SEHEMU YA 22
Kwenye kiti kile wakaniweka na kuanza kuniuliza maswali kuhusu yule mzee niliyekuwa nimemuokoa na almasi. Nilichokigundua ni kwamba hawakujua ni mlinzi gani aliyekuwa amemuokoa yule mzee na mbaya zaidi hawakujua ni nani alikuwa na almasi waliyokuwa wakiitaka.
Kila walichoniuliza, niliwaambia kwamba sifahamu chochote kuhusu almasi lakini nilisikia kuhusu mzee huyo kwamba alitakiwa kuuawa.
“Wewe ulikuwa wapi?” aliniuliza.
“Nilikuwa Kimanzichana kwa mama! Nilipewa likizo ya siku saba,” niliwajibu kwa sauti ya chini.
“Kwa hiyo hujui chochote kuhusu almasi?”
“Hapana mkuu! Sijui chochote kile, hata huyo mzee niliambiwa tu,” nilimjibu mwanaume aliyekuwa akiniuliza.
Niliwadanganya, walionekana kuniamini lakini hiyo haikuwa sababu ya kuniacha, waliendelea kunitesa mno, soku hiyo ilikuwa ni ya hatari sana kwangu, muda wote nilikuwa nikilia lakini watu hao hawakutaka kuniacha, waliendelea kunitesa zaidi na zaidi kiasi kwamba mpaka ukafika muda nikahisi kabisa mwili mzima ulikufa ganzi na sikuwa nikiskia maumivu yoyote yale.
Siku hiyo nilitakiwa kuwa humo huku nikisikia maumivu makali mwilini mwangu. Walipanga itakapofika majira ya saa saba usiku waniue na kwenda kuutupa mwili wangu katika soko la Kariakoo kwa ajili ya kuwatisha walinzi wenzangu kama walivyokuwa wamefanya kwa wengine.
Nilitakiwa kupambana, ni kweli nilikuwa mateka lakini nilijua kabisa kwamba endapo ningepambana ningeweza kuchomoka ndani ya chumba hicho.
Humo niliachwa na jamaa mmoja ambaye alionekana kuwa kama mlinzi, yeye ndiye ambaye alitakiwa kuhakikisha nakaa humo, sifanyi kitu chochote mpaka muda wa kuchukuliwa na kuuawa utakapofika.
Nilimwangalia jamaa mwenyewe, kiukweli nilitakiwa kufanya kila liwezekanalo kuhakikisha natoka ndani ya chumba hicho. Sikuwa na nguvu lakini mdomo wangu nilihisi kabisa ulikuwa na nguvu za kuongea, nikamuita kwa kuwa nilihitaji nimshawishi ili twende sawa.
“Bro! Njoo tuongee,” nilimwambia, akanisogelea, alijua sina nguvu kwa kuwa niliteswa sana lakini kupitia mwanaume huyohuyo ilitakiwa nifanye kila liwezekanalo kuhakikisha natoka.
“Unasemaje?” aliniuliza kwa sauti ya kibabe.
Sehemu ya 23
“Unasemaje?” aliniuliza kwa sauti ya kibabe.
“Ninamjua mtu mwenye almasi. Kuna jamaa nilimsikia akituambia kwamba aliokota kitu kilichokuwa kama chupa, ila sikujua kama ni almasi,” nilimwambia, akaniangalia vizuri, akalisogeza sikio lake karibu mwangu.
“Unasema kweli?”
“Ndiyo! Ninamjua! Kama mtakuwa tayari niwapeleke,” nilimwambia.
Mwanaume huyo akawaita wenzake na kuwaambia nilichomwambia. Wote hawakuamini kama mwisho wa siku ningekubaliana nao na kuwaambia kuhusu mtu aliyekuwa na almasi hiyo.
Wakaanza kuniuliza maswali mengi, nilikuwa makini kwenye kutoa majibu yangu, niliwaambia kila kitu kwamba kama tungemtafuta huyo mtu kwa kwenda kwao basi ilikuwa ni lazima tuipate hiyo almasi.
“Anaitwa nani huyo?” aliniuliza mwingine.
“Alfred!”
“Anaishi wapi?”
“Jirani yangu kulekule Kariakoo! Kama mtataka kumpata, twendeni,” niliwaambia.
Hakukuwa na mtu aliyeitwa kwa jina la Alfred lakini waliniamini kwa sababu ya hali niliyokuwanayo. Walijua kwamba kwa jinsi nilivyokuwa nimeteswa basi kila kitu ambacho ningekisema mahali hapo kingekuwa ni ukweli kabisa.
Niliwaambia kwamba nilisikia mwanaume huyo alitaka kuiuza almasi hiyo huko maeneo ya Posta keshokutwa ila kama kweli waliitaka bai ningekuwa radhi kuwapeleka mpaka huko.
Waliniangalia, kwa jinsi nilivyoonekana, mateso niliyopewa kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba kile nilichokuwa nikikizungumza kilikuwa kweli kabisa.
Hawakumjua Alfred, ili kufika huko ilikuwa ni lazima niende nao. Waliitana na kujadiliana, sikujua walichokiongea, wakanichukua, tukapanda gari na kuelekea huko.
Njiani nilikuwa kimya kabisa, akili yangu ilikuwa ikifikiria mambo mengi mno kwamba mara baada ya kufika huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwatoroka.
Mtu ambaye nilimfikiria mara ya kwanza alikuwa ni polisi, yaani niende kwenye nyumba moja yenye wapangaji wengi halafu niwaambie kwamba huyo Alfred alikuwa akikaa humo na kama walitaka niende kuwaitia napo kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Safari hiyo ilichukua kama dakika arobaini na tano hivi, tukafika karibu na nyumba hiyo. Nakumbuka muda huo ulikuwa ni saa moja usiku, niliwaoyeshea nyumba aliyokuwa akiishi huyo Alfred na hivyo walitakiwa kwenda kumuulizia.
Jamaa mmoja akateremka na kuelekea huko, akapiga hodi kwenye nyumba hiyo ya wapangaji wengi, mlango ukafunguliwa, akaulizia na kuambiwa kwamba hakuna mtu mwenye jina hilo, hivyo akaja kutuambia.
“Kwa nini umetudanganya?” aliniuliza mwanaume mmoja.
“Jamani! Nimewaambia huyu Alfred ana almasi, hivi mnadhani naye ni mjinga kiasi cha kukubali kwamba yupo? Inawezekana amewaambia wapangaji wenzake kwamba akiuliziwa na mtu yeyote waseme hayupo au hakuna mtu kama huyo. Hivi kama ni wewe mkuu, una almasi ndani halafu kaja mtu usiyemjua kukuulizia, ataambiwa kama upo ndani?” niliwauliza swali ambalo lilikuwa na maana kubwa sana.
Wakajifikiria na kukubaliana kwamba inawezekana kabisa niliwaambia ukweli kwani kwa akili ya kawaida tu kama ndani kulikuwa na mtu ana almasi halafu akauliziwa na mtu asiyemjua, ukweli ni kwamba asingeweza kutoka na kusema kwamba yupo.
“Ila kweli! Kwa hiyo tufanyeje?” aliuliza mwanaume mmoja, nikaona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yangu.
“Nenda naye! Mkifika aulizie yeye!” alisema mwanaume mwingine.
Nikateremshwa na mwanaume mmoja na kuelekea kule, tulipoufikia mlango, nikaugonga na ulipofunguliwa tu nikaulizia Alfred, nilikuwa namuhitaji.
“Jamani! Si nimeshasema kwamba hakuna Alfred humu ndani,” alisema mwanamke aliyeufungua mlango.
“Dada! Najua hunifahamu! Mimi ni mlinzi mwenzake!” nilimwambia.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikizungumza nilionyesha dalili zote za kuwa hoi, nilihitaji mwanamke yule anisome kwanza ili ajue ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Nahisi alilijua hilo kwani kila aliponiangalia aligundua kabisa huyu mtu hayupo sawa. Alichokisema ni kwamba hakukuwa na mtu huyo ila angetuitia mwanaume ambaye inawezekana alijua kila kitu kuhusu huyo Alfred.
Tukamwambia sawa, akatuitie. Akarudi ndani. Kwa yote niliyomuonyeshea tu nilijua angekwenda kumuita yule polisi. Ni ndani ya sekunde chache, mwanaume huyo akatokea huku akiwa na kaoshi tu, akasimama mlangoni na kutuangalia.
“Mnataka nini?” aliuliza kibabe.
“Tunamuulizia Alfred!” alijibu mwanaume yule huku akijiandaa kuupeleka mkono wake kiunoni kwa nyuma.
Hilo lilionekana kuwa kosa kubwa kwani mwanaume aliyekuwa ameufungua mlango na kuja, alikuwa na bastola yake na aliambiwa kwa kifupi kilichokuwa mlangoni, yaani mpaka leo hii namshukuru yule dada.
Jamaa alipoanza kuupeleka mkono kwa nyuma, yule polisi ambaye alifundishwa sana huko mafunzoni alijua tu alikuwa akifuata nini, kwa kasi ya ajabu akatoa bastola yake na kumpiga mbili za mguu na mkono, akaanguka chini, wale jamaa waliokuwa kwenye Noah, wakawasha gari na kuondoka mahali hapo kwa kasi.
Nilishukuru Mungu, mwanaume yule akatuweka chini ya ulinzi, akampekua jamaa yule na kuichukua bastola yake na kutuchukua kutupeleka kituoni.
Huko ndipo nilipoelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea, kwamba nilitekwa na watu hao kwa lengo la kuuawa kama wenzangu kisa tu kumuokoa mzee fulani.
“Ulitekwa?”
“Ndiyo! Tangu jana! Niliwekwa kwenye chumba cha mateso na kuanza kuchapwa, hebu angalia,” nilisema huku nikiwaonyeshea mgongo.
“Mungu wangu! Ulipelekwa wapi? Unapajua?” aliniuliza polisi mmoja.
“Napajua! Naweza kuwapeleka ila naogopa sana,” niliwaambia.
“Wewe tupeleke tu sisi tutakulinda,” aliniambia polisi mmoja na hivyo kukubaliana nao.