Simulizi: Nyumba Iliyojaa Dhambi

Simulizi: Nyumba Iliyojaa Dhambi

Sehemu ya 23

“Unasemaje?” aliniuliza kwa sauti ya kibabe.
“Ninamjua mtu mwenye almasi. Kuna jamaa nilimsikia akituambia kwamba aliokota kitu kilichokuwa kama chupa, ila sikujua kama ni almasi,” nilimwambia, akaniangalia vizuri, akalisogeza sikio lake karibu mwangu.
“Unasema kweli?”
“Ndiyo! Ninamjua! Kama mtakuwa tayari niwapeleke,” nilimwambia.
Mwanaume huyo akawaita wenzake na kuwaambia nilichomwambia. Wote hawakuamini kama mwisho wa siku ningekubaliana nao na kuwaambia kuhusu mtu aliyekuwa na almasi hiyo.
Wakaanza kuniuliza maswali mengi, nilikuwa makini kwenye kutoa majibu yangu, niliwaambia kila kitu kwamba kama tungemtafuta huyo mtu kwa kwenda kwao basi ilikuwa ni lazima tuipate hiyo almasi.
“Anaitwa nani huyo?” aliniuliza mwingine.
“Alfred!”
“Anaishi wapi?”
“Jirani yangu kulekule Kariakoo! Kama mtataka kumpata, twendeni,” niliwaambia.
Hakukuwa na mtu aliyeitwa kwa jina la Alfred lakini waliniamini kwa sababu ya hali niliyokuwanayo. Walijua kwamba kwa jinsi nilivyokuwa nimeteswa basi kila kitu ambacho ningekisema mahali hapo kingekuwa ni ukweli kabisa.
Niliwaambia kwamba nilisikia mwanaume huyo alitaka kuiuza almasi hiyo huko maeneo ya Posta keshokutwa ila kama kweli waliitaka bai ningekuwa radhi kuwapeleka mpaka huko.
Waliniangalia, kwa jinsi nilivyoonekana, mateso niliyopewa kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba kile nilichokuwa nikikizungumza kilikuwa kweli kabisa.
Hawakumjua Alfred, ili kufika huko ilikuwa ni lazima niende nao. Waliitana na kujadiliana, sikujua walichokiongea, wakanichukua, tukapanda gari na kuelekea huko.
Njiani nilikuwa kimya kabisa, akili yangu ilikuwa ikifikiria mambo mengi mno kwamba mara baada ya kufika huko, kitu cha kwanza kilikuwa ni kuwatoroka.
Mtu ambaye nilimfikiria mara ya kwanza alikuwa ni polisi, yaani niende kwenye nyumba moja yenye wapangaji wengi halafu niwaambie kwamba huyo Alfred alikuwa akikaa humo na kama walitaka niende kuwaitia napo kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Safari hiyo ilichukua kama dakika arobaini na tano hivi, tukafika karibu na nyumba hiyo. Nakumbuka muda huo ulikuwa ni saa moja usiku, niliwaoyeshea nyumba aliyokuwa akiishi huyo Alfred na hivyo walitakiwa kwenda kumuulizia.
Jamaa mmoja akateremka na kuelekea huko, akapiga hodi kwenye nyumba hiyo ya wapangaji wengi, mlango ukafunguliwa, akaulizia na kuambiwa kwamba hakuna mtu mwenye jina hilo, hivyo akaja kutuambia.
“Kwa nini umetudanganya?” aliniuliza mwanaume mmoja.
“Jamani! Nimewaambia huyu Alfred ana almasi, hivi mnadhani naye ni mjinga kiasi cha kukubali kwamba yupo? Inawezekana amewaambia wapangaji wenzake kwamba akiuliziwa na mtu yeyote waseme hayupo au hakuna mtu kama huyo. Hivi kama ni wewe mkuu, una almasi ndani halafu kaja mtu usiyemjua kukuulizia, ataambiwa kama upo ndani?” niliwauliza swali ambalo lilikuwa na maana kubwa sana.
Wakajifikiria na kukubaliana kwamba inawezekana kabisa niliwaambia ukweli kwani kwa akili ya kawaida tu kama ndani kulikuwa na mtu ana almasi halafu akauliziwa na mtu asiyemjua, ukweli ni kwamba asingeweza kutoka na kusema kwamba yupo.
“Ila kweli! Kwa hiyo tufanyeje?” aliuliza mwanaume mmoja, nikaona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi yangu.
“Nenda naye! Mkifika aulizie yeye!” alisema mwanaume mwingine.
Nikateremshwa na mwanaume mmoja na kuelekea kule, tulipoufikia mlango, nikaugonga na ulipofunguliwa tu nikaulizia Alfred, nilikuwa namuhitaji.
“Jamani! Si nimeshasema kwamba hakuna Alfred humu ndani,” alisema mwanamke aliyeufungua mlango.
“Dada! Najua hunifahamu! Mimi ni mlinzi mwenzake!” nilimwambia.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikizungumza nilionyesha dalili zote za kuwa hoi, nilihitaji mwanamke yule anisome kwanza ili ajue ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Nahisi alilijua hilo kwani kila aliponiangalia aligundua kabisa huyu mtu hayupo sawa. Alichokisema ni kwamba hakukuwa na mtu huyo ila angetuitia mwanaume ambaye inawezekana alijua kila kitu kuhusu huyo Alfred.
Tukamwambia sawa, akatuitie. Akarudi ndani. Kwa yote niliyomuonyeshea tu nilijua angekwenda kumuita yule polisi. Ni ndani ya sekunde chache, mwanaume huyo akatokea huku akiwa na kaoshi tu, akasimama mlangoni na kutuangalia.
“Mnataka nini?” aliuliza kibabe.
“Tunamuulizia Alfred!” alijibu mwanaume yule huku akijiandaa kuupeleka mkono wake kiunoni kwa nyuma.
Hilo lilionekana kuwa kosa kubwa kwani mwanaume aliyekuwa ameufungua mlango na kuja, alikuwa na bastola yake na aliambiwa kwa kifupi kilichokuwa mlangoni, yaani mpaka leo hii namshukuru yule dada.
Jamaa alipoanza kuupeleka mkono kwa nyuma, yule polisi ambaye alifundishwa sana huko mafunzoni alijua tu alikuwa akifuata nini, kwa kasi ya ajabu akatoa bastola yake na kumpiga mbili za mguu na mkono, akaanguka chini, wale jamaa waliokuwa kwenye Noah, wakawasha gari na kuondoka mahali hapo kwa kasi.
Nilishukuru Mungu, mwanaume yule akatuweka chini ya ulinzi, akampekua jamaa yule na kuichukua bastola yake na kutuchukua kutupeleka kituoni.
Huko ndipo nilipoelezea kila kitu kilichokuwa kimetokea, kwamba nilitekwa na watu hao kwa lengo la kuuawa kama wenzangu kisa tu kumuokoa mzee fulani.
“Ulitekwa?”
“Ndiyo! Tangu jana! Niliwekwa kwenye chumba cha mateso na kuanza kuchapwa, hebu angalia,” nilisema huku nikiwaonyeshea mgongo.
“Mungu wangu! Ulipelekwa wapi? Unapajua?” aliniuliza polisi mmoja.
“Napajua! Naweza kuwapeleka ila naogopa sana,” niliwaambia.
“Wewe tupeleke tu sisi tutakulinda,” aliniambia polisi mmoja na hivyo kukubaliana nao.
woyoooo my pipo watu wakutupa raha
 
SEHEMU YA 26

Japokuwa nilikuwa naogopa lakini sikuwa na jinsi, nikawachukua polisi na kuondoka nao kuelekea katika nyumba ile iliyokuwa huko Kinondoni.

Kila mmoja ndani ya gari alikuwa kimya, wale polisi wanawake walishindwa kuvumilia, kila walipouangalia mgongo wangu, kwa jinsi ulivyochakazwa walishindwa kuamini kama nilipona.

Nilichokihitaji sana ni kwenda hospitali tu kupata matibabu lakini kutokana na polisi wale kutaka kuifahamu nyumba hiyo, nikawachukua na kwenda huko.

Hatukuchukua muda mrefu tukafika, tukateremka na kuingia ndani. Hakukuwa na mtu yeyote yule, nahisi walijua kwamba polisi wangefika mahali hapo, walikimbia, polisi wakapitiliza mpaka kwenye kile chumba, picha waliyoiona wao wenyewe iliwatisha.

Huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kufuatilia kuhusu watu hao, sikutaka kuendelea kuwauliza ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo kwani nilipoondoka, sikutaka kurudi kituoni, nilipotea na kwenda hospitalini.

Hospitalini madaktari walikuwa wakishangaa, hawakuamini walichokuwa wakikiangalia, mgongo wangu ulichakazwa sana kiasi cha nyama ya ndani kuonekana.

Kila walipokuwa wakinigusa nilisikia maumivu makali hivyo hatua ya kwanza walichokifanya kilikuwa ni kunisafisha na kunipaka dawa ya kuua vijidudu.

Sikujua kwa Nurat ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, hakujua kama nilikuwa hospitalini, mara ya mwisho kuondoka nyumbani siku iliyopita ni pale nilipokwenda dukani, na sikurudi tena.

Nilijua kwamba alikuwa akijiuliza sana, ilibidi niwasiliane naye na kwa sababu nilimpenda na kumtamani sana, hata namba yake iliniganda kichwani, hivyo nikamuomba daktari simu yake na kumpigia.

“Naongea na nani?” niliisikia sauti yake nyororo.
“Edward!”
“Edward! Ooh my gosh! Upo wapi?” aliniuliza kwa mshtuko.

“Nilitekwa!”
“Ulitekwa? Na nani? Kisa nini? Ilikuwaje?” aliniuliza maswali kadhaa ambayo sikujua nimjibu lipi.

“Nurat! Nipo hospitali hapa Palestina! Naomba uje kuniona,” nilimwambia.
Nikakata simu na kuanza kumsikilizia, ilipita kama dakika thelathini hivi Nurat akafika hospitalini hapo, akaulizia, na kwa sababu ulikuwa muda wa kuona wagonjwa, akaruhusiwa na kuja kuniona.
 
SEHEMU YA 27

Alishangaa na kile alichokikuta, nililala kifudifudi huku mgongo mzima ukiwa na pamba. Alishindwa kuvumilia, akaanza kububujikwa na machozi, alionekana kuumia sana na kile alichokuwa amekikuta.

Akaniuliza kilichotokea kwani tangu nilipoondoka kwenda dukani kufuata soda sikurudi tena. Nikamuhadithia kila kitu kilichotokea kitu kilichomshtua kupita kawaida.

“Unasema walikuteka?”
“Ndiyo!”
“Kwa sababu gani?”
“Kwa sababu ya baba yako!”
“Baba yangu? Kivipi?” aliniuliza huku akishangaa.

Nilimwambia kuhusu kile kilichotokea usiku wa siku ile, watu wale walitumwa kwa sababu walikosa walichokuwa wakikifuata kwa baba yake ila sikumwambia ni kitu gani, nikaongezea kuwa kulikuwa na walinzi wenzangu ambao waliuawa na bila shaka watu wale ndiyo waliokuwa wamewaua kwa sababu niliwasikia wakiongea kuhusu hilo.

Ilikuwa ni stori fupi lakini iliyomsisimua mno. Akanisogelea na kunibusu shavuni, yaani hilo busu likanipa nguvu ya ajabu kupita kawaida. Kuanzia siku hiyo akaanza kuja hospitalini hapo kuniona akiwa na ndugu zake wengine ambao walinionyeshea thamani kwa kuwa niliyaokoa maisha ya baba yao.

Kichwa changu kilikuwa kikifikiria kuhusu ile almasi iliyokuwa chumbani kwangu, nilitamani sana niiuze, nipate mamilioni na kuendelea na maisha yangu.

Nilikaa hospitalini hapo kwa wiki moja huku Nurat na mama yake wakigharamia matibabu, na nilipopata nafuu, nikaruhusiwa kuondoka.

Nilipofika nyumbani kwangu, sikutaka kukaa humo, nilipekua nilipoificha almasi ile, nikaichukua na kuondoka zangu.

Kumbuka sikuwa na pesa lakini ilikuwa ni bora kukaa mitaani, niteseke nikitafuta duka la almasi kuliko kubaki mule chumbani kwani niliamini kwamba vijana wale wangefika na kuniua kama walivyokuwa wakipanga.

Maisha yakawa mtaani. Sikumwambia Nurat kuhusu maisha hayo, nilijua kwamba angenitafutia chumba kitu ambacho sikutaka kabisa kuona kikitokea.

Niliamua kufanya hivyo makusudi kabisa, unajua watu wa mitaani hawafuatiliwi kwa kuwa wanaaminika kwamba hawana pesa wala kitu chochote kile cha thamani na ndiyo maana na mimi nikajifanya kuwa mtu wa huko.
 
SEHEMU YA 28

Nusrat alipotaka kuonana nami, nilitafuta sehemu ya kawaida na kuonana naye huku nikimwambia kwamba kulikuwa na kazi nafanya ambayo iliyaendesha maisha yangu.

“Pole sana! Ila nitakusaidia,” aliniambia kwa sauti ya chini.
“Nitashukuru mno. Naweza kuuliza swali?” nilimuuliza.

“Uliza tu!”
“Nina lengo la kwenda Shinyanga kuchimba dhahabu ila tatizo ni moja tu, kama nikipata dhahabu huko nitakwenda kuiuza wapi?” nilimuuliza makusudi, nilihitaji kujua kuhusu hilo.

“Kule huwa kuna makampuni, hutakiwi kutoka nayo!”
“Najua! Tufanye nimefanya magumashi, nikafanikiwa kutoka nayo, niende wapi?’ nilimuuliza.

“Kwenye maduka ya kuuza dhahabu na almasi!”
“Sonara?”
“Hahaha! Hebu acha hizo. Nenda hata Posta, kuna duka moja pale linanunua vitu hivyo, ukipata niambie nikupeleke,” aliniambia Nurat.

Nilikuwa makini kumsikiliza, aliniambia mambo mengi pasipo kugundua kwamba nilikuwa na almasi ndani. Tuliongea mambo mengi siku hiyo na akaamua kuondoka zake huku akiniachia kiasi cha shilingi elfu hamsini kwa ajili ya matumizi yangu.

Mpaka siku hiyo sikuwa nimemwambia lolote lile, nilihofu moyoni mwangu, nilimwangalia jinsi alivyokuwa, mtoto wa Kiarabu, mzuri, mwenye shepu bomba, halafu nikajiangalia na kapuku mimi, nilivyokuwa kituko, yaani niligundua kabisa nisingeweza kufanikiwa kuwa na mtoto mzuri kama yeye.

Siku iliyofuata tu nikaondoka na kuelekea huko Posta kulitafuta duka hilo. Almasi hiyo nilikuwa nayo, nilivalia suruali yangu ya jinsi, kwa ndani nilifunga kamba fulani ambayo niliiunganisha kwenye kitambaa cha peke yake na kuiweka ile almasi.

Sikutakiwa kumwamini mtu yeyote yule, na hata nilivyokuwa nikitembea, sikuwa nikijiamini hata kidogo. Nilifanikiwa kufika kwenye hilo duka, nikaingia ndani, nikamkuta mzee wa Kihindi na vijana wawili, nikawasalimia na kuomba kuuliza.
“Kuna nini?” aliniuliza yule mzee.

“Nataka niuze mali yangu!” nilimwambia.
“Mali gani?” aliniuliza.

Sikumjibu, nilibaki nikimwangalia. Wote watatu walinikodolea macho, mzee huyo alijua kwamba najishtukia, akanichukua na kunipeleka ndani ya chumba kimoja, tukakaa na kuanza kuzungumza.
 
SEHEMU YA 29

Nilimwambia ukweli kuhusu ile almasi, akahitaji nimuonyeshee, nikafanya hivyo, alishtuka, hakuamini kama ningekuwa na almasi kubwa kiasi hicho.
“Umeipata wapi?”

“Nimeitoa mgodini. Mimi ni mchimbaji, zali tu limeniangukia,” nilimwambia.
“Hii ni kubwa sana. Nikupe kiasi gani?” aliniuliza, najua alihitaji kujua uwezo wangu wa kugundua kuhusu madini.

“Wewe una kiasi gani?”
“Milioni mia tano?” aliniambia, nikashtuka lakini nilijua yeye ni mfanyabiashara, kiasi hicho kilikuwa kikubwa kwangu lakini kwake, kulingana na mzigo, kilikuwa kiasi kidogo mno.
“Duuh!” nilitoa mguno.
“Niambie hata sasa hivi nakupa!”

“Yaani nikuuzie kwa milioni mia tano! Mzigo huu? Mzee unazingua,” nilimwambia, sikutaka kubaki hapo, nikairudisha na kusimama kutaka kuondoka.

“Sasa mbona unaondoka? Usifanye hivyo, rudi tuongee,” aliniambia huku akinishika mkono, alijua tu kwamba nilitaka kwenda kwenye duka jingine.

“Mzee unazingua, halafu unaniona mimi wa kuja, bora niende kwenye duka la mzee Sunil atanipa kiasi kinachostahili,” nilimwambia, hilo jina lenyewe nililitunga hapohapo.

“Hakuna! Hii biashara! Basi niambie nikupe kiasi gani.”
“Hapana nahitaji 1.2 B,” nilimwambia.
“Bilioni 1.2?” aliniuliza kwa kushtuka.

“Mzee! Nakuuzia almasi kubwa, sikuuzii dhahabu. Ndiyo maana nilisema kama hutaki acha niondoke nikale bilioni mbili,” nilimwambia kwa kujiamini.

Mpaka hapo niliweza kumdanganya kwa muonekano wangu, sikwenda kimama, nilikwenda kama mtu ambaye nilijua sana madini.

Mzee akaniambia ukweli tu kwamba kwa ile almasi niliyokuwanayo, gharama yake ilikuwa ni shilingi bilioni 1.5 ila kama ningependa nimuuzie hiyo bilioni moja ili akiiuza apate faida ya milioni mia tano.

“Yaani upate nusu yangu? Hapana! Weka bilioni moja pointi mbili, kama hutaki naondoka,” nilisema huku nikiinuka na kuufungua mlango.
“Subiri kwanza!” aliniambia.
 
SEHEMU YA 30

Ilikuwa ni kama utani lakinid ndiyo tukawa tunazungumzia pesa nyingi.

Akaingia kwenye chumba fulani na aliporudi alikuja na chombo fulani cha kuangalia kama ile ilikuwa almasi kweli ama la.

Akaipima, mzigo ulikuwa wenyewe.

Akatoa tabasamu pana, nikajua tu kuwa aligundua ina thamani sana, ila kwa kuwa na mimi sikujua kitu, nikaona poa tu, hata nikipigwa, kwani nilinunua?

Akakubaliana nami na kunichukua kuelekea benki kufungua akaunti na kuniingizia kiasi hicho cha pesa.

Zilikuwa pesa nyingi mno, nilichanganyikiwa, sikuamini kama mimi, Edward nilikuwa na pesa hizo kwenye akaunti yangu.

Nilichokumbuka ni watoto wazuri, si walinikataa, wakajiona wao ndiyo wao, si waliniambia mimi kapuku, sina pesa, halafu yule Issa si alitembea na demu wangu, halafu hakukumbuka kama ana wadogo zake, na huyohuyo Issa naye ana demu wake aliyetaka kumuoa, sasa nitaanza nao hao kwanza, halafu ndiyo nitadili na wengine, kuhusu huyo demu wake, hata kama amemuoa, nitatembea na mkewe kulipa kisasi, pesa ndiyo itaongea lugha tamu ya kumshawishi.

Je, nini kitaendelea?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom