Sehemu ya 05
Nilimsifia sana mwanamke yule pasipo kujua kama nilikuwa nikikaribisha maumivu moyoni mwangu.
Nilitaka Issa anione kama nilikuwa na bahati kumbe ndiyo nilikuwa nikimpa demu wa kuenjoi naye.
Kila siku ilikuwa kazi yangu kumwambia Issa nimpigie simu mwanamke huyo kumbe upande wa pili naye akaanza kujitengenezea mazingira na kuanza kumtongoza, na sijui msichana huyo alidanganyika na nini, akamkubalia na kukubaliana kulala pamoja, na hilo likatokea.
Sikuwa nikifahamu kipindi hicho, nilimuona Issa kama mshikaji wangu kumbe alikuwa akinizunguka tu. Sikujua kama alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo, sikujua kama walionana mpaka kufanya mapenzi.
Baada ya wiki moja akarudi tena. Sikufichi, mpaka muda huo sikujua hata jina lake, ila siku hiyo akaniambia kwamba aliitwa Aisha, nilifurahi sana lakini wakati alipokuja nilipokuwa, nilishangaa sana akimchangamkia mno Issa kuliko hata mimi.
Hilo likaipa wasiwasi, niliumia sana lakini nikapiga moyo konde pasipo kugundua kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia.
Nilipoona wanazungumza wao tu, nikamchukua Aisha na kuondoka naye.
Alikwenda kulekule kwa siku ile, nilivimba moyoni, wivu ulinijaa, nilitamani nimuulize zaidi kuhusu Issa lakini nikaamua tu kutulia.
“Aisha! Unajua nakupenda sana,” nilimwambia, nilifanya hivyo kwa kuwa nilijua tu kama ningechelewa, Issa angeniwahi.
“Unanipenda mimi?”
“Ndiyo! Ninakupenda Aisha,” nilimwambia!”
“Huniwezi Edward!”
“Kwa nini! Unadhani kwa gitaa dogo siwezi kutumbuiza uwanja wa taifa?” nilimuuliza kwa utani huku nikicheka.
“Utanilisha nini?” aliniuliza swali dogo sana ambalo lilikuwa na maana kubwa.
Nilibaki kimya nikimwangalia, sikutarajia kupata swali kama hilo kutoka kwake.
Ni kweli alikuwa na uhuru wa kuuliza kuhusu majukumu yangu kama mwanaume kwake.
Alikuwa akipendeza sana, hii ilimaanisha kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakifanya kazi hiyo, yaani kulikuwa na mwanaume aliyekuwa akishughulika na mavazi tu, mwingine nauli za usafiri mwingine viatu na mwingine make up, sasa mimi ningeshughulika na nini?
Hata kama angeniambia nishughulike na vocha tu nisingeweza kutokana na kiasi cha pesa kilichokuwa kikihitajika.