke yake.

Safari ya kuelekea Dodoma ilianza saa mbili na nusu asubuhi. Gari lao lilikuwa Toyota Prado nyeusi, lenye vioo vya giza. Moreen alikuwa dereva. Kinu aliketi mbele na ramani yake ya siri, huku Mama Lutu akiwa nyuma akitazama dirishani kwa muda mwingi kana kwamba alikuwa akiagana na mandhari aliyoyaficha mengi kuliko alivyoyasimulia.

Walipita maeneo ya Pugu, wakakata Kongowe kisha wakaunganisha njia ya Bagamoyo kabla ya kuingia barabara kuu kuelekea Morogoro. Njiani, milima na mabonde vilicheza kwa utulivu wa tahadhari, huku hewa ya asubuhi ikiwa imebeba harufu ya udongo ulioamka kwa baraka za siku ngeni.

Moreen alivunja ukimya.
“Kwa nini kila tukipata amani kidogo, kuna kivuli kinatufunika?”

Kinu akamjibu bila kumtazama. “Kwa sababu tupo kwenye vita isiyo na bunduki tu, bali silaha ya hofu. hofu hiyo... ndio silaha pekee ambayo DEKA wameizoea kushinda nayo.”
Walipofika eneo la Gairo, jua lilikuwa juu. Ndipo simu ya Mama Lutu ilitetemeka kimyakimya. Aliiangalia haraka ujumbe mfupi wa namba isiyo na jina:

“Usisahau. Dodoma ndio pango la mwisho. Fungua mlango, usionekane ukishika kitasa.”

Aliifuta kwa haraka, na kuweka simu hiyo chini ya kiti.
Walifika Dodoma saa kumi na dakika ishirini. Jiji lilionekana kama jukwaa la sinema, barabara zake safi na majengo yake ya kisasa yalikuwa kimya kama waombolezaji waliovaa mavazi meusi. Magari yalipita taratibu. Polisi walionekana pembeni wakiwa na sura zisizotabasamu, kama walikuwa na namba za siri walizotakiwa kuzilinda kuliko roho zao.

Walielekea kwenye nyumba ya mkongwe wa zamani wa bunge, aliyewahi kuwa mpigania uhuru. Jina lake lilifutwa kwenye kumbukumbu rasmi, lakini kwa wale waliotembea ndani ya misingi ya Taifa, bado walimwita Babu Njoka.

Babu Njoka aliishi nje kidogo ya mji, kwenye kijiji kiitwacho Mahoma Makulu. Nyumba yake ilikuwa ya zamani, kuta zake zikiwa na mipasuko ya muda, lakini ndani yake kulikuwa na maktaba yenye taarifa nyingi kuliko hata baadhi ya ofisi za kiintelijensia za Serikali.
Walipofika, walimkuta ameketi kwenye mkeka wa nyasi, akisoma gazeti la mwaka 1998. Miwani yake ilikuwa imefungwa kwa utepe wa bluu.

“Ahaa… hatimaye watoto wa nchi wamefika,” alisema kwa sauti ya kuvuta maneno kama moshi wa tumbaku.
Kinu alimsogelea. “Babu Njoka… tunahitaji kujua kilichofichwa. Tuliahidiwa kuwa una ushahidi wa nyaraka za watu waliohusika moja kwa moja kuunda Deka.”
Babu Njoka alitabasamu kwa macho, si mdomo. “Ninao. Lakini msije mkadhani kila mwenye nyaraka ni shujaa. Wapo waliouawa kwa kuwa walizihifadhi, na wapo waliouawa kwa kuzisoma tu.”

Aliwaingiza ndani. Ndani kulikuwa na mafaili ya zamani, ramani, rekodi za simu, na mkanda mmoja wa kaseti ulioandikwa kwa herufi nyekundu: “Watu wa Ndani.”
Wakati wakiwa ndani wakichambua taarifa hizo, kwenye ghorofa moja ya siri ndani ya Dodoma, mtu mmoja aliketi kwenye giza, akiwa amevaa suti ya kijivu. Meza yake ilikuwa tupu isipokuwa kwa picha tatu: Kinu, Moreen, na... Mama Lutu.

Aliinua simu ya mezani, akapiga namba moja tu:
“Wapo Dodoma. Mama yupo nao. Endeleeni na mpango.”
Simu ikakatwa. Mvua ilianza kunyesha kimyakimya… Dodoma ikafunikwa na moshi wa ahadi za damu.
******

Ndani ya chumba cha udongo, chini ya paa la mabati yaliyochakaa kwa kutu ya muda mrefu, kulikuwako ukimya wenye hadhi ya maktaba. Vitabu vya historia, orodha za wanamapinduzi, picha za maandamano ya miaka ya sabini, vyote vilikuwa kimya, lakini vikiwa vinapiga kelele ndani ya mioyo ya waliovitazama.

Babu Njoka alisimama mbele ya meza ya mbao, akishikilia fimbo ya muanzi akiwa amevaa kanzu iliyobeba historia.

“Watoto wa nchi,” alisema kwa sauti ya utulivu, “Watu wamepoteza maana ya uzalendo. Wanadhani uzalendo ni kuvaa bendera tu shingoni siku ya uhuru. Hapana. Uzalendo ni kukataa kuuza dhamira yako kwa noti chafu. Uzalendo ni kuamka usiku kulinda nchi hata kama huna cheo. Uzalendo ni kumkemea mwizi, hata kama ni baba yako."
Aliweka fimbo chini, akavuta kiti chake cha kamba na kuketi.

“Na uwajibikaji… ni kiapo kisichosemwa, lakini kinacholindwa na dhamira. Kiongozi anayekosa uwajibikaji ni kama mzazi anayewatelekeza watoto wake porini. Anazaa hofu badala ya matumaini.”

Kinu alikuwa ametulia. Moreen alikuwa anaandika, lakini macho yake yalikuwa yameshika maneno ya Babu Njoka kana kwamba ni mwalimu wa kizazi cha mwisho.

“Uadui mkubwa tuliobeba,” aliongeza kwa sauti ya kutetemeka “Sio wa mzungu wa kale aliyekuja na Biblia na bunduki. Hapana. Uadui wetu sasa ni ukoloni mweusi, ndugu zetu waliovaa suti, kuimba Taifa letu, lakini kwa ndani ni matapeli wa tumbo. Wanaiba ndoto za watoto wetu, halafu wanatupa takwimu za uongo kwenye runinga.”

Kisha akainuka tena. Akatoa faili kutoka chini ya meza.
“Ndani ya faili hili kuna barua za siri kutoka kwa maafisa wawili waliowahi kuhudumu ndani ya DEKA kabla hawajatoroka. Walikimbilia Kenya na Uganda. Wote walikufa mwaka mmoja baada ya kuandika barua hizi. Mmoja alitupwa mtoni, mwingine alitekwa akiwa na familia yake. Hakuna aliyepatikana hadi leo.”
Kinu alichukua faili hilo, Moreen aliinua kamera yake ndogo na kuanza kupiga picha ukurasa kwa ukurasa.

Ndani ya faili kulikuwa na majina matatu ya viongozi wa juu waliokuwa wanapokea hongo kutoka makampuni ya nje ili kufanikisha mikataba ya kifisadi. Mmoja wa hao majina alikuwa kwenye serikali ya sasa.

Lakini kabla hawajamaliza, simu ya Mama Lutu ilipokea ujumbe kimyakimya. Ilikuwa imezimwa, lakini aliiwasha ghafla na kusoma. Ujumbe ulisomeka:

“Taarifa kamili ya kuingia kwao imeshapatikana. Endelea kuwashika karibu. Tutawakusanya wote kwa mkupuo mmoja.”
Alisogeza simu chini ya kanga yake, akawa amekunja uso kama mtu aliyesikia habari ya ugonjwa wa jirani. Akatabasamu. Akasema,

“Babu Njoka, chai yako ni tamu kweli… umeichanganya na nini?”

Babu Njoka akajibu kwa tabasamu la ujanja, “Ninachanganya maumivu ya nchi hii, mwanangu.”

Usiku ulipoingia, Moreen alienda kulala kwenye chumba cha jirani. Kinu alibaki kwenye meza ya kujisomea akiangalia ramani ya mji wa Dodoma, akisoma mikondo ya barabara na maeneo yenye mashaka. Mama Lutu alijitenga nje, akipiga simu ya kawaida, akidai anazungumza na mjukuu wake. Lakini aliyekuwa upande wa pili wa simu alikuwa mpangaji wa mauaji.

Saa sita usiku, Moreen aliamka kwa kishindo cha ndoto. Alikuwa anatweta. Ndoto yake ilikuwa ya moto. Moto ulioteketeza watu wenye sauti yenye Nia ya ukombozi. Watu waliopaza sauti ya haki. Watu waliopotea bila mazishi.

Asubuhi yake, taarifa ziliwasili kutoka kwa mtoa taarifa wa Kinu aliyekuwa Tabora. Mwanaume aliyekuwa jasusi wa kujitegemea, aliyejificha kama mchuuzi wa vifaa vya kilimo.
Kinu alichukua simu, akafungua ujumbe. Alipoutazama, alisita. Moreen alimkaribia.

“Vipi?”

Akamwonyesha:
“Aliyekuwa anawasaidia kule Tabora yule aliyekuwa ameigiza kufa kwenye ajali ya moto amepatikana akiwa ameuawa. Mwili wake umetupwa karibu na kambi ya kijeshi ya zamani, umeungua vibaya. Walimtambua kwa meno yake ya dhahabu.”

Moreen alifunika mdomo wake kwa mshangao. Macho yake yakamiminika machozi.
Mama Lutu alikuja kwa haraka, akijifanya hajui kitu.

“Nini tena? Mbona nyie mnakuwa na huzuni?”
Kinu akamjibu, “Mmoja wetu kule Tabora… yule aliyekuja kutoa faili la kwanza… ameuawa.”
Mama Lutu alitikisa kichwa polepole. “Damu ya wasemaji wa kweli huwa haikai ardhini. Hutiririka hadi ifike kwenye mto wa haki.”

Lakini Moreen alimwangalia kwa macho ya wasiwasi kwa mara ya kwanza. Alihisi kitu hakikuwa sawa. Kitu kisichoelezeka.
Na kabla ya jioni hiyo, taarifa nyingine ilifika kutoka kwa mshirika wao wa Singida.

Mwili wa mzee mstaafu aliyewahi kuwa Katibu wa Fedha wa zamani, uliokotwa kandokando ya reli. Shingo yake ikiwa imevunjwa. Alikuwa ndiye aliyetoa orodha ya mikataba ya kifisadi iliyoanzisha DEKA.

Ukweli ulikuwa unazidi kuzama kwenye dimbwi la damu. Maiti zilikuwa hazina kauli tena lakini ziliacha ushahidi.
Na usaliti bado haujafichuka… lakini harufu yake ilianza kusambaa kama moshi wa mnara wa moto.

Chungu cha 06 kinakuja…

Itaendelea
 
Hakuna Aliye Salama
Mtunzi: Robert Heriel
Chungu cha 06:

Usiku ulijaa kimya kilichokuwa na mshindo katika nafsi zilizokuwa na Mashaka. Dar es Salaam ilikuwa kama mama aliyejifunika uso wake kwa kanga ya huzuni. Pembezoni mwa ranchi ya Andrew Kamage kulikuwa kimya l. Miti mirefu ya minazi ilikuwa kama walinzi waliolala kwa macho ya nusunusu. Tukio la kuuawa dereva wa shamba liliongeza historia na hali ya kutisha katika ranchi hiyo.

Moreen alikuwa na hofu, lakini hofu hiyo haikupata nafasi ya kumshinda. Maji alikuwa ameshayavulia nguo. Sasa uamuzi ulikuwa wake aoge au anawe au ayanywe. Ilikuwa ni hofu ya jasiri, ile inayokufanya usimame japo miguu ikiwa inatetemeka.

Tangu walipowasili katika maficho ya Andrew Kamage, moyo wake haukuwa sawa. Kulikuwa na hisia nzito ambazo Moreen hakuweza kuzipuuzia tena. Mama Lutu alikuwa akibeba tabasamu lililopwaya, tabasamu la mtu anayeishi kati ya ukweli na siri nzito.

Alipomwona Mama Lutu ameenda sehemu ya kupumzikia nje, alichukua funguo ya chumba chake kinyemela na kujivisha utulivu wa njiwa. Akaenda kungua mlango taratibu ambapo Harufu ya manukato ya karafuu ilimkaribisha. Ndani, kila kitu kilionekana kawaida isipokuwa simu ndogo ya mchina, ambayo ilikuwa juu ya meza, ikiita kwa mtetemo.

Aliichukua na kubonyeza kitufe cha menyu. Ujumbe wa mwisho ulisomeka:

“Saa moja usiku. Kijitonyama. Wasiliana na M-02. Usisahau ushahidi.”
Kuna majina mengine yalikuwa yamehifadhiwa kwenye simu hiyo: Ngome, Kiongozi, M-02. Moreen alihisi kuganda kwa damu mwilini. Aliirudisha simu mahali pake harakaharaka na kutoka nje bila kushtukiwa. Ndani ya moyo wake kulikuwa na mzuka wa ukweli. Mzuka wa hofu. Mzuka ulioanza kuujua ukweli uliokuwa umewazunguka kama rafiki lakini kumbe ni adui hatari sana..
******

Saa Moja Usiku, Kijitonyama
Baridi ilikuwa imeambatana na upepo wa bahari. Moreen alichukua koti lake lenye Kofia akalivaa, na kitenge cheusi. Alikata kona kwa kona, akimfuatilia Mama Lutu ambaye alikuwa kwenye pikipiki, ikiendeshwa na kijana aliyevaa jaketi la Puma.

Walifika kwenye kona ya barabarani karibu na stoo ya zamani ya nguo. Mama Lutu alishuka na kuingia kwenye jengo la ghorofa moja lililokuwa na mwanga hafifu. Yule kijana mwenye pikipiki akaondoka. Moreen hakutaka kungojea, akaiweka simu yake tayari akiwa amejificha nyuma ya gari lililokuwa limeegeshwa karibu.

Dakika tano baadaye, wanaume watatu walitokea. Mmoja alikuwa amevaa suruali ya kijivu na viatu vya kijeshi. Mwingine alikuwa na koti jeupe, na mweusi wa mwisho alikuwa na madoadoa ya makovu usoni. Walizungumza na Mama Lutu kwa dakika kadhaa.

Moreen alipiga picha. Kisha video. Akazituma kwa Kinu kwa haraka, lakini wakati anafanya hivyo taa ya gari iliwamulika. Mmoja wao alipiga kelele:

“Yule pale! Mkamate!”

Moreen alikimbia, kama upepo wa mvua za vuli. Aliruka ua la nyumba ya iliyokuwa jirani, akatumbukia kwenye mtaro wa maji. Mvua ya manyunyu ilikuwa ikiendelea ililoanisha nguo zake. Miguu yake iliteleza lakini moyo wake ulikaa sawa.
Kama panya aliingia ndani ya duka lililokuwa limefungwa, kupitia dirisha la pembeni. Akasubiri hadi mlio wa magari ulipopita. Aliwazidi ujanja.

Wakati huohuo… Geneva
Kinu alikuwa ndani ya jengo refu la mawe, ofisi ya Haki za Binadamu ya Kimataifa. Mbele yake aliketi mwanaume mwenye sura ya kukunjamana kwa maumivu ya muda mrefu. Mwanaume huyo alikuwa Marcus raia wa Sweden aliyewahi kufanya kazi Afrika Mashariki.

Kinu aliweka mezani faili lake la ushahidi. Marcus alilisoma kwa ukimya. Picha. Ramani. Majina. Mahali pa matukio. Mauaji ya wanaharakati. Orodha ya waliotekwa.

Marcus aliinua kichwa chake:
“Unajua ni nini hatari ya DEKA? Sio tu kuwa wanaua. La hasha. Ni kuwa wanaua ukweli. Wanaua ndoto. Na Taifa lisilo na ndoto ni kaburi lenye bendera.”

Akainua kidole chake, akaanza kueleza:
Mbinu ya Kwanza: Unda vyombo mbadala vya habari. “Wakati vyombo vya kitaifa vimefungwa midomo, jenga mitandao ya kidijitali, podcast, video za mtaani. Fikisha sauti yako kupitia njia ambazo DEKA haijazidhibiti.”

Mbinu ya Pili: Shirikisha sanaa, utamaduni na ucheshi. “Watu hawasomi ripoti ndefu. Lakini wanatazama video. Wanapenda vichekesho. Sanaa inaweza kuwa silaha. Tenzi, mashairi, katuni zenye ujumbe. Huko ndiko vita inapaswa kwenda.”

Mbinu ya Tatu: Gawanya mfumo kutoka ndani. “Tafuta watu waliomo ndani ya mfumo lakini hawaridhiki. Wapeni nafasi ya kusema. Jenga uaminifu nao. Wanaweza kukupa nyaraka, sauti, hata ramani ya mikakati.”

Kinu aliandika kila neno. Alipoinua macho yake, Marcus alimwambia:

“Ukianza kutengeneza mapinduzi ya kweli, lazima ujue, haitakuwa ya haraka. Lakini kila tone la ukweli unalolitoa, linaweza kuwa tone la mwisho kwenye kikombe cha udanganyifu.”

Usiku huo…
Moreen alirejea mafichoni ya Andrew Kamage akiwa anatetemeka. Simu yake ilikuwa salama. Aliketi pembeni ya Kinu, akampa simu. Kinu alitazama picha. Alimtazama Moreen kwa macho ya mshangao.

“Sasa tumeona… sura zao. Wapo.”
Moreen akasema kwa sauti ya chini, “Lakini hatujui nani ni mkubwa wao.”
Kinu alishika mkono wa Moreen, akasema kwa msisitizo:

“Hakuna aliye salama. Lakini pia… hakuna aliye peke yake.”
********

Usiku ulikuwa mrefu kama sala ya mwenye huzuni. Upepo wa Bahari ya Hindi uligonga kuta za jengo la ranchi ya Andrew Kamage kwa sauti ya manung’uniko. Ilikuwa ni sauti ya mashaka, sauti ya historia iliyojificha ikitaka kuzungumza kwa haki iliyopotea.

Moreen alikaa ukingoni mwa kitanda, akiwa amevua koti la mvua na kupunguza sauti ya simu yake. Kinu alikuwa amesimama pembeni ya dirisha, akitazama anga la usiku lililofunikwa na nyota zilizokaa kimya kama mashahidi wa jinai ya karne.

“Tumemgundua,” Moreen alisema taratibu, “lakini hatuwezi kumkabili sasa. Haitakuwa busara.”
Kinu aligeuka, macho yake yakiwa yamejaa uzito. “Mama Lutu ni sehemu ya DEKA. Na sisi tupo naye hapa. Hatuna hakika ni lini atachoma moto hii nyumba. Tusipofanya tahadhari na kwaakili atatuunguza wote.”

“Tutamnyamazia,” Moreen aliongeza, “Tutamcheka, tutamkaribisha mezani, lakini mioyo yetu itamfungia milango yote.”
Walikubaliana. Hakuna atakayemwambia Mama Lutu kwamba siri yake imeshavuja na ameshajulikana. Ilikuwa ni vita ya akili na kwenye vita hii, uhai wao ulikuwa ni mshahara wa kila uamuzi.

Usiku huo huo…
Mama Lutu alirudi ranchini akiwa na uso wa uchovu na begi la mgongoni. Alimkumbatia Moreen kwa kicheko cha kinafiki, akasema,
“Nilijaribu kwenda kutafuta taarifa za wanaharakati waliopotea. Nimefanikiwa kuzungumza na mtu mmoja pale Kurasini.”

Moreen alitabasamu, akasema,
“Pole na safari Mama. Karibu tena.”
Hakujua kuwa Mama Lutu alikuwa na misheni mpya. Kwenye pochi yake kulikuwa na vinasa sauti vidogo vitatu, vya teknolojia ya kisasa isiyotambuliwa na mitambo ya kawaida. Alipewa kazi na Kiongozi msaidizi wa DEKA akafunge vifaa hivyo kwenye maeneo ya mkutano wa Andrew Kamage, chumba cha mikutano, na ofisi ya siri ya Kinu.

Alifanya kazi hiyo kwa ustadi. Usiku huo, wakati wote wakiwa wamejikusanya kuangalia video ya ushahidi mpya kutoka Geneva, Mama Lutu alijitosa jikoni. Akaacha kifaa cha kusikiliza ndani ya picha ya ukutani, nyingine kwenye dirisha la jalalani, na ya mwisho kwenye kitabu bandia kwenye kabati la vitabu cha Andrew Kamage.

Akiwa anamaliza, alitabasamu kwa kijicho la kifedhuli. Mchezo wa usaliti ulianza kwa tabasamu, ukaendeshwa kwa ukimya na tahadhari. Kumjua Msaliti ni hatua Moja na kumdhibiti ni hatua nyingine. Kila hatua ni muhimu na inahitaji uangalifu mkubwa.

Siku mbili baadaye
Kinu alianza kutekeleza mbinu za Marcus. Alianza na mbinu ya kwanza: Vyombo mbadala vya habari.

Akiwa na kijana wake wa zamani wa chuo, David ambaye sasa ni fundi wa mitandao, walifungua tovuti isiyojulikana, yenye jina bandia “Mwangaza ulipotea”. Tovuti hiyo ilianzisha kurasa za siri zilizokuwa na makala, video, sauti za simulizi, na picha kutoka kwa mashahidi halisi wa mateso ya DEKA.

Kisha akamuita Moreen alafu Waliandaa video fupi ya dakika tatu iliyotumia sauti ya bandia, ya mwanamke aliyefungwa jela kwa miaka mitano baada ya kupinga ukatili wa polisi. Video ilianza kuenea kwenye WhatsApp, TikTok na Telegram.

Mbinu ya pili ilifuata: Sanaa na utamaduni.
Wakampata msanii wa uchoraji wa mtaani, Baraka, aliyekuwa amejeruhiwa mwaka 2021 kwenye maandamano ya wanafunzi. Baraka alichora katuni ya mtu mwenye midomo iliyofungwa kwa minyororo, huku macho yake yakitoa damu. Katuni hiyo iliwekwa kwenye video za mitandaoni ikiwa na mashairi ya Moreen.

“Simu yangu si bunduki, lakini ina risasi ya sauti.
Kalamu yangu si upanga, lakini huchanja udhalimu.
Mimi si askari, lakini najua kupigana bila damu.”
Watu wengi waliguswa na mashairi ya Moreen lakini haikujulikana Moja Kwa Moja aliyeimba nyimbo hizo ni nani. Kwani Moreen alijificha nyuma ya teknolojia. Taarifa zilianza kufika kwa waandishi wa habari huru walioko Afrika Kusini, Nigeria na hata Marekani.

Mbinu ya tatu — kupenya ndani ya mfumo, ilihitaji muda. Kinu alianza kuwasiliana na mwanasheria mmoja aliyeachishwa kazi miaka mitatu iliyopita baada ya kujaribu kufungua kesi dhidi ya kiongozi wa DEKA kwa tuhuma za utekaji. Mwanasheria huyo alijulikana kwa jina la Bi. Zalia alikubali kushirikiana nao, lakini kwa masharti ya usalama wake

Usiku uliofuata
Wakiwa ndani ya jengo la Andrew Kamage, Kinu aliita kikao cha ndani usiku wa manane. Wakiwa wameketi kwenye meza ya mbao iliyozeeka kwa heshima, aliwapa taarifa za hatua walizofikia. Andrew alimsikiliza kwa makini, akavuta pumzi ndefu, akasema:

“Mnajua mnachokifanya kinaweza kuokoa vizazi. Lakini pia kinaweza kuua kizazi chenu. Mnapaswa kujua, hii si vita ya siku kumi. Hii ni mapambano ya kubadilisha urithi wa Taifa.”

Moreen alimtazama Andrew kwa macho ya tumaini. “Tutapambana. Hata kama ni kwa gharama ya maisha yetu.”

Lakini wakati huo huo kwenye kona ya jengo, redio ndogo ilikuwa inawasilisha kila sauti yao moja kwa moja kwenda kwa mtu aliyekuwa ameketi katika chumba kidogo Cha ofisi ya ghorofa ya saba, akisikiliza huku akivuta sigara na kuchezesha bastola mezani.

Mchezo ulikuwa umeanza kwa sura mpya.
*********

Ndani ya jengo la mawe lenye mwangaza hafifu, mashine ya kisasa ya kusambaza taarifa ilikuwa ikitoa sauti ya ‘tik tik’ kama saa ya bomu.
Kwenye kona ya meza ya Andrew, palikuwa na ramani tatu: ramani ya Dar es Salaam, ya Dodoma na ya Tabora. Mistari nyekundu ilikuwa imechora njia zao ambazo wangezitumia. Miduara ya buluu ilionyesha maeneo salama. Lakini ilionekana wazi maeneo hayo yalianza kuwa machafu yenye kufuatiliwa na DEKA ingawaje Bado hayakuwa yametiwa nguvuni. Sura za usalama zilianza kuchafuliwa na alama za kuuliza.

Andrew alisimama dirishani, akitazama nje kwenye giza. Alikunywa kikombe cha kahawa baridi, halafu akageuka na kusema,

“Wapo mbele yetu. Wanajua tunakoenda kabla hatujaamua kwenda. Kuna mdomo unavuja.”
Andrew Kamage hakujua kama Mama Lutu ni Msaliti. Kinu na Moreen hawakutaka kufanya haraka kumwambia.

Kinu aliinamisha kichwa chini. Alijua wazi, uwepo wa vinasa sauti walivyogundua vilikuwa vimeshasambaza mengi kwa adui. Lakini hakuonyesha hofu. Aliweka kwenye meza picha zilizotumwa na mwanaume mmoja aliyefanya kazi bandarini. Picha zilionyesha makontena matano yaliyokuwa yanapakiwa usiku kwenda Afrika Kusini, yakifichwa ndani yake vifaa vya kijasusi na silaha.

“DEKA hawapambani tu kwa maneno,” Kinu alisema, “Wana silaha. Na sasa wana taarifa zetu.”
Andrew alimgeukia Moreen, “Tuna dakika chache. Tutoke humu. Lakini si wote.”

Moreen alishtuka. “Unamaanisha nini?”
Andrew akatabasamu kwa uchungu, “Kuna mtu lazima abaki, aendelee kuwaaminisha. Awaonyeshe kuwa bado anacheza nao. Na huyo mtu…”
Walitazamana. Hakuna aliyehitaji kusema. Kila mmoja alijua, Mama Lutu atabaki. Haikujulikana kwa nini Andrew alimchagua Mama Lutu kubaki. Lakini Kinu alihisi huenda Andrew naye amemjua Msaliti.

Saa kumi alfajiri
Gari aina ya Defender liliondoka taratibu kwenye njia ya vumbi. Kinu na Moreen walikuwa ndani. Walikuwa na ramani mpya, maeneo mbadala, na vifaa vichache walivyofanikiwa kuficha visijulikane na Mama Lutu. Wakiwa njiani, Moreen alichukua simu yake na kufungua barua pepe aliyotumiwa na Marcus.

Kulikuwa na orodha ya majina 14 ya wanachama wa zamani wa mfumo wa DEKA waliokataa kufanya kazi DEKA. Wengine walikuwa wamepotea. Lakini watatu walikuwa hai, wakiwa mafichoni. Mmoja alikuwa mwanamke aliyekuwa mkuu wa itifaki, mwingine alikuwa mwanasheria wa zamani wa DEKA, na wa tatu alikuwa mkuu wa kitengo cha habari ndani ya serikali, aliyestaafu kwa ghafla.

Mpango mpya ulianza: Kuwatafuta hawa watu. Kuwapata kabla DEKA hawajawapata. Kwani kila mmoja aliwasaka Kwa udi na uvumba.

Wakati huohuo… ndani ya jengo

Mama Lutu aliketi kwenye kochi la ngozi, akijifanya kuwa na usingizi. Lakini ndani ya pochi yake, palikuwa na redio ndogo ya DEKA, ikipokea sauti. Alibonyeza kitufe cha SOS na kusema kwa sauti ya chini,

“Target moved. Only me remained. Awaiting instructions.”

Sauti ya kiume ikamjibu kwa ukali wa chuma kilichochomwa:
“Delay no further. Prepare the final sweep.”
Mama Lutu alifunga pochi. Uso wake ulikuwa wa huzuni. Lakini moyoni alijua mchezo ulikuwa umekaribia mwisho. Haikuwa rahisi kumdanganya Andrew Kamage kwa muda mrefu. Na hakujua kuwa wakati huo huo, Andrew alikuwa katika ghorofa ya pili, akiangalia rekodi mpya ya kamera iliyokuwa imepandikizwa juu ya dari ikimuonyesha Mama Lutu akibonyeza pochi yake taratibu.

Andrew aliketi kimya. Kinywa chake kilitamka polepole:
“Sanaa ya usaliti… ni kama nguo iliyoshonwa kwa sindano ya shaba.

Itaendelea....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom