SEHEMU YA 18
“Kwa hiyo unahisi watu wanaanza kutuua sisi walinzi? Kama wanatuua, kwa nini hawaibi?” aliuliza mwingine, huyu aliitwa Msekwa.
Kiukweli hili lilinichanganya kichwa sana lakini wenzangu hawakuwa na hofu hata kidogo.
Nilichanganyikiwa mno ila kwa kuwa wenzangu hawakuonekana kuwa na hofu, basi na mimi nikajifariji kwamba hakukuwa na tatizo hivyo sikutakiwa kuhofia hata kidogo.
Japokuwa nilikubaliana nao lakini sikutaka kupotezea kabisa, kichwa changu kiliniambia kwamba kulikuwa na jambo lililokuwa likiendelea nyuma ya pazia.
Asubuhi ilipofika, huku nikiwa katika chumba changu, Nurat akapiga simu kwamba alikuwa akija kuniona kwa kuwa hakwenda chuo siku hiyo.
Nikamkaribisha! Ndani ya dakika chache, akafika, akatulia na kumwambia niende kumnunulia kinywaji dukani. Alikataa lakini si unajua lazima mwanaume uonyeshe umwamba, nikaenda hivyohivyo huku yeye akinisubiri ndani.
Duka halikuwa mbali sana na mahali hapo, kulikuwa na vichochoro vichache kabla ya kuingia kwenye barabara kubwa iliyokuwa na maduka mengi.
Nilipofika kwenye barabara hiyo, macho yangu yakatua kwenye gari moja lililosimama pembeni, ilikuwa Noah Nyeusi. Sikulitilia maanani, nilielekea dukani, nikanunua soda na kuanza kurudi.
Ghafla mlango wa gari lile ukafunguliwa na mwanaume mmoja kuteremka huku akiwa na sigara mkononi. Akaniita kwa kuniomba sana, nikamsogea.
“Samahani ndugu yangu, wewe ni mwenyeji maeneo haya?” aliniuliza huku akiniangalia.
“Ndiyo! Kuna nini bosi?”
“Unamfahamu huyu?” aliniuliza huku akinionyeshea picha ya mwanamke mmoja.
Niliiangalia kwa makini, sikuwa nikimfahamu na sikuwahi kumuona hata siku moja. Nilimrudishia na kumwambia kwamba sikuwa nikimfahamu.
“Haina shida! Unaweza kuingia ndani ya gari twende tukazungumze?” aliniuliza huku akiwa na tabasamu pana.
“Ndani ya gari? Hapana! Nina haraka,” nilimwambia.
“Kweli?” aliniuliza huku akinionyeshea bastola yake iliyokuwa kiunoni.
Nilishtuka mno, nilitamani kukimbia lakini nilipokumbuka kwamba bastola ilikuwa na uwezo wa kukuua hata ukiwa mbali, niliogopa kupita kiasi.