Simulizi ya kichawi: Makaburi ya wasio na hatia (The Graves of The Innocents)

Sehemu ya pili - 2

ILIPOISHIA:
Tulipokaribia nyumbani kwa mzee huyo, baba alinionesha ishara kwamba nisimame, nikafanya hivyo, tukawa tunasikia sauti za watu wengi wakilia kutoka nyumbani kwa mzee huyo, baba akanionesha ishara kama anayesema ‘unaona?’, nikashika mdomo kwa mshangao. Sikutaka kuamini kwamba kweli mzee Mwankuga alikuwa amefariki dunia.

SASA ENDELEA...
Nilijikuta nikishusha lile furushi la dawa na panga, nikawa nataka niende kushuhudia mwenyewe kama ni kweli lakini baba aliniambia nisithubutu kufanya hivyo, hasa kutokana na uhasama uliokuwepo kati yetu na familia hiyo. Bado niliendelea kuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kama ni kweli yule mzee amekufa.

Ilibidi baba anishike mkono, tukaenda mpaka nyumbani ambapo baba aliingia kwenye chumba chake cha uganga na kuanza kuchambua zile dawa tulizotoka nazo porini. Ni kama alijua kwamba nitamtoroka na kurudi kule msibani kwenda kushuhudia kilichotokea kwani aliniambia nikae palepale, nimuangalie jinsi alivyokuwa akichambua dawa.

Kweli nilitii maagizo yake, nikakaa pale lakini bado nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kilichoendelea. Nilipomuona baba amezama kwenye kazi yake hiyo, niliinuka na kuanza kuelekea mlangoni, akaniwahi na kuniuliza ninakokwenda.

“Naenda kujisaidia baba,” nilimdanganya baba, akanitazama usoni kisha akaendelea na kazi yake. Nilitoka na kwenda chooni ambako nako nilizunguka nyuma, nikatokomea huko na kwenda kutokea upande wa pili, nyumbani kwa mzee Mwankuga.

Kwa kuwa watu walikuwa wengi, hakuna aliyenitazama vizuri, kwa hiyo nikapata nafasi ya kujichanganya na waombolezaji ambao kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele ndivyo walivyokuwa wakizidi kuongezeka.
“Kwani alikuwa anaumwa?”

“Hapana alikuwa mzima wa afya kabisa na alikuwa akiendelea na kazi zake, mara akaanza kulalamika kwamba kichwa kinamuuma sana, damu zikawa zinamtoka puani na mdomoni, ghafla akadondoka na kugeuza macho, muda mfupi baadaye moyo wake ukasimama,” nilimsikia ndugu mmoja wa Mwankuga akimuelezea mmoja wa waombolezaji.

Ni hapo ndipo nilipoamini kwamba kweli Mwankuga alikuwa amekufa, kwa kuhofia kuonekana na watu, hasa ndugu zake ambao kama nilivyosema tangu awali hatukuwa na uhusiano nao mzuri, nilirudi kinyumenyume, kisha nikaondoka haraka kurudi nyumbani.

Nilimkuta baba akiwa amesimama nje ya nyumba yetu, akinitazama, nadhani alishashtukia kwamba nimemtoroka, aliponiona tu natokeza, akanibana kwa maswali magumu.

“Ulikuwa wapi?”
Nilikosa cha kujibu, nikawa najiumauma, baba akaniambia nina bahati sana vinginevyo angenifunza adabu, tukaingia ndani ambapo tulienda mpaka kule kwenye chumba cha uganga, baba akanikalisha chini na kuanza kuzungumza na mimi.

“Unajua wewe ndiyo mwanangu kipenzi na sasa umeshakuwa mkubwa, sina sababu ya kuendelea tena kukuficha mambo yangu ndiyo maana leo nimekuonesha baadhi ya mambo.

“Dunia imebadilika sana mwanangu, binadamu tunaishi kwa ubaya sana, hakuna anayemtakia mwenzake mema, watu wanawaonea wengine bila sababu, watu wasio na hatia wanakufa kila siku, ukienda makaburini, yaliyojaa ni makaburi ya watu wasio na hatia! Kila mmoja lazima ajilinde mwenyewe na ukishaweza kujilinda mwenyewe, unaweza pia kuwalinda wenzako,” alisema baba, maneno ambayo yaliniingia lakini bado sikuwa naelewa kile alichokuwa anakimaanisha.

Bado nilikuwa nataka ufafanuzi wa kifo cha mzee Mwankuga kwa sababu kwa akili yangu, niliona kama hakuwa amefanya jambo lolote kubwa kustahili adhabu ya kifo. Ni kama baba aliyaona mawazo yangu, akaniambia anajua najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kuhusu kilichotokea kule msituni.

“Kuna yule rafiki yako aliyekufa kwa kutumbukia kwenye kisima mwaka jana, unamkumbuka?”

“Alfred? Ndiyo namkumbuka,” nilimjibu baba huku nikiwa na shauku ya kutaka kusikia anachotaka kukisema.

Akaniambia mazingira ya kifo cha Alfred, yalikuwa yamejaa utata wa hali ya juu na kwamba baada ya kuchunguza kwa kina, aligundua kwamba Alfred hakufa kifo cha kawaida, bali aliuawa.

Akaendelea kuniambia kwamba hata huko kuuawa kwenyewe, japokuwa kila mtu alikuwa anajua ni kweli amekufa na kuzikwa, lakini ukweli ni kwamba hakuwa amekufa bali alichukuliwa msukule.

“Kwani kuna tofauti gani kati ya mtu aliyekufa na mtu aliyechukuliwa msukule?” Nilimuuliza baba, akaniambia kwamba mtu aliyekufa kwa kifo cha amri ya Mungu, huwa mwili unatengana na roho, mwili unaenda kuzikwa kaburini na huo ndiyo unakuwa mwisho wa maisha ya kawaida ya hapa duniani.

Akaniambia pia kwamba kwa kawaida, nafsi au roho ya mtu huwa haiishi ila baada ya kutengana na mwili, huhama kutoka kwenye ulimwengu wa kawaida na kwenda kwenye ulimwengu mwingine. Nilipotaka kumuuliza kuhusu huo ulimwengu mwingine, aliniambia kwamba atanifafanulia siku nyingine.

Akaendelea kunieleza kwamba mtu anayechukuliwa msukule, huwa hafi bali anabadilishwa kichawi kiasi cha kila mmoja kuamini kwamba ni kweli amekufa lakini kinachotokea, huwa anachukuliwa na wachawi na kwenda kutumikishwa kichawi kwenye kazi mbalimbali, mpaka siku ambayo atakufa kwa amri ya Mungu lakini kwa kipindi chote hicho, huwa anaishi kama msukule.

“Sasa mbona Alfred alipokufa tulienda kumzika makaburini na hata siku ya kuaga mwili wake, wote tulipita kwenye jeneza lake na mimi mwenyewe nilimshuhudia akiwa amelala ndani ya jeneza?”

“Ni vigumu sana kunielewa hiki ninachokisema kwa maneno, lakini nataka nikuhakikishie kwamba rafiki yako hakufa na aliyefanya yote hayo ni huyu mshenzi Mwankuga,” alisema baba akionesha kuwa na jazba, akaendelea kunieleza kwamba, licha ya Alfred, walikuwepo watu wengine wengi tu ambao wengine waliuawa kwelikweli lakini kwa ushirikina, ikiwa ni uonevu unaofanywa na wachawi hasa wanapokaribia kutoa makafara yao, na wengine huchukuliwa misukule.

Bado sikuwa namuelewa anachokisema, akaniambia anataka akanithibitishie kwamba Alfred hakufa. Aliacha kila alichokuwa anakifanya, tukatoka nje ambapo watu walikuwa wakizidi kufurika kwenye msiba wa Mwankuga na sasa vilio vya wanawake vilikuwa vikizidi kuongezeka.

Wala baba hakujali chochote, tukatoka na kuelekea makaburini ambayo yalikuwa eneo maarufu linalofahamika kama msalabani, nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kujionea mwenyewe kile alichokuwa anakisema baba kama ni kweli.

“Unakumbuka alizikwa kwenye kaburi gani?” baba aliniuliza, nikamwambia nakumbuka vizuri kwa sababu enzi za uhai wake, Alfred alikuwa rafiki yangu mkubwa na kifo chake cha ghafla, kiliniumiza mno moyo wangu. Kwa kuwa hata siku ya mazishi yake nilikuwepo mpaka makaburini, nilikuwa nalikumbuka vizuri kaburi lake.

Nikamuongoza baba mpaka kwenye kaburi la Alfred ambalo juu yake kulikuwa na msalaba ulioandikwa jina lake kamili, tarehe ya kuzaliwa na tarehe ya kufa kwake.

Akaniambia niwe makini kwa kila atakachokuwa anakifanya, nikatingisha kichwa huku hofu kubwa ikiwa imetanda ndani ya moyo wangu kwani kiukweli nilikuwa nikiogopa sana makaburi na maiti.

Je, nini kitafuatia?
Subscribed
 
Sehemu ya kumi na Moja ---11



ILIPOISHIA:

Bado sikuwa na majibu na hakukuwa na mtu yeyote wa kunijibu zaidi ya baba mwenyewe. Jambo kubwa ambalo lilikuwa likijirudia ndani ya kichwa changu, lilikuwa ni je, kweli baba ni mchawi?

“Unasemaje?” nilisikia sauti ya baba akiniuliza kwa ukali, nikageuka huku na kule lakini baba hakuwepo.

SASA ENDELEA…

“Sijaongea kitu,” nilijibu, nikasikia baba akiachia msonyo mrefu kisha ukimya ukatawala. Kumbe nilipotamka lile neno ‘sijaongea kitu’, niliongea kwa sauti kubwa kiasi cha kuwafanya abiria wengi ndani ya basi, wanisikie.

“Kaka, unaongea na nani?” sauti ya msichana aliyekuwa akicheka kwa sauti ilisikika, ikifuatiwa na abiria wengine, ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo. Nikashtuka na kukaa vizuri kwenye siti yangu.

“Anaogopa ajali huyo,” alipaza sauti abiria mwingine, watu karibu wote kwenye basi wakacheka. Nilimgeukia mama, nikamuona yeye yupo siriasi tofauti na abiria wengine, nikageuka na kukaa vizuri kwenye siti yangu.

Yule msichana aliyekuwa amekaa siti ya upande wa pili na pale nilipokuwa nimekaa, alivua ‘headphones’ zake, akawa anaendelea kunitazama huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.

Tangu tunaanza safari wala sikuwa najua kwamba kuna mtu kama yeye ndani ya gari, ni mpaka pale alianza kunicheka ndipo nilipoanza kumtilia maanani. Alikuwa ni msichana mdogo lakini wa kisasa, akiwa na simu ya kisasa mkononi, halafu akiwa amevalia mavazi kama wasichana wa mjini ambao nilizoea kuwaona kwenye TV.

Nilipoendelea kumtazama kwa macho ya kuibia, niligundua kwamba alikuwa na sura nzuri sana halafu akitabasamu kuna vishimo kwenye mashavu yake vinajitokeza, nikajikuta navutiwa kumtazama.

Safari iliendelea lakini mara kwa mara yule msichana alikuwa akinigeukia na kunitazama, tofauti na mara ya kwanza ambapo alikuwa kama anacheka kwa kunidharau, safari hii alikuwa akinitazama kwa makini.

Katika ujanja wangu wote niliokuwa nikiuonesha kijijini kwetu, makongorosi, Chunya, hakuna kitu nilichokuwa nakiogopa kama kuzungumza au kujichanganya kwa namna yoyote na wasichana, hasa wa rika langu.

Tangu naanza kupevuka, mpaka namaliza shule ya msingi na hata baada ya kuanza maisha ya mtaani, sikuwahi kuwa na mazoea na msichana yeyote, zaidi ya dada zangu kwa hiyo kitendo cha msichana huyo kuwa ananitazama mara kwa mara, tena msichana mwenyewe mrembo kwelikweli, kilinikosesha mno utulivu.

Kuna wakati nilikuwa natamani hata nirudi kule kwenye siti yangu ya mwanzo, nilikokuwa nimekaa namama na ndugu zangu lakini nilipofikiria kuhusu kazi nzito niliyopewa na baba, ilibidi nijikaze kiume.

Nilipoona anazidi kunitazama, kuna wakati nilifumba macho na kujifanya nimelala lakini nikasikia ile sauti ya ajabu ya baba ikinijia, akaniambia sitakiwi kulala kwa sababu nina jukumu la kuhakikisha safari inakuwa salama.

Nikawa sina cha kufanya zaidi ya kujikaza kiume, safari hii na mimi niliamua kuwa namtazama. Kama kawaida yake, alinigeukia, akawa ananitazama kwa makini, ikabidi na mimi nimgeukie, tukawa tunatazamana. Cha ajabu, alipoona na mimi namtazama japo kwa uso uliojawa na aibu, aliachia tabasamu pana.

Nikajikuta na mimi nikitabasamu, haraka nikakwepesha macho yangu na kugeukia upande wa dirishani, nikawa natazama nje. Safari iliendelea huku nikiendelea kujishtukia, baadaye nilipomgeukia tena yule msichana, niligundua kwamba tayari alishalala huku headphones zake zikiwa masikioni.

Nikashusha pumzi ndefu kama mtu aliyetua mzigo mzito kichwani, nikakaa vizuri kwenye siti yangu na kuendelea nakazi niliyopewa na baba. Kwa bahati nzuri, safari hii hakukuwa na kipingamizi chochote, safari ikaendelea mpaka tulipofika sehemu maarufu iitwayo Chalinze Choma Nyama.

Dereva alipunguza mwendo na kusimamisha basi, akatutangazia abiria kwamba anatoa dakika kumi tukachimbe tena dawa na kujinyoosha. Bila kupoteza muda, abiria walianza kuteremka, mimi nikageuka na kutazama pale mama na wale ndugu zangu walipokuwa wamekaa, nikawaona nao wakiinuka.

Ilibidi nisubiri abiria wengine wapite, ndugu zangu walipokaribia, niliinuka na kuungana nao, tukawa tunataniana na kaka na dada zangu kama kawaida yetu tunapokutana. Cha ajabu, eti nao walikuwa wakinicheka kwamba woga wa kupata ajali ulisbabisha niwatie aibu kwa kupayuka kwenye basi.

Wakawa wananicheka na kunisukumasukuma, jambo ambalo sikupendezewa nalo. Tuliposhuka chini, waliendelea kunitania lakini kwa kuwa sikuwa naupenda utani wao, niliamua kujitenga nao, nikazunguka mpaka nyuma ya gari, nikasimama nikiegamia basi huku nikitazama kule tulikotokea, uso wangu ukiwa umekosa amani.

*(Usikose kutembelea Simulizi za Majonzi)

“Hawa washenzi wangejua mimi na baba ndiyo tuliowalinda wasipate ajali wasingekuwa wananicheka hivi,” nilisema huku nikikumbuka pia vicheko vya abiria wengine ndani ya basi, muda ule nilipopayuka kwa nguvu ndani ya basi.

Mawazo yangu yalizama kwenye hisia chungu, nikawa naendelea kuwaza mambo mengi ndani ya kichwa changu. Ghafla nilishtushwa na sauti ya kike pembeni yangu.

“Mambo!”

“Safi tu,” nilijibu huku nikianza kujichekesha, aibu zikiwa zimenijaa baada ya kugundua kuwa ni yule msichana wa kwenye basi aliyekuwa akinitazama sana.

“Mbona umekaa peke yako huku halafu unaonekana kama una mawazo sana?”

“Ahh! Kawaida tu, nahisi uchovu wa safari,” nilimjibu, huku lafudhi ya kijijini ikishindwa kujificha kwenye mazungumzo yangu. Aliendelea kunipigisha stori za hapa na pale, akionesha kuchangamka mno utafikiri tunafahamiana.

“Nisindikize kule upande wa pili nikanunue soda za kopo, naona huku hakuna,” alisema msichana huyo ambaye manukato yake mazuri aliyojipulizia, yalizifurahisha mno pua zangu.

Tulisimama pembeni ya barabara, akageuka huku na kule kuangalia kama hakuna gari linalokuja, na mimi nikawa namfuatisha kwa sababu sikuwa mzoefu sana wa barabara ya lami na sikuwa najua vizuri namna ya kuvuka barabara. Alipohakikisha kwamba hakuna gari, alinishika mkono, nadhani aliniona jinsi nilivyokuwa na hofu moyoni, tukaanza kuvuka.

Mikono yake ilikuwa laini mno kiasi kwamba nilifurahia jinsialivyonishika. Kwa mara ya kwanza maishani mwangu, nikaanza kuhisi hali isiyo ya kawaida. Tulivuka mpaka ng’ambo ya pili, akafungua pochi yake ndogo na kutoa noti ya shilingi elfu kumi, akampa muuzaji wa vinywaji aliyekuwa na kibanda chake pembeni ya barabara.

“Unakunywa soda gani?” aliniuliza huku yeye akichukua soda yake, nikakosa cha kujibu zaidi ya kuanza kuchekacheka tu.

“Nakuchagulia, nataka unywe ninayokunywa mimi,” alisema huku akinigeukia, akanipa soda ya Sprite ya kopo, akafungua ya kwake na kuingiza mrija, mimi nikawa nashangaashangaa kwa sababu sikuwahi kunywa soda ya kopo hata mara moja wala sikuwahi kutumia mrija.

Akiwa ameshapiga funda moja, alichukua lile kopo la soda mikononimwangu, anaipa ile ambayo alishaifungua na kunywa kidogo, nikawa namshangaa kwani hayo yalikuwa mambo mageni kabisa kwangu, nilizoea kuyaona kwenye video.

Alifungua na ile nyingine, nayo akapiga funda moja, nikawa sina cha kufanya zaidi ya kuendelea kunywa, akawa ananitazama kwa macho yaliyobeba ujumbe mzito.

“Unaitwa nani?”

“Togo,” nilimjibu kwa kifupi, akageuka kama anayetazama upande wa pili wa barabara, nikapata fursa ya kulisanifu vizuri umbo lake. Alikuwa ni msichana mzuri sana, upande wa nyuma alikuwa amejazia huku kiuno chake kikiwa kimegawanyika, kama nyigu ambao kule kijijini tulikuwa tukiwaogopa kutokana na sumu yao wanapokung’ata.

Suruali ya jeans aliyovaa, ililifanya umbo lake lijichonge vizuri, ghafla akageuka, akanibamba nikiwa namtazama kwa nyuma, nikazidi kujisikia aibu.

Je, nini kitafuatia?
 
Hakuna mganga anaekufa kifo cha amani. Wote vya utata. Mganga yupo kwenye vita na mashambulizi mda wote wa maisha yake. Anawindwa na waganga wenzake, wachawi, Wana maombi, karma,laana ya marehemu aliowaua kichawi,pia shetani mwenyewe akikosea masharti. Thus huwezi kuta mganga mwenye nuru.
 
Hakuna mganga anaekufa kifo cha amani. Wote vya utata. Mganga yupo kwenye vita na mashambulizi mda wote wa maisha yake. Anawindwa na waganga wenzake, wachawi, Wana maombi, shetani mwenyewe akikosea masharti. Thus huwezi kuta mganga mwenye nuru.
Uchawi hauna faida🤝
 
Hakuna mganga anaekufa kifo cha amani. Wote vya utata. Mganga yupo kwenye vita na mashambulizi mda wote wa maisha yake. Anawindwa na waganga wenzake, wachawi, Wana maombi, karma,laana ya marehemu aliowaua kichawi,pia shetani mwenyewe akikosea masharti. Thus huwezi kuta mganga mwenye nuru.
Sure
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom