SEHEMU YA 44
“Ila Jackson. Siku kama kuna lolote litatokea, mwambie Catherine nina akili na ndiyo maana ninafanya hivi,” alisema Gosling.
“Akili? Kivipi?”
“Wewe mwambie hivyo tu!” alisema Gosling.
Ishu ya talaka ilikuwa ni ya siri kubwa, aliwashirikisha marafiki zake wa karibu na wote kumwambia alitakiwa kufanya kile alichokifanya lakini kitu cha ajabu kabisa, Maggie akaambiwa na mmoja wa marafiki hao mpango mkubwa aliokuwanao mume wake.
Alichanganyikiwa, alikasirika kwa kuona kama asingefanya jitihada za kummaliza mwanaume huyo mapema basi asingepata mali zote hizo, hivyo alichokifanya ni kuanza kupanga mipango ya kummaliza.
Kundi ambalo lilitakiwa kufanya kazi hiyo ni lile la Brothers! Walichotakiwa kufanya ni kutengeneza ajali ya gari, baada ya hapo walilipue gari hilo na kuondoka zao.
Jinsi ya kumpata mume wake halikuwa tatizo, alijua ni kwa jinsi gani jambo hilo lingefanyika kwani alihisi kulikuwa na ufundi mkubwa ambao haujawahi kufanyika duniani kote.
Alichokuwa akikihesabu ni siku tu, vijana hao wakajipanga tayari kwa kutekeleza mpango wao wa kumuua Gosling. Baada ya siku tatu wakampigia simu Maggie na kumwambia mipango yote ilikuwa tayari hivyo walichotakiwa ni kumuua haraka iwezekanavyo.
“Nashukuru sana! Ngoja nifanye mipango yangu pia,” alisema mwanamke huyo na kukata simu huku uso wake ukiwa na tabasamu pana, aliamini piga ua ilikuwa ni lazima kummaliza mwanaume huyo kisha kumiliki mali zote za mumewe na utajiri aliokuwanao.
.
.
Je, nini kitaendelea?