SEHEMU YA 36
Huyu alikuwa muuaji aliyekuwa akitabasamu, alihitaji kuniua huku akiachia tabasamu pana usoni mwake. Sikutaka kuonyesha wasiwasi wowote ule, na mimi nikaendelea kutabasamu huku nikionekana kuwa na furaha tele, kumbe ukweli ni kwamba moyo wangu ulichoma kupita kawaida.
Siku hiyo sikulala usiku mzima, nilikuwa nikimfikisia Scaila tu, yale madudu yake yalinichanganya kupita kawaida. Kuna wakati nilimkumbuka sana Shasta, yule msichana japokuwa alikuwa akiolewa lakini niliamini moyoni mwangu kwamba alikuwa mtu pekee aliyeumbwa kwa ajili yangu.
Nilifanya haraka sana kumchukua Scaila, ilikuwa ni lazima nipate muda wa kumchunguza na ndipo nifanye maamuzi ya kuishi naye lakini sikufanya hivyo, nilivua nguo na kutumbukia baharini pasipo kuangalia ni baridi kiasi gani maji hayo yalikuwa.
Mpaka asubuhi inaingia sikumuonyeshea tofauti yoyote ile japokuwa kwa kipindi hicho nilitakiwa kuwa makini sana. Kama kawaida yangu nilimsogelea na kumbusu shavuni, nikainuka kitandani, nikaenda bafuni na kuanza kuoga.
Kwa kweli moyo wangu ulivurugika mno, kuna kipindi nilifikiria kumuacha lakini nikalifuta wazo hilo kwa sababu sikuwa na ushahidi wa kutosha, yaani kama ningemuacha, angeniuliza kwa sababu gani na mimi nisingekuwa na jibu lolote lile.
Nilichokifanya ni kuendelea kuishi naye huku nikihitaji kukusanya ushahidi kwa kiasi kikubwa, siku nikija kumuacha, basi nimuache huku mwenyewe akiona kweli alizingua na alistahili kuachwa.
Wakati nikiendelea kufikiria hayo, nikamkumbuka Hiza. Siku ambayo alikuja nyumbani na Ally na kuwatambulisha kwa Scaila, alionekana kushtuka sana kumuona mahali pale.
Japokuwa nilimuuliza juu ya mshtuko wake lakini alizungumza mambo ambayo hayakuniingia akilini hata kidogo. Nilihisi kulikuwa na kitu fulani hivi alichokuwa akikifahamu ambacho ilikuwa ni lazima na mimi nikifahamu.
Haraka sana nilipomaliza kuoga na kuvaa, nikamkumbatia na kumuaga nakwenda kwenye biashara zangu, akanibusu mfululizo huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.