Simulizi: Nyumba Iliyojaa Dhambi

Shunie

JF-Expert Member
Aug 14, 2016
152,998
453,962
Mtunzi
Nyemo Chilongani
Sehemu ya 01

Ukimya ulitawala ndani ya Jiji la Dar es Salaam, yale magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi katika barabara nyingi jiji humu yalikata kabisa.

Watu wengi waliokuwa wakienda huku na kule hawakuwa wakionekana kama nyakati za mchana.

Kila kitu kilibadilika usiku huo, katika mitaa mingi ya Kariakoo hakukuwa na watu kabisa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama nyakati za mchana kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakipita huku na kule.

Katika muda huo, nilikuwa katika Mtaa wa Kongo. Hapo, ndipo kulipokuwa na maisha yangu, niliyaendesha humo, si kama mfanyabiashara bali nilifanya kazi hapo katika kusafisha barabara kila siku usiku.

Kwa jina ninaitwa Edward Francis. Nimeamua kukusimulia maisha yangu yalivyokuwa, najua kuna watu wanamuona mtu fulani amefanikiwa halafu wakahisi kabisa alitoka kwenye familia ya kitajiri, leo watu wanavyoniona nina nyumba kubwa, magari ya kifahari na hata biashara nyingi wanadhani kwamba nilizaliwa kwenye familia ya kitajiri, ndugu yangu, nilizaliwa kwenye familia ya kimasikini tena inawezekana zaidi ya hiyo yako, nilihangaika mno mpaka kufika hapa nilipo.

Maisha yangu ni simulizi nzuri kwako, kuna mambo mengi mazuri niliyoyafanya, ila kumbuka kwamba kuna mengi mabaya ambayo niliyafanya pia. Mabilionea wengi wa leo wakikusimulia maisha yao, watachambua, watakwambia yale mazuri lakini mabaya yatabaki moyoni mwao.

Ninaamua kuyafungukia maisha yangu leo, nitakwambia kila kitu, najua kuna watu wengi watajifunza kupitia maisha yangu.

Kuna mafunzo machache sana yanapatikana katika yale mambo mazuri uliyowahi kuyafanya ila kuna mafunzo makubwa yanayopatikana kwenye magumu na dhambi nyingi ulizopitia.

Mishemishe zangu zilikuwa Kariakoo, sikuwa na mahali pa kuishi, wazazi wangu walifariki miaka mingi iliyopita, sikuwahi kuziona sura zao, walifananaje?

Walikuwa wembambamba ama wanene? Weusi ama weupe? Kwa kweli sijui kitu chochote kile kuhusu wao.

Hapo Kariakoo nilikuwa mkimya, sikuwa muongeaji sana, nilijua kufanya kazi zangu nyingine kama kawaida.

Nakumbuka kila siku nilipokea kiasi cha shilingi elfu tano kila nilipokuwa nikimaliza kufanya usafi.




20180905_205402.jpeg
 
Sehemu ya 02

Ilikuwa kazi ngumu, barabara ilikuwa ikichafuka mno, na nilipokuwa nikianza kusafisha nilichoka sana.

Kuna wakati nilitamani kuacha kazi hiyo, sikuipenda lakini sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuendelea kuifanya zaidi na zaidi.

Kila siku katika maisha yangu nilitamani kuwa na pesa, demu mkali, nyumba nzuri lakini kwa jinsi nilivyokuwa nikiishi kipindi hicho niliamini kwamba maisha yangu yangeendelea kuwa hivyohivyo.

Hapo Kariakoo nyakati za asubuhi, mchana na jioni kulikuwa na watu wengi, wanawake wazuri ambao kila nilipowaangalia, niliwapenda. Nilifikiria sana wanawake, katika maisha yangu nimekuwa nikiwapenda mno lakini nilishindwa kuwa nao kwa sababu tu sikuwa na pesa.

Niliamini katika pesa, sikuamini kama ningekuwa na msichana ambaye angekubali kuwa nami na wakati sikuwa na lolote mfukoni, ili niwe na mwanamke mzuri basi ilikuwa ni lazima nitafute pesa kwanza, halafu hao wazuri wangekuja wao wenyewe.

Kila siku kazi yangu ilikuwa ni kuwasalimia wanawake na kuwasifia kwamba walipendeza, ningefanya nini sasa? Sikuwa na cha kufanya zaidi ya hicho. Kulikuwa na wanawake wanene, waliojaa, wale mamodo, wembamba, vifua vya kuvutia na walitembea kama twiga awapo mbugani.

Walinichanganya sana lakini tatizo lilikuwa pesa tu, haikuwa kazi nyepesi kuwapata kwa sababu sikuwa na kitu, yaani hata kama msichana akikubali, aniambie twende tukale raha, tutakulaje raha na wakati nina elfu tano mfukoni?

Yaani kwa kifupi sikuwa na meno hivyo nisingeweza kutafuna hata nyama laini.
“Dada mambo!” nilimsalimia msichana mmoja, alikuwa mrembo sana, alipendeza mno, nilimuona siku ya kwanza, sikumjua, alikuwa akitembea huku akiangalia vitu vya kununua. Si unajua mtaa wa Kongo unayokuwa na watu wengi?

Msichana huyo akageuka na kuniangalia, jicho lake tu lilionyesha ni kwa jinsi gani alionekana kuchukizwa na mimi, sikuwa mzuri sana, mavazi yangu yalionyesha kile nilichokuwanacho maishani mwangu.

“Umependezaaaa...” nilimwambia huku nikijitahidi kutoa tabasamu pana lakini wapi! Hakunichangamkia hata kidogo.
 
Sehemu ya 03

Huyo hakuwa wa kwanza wala wa mwisho, nilikuwa mzee wa shobo sana, kila msichana ambaye nilimuona na kuvutiwa naye, cha kwanza ilikuwa salamu, cha pili kikawa ni kumsifia.

Wapo wengine waliitikia lakini hawakutaka stori zaidi, hao waliondoka zao.
“Dada umependeza kama shangazi yangu,” nilimwambia msichana mwingine, alipendeza mno.

“Ahsante sana kaka yangu!”
“Unakwenda wapi? Huogopi kupotea?” nilimuuliza huku nikitoa tabasamu pana ambalo niliamini kwamba lilikuwa na ushawishi mkubwa mno.

“Hahaha! Nipotee Dar? Basi makubwa!”
Kwa jinsi alivyokuwa akinijibu moyo wangu ukafarijika. Nilijiona kuwa na thamani sana, yaani masikini mimi, ambaye kila siku sikuwa na pesa na nilidharauliwa na mademu eti leo huyu mwanamke alikuwa akijibu huku tukipiga stori za hapa na pale.

“Nichukue namba yake ya simu?” nilijiuliza lakini sikuwa na simu kwa maana hiyo hata kama ningechukua namba yake ingekuwa kazi bure tu.

Alikuwa akitembea kwenda kule kulipokuwa na nguo za wanawake, sikujua alikuwa akienda kununua nini, kitendo cha mimi kuwa naye, kupiga stori kilinifanya niridhike na kujiona mtu mwenye thamani kubwa kuliko wote katika dunia hii.

“Ila umependeza sana, unajua siwezi kuvumilia kusema ukweli,” nilimwambia huku nikimwangalia.

“Mara ya pili unaniambia hivyo!”
“Ni kwa sababu umependeza kweli, halafu mzuri! Uzuri huo umeridhi wapi?” nilimuuliza.

“Kwa mama! Mama yangu Mzigua!”
“Ooh! Mtoto wa Kitanga. Mzuri hasa na hata nikiangalia nyuma, mtoto mashallah!” nilisema huku nikiyapeleka macho mgongoni kwake, akageuka.
“Ooh! Usifanye hivyo bhana!” aliniambia huku akitabasamu.

“Usijali!”
Tulifika alipokuwa akienda, akanunua dela na kuondoka, nilichokifanya ni kuchukua namba ya simu yake na kuiandika kwenye kikaratasi halafu akaingia kwenye daladala.

Niliuchukia sana umasikini, uliniuma kwa sababu pale alipoingia ndani ya gari, kulikuwa na wanaume waliokuwa wakimwangalia kimatamanio, na hata kwenye siti aliyokwenda kukaa, kulikuwa na mwanaume mmoja ambaye bila aibu, hata kabla gari halijaondoka, akamsalimia na kuanza kupiga naye stori.
 
Sehemu ya 04

Iliniuma mno kwani niliamini kwa safari ya kutoka hapo Kariakoo mpaka kwao Mabibo, yule msela angechukua namba ya simu na kuanza kuwasiliana na mwisho wa siku kulala naye kitanda kimoja.

Hiyo ilikuwa sababu ya kwanza kuuchukua umasikini. Msichana yule hakutakiwa kupanda daladala, yaani ilifaa kuingia ndani ya gari langu na kumpeleka mpaka kwao ila kwa sababu nilikuwa kapuku, sikuwa na jinsi. Nikarudi kule Mtaa wa Kongo na kuendelea na mishe zangu kama kawaida.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu, nilipenda sana wanawake lakini sikuwa na makali yoyote yale. Kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuwasalimia, wakati mwingine walinitukana, walinichunia lakini sikutaka kujali hilo, niliendelea kufanya hivyohivyo kama kawaida.

“Issa! Naomba simu yako mara moja,” nilimwambia rafiki yangu Issa, huyu jamaa alikuwa akiuza duka moja hapo Kariakoo, ni duka la familia kwani alikuwa na dada zake wawili, Halima na Shamila ambao walipokezana, walikuwa wazuri lakini kwa jinsi umasikini ulivyonipa uoga na hali ya kujiamini, hata kuomba namba zao za simu sikuwahi.

“Ya nini?”
“Kuna demu nataka nimpigie! Niongee naye,” nilimwambia.
Issa alikuwa mshikaji wangu sana, ishu ndogo kama simu asingeweza kuninyima hata kidogo, akanipa, nikachukua kile kikaratasi ambacho nilipewa jana yake na yule msichana na kumpigia.

Simu ikaanza kuita na baada ya sekunde chache ikapokelewa na msichana huyo. Nikaanza kuzungumza naye, nilijitambulisha, alionekana kufurahi mno.

Tuliongea kana kwamba tulifahamiana miaka mingi iliyopita.
“Leo sijakuona, nimekumisi sana,” nilimwambia.

“Nimekumiss pia ila nipo bizebize, nikipata nafasi nitakuja!”
“Kweli?”
“Niamini baby boy!”
“Sawa haina shida.”

Niliongea naye kwa dakika kadhaa na kumrudishia simu Issa na kumshukuru kwani bila kutumia urafiki wetu na ukaribu mkubwa asingeweza kukubali.

“Nani? Mama au?”
“Hapana! Kuna demu nilikutana naye jana. Mnene, mweupe, kajaajaa, kama Kajala!” nilimwambia na kuanza kucheka.
“Acha masihara!”

“Ooh! Ni shida mzee baba! Halafu mzuri, sura ya kitoto, sijui nikwambiaje!” nilimwambia Issa.
 
Sehemu ya 05

Nilimsifia sana mwanamke yule pasipo kujua kama nilikuwa nikikaribisha maumivu moyoni mwangu.

Nilitaka Issa anione kama nilikuwa na bahati kumbe ndiyo nilikuwa nikimpa demu wa kuenjoi naye.

Kila siku ilikuwa kazi yangu kumwambia Issa nimpigie simu mwanamke huyo kumbe upande wa pili naye akaanza kujitengenezea mazingira na kuanza kumtongoza, na sijui msichana huyo alidanganyika na nini, akamkubalia na kukubaliana kulala pamoja, na hilo likatokea.

Sikuwa nikifahamu kipindi hicho, nilimuona Issa kama mshikaji wangu kumbe alikuwa akinizunguka tu. Sikujua kama alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo, sikujua kama walionana mpaka kufanya mapenzi.

Baada ya wiki moja akarudi tena. Sikufichi, mpaka muda huo sikujua hata jina lake, ila siku hiyo akaniambia kwamba aliitwa Aisha, nilifurahi sana lakini wakati alipokuja nilipokuwa, nilishangaa sana akimchangamkia mno Issa kuliko hata mimi.

Hilo likaipa wasiwasi, niliumia sana lakini nikapiga moyo konde pasipo kugundua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.

Nilipoona wanazungumza wao tu, nikamchukua Aisha na kuondoka naye.
Alikwenda kulekule kwa siku ile, nilivimba moyoni, wivu ulinijaa, nilitamani nimuulize zaidi kuhusu Issa lakini nikaamua tu kutulia.

“Aisha! Unajua nakupenda sana,” nilimwambia, nilifanya hivyo kwa kuwa nilijua tu kama ningechelewa, Issa angeniwahi.

“Unanipenda mimi?”
“Ndiyo! Ninakupenda Aisha,” nilimwambia!”
“Huniwezi Edward!”

“Kwa nini! Unadhani kwa gitaa dogo siwezi kutumbuiza uwanja wa taifa?” nilimuuliza kwa utani huku nikicheka.

“Utanilisha nini?” aliniuliza swali dogo sana ambalo lilikuwa na maana kubwa.
Nilibaki kimya nikimwangalia, sikutarajia kupata swali kama hilo kutoka kwake.

Ni kweli alikuwa na uhuru wa kuuliza kuhusu majukumu yangu kama mwanaume kwake.

Alikuwa akipendeza sana, hii ilimaanisha kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo, yaani kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akishughulika na mavazi tu, mwingine nauli za usafiri mwingine viatu na mwingine make up, sasa mimi ningeshughulika na nini?

Hata kama angeniambia nishughulike na vocha tu nisingeweza kutokana na kiasi cha pesa kilichokuwa kikihitajika.
 
Sehemu ya 06

“Kwani wewe unataka nini?” nilimuuliza ili nijue.
“Matunzo! Mtoto mzuri kama mimi nitunzwe, nitolewe out, niletewe baga, pizza, ice cream, uninunulie pafyumu, ninukie, au hutai demu wako ninukie vizuri?” aliniuliza.

“Nataka! Tena napenda sana.”
“Sasa je! Utaweza kunitunza?” aliniuliza.
Mtu mzima sikujua nimjibu nini, hilo swali lilikuwa kubwa kuliko uwezo wangu.

Nilimwangalia tu, kwa kawaida hata kama huwezi, kwa mwanaume ni MARUFUKU kusema neno siwezi, ni lazima useme unaweza halafu umkimbie.

“Kwa nini nisiweze? Tena umenikumbusha, nataka siku nikuchukue tukale pizza,” nilimwambia.

“Waooo! Lini bebi?”
“Tufanye Ijumaa!” nilimwambia, siku hiyo ilikuwa Jumatatu.

Sikia! Mimi nilikuwa nasikia sana kuhusu pizza ila kiukweli sikuwahi kula hata siku moja. Nilitamani vyakula vinono lakini sikuwa na pesa.

Hebu fikiria, kwa siku napokea elfu tano, halafu hapo pizza inauzwa elfu kumi na mbili mpaka nyingine elfu hamsini, hivi ningeweza kumgharamia yote hiyo? Kwangu ilikuwa vigumu, ila nilimwambia kwamba ningemtoa out kwa sababu tu nilitaka kujitia ubabe mfukoni.

“Basi naisubiri hiyo siku! Zimebaki siku nne, nitakutafuta bebi nikale pizza,” aliniambia kwa tabasamu na kisha kuagana huku moyo wangu ukijisikia burudani sana kwa kuamini kwamba nimeshinda vita kumbe ndiyo kwanza nilikuwa nikiingia kwenye vita na watu waliokuwa na nguvu kuliko mimi.

Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom