TEMBELE LA UWANI
SEHEMU YA SITINI NA SABA
MTUNZI
Mbogo EDGAR
ILIPO ISHIA SEHEMU YA SITINI NA SITA: Sina alipo lifikia gari tu! ghafla mlango wa gari ukafunguliwa, na hapo hapo akashangaa kumuona mwanamke alievalia niqab usoni mwake na kubakiza macho, lakini licha ya hayo lakini Sina aliweza kumkumbuka mschana huyu kuwa, ni yule ambae alishirikiana na Idd kumuwekea dawa za kulevya kwenye Juice ili akabakwe na bahati nzuri alikimbia, Sina mengi aligeuka haraka kutazama alikotoka… ENDELEA NAYO……..
Nakutaka kukimbia, lakini Soraya akawahi kutoa tahadhari, “weeeeee! ukinyanyua mguu mmoja tu nakupigia kelele za mwizi watu wakupigeee mpaka ufe” alisema Soraya, na hapo Sinamengi alie jiona anamikosi akageuka alikokuwa Soraya, “dada yangu kwa kweli mimi nilipewa tu ile juice niitunze halafu nikuletee mezani, ukweli si husiki na mpango wake mwingine, naomba unisamehe dada yangu” alisema Sina mengi kwa sauti ya kuomboleza, huku anakusanya mikono yake kifuani, “muongo wewe ndie ulieitia dawa ile juice, kwanini ulifanya hivyo?” aliuliza Soraya kwa sauti ya ukali, “hapana dada yangu, naomba unielewe, mimi nilipewa ikiwa tayari imesha wekwa dawa, kwasababu sikuifungua niliitunza vile vile mpaka mlipokuja” alijibu Sina kwa sauti iliyojaa uoga, “kwani huyu ndie alie wapa juice yenye dawa siku ile?” aliuliza Laylah, huku anamtazama Sina kwa macho ya mshangao, “ndiyo yaani huyu leo nitampeleka polisi bora anieleze ukweli” alisema Soraya kisha akamgeukia Sinamengi, “nani aliekupa hiyo Juice na alikuwa anataka nini?” aliuliza Soraya kwa sauti ya ukali, japo ilimezwa kwa unyororo wake, “alinipa yule kaka uliekuja nae, alisema ukinywa na kulewa aku.. aku ingilie” alisema Sinamengi kwa sauti iliyotawaliwa na uoga huku akimtazama Soraya kwa macho ya wasi wasi.
Soraya na Laylah, wakatazamana kwa macho ya mshangao kabla Laylah hajamtazama Sinamengi, “kwahiyo unataka kusema kuwa Idd alikupatia Juice uitunze kisha umpe huyu?” aliuliza Laylah kwa sauti ambayo ilionyesha mshangao Sinamengi akaitikia kwa kichwa, “we muongo, hata kama Idd anahusika lakini wewe ndie uliweka dawa, mbona sikumuona akiwa ameibeba ile juice na tulipoagiza wewe ndie ulikuja nae ukitokea kule ndani?” aliuliza Soraya akimkazia macho Sinamengi, “ni kweli dada yangu yule kaka ndie alienipatia ile juice” alisema Sinamengi na kuanza kueleza jinsi ilivyokuwa, na hata baada ya kugunduwa kuwa Soraya amekimbia na wao kuamua kupeana wenyewe na pasipo kumficha chochote, Sinamengi alieleza kila kitu walicho kifanya usiku wa siku ile, “tena licha ya kunifanya kote huko akunipa hata hela ya sabuni na meno yangu akayavunja, yani hapa natoka Hospital kuuulizia mengine wamesema nitoe elfu kumi na tano” alimaliza kueleza Sinamengi, huku Soraya na Laylah wakitazamana kwa mshangao na mastaajabiko makubwa, huku wakitafakari juu ya simulizi ya kutisha ya Idd, “kumbe Idd ni mshenzi kiasi hiki, kwahiyo alitaka anibake sivyo?” aliuliza Soraya, huku akimtazama tena Sinamengi ambae aliitikia kwa kichwa.
Naam baada ya hapo kikapita kimya kifupi, ni kama walikuwa wanaendelea kutafakari kabla Soraya hajainuwa uso wake akionyesha amepata jibu, “Laylah, nimekumbuka unajuwa mida hii baba yupo kwa wazee wa baraza sivyo?” aliuliza Soraya huku anatazama muda kwenye simu yake, “ndiyo mama si alisema itakuwa saa saba” alisema Laylah, na hapo Soraya akamtazama Sinamengi, “sikia wewe mama, nimeona nikuachie nisikupeleke polisi, lakini kuna kitu nataka ukifanye kabla hatuja kuachia, tena ukifanya kama tutavyo kuambia sisi na hela ya kutengeneza meno mapya utaipata” alisema Soraya, na Sina mengi akakubari kwa kichwa, hapo Soraya akaanza kumpa maelekezo kamili.********
Naam mama Higgno alifanikiwa kuingia kwenye ward aliyolazwa mzee Komba, ukweli hali aliyoikuta mama Higgno kwa mzee Komba ilikuwa ina sikitisha kwa kweli, japo alikuwa ameshaanza kuongea lakini hakuwa na uwezo wa kuinuka toka kitandani, na alikuwa anatumia mguu mmoja tu! mmoja ulikosa nguvu, yeye alikuwa anasema kuwa nauona kwa macho tu, lakini akuwa anauhisi, kama bado hupo mwilini mwake, hivyo hivyo kwa mkono wake wakushoto, Hivyo basi mzee Komba alikuwa ana jimalizia haja zote pale pale,
akiwa ameachiwa ndoo kwaajili ya kazi hiyo, ukweli ili huzunisha sana, hata alipomuona mama Higgno, alitamani kuangua machozi, “mama Higgy, mwenzio ameniacha hapa Asubuhi mpaka sasa hajarudi” alilalamika mzee huyu aliekuwa anahitaji muangalizi wa karibu akiwa amesahau kuwa chanzo cha yote haya ni kutaka kuichawia familia hii inayo msaidia, baada yake ameichawia familia yake mwenyewe na kusababisha mke na mwanae walale na mtu mmoja, tena kibabu kichawi kweli kweli, ambacho hata yeye mwenyewe alikiogopa.
Na kutokana na muda mchache aliobahatika kumuona mgonjwa, akitakiwa kutoka saa saba kamili mama Higgno alifanikiwa kukutana na Nurse mmoja ambae ni mama mtu mzima mkazi wa kule kule Luhilah lakini ni upande wa pili wa barabara na kumuomba ajitahidi kutumia muda wake kumpatia huduma nzuri jirani yao huyo, huku akimuachia kiasi cha fedha ambacho kingekuwa ni chachu ya mama yule Nurse kufanya kile alicho ombwa na mama Higgno, huku wakipanga kutafuta utaratibu wa kumuweka mzee huyu karibu na watu watakao msaidia, maana waliona kama atakuwa mbali na nyumbani basi atapata tabu sana, kwasababu hakukuwa na dalili ya mke wake kuja kumsaidia, na bahati nzuri ni kwamba, walikuwa wanamfahamu mama Hilda kwa ulevi wa ulanzi, ukiachilia binti yake ambae anatabia chafu zaidi, ambayo imempatia jina la TEMBELE LA UWANI
Alipotoka hapo mama Higgno alianza kuelekea mjini kati huku akiwasiliana na mume wake, ili ajuwe yupo wapi kwa muda ule.*******
Naam saa saba na nusu ndani ya ukumbi wa baraza wa msikiti wa mkoa uliojaa watu kibao kama thelathini na nne hivi, tayari kikao kilishaanza na bwana Mahamud kusomewa shitaka lake na mwenyekiti akimtaka atoe ufafanuzi wa jambo hilo, “kwanza kabisa ni waombe msamaha kwa usumbufu uliojitokeza kiasi cha kuacha kazi zenu na kukusanyika hapa” aliongea Mahamud, ukiwa ndiyo mwanzo wa kuanza kutoa maelezo yake kama alivyo elezwa na mwenyekiti wa baraza.
Wazee na wajumbe waliopo mule ndani wote walimtazama kwa umakini wakiwa wametega masikio yao kusikiliza maelezo yake, Idd pia alikuwa mmoja wao, akiwa amekaa mita chache toka kwa baba yake, huku wote wawili wakiwa wanasubiri kwa hamu kusikia akishinikizwa kumuozesha binti yake kwa Idd, “lakini ningeomba niwaeleze kuwa habari hizo si za kweli na nina uhakika alievumisha uzushi huo ana nia mbaya na mimi pamoja na familia yangu” alisema Mahamud kwa sauti ambayo iliyoonyesha kabisa kuwa anachosema kinatoka moyoni mwake, “kivipi bwana Mahamud, inawezekana kweli mtu aamue tu kukuzushia jambo kubwa kama hili?” aliuliza mjumbe mmoja huku mwingine akidakia, “yaani ni aibu sana kwa sisi sote hapa mkoani, inaonekana tunafahamu swala hili na tunalifumbia macho” na hapo Mahadhi akapata nafasi ya kuchomekea la kwake ili kuvuruga maelezo ya Mahamud, “kinacho niuma mimi ni kitendo cha Mahamud kukubali nilite posa ya kijana wangu halafu yeye anatengeneza mazingira ya kukataa na kumsingizia mwanangu mambo chungu mzima, sijui hooo! alimuwekea dawa kwenye kinywaji…” hapo mwenyekiti akaingilia kati, “jamani hapa sio sokoni, mimi ndie niliewaita kuja kumsikiliza mwenzetu, sasa hizo hoja nyingine zinatoka wapi, hebu tumsikilize kwanza” alisema mwenyekiti na hapo watu wote wakatulia, huku Mahadhi na mwanae Idd wakikonyezana kwa kuona kuwa ni mwanzo mzuri kwao.
Baada ya watu kutulia ndipo mwenyekiti akamtaka Mahamud aendelee kuongea, “hizo tuhuma si za kweli na zime nihuzunisha sana mimi pamoja na familia yangu na ndugu wa karibu, nadhani kwa wale ambao wapo hapa Songea muda mrefu kama mwenyekiti wanaweza kukubaliana na mimi kuwa nimeanza biashara zangu miaka mingi iliyopita kabla sijaoa na kumpata mtoto, yani huyo binti yangu na bado biashara zangu zilikuwepo, sijawahi kwenda kwa mganga wala mtu wa kisomo kwaajili ya kuomba utajiri wala pesa, hizi mali na biashara ni za miaka na miaka hata mimi nimezikuta toka kwa mama yangu, ambae alipewa na marahemu baba yangu bwana Abdulkarim, na pia ningependa niwafahamishe kuwa katika watoto wa Abdulkarim mimi pekee ndie mwenye fedha ndogo kabisa, kwa kifupi hizi ni fedha halali, ambazo zinapatikana kwa biashara halali kabisa, na huyo alieandika upuuzi huo hakika hanifahamu vizuri, maana kama angekuwa ananifahamu asinge andika uongo wa kipuuzi kama huo” alisema Mahamud kwa sauti iliyojaa machungu na msisitizo, hapo watu wakatazamana kwa macho ya viulizo, “sisi tutaamini vipi, na kwanini mtu aandike vile kwa kukusingizia” aliuliza mmoja wa wajumbe na mwenyekiti akamtaka Mahamud ajibu swali hilo, “kwa kweli mimi binafsi sijajuwa kwanini amefanya hivi, ila naamini sina adui hata mmoja, hata huyo aliefanya hivyo naamini sio adui yangu, ila kuna kitu anahitaji toka kwangu” alisema Mahamud kwa sauti iliyojaa uhakika, Mahadhi akatazama chini, huku anakisemea moyoni, “hooo! hapa bila kushidilia misumari, anaweza kupangua kesi” ndivyo alivyo jisema Mahadhi, “ndio tunataka kujuwa kama kweli ni shutuma hizo ni za uongo basi tuambie kwanini amefanya hivyo na anataka nini kwako?” alisema mwingine, kwa sauti iliyojaa shauku na jazba akionyesha kuwa anaamini kuwa Mahamud alikuwa anajitetea bure, “kwa upande wangu nimesha sema mtu huyo sijui anataka nini, ila nina uhakika kama atajitokeza na kuliongea hadharani sio mimi tu, hata nyie mtafahamu kuwa anahitaji nini?” alisema Mahamud na hapo akautekenya kwa mara ya pili moyo wa Mahadhi, safari hii hata kijana wake alitekenyeka.
Mahadhi akaona kama asipotia neno basi atapotezeza karata yake kwa mara nyingine, hapo akakurupuka ghafla, “lakini lazima huyo atakuwa ni mtu wako wa karibu, hawezi kutoka mbali, mimi kinachoniuma ni kitendo cha kumchafua kijana wangu na kumsingizia kuwa alikuwa anakunywa pombe na pia alimuwekea binti yako dawa, wakati wewe mwenyewe umeyapanga hayo ili kumzuia binti yako asiolewe” alisema Mahadhi akionyesha jazba ya hali ya juu, na mwingine akadakia, “na kama hizo habari ni za uongo kwanini basi utumie ujanja kumzuia binti yako asiolewe?” alikuwa ni mmoja kati ya wale jamaa wawili waliobebwa kwenye gari la Mahadhi siku ile, “ni kweli kabisa jamani, hata kama ni uongo lisemwalo, sasa kwanini bwana Mahamud unatumia mbinu mbali mbali kumzuia binti yako asiolewe, mfano siku ile ukasingizia binti yako ametekwa na mpaka leo hatujaona juhudi zozote za kuwasaka watekaji, haya tuyaache hayo na vipi binti alipopatikana, anakuja kusema kuwa ana mchumba, kweli si kutufanya sisi kuwa ni wa jinga, hapo unadhani utaeleweka vipi kama ukisema kuwa haya yaliyo andikwa kwenye messeji ni ya uongo?” alisema mwingine na hapo Mahamud akainamisha kichwa chini akitafakari ajibu nini, kwasababu aliekuwa anamuhisi kwa asilimia mia moja ndie anaechochea maneno.
Na kabla hajajibu kitu tayari mwingine alisha dakia, “hata kama wanamsingizia hapa kuna jambo moja tu la kufanya ili kujisafisha yeye na sisi kama wazee wa baraza, nalo ni kuhakikisha binti yake anachumbiwa haraka iwezekanavyo” alisema mmoja wa wajumbe wa baraza na hapo kila mmoja akaunga mkono swala hilo huku Mahadhi na kijana wake Idd wakitabasamia chini, huku minong’ono ya kuunga mkono swala lile ikiendelea chini kwa chini, “haya jamani, hebu tukae kimya kwanza tumsikie Mahamud mwenye, tujuwe anasemaje juu ya hilo, maana niwazi kuwa kuolewa kwa binti yake ndio kutaondoa hii kashfa” alisema mwenyekiti kwa sauti ya kuwa nyamazisha wengine, hapo ukapita ukimya mkubwa huku watu wote wakimtazama Mahamud na kusubiri kwa hamu jibu lake, “ndugu zangu, jambo la kuolewa kwa binti yangu hilo ni jambo la kheri na siwezi kukataa hata kidogo” alisema Mahmud na hapo Mahadhi akaachia tabasamu pana huku anamtazama Idd, ambae pia alikuwa ameachia tabasamu pana kama la baba yake kama walivyo fanya wengine pia, ambao walifurahi kusikia vile, “tuna shukuru sana kusikia hivyo bwana Mahamud, kwahiyo taratibu zianze lini?” aliuliza Mwenyekiti kwa sauti ambayo ilionyesha wazi kujawa na furaha.
Naam Mahadhi na kijana wake ni mmoja mwawatu waliotulia kwa umakini huku mioyo yao ikichanua kwa matabasamu ya matumaini, wakiamini kuwa tayari wameshapata walichokuwa wanakitafuta, “mwenyeketi juu ya taratibu hayo ni mambo ya kifamilia, hasa huyo kijana anaemchumbia binti yangu ndie mwenye kujuwa lini ataleta barua na baada ya hapo tegemeni mualiko wa kuja kwenye harusi ya binti yangu” Mahamud aliongea hayo akiwa anatabasamu, hata mimi sijui kwanini aliamua kusema hivyo, lakini kwa hisia naweza kusema hakuhitaji binti yake aolewe na kijana Idd, ambae amesha zisikia sifa zake mbovu, Idd na baba yake waliduwaa kwa mshangao, mioyo yao ikaingia ganzi kwa mshtuko mkubwa walioupata, hawakuamini masikio yao.*********
Naam mita chache toka msikiti wa mkoa lilonekana gari aina ya Land Rover discovery, likiwa limeegeshwa sehemu na bila kushuka mtu, ingekuwa vigumu kwa mpita njia kuona ndani ya gari hilo lenye vioo vyeusi vya tinted vilivyopandishwa mpaka juu kuwa kulikuwa na waschana wawili, yaani Soraya na Laylah waliokuwa wanatazama msikitini wakimtazama mwanamke ambae anafahamika kwa jina la Sina, muhudumu maarufu pale mjini Songea aliekuwa amesimama karibu kabisa na msikiti akitazama kwenye mlango wa ukumbi wa baraza la wazee, akionyesha kuwa alikuwa anamsubiri mtu fulani, “yaani Laylah nimemmissi Higgno” alisema Soraya huku anatafuta simu yake na kusaka namba za Higgno, “mnapendana wenyewe mpaka raha” alisema Laylah huku wakiendelea kutazama kule msikitini, na huyu mshenzi Idd leo lazima aipate fresh” alisema Soraya huku anapiga namba zile na kuweka simu sikioni, nayo ikaanza kuita, “nampenda kweli halafu usimwone mpole vile ana maneno yule” alisema Soraya huku anacheka cheka na wakati huo huo simu ikapokelewa.******
Naam tayari mzee Frank alikuwa amesha fanya karibu robo tatu ya manunuzi ya vitu vya dukani kwake, ni mara mbili ya vile vya duka la mwanzo, na wakati anadelea kumalizia manunuzi ndipo aliposikia simu yake ikiita toka mfukoni kwake, alipotoa mfukoni na kuitazama ili kuwa ni namba ya Higgno, kwanza akajicheka kidogo huku anapokea simu nakuiweka sikioni, “yaani nilisha kusahau kabisa, vipi upo wapi sasa” aliuliza mzee Frank, huku kicheko kikiendelea, “mimi nipo mjini muda mrefu niliishiwa vocha ndio nimeweka sasa hivi, kwani wewe umesha kuja mjini” aliuliza Higgno kwa sauti ya furaha pia, nadhani ni furaha ya kuongea na mzee Mahamud, “nimekuja zamani sana, karibu namaliza manunuzi, wewe upo wapi?” aliuliza Frank ambae alikuwa anatazama wapakiaji wa mizigo waliokuwa wanapakiza mizigo kweny gari alilolikodi, “nipo karibu na soko kuu, wewe upo wapi?” aliuliza Higgno akionyesha kuwa mwenye shauku ya kukutana na baba yake, “njoo kwenye maduka ya wahindi hapa chini nipo kwenye duka la tatu toka upande wa sokoni” alielekeza mzee Frank, na simu ikakatwa na yeye akaiweka simu na kuendelea kuangalia mizigo iliyokuwa inapakizwa, lakini kabla hajakaa sawa akasikia tena simu yake inaita, “mh! huyu nae na hicho kisimu chake kipya” alisema mzee Frank huku anatoa simu mfukoni na kuipokea kisha akaiweka sikioni, “vipi umeshafika mbona sikioni?” aliuliza Frank, huku macho yake yakiwa busy na wachukuzi wasije wakaiba mzigo hata mmoja, “nimeshafika wapi, wakati sasa ndio natoka hapa Hosptal?” hapo ndipo Frank alipokumbuka kuwa alimuacha mke wake pale Hospital akienda kumtazama mzee Komba, “hooooo! kumbe ni wewe nilidhania naongea na Higgno, ok! njoo moja kwa moja kwenye maduka ya wahindi nipo kwenye duka la tatu toka upande wa sokoni” alielekeza mzee Frank huku anajicheka kidogo, sijui alichanganyikiwa na nini, “mh! kwani Higgno ana simu?” aliuliza mama Higgno kwa mshangao, “hivi sikukuambia, Higgno bwana ana simu, sasa anavyojidai utadhania amenunua gari” alisema mzee Frank na wote wawili wakacheka na kukata simu.
Naam ile anaiweka simu mfukoni tu, Higgno nae akaingia, “shikamoo baba” alisalimia Higgno na kuwa kama anamshtua baba yake, ambae hakuwa amemuona kabla, “marahaba, vipi Higgno, ulikuja muda mrefu sana au ndiyo unaingia?” aliuliza mzee Frank huku anamtazama mwanae aliebeba mfuko wa Rambo mkononi, “nimekuja muda mrefu, sema nilikuwa naongea na mzee Mahamud” alisema Higgno na kumfanya baba yake ashangae kidogo, “mzee Mahamud, huyu ninaemfahamu, vipi umeongea nae kuhusu kazi?” aliuliza mzee Frank kwa mshangao wenye furaha ndani yake.
Hapo Higgno akaanza kumsimulia baba yake, jinsi ilivyokuwa na jinsi maongezi yao yalivyo kuwa, “kwahiyo Higgno sasa unarafiki wa kike?” aliuliza mzee Frank kwa mshangao wa furaha, “tena mzuri kweli kweli” alisifia Higgno, “lakini mpaka umkatae mtoto wa mahamud una uhakika kuwa huyo mwanamke mzuri kama yule mtoto wa Mahamud?” aliuliza mzee Frank kwa mshangao, japo alionyesha furaha, “ni mzuri huyo mschana, yaani ukimuona wewe mwenyewe utashangaa, utasema nimemuendea kwa mabudi” alisema Higgno na wote wakacheka, “kwani wewe baba unamfahamu huyo mtoto wa Mahamud?” aliuliza Higgno, “mh! nisikudanganye, kiukweli simfahamu, japo nahisi ni huyu mschana ambae ananisaidia kurudisha duka langu, wanaweza kuwa na undugu nae, kwasababu lile gari nalionaga linatokea kwa Mahamud, halafu na yeye ni mwarabu, vipi wewe ukimuona unamfahamu?” aliuliza mzee Frank, “mh! sijawahi hata kumuona, ila na yule wa kwangu ana gari lake zuri japo sijawahi kulipanda” alisema Higgno wakacheka tena kwa furaha, “ila Higgno najivunia kuwa na mtoto kama wewe, sasa unaniletea heshima, ona sasa kama Mahamud mwenyewe amesema kuwa yupo tayari kuwa mshenga na kukusaidia” waliongea hili nalile mpaka walipo gusia habari za mfadhiri wa baba yake, “vipi huyo mwanamke anae kusaidia ni mzuri sana” aliuliza Higgno, “weeee! sidhani kama kuna mwanamke mwingine unaweza kukutana nae halafu ukamlinganisha na huyo, ni mzuri mpaka kuku wanamshangaa, sema tayari anamchumba wake yupo kule kule Luhila na mimi ndie mshenga wake” alisema Frank akimwaga sifa kama zote bila kujuwa kuwa mke wake ameshafika na yupo nyuma yao anawasikiliza na kufuatilia maongezi yao, “we baba hujamuona mchumba wangu, ni mzuri kinoma, amelala kule shamba sijasikia hata kelele za panya” alisema Higgno ambae hata mimi sikujuwa alikuwa anamaanisha nini, “sasa vurugu za panya na huyu mwanamke wako vinahusiana nini?” aliuliza mzee Frank, akiachia na kicheko huku mke wake akiendelea kuwasikiliza, hakika usingesema kuwa Higgno huyu mwenye sauti ya upole ndie aliekuwa anaongea na baba yake, “waanzaje kufanya fujo wakati muda wote wanamshangaa yeye” kwa kauri hiyo hata mama Higgno aliekuwa nyuma yao akashindwa kujizuia akaangua kicheko cha mwaka kama kile alichoachia mzee Frank, na mwisho wakajikuta wanaongea kwa pamoja, “basi mlete nyumbani tumuone” hapo ndipo mzee Frank alipogundua kuwa mke wake ameshafika, “kwani umekuja muda mrefu hapa” aliuliza mzee Frank huku anageuka kumtazama mke wake kwa macho ya mshangao, kama Higgno ambae alishatoa macho kitambo, “kwani dhambi kusikia habari njema” alisema mama Higgno na kuanza kuwasimulia hali aliyoikuta kule Hospital kwa mzee Komba, na hatua alizo zichukuwa ili kumsaidia mzee Komba, huku muda wote wakisaidiana kununua mahitajio ya duka.
Naam wakiwa wamesha maliza kununua mahitajio na wanaingia kwenye gari, mama yake akiwa amepanda mbele yeye na baba yake wanapanda nyuma, tayari kuondoka, mara Higgno akasikia simu yake inaita, alipotazama mpigaji alikuwa ni Soraya, kwanza akajitabasamia mwenyewe, “huyooo anapiga” alisema Higgnio huku baba yake akianza kutabasamu ni baada ya kuthibitisha kuwa ni kweli mwanae ana mwanamke, “pokea weka loud speeker” alisema mzee Frank huku gari likianza kuondoka, haina loud speeker, alisema Higgno huku anapokea simu, “hallow mambo” alisalimia Higgno kwa sauti tulivu na nzito, “poa Higgy upo wapi?” aliuliza Soraya kwa sauti nyororo yenye dalili ya aibu, “nilikuwa mjini, sasa nipo kwenye gari naelekea nyumbani” alijibu Higgno kwa sauti ile ile nzito ya upole, “hiii jamani Higgy kwanini huku niambia kama upo mjini, si ningekupeleka kwa mama akakuone” alisema Soraya kwa sauti ya manung’uniko huku mzee Frank akifuatilia maongezi kwa ukaribu zaidi, “mh! unipeleke kwenu kabla hatuja fanya taratibu zozote?” aliuliza Higgno kwa mshangao, “sasa wasi wasi wa nini wewe si mchumba wangu?” aliuliza Soraya, “lakini ninge kuambiaje kama nipo mjini wakati wewe ulisema ukichukuwa simu utanipigia?” aliuliza Higgno kwa sauti ile ile kama kawaida yake, “basi tuyaache hayo, mwenzio paliendelea kuuma yaani sasa hivi ndio panaanza kupoa, nitakuja baadae unipepee kama jana usiku” alisema Soraya kwa sauti nyororo akimalizia na kicheko, “hoo! halafu nime kumbuka, nadhani mambo yanaenda vizuri nimesha mpata mshenga” alisema Higgno kwa sauti iliyochangamka, “waoo Higgno kumbe unanipenda kweli umeshatafuta mshenga wakuja kwetu, mbona hata mimi nilishakutafutia wa kule kule kwenu” alisema Soraya akionyesha furaha ya hali ya juu huku gari iliingia barabara kubwa na kuongeza mwendo, “basi hakuna tatizo, ila nikikutajia mshenga wewe mwenyewe utazimia” alisema Higgno lakini nadhani Soraya hakumsikia vizuri, “hallow mbona upepo mkali sana sikusikii” alisema Soraya, “basi tutaongea baadae ukija, anakusalimia baba yangu” alichomeakea Higgno, “msalimie pia, utanipeleka nikawasalimie” alisema Soraya na simu ikakatwa, “sasa nime amini” alisema mzee Frank huku safari inaendela.*******
Ukumbi mzima uliachama kwa mshangao, baada ya kusikia kauli ya Mahamud, maana walitegemea kuwa Idd ndie mlengwa katika kumchumbia Soraya, “unamanisha sio kijana wa Mahadhi?” aliuliza mwenyekiti, “ndio bwana mwenyekiti, tayari binti yangu alishakutana na mwenzie na wakapenda na ndie aliemuona anamfaa, ni kama alivyo sema siku ile ya jumapili, na pale alidhania kuwa ni huyo kijana ndie alieleta barua ya posa” alisema Mahamud kwa kujiamini, japo alikuwa anajuwa kuwa binti yake bado hajakutana na huyo kijana, “na itakuwaje kwa mimi na kijana wangu ambao tumedhalilishwa mbele za watu kwa kumsingizia Idd ni mlevi na amemuwekea dawa Soraya?” aliuliza Mahadhi kwa jazba, hapo watu wakatazamana kidogo hata Mahamud akaduwaa maana hakutegemea kama Mahadhi angepata ujasiri wakuliongea hilo hadharani, “nadhani kama tumejirizisha kuwa Idd alisingiziwa juu ya hilo basi familia ya bwana Mahamud haina budi kumuomba radhi Idd na wazazi wake” alisema mwenyekiti na wajumbe wengine wakaunga mkono kwa kuitikia kwa vichwa wakikubaliana na mwenyekiti, “hapana radhi itasaidia nini kwa heshima ambayo tume potezewa, kama kweli atahitaji msamaha basi hana budi kukubali Idd amuoe Soraya na hapo hakuna cha kusema kuwa anamchumba wala nini, ni mbinu nyingine ya kuzuia binti yake asiolewe” hiyo ilikuwa kauli ya Mahadhi ambayo aliitoa kwa sauti iliyojaa pingamizi na msimamo, hapo wajumbe wote wakatazamana kwa mshangao, na maswali ya sinto fahamu, mwenyekiti aliona kweli hii ilikuwa ni ngoma nzito, lakini Mwenyekiti huyo alipomtazama Mahamud akashangaa kumuona anatabasamu, “bwana Mahadhi nadhani unashindwa kuelewa kuwa huyu kijana wako ni mtu wa aina gani, au pengine unafahamu lakini una wapumbaza wajumbe wa baraza ili wakuunge mkono kwa kile unachokifanya, nadhani hata wao wangemfahamu wasinge jiuliza ile messeji imetokea wapi, sasa basi nakupa nafasi ya kukataa ukweli huo wa kuwa kijana wako alijaribu kumuwekea dawa binti yangu kwenye juice ili atimize malengo, na ukifanikiwa kujisafisha kuwa sio kweli, nitamuozesha binti yangu kwa mahali ndogo sana, kwasababu ni sheria, lakini basi kama itatokea iwe leo kesho au mwakani, nikagundua kuwa muna husika juu ya mpango huu wa messeji, basi hakika sitohitaji mtu yoyote kuja kuzuia kile nitakacho kifanya kwako na kwa kijana wako, hakika mtaozea jela” alisema Mahamud, na hapo watu wote wakamtazama Mahadhi ambae alikuwa anakwepesha macho huku anasonya sonya kwa hasira, hapo Idd ndiyo hakuweza kukaa kabisa, akatoka ukumbini kwa hasira, “nadhani kikao kimelenga kunidhalilisha zaidi” alisema Mahadhi ambae pia aliinuka na kuanza kutoka nje.
Lakini kabla mzee Mahadhi hajaufikia mlango, mara wakamuona Idd akirudi ndani kwa haraka nusu amkumbe baba yake pale mlangoni, ikionyesha wazi kuwa Idd alikuwa anakimbia kitu kule nje, na wakati wanashangaa na kujiuliza kulikoni mara wanamuona mwanamke mmoja mtu mzima akiingia pale mlangoni, “weeeee! weeeee! we kaka leo hunikimbii naomba unilipe….” ghafla yule mwanamke alisita na kusimama akionekana kuwa hakutegemea kama angekuta watu wengine pale ndani, “weye unaingiaje humu ndani namna hiyo hebu toka nje weweee” aling’aka mzee Mahadhi huku akimdaka yule mwanamke mtu mzima na kuanza kumsukumia nje……… ITAENDELEA USIKU