SEHEMU YA 46
“Yaani huko ndiyo nakwenda kama kariakoo vile, I’m just flying anytime ninayotaka,” aliniambia.
“Hebu niambie kwanza China kupo vipi, yaani nataka nijue bhana,” nilimwambia kwa lengo la kumfanya aendelee kujisifia kama alivyofanya.
Nyie hapa duniani kuna watu wanajua kujisifia, aliniambia mambo mengi, sijui alikwenda China, alifanya biashara nyingi mpaka akakutana na Jack Ma, yule bilionea wa China.
Nilibaki nikizisikiliza tu pingu alizokuwa akinifunga, hakujua kama mimi ni mjanja basi akajiona anajua sana kumbe na mimi nilikuwa na tageti zangu.
“Daah! Kati ya watu waliofanikiwa, wewe ni mwanamke wa chuma,” nilimwambia.
“Yaani usione hivi. Maisha haya nisingepambana hata gari nisingenunua.”
“Naona jitihada zako, umekuja na Verrosa new model.”
“Kuna nyingine nimeiacha nyumbani, ni Range SUV. Niliinunua kwa kuiagiza kutoka Japan, ila siipendi kwa kuwa ipo juu juu sana.
Mimi napenda kama Verrosa. Kuna Hammer moja niliagiza, nikaona kama it is not my type, nikampa my young sister, naye ikamshinda manake inakula sana mafuta, she sold it,” aliniambia.
Kwanza nikashusha pumzi ndefu, nilitamani kucheka lakini nikapiga moyo konde niendelee kumsikiliza. Alinipiga sana fiksi na mwisho wa siku nikaanza kumwambia kuhusu mpango wangu.
Alinisikiliza, kwa jinsi nilivyoonekana tu alinichukulia kawaida sana kwa kuwa nilivalia kikawaida mno. “Unataka kununua kiwanja changu?” aliniuliza.
“Ndiyo! Natamani niwe nacho, kimekaa sehemu nzuri kidogo,” nilimwambia.
“Una hela? Mimi mwenzio Mchaga, pesa mbele kama tai,” aliniambia.
“Sina hela ya kutosha, kwani unakiuza kiasi gani?”
“Milioni kumi!”
“Milioni kumi?” niliuliza kwa mshtuko.
“Ndiyo!”
Kwanza nikabaki kimya, nilikuwa na pesa lakini haikuwa ya kutumia hovyo kiasi hicho, kama kweli alikuwa akikiuza kwa bei hiyo inamaana kwamba nisingeweza kununua kwa sababu tu nilijiandaa kukinunua kwa shilingi milioni tano tu.
Huyu mwanamke aliyeitwa Maria japokuwa alikuwa mtu wa sifa lakini namsifu sana kwa kuwa alikuwa na akili mno. Unajua kwa nini? Ngoja nikwambie kilichotokea hapo baada ya kuona nasitasita kutoa milioni kumi.