Sehemu ya 08
Nilimkubalia ili tu kuiacha siku ile ipite pia kutokana na hali yake, lakini bado sikupata jibu la dada Monika amekufa kweli, japo shemeji alinihakikishia amekufa. Na kama amekufa amezikwa wapi au ndio yaleyale niliyoelezwa kuwa mwili wake umefichwa ndani.
Moyoni nilibakia njia panda kutaka kujua ukweli kuhusu dada Monika, nilipanga kama mama atashindwa kunieleza basi nitamvaa baba na ukali wake ili nijue amekufa au mzima na kama amekufa amezikwa wapi.
Sikutaka kuliulizia jambo lile haraka kutokana na hali ya mama, niliamua kukaa kimya, lakini moyoni sikuwa na raha kutaka kujua ukweli wa kifo cha dada Monika.
Siku moja asubuhi kabla ya kwenda shule mama alinifuata chumbani kwangu na kunieleza nisiende shule kuna sehemu anataka kunituma.
Nilibadilisha nguo zangu za shule na kuvaa za nyumbani, wakati huo alikuwa akijiandaa kwenda shambani. Lakini siku ile hakuwahi kama ilivyokawaida yake.
Tuliondoka nyumbani pamoja kuelekea shamba, baada ya muda wa chai, kutoka nyumbani mpaka shambani ni mwendo wa dakika 45. Tulikwenda huku tukizungumza, mama aliniulizia habari za shule, nilimuelezea maendeleo yangu japo hakuwahi hata siku moja kushika madaftari yangu kuyaangalia.
Katika kumbukumbu zangu nilielezwa kuwa mama aliishia darasa la sita baada ya kupewa ujauzito na baba kisha kumtorosha. Taarifa hizo alinipa marehemu ambaye sina uhakika kama kweli amekufa au maiti yake imefungiwa katika chumba kisichofunguliwa.
Dada Monika alinieleza kuwa mama yetu alitengwa na familia yake baada ya kubebeshwa ujauzito na baba na kutoroshwa. Kitendo kile ndicho kilichofanya mama aishi maisha ya peke yake bila ndugu, ndugu yake mkubwa alikuwa baba kitu kilichofanya baba amnyanyase kwa kujua hana pa kwenda.
Sababu ile ndiyo iliyomfanya mama aishi kama mtumwa kwa vile kila alipofanya kosa baba alimtishia kumfukuza. Kwa kweli kitendo cha baba nilikiona cha kikatili sana, kila dakika nilijikuta nikimchukia baba kwa roho mbaya ya kuitesa familia yake kwa ajili ya mali.
Niliamini mateso ya muda mrefu na shuruba zote, baada ya kupata utajiri wa kushirikina, basi alitakiwa mama atulie na kufaidi matunda ya uchawi wao.
Lakini imekuwa tofauti mama kila kukicha amekuwa mtu wa kusurubika. Kilichonishangaza ni ndugu zangu kushindwa kumsimamia mama, mateso ya kulima kupasua kuni. Kila nilipomtazama mama yangu roho iliniuma na kujiapiza kama Mungu atanisaidia kupata kazi na kuwa na maisha mazuri basi nitamuondoa kwa baba.
Moyoni nilijiapiza kutokukubali kuishi maisha machafu ya ndugu zangu ya kutoa familia zao kwa ajili ya kafara ya hatari na kujiona kama wataishi milele. Nilijiuliza dada Mihayo atamwambia nini mwanaye mbele ya Mungu, aliyemtoa kafara kwa ajili ya utajiri na baadaye kuendelea kuteza kwa kumlaza kwenye chumba.
Kuna kitu alinieleza dada Monika juu ya mama na kuniomba nimchunguze, nakumbuka siku hiyo alinieleza:
“Masalu, mama yetu anaishi maisha ya mateso makubwa sana, baba ni shetani asiyefaa mbele ya jamii. Nataka nikueleze kitu kimoja ambacho mimi wananikataza. Kwa taarifa yako nilikatazwa kulala na mwanaume lakini baba ana mwanamke kamjengea nyumba ya gharofa moja.”
Dada Monika aliendelea kunieleza jinsi watu wanavyotumia pesa huku mama akiteseka, alinieleza:
“Mdogo wangu familia yetu yote tutateketea kwa moto wa kiama, hebu ona maisha ya mama yanalingana na utajiri tulionao, hata kama kuyumba hatuwezi kuishiwa kiasi cha kutisha, sawa na tembo kuugua maralia hawezi kukonda kama mbwa.
“Masalu, sema tu mama mbishi, nilimueleza mapema tuondoke pamoja ili aepukane na maisha ya mateso, lakini mama kama amerogwa na baba haelewi hasikii.
Hivi kweli mama yetu ni wakuvaa kandambili za kufunga na kamba?” Nakumbuka siku hiyo dada Monika alizungumza huku akibubujikwa machozi.
Mama anateseka dada Mihayo anamuhonga bwana wa pembeni gari, Masalu inauma lakini sina uwezo. Kama kidonda hiki angekuwa nacho mtu mwingine na mimi kuwa na uwezo wa dada Mihayo hata kwa kutoa kafara ya mtoto mama yangu angeishi kama malaika.
Lakini sina uwezo, hata hili kidogo ninachokipata nikimpelekea mama hatakitumia zaidi ya kugeuzwa ndondocha na baba.”
Kila nilipoyakumbuka maneno ya dada nilijikuta nikitokwa na machozi. Nilikumbuka neno moja ambalo dada Monika alinieleza nilifanyie kazi, aliniambia:
“Masalu, mchunguze mama muda mwingi akiwa peke yake mkono huwa shavuni, na kama utamfuatilia kwa muda baada ya kutoa mkono shavuni utikisa kichwa na kufuta machozi. Katika maisha yetu toka tupate utajiri wa kishirikina furaha ya mama umetoweka, kutabasamu kumekuwa kama ajali lakini kulia kumekuwa kitu cha kawaida.
Mara nyingi mama amekuwa kila akiwa peke yake kanga huwa mkononi ili kufuta machozi. Vitu vile nilivifanyia kazi na kumueleza dada Monika yote aliyonieleza ni kweli. Aliniuliza swali lingine:
“Masalu umeisha muona mama akivaa nguo mpya?”
“Hapana,” nilimjibu.
“Hebu jifikirie mama yetu ni wa kuvaa nguo zilizoachwa na wanawe?”
“Nilikuwa sijui.”
“Kama hujui, hata macho yako hayaoni, Masalu sasa hivi wewe si mtoto unaona vitu ambavyo baadaye vinataka majibu kwa kile ulichokiona.”
“Huwezi kuamini dada nilikuwa kama nimefungwa akili, unachonieleza sasa hivi ndiyo kama kwangu kunapambazuka baada ya kukaa kizani kwa muda mrefu. Kama usingenieleza haya ningekufa kibudu.”
Niliamini kabisa kama dada Monika kama kweli amekufa, basi alikuwa amekufa na mengi moyoni sawa na samaki mwenye mengi ya kuzungumza lakini kila alipofumbua mdomo maji yalimjaa mdomoni. Kama alivyonieleza shemeji kabla ya kufa kutokana na maelezo yake mengi angenieleza mengi mazito.
Tulipofika shambani mama hakuonesha kama anataka kulima, aliniweka chini ya mti huku akionekana mwingi wa mawazo. Baada ya ukimya mfupi mama aliniita jina langu.
“Masalu”
“Naam mama.”
“Najua umesikia mengi juu ya maisha yetu, lakini hakuna ukweli kwa yote uliyosikia nakuomba uwapuuze, sawa baba.”
“Lakini mama mbona yote niliyoelezwa yana ukweli.”
“Ukweli upo?
”Mama kwanza naanza na wewe, toka nipate akili sijawahi kukuona ukifurahi kila siku mtu wa masikitiko na kutokwa na machozi”
“Ha! Masalu umejuaje?”
“Mama dada Monika kanieleza mambo mengi sana ambayo niliyafanyia kazi na kuupata ukweli juu yako.”
“Ukweli gani?”
“Kuhusu muda mwingi kuweka mkono shavuni na kutokwa na machozi, nilikufuatilia bila wewe kujijua na kuupata ukweli, pia uvaaji wako wa nguo mama toka nipate akili sijakuona akivaa nguo mpya au zilizo nzuri pia mama hebu angalia ndala zako. Kwa maisha tunayoishi wewe si wa kuvaa ndala za kufunga na waya”
Niliposema vile mama alijiangalia kama hakujua alichokivaa wakati wakutoka nyumbani.
“Mama najua yote haya yanatokea kwa ajili ya nini.”
“Kwa ajili gani?”
“Haya ni mateso anayokupa baba, baada ya kutengwa na ndugu yako, na chanzo cha yote ni yeye. Kutokuwa na ukaribu na familia yako, katumia ni fimbo ya kukuadhibia. Hivi mama hata wanao wengine wanajijali wao na kukusahau , bila wewe wangeijuaje dunia?
“Mama maisha haya unayoishi siyo mazuri, nilisikia eti baba alikutishia maisha kama utataka mambo makubwa. Haya ndiyo aliyoyakataa dada Monika kidonda akitunze yeye wengine wale maisha mazuri. Matokeo yake mnaamua kumuua na kuificha maiti yake”
“Masalu nani kaificha maiti ya Monika”
“Ipo wapi?”
“Masalu swali gani hilo , kila anayekufa si uzikwa”
“Mbona mtoto wa dada Mihayo hakuzikwa?”
“Masalu una uhakika gani?”
“Dada Monika hakunificha yote nisemayo ni yeye aliyeniambia ni mengi sana nayajua kuliko mtu mwingine.”
“Masalu yote usemayo ni kweli, nakuomba usimwambie mtu yoyote habari hizi”
“Kama ni kweli naomba kuanzia leo kazi ya kulima aachiwe mtu mwingine, uvae nguo nzuri ili ulingane na utajiri wa familia yetu.”
“Masalu hilo haliwezekani”
“Kwa nini?”
“Baba yako ataniua, naomba mwanangu yote unayoyaona yaache kama yalivyo, na ukizidi kumchokonoa anaweza kukuua”
“Kama alivyomuua dada Monika?”
“Usiseme hivyo Masalu”
“Mama tunafichana nini, hivi utajiri ndiyo unaotufanya tukose huruma kwa wenzetu?”
“Masalu nakuomba usichimbe sana.”
“Hapana mama huwezi kujua sasa hivi tunaonekana vipi mbele ya macho ya watu, kwa taarifa yako inasemekana Monika hajazikwa amewekwa ndani kwa imani za kishirikina”
“Nani kasema?”
“Aliyekuwa akikaa na dada Monika ndiye anayeeneza habari hizi”
“Yeye kajuaje?”
“Mama ina maana ninapozungumza na wewe unakuwa wapi? Nilikueleza kuwa kabla ya kufa dada Monika alimpa siri kubwa ya maisha yetu na sababu ya kifo chake. Pia alimueleza kuwa alikuwa na siri nzito ambayo asingemwambia zaidi yangu mimi.”