Simulizi: Nyumba Iliyojaa Dhambi

SEHEMU YA 31

Nilikuwa bilionea, tena mkubwa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama nilikuwa na kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia mbili kwenye akaunti yangu. Sikuamini kama ni mimi kweli ndiye nilikuwa na kiasi hicho cha pesa.

Niliondoka Posta huku nikiwa makini kuliko siku zote katika maisha yangu. Nilihisi kama ningegongwa na gari na hivyo kupoteza kiasi changu chote hicho kilichokuwa benki.

Nilitembea kwa tahadhari sana na si hivyo tu, yaani siku hiyo hata daladala sikupanda kwa kuhisi kwamba ingeweza kupata ajali, abiria wote wakafa nikiwemo mimi.

Yaani niliogopa kufanya mambo mengi, nilikuwa natembea tu kurudi mtaani lakini sikutaka kupita barabarani kwani bado mawazo ya ajaliajali yalikuwa yakinijia kichwani mwangu.

Nilikuwa bilionea lakini nilivyokuwa nikitembea nilionekana kama sina pesa. Kichwani mwangu kulikuwa na picha za wanawake wengi wazuri, niliwakumbuka marafiki zangu walipokuwa wakiniambia kuhusu mademu wakali waliokuwa wakipatikana katika klabu za usiku, achana na hao, niliwakumbuka wale mademu wakali waliokuwa wakionekana kwenye video nyingi za hapa Bongo, yaani kwa akili yangu, nilitaka nilale na wote hao.

Niliondoka mpaka mtaani, nikatulia kwanza na kuanza kuyafikiria maisha yangu, sikuamini kama kweli nilifanikiwa kuwa na kiasi hicho cha pesa. Nilitaka nikachukue kidogo kwa ajili ya kwenda kutumia.

Nilikuwa na kadi yangu ya ATM, kutokana na ushindani mkubwa wa kibenki, kipindi hicho ulipokuwa unajisajili tu na kupata akaunti yako ulikuwa ukipewa kadi yako hapohapo na si kama zamani ambapo ulitakiwa kusubiri kwa wiki nzima.

Nilikwenda mpaka kwenye mashine ya ATM iliyokuwa Sinza. Niliwaona watu wakiwa wamepanga mstari wakiingia kwa zamu kuchukua pesa.

Nilitamani nisimame na kuniambia wanipishe kwani mimi nilikuwa na pesa zaidi yao wote, hata ukizichanganya wasingeweza kunifikia.

“Jamani! Mpaka pesa ziishe humo!” nilisema kwa hasira mpaka jamaa aliyekuwa mbele yangu kuanza kucheka
 
SEHEMU YA 32

Zamu yangu ilipofika, nikaingia kwenye kibanda kile. Tangu nizaliwe sikuwahi kuingia sehemu kama hiyo lakini sikutaka kupata maelekezo kwa mtu yeyote yule kwa kuwa sikutaka watu wajue kama nilikuwa na kiasi hicho cha pesa.

Nilifuata maelekezo na hatimaye kuchagua lugha ya Kiswahili na kutoa kiasi cha shilingi milioni mbili na kuondoka zangu. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kununua simu ya kupangusa kisha kuanza kuulizia kuhusu nyumba.

Kwanza sikutaka kufikiria kuhusu biashara, makazi yalikuwa bora kabisa. Niliulizia madalali, hatimaye nikakutana na mmoja na kumwambia hitaji langu la nyumba.

“Unataka nyumba ya kiasi gani?” aliniuliza.
“Yoyote nzuri! Kwanza zinapatikana?” nilimuuliza.

Dalali yule hakuniamini, kwa jinsi nilivyoonekana na kumwambia kwamba nilitaka kununua nyumba vilikuwa vitu viwili tofauti.

Nilichoka, sikuwa na nguo mpya, yaani kwa akili yangu ilivyokuwa, nilianza kununua simu kabla ya nguo.
“Twende huku tajiri,” aliniambia japokuwa bado hakuonekana kuniamini.

Tulikwenda mpaka kwenye nyumba moja kubwa. Ilikuwa Kijitonyama, haikuwa nzuri sana lakini kwa kuwa nilikuwa na pesa, nilijua ningeirekebisha na kuifanya nitakavyo.

Nikapelekwa mpaka ndani na kuonana na mwenye nyumba, dalali akaanza kuongea naye na kumwambia kwamba mimi ndiye nilikuwa mteja pekee niliyepatikana.

Mwenye nyumba akaniangalia, alionekana kunishangaa, ilikuwaje niwe na pesa za kununua nyumba na wakati muonekano wangu tu nilikuwa kama fukara fulani hivi.

“Huyu ndiye anataka kununua nyumba?” alimuuliza dalali huku akionyesha mshangao.

“Ndiyo!”
“Acha masihara!”
“Huyu ndiye bosi. Niambie, kiasi gani?” alisema dalali.

Mzee yule hakutaka kujibu kitu, bado alikuwa akinishangaa, kwake nilionekana kuwa kama kituko fulani hivi.

Akatuambia kwamba alikuwa akiiuza kwa shilingi milioni themanini kwa kuwa alitaka kuondoka hapo na kwenda kuishi Mbagala, maisha ya mjini eti yalimchosha.

“Mbona nyingi sana?” nilimuuliza mzee huyo.

“Si unaona Juma! Nilikwambia umeniletea mhuni unabisha! Sasa milioni themanini ina wingi gani?” aliuliza baba mwenye nyumba.
 
SEHEMU YA 33

Maneno yake yalinikera sana, nilitamani ninunue nyumba yake na nimnunue mpaka yeye mwenyewe. Ila pamoja na kuumia hivyo, sikutaka kuonyesha hasira zozote zile zaidi ya tabasamu pana.

“Basi sawa! Nitakulipa hizo milioni themanini,” nilimwambia ili kuepusha maneno.

Nilichomwambia ni kutaka kuona hati ya nyumba hiyo. Hilo halikuwa tatizo, akamuita mtoto wake wa kike aliyeitwa Zamaradi ili alete hati ya nyumba.

Kwanza hiyo sauti ya huyo Zamaradi ilivyoitikia, jinsi ilivyosikika masikioni mwangu, nikajua tu kwamba huyo angekuwa bonge moja la demu.

Baada ya sekunde kadhaa, kweli hati ikaletwa, huyo Zamaradi nilipomuona, alikuwa bonge la demu.

Mtu mzima udenda ukanitoka, shetani aliyekuwa ameniacha, akanirudia na kunipa mtego mkubwa.

“Hapa hatoki mtu,” nilijisemea.
Nikabaki namwangalia tu Zamaradi mpaka akashtuka kwamba nilikuwa namkodolea macho.

Akayageuza macho na kuniangalia, mtoto jicho kama kala kungu, macho yalirembulika mpaka nikachanganyikiwa.

“Mzee mimi ndiye nataka ninunue hiyo nyumba,” nilimwambia mzee huyo pasipo kutarajia.

“Haina shida. Usiwe na hofu kijana. Ni milioni themanini tu,” aliniambia.
“Hakuna shida nitalipia,” nilisema na Zamaradi kuondoka hapo.

Unajua kwa nini nilisema hivyo? Ni kwa sababu Zamaradi alikuwepo hapo. Yaani kwa jinsi tulivyoonekana, dalali alionekana kama mnunuaji na mimi nilionekana kama dalali.

Nikaichukua ile hati na kuiangalia, kulikuwa na jina la huyo mzee. Niliporidhika nikampa.

Kichwa changu kilikuwa kikifikiria kuhusu Zamaradi tu, alikuwa demu bomba ile kinoma, akili yangu iliniambia kwamba piga ua lazima nikaongee naye lakini si kuvumilia kubaki sebuleni hapo.

Kwa kuwa huyo mzee hakuwa na nguvu sana, nikamwambia ninahitaji kwenda chooni kujisaidia, niliamini kwamba angemuita Zamaradi kumpeleka mgeni kwenda huko, na mimi ningefanya yangu.

Kweli bwana! Akamuita msichana huyo na kumwambia anipeleke chooni. Mungu anipe nini tena? Nikasimama na kuanza kwenda huko huku tukiwaacha wao sebuleni pale.
 
SEHEMU YA 34

Nilibaki nyuma ya Zamaradi huku nikimwangalia alivyoumbika. Jamani Mungu fundi, acheni masihara.

Mpaka leo ninaamini kuna watu aliwaumba akiwa kwenye mood nzuri sana, na wengine aliwaumba kwa kuwaambia “Na nyie kaijazeni dunia tu manake hakuna namna.”

Ila kwa mtoto kama Zamaradi, nikahisi kwamba Mungu alisubiri siku ya wikiendi, ambayo hana kazi nyingi, siku aliyokuwa na furaha na kuanza kumtengeneza huyu mtoto.

Yaani alikamilika kila idara kiasi cha kuedelea kunitoa udenda.
“Zamaradi!” nilimuita, nilishindwa kuvumilia, akageuka na kuniangalia.
“Abee bosi!” aliitikia, nikaachia tabasamu.

“Mungu fundi sana, anajua kuumba si mchezo!” nilimwambia.
“Kwa nini?”

“Umeumbika mno, u mzuri mpaka unaboa. Hebu naomba namba yako ya simu kwanza,” nilimwambia.

Mtoto alishasikia mimi ndiye niliiyetaka kununua nyumba yao, nilishatamba pale sebuleni, ataachaje kunimba namba, akanipa na kuniambia nimbipu manake alihisi asije akawa amekosea, nilivyofanya hivyo ikaita.

“Nakupenda sana,” nilimwambia, sikutaka hata kujivunga.
“Mh! Jomoniiii! Hebu nenda chooni kwanza.”

“Sijabanwa na haja nilitaka tu kuongea na wewe,” nilimwambia.
Mwenyewe akafurahi.

Hapo ndipo nilipoamini kwamba mimi ni rijali, yaani sijui ilikuwaje ila nikajikuta nipo karibu naye na kuanza kubadilishana mate.

Pesa! Pesa! Pesa! Aliyezianzia Mungu anamuona, sijajua alikuwa na lengo gani kwenye dunia hii.

Yaani ndiyo kwanza Zamaradi aliniona kwa mara ya kwanza, hakunijua nilikuwa nani lakini alivyonipokea mikononi mwake, kama mpenzi wake ambaye aliishi naye kwa miaka kumi.

“Nakupenda sana,” nilimwambia kwa sauti ndogo ambayo niliamini kuwa itampagawisha.
“Nakupenda pia!”

Baada ya hapo nikajiweka sawa na kurudi sebuleni na kuanza kuendelea kuongea nao. Tulikubaliana malipo kufanyika kesho, tena cash, hivyo tukaondoka.

Nilienda kuchukua chumba hotelini, nilipoingia tu, kitu cha kwanza kilikuwa ni kumpigia simu Zamaradi, alinipagawisha mno na kuanza kuonja utamu wa pesa.

“Bebi! Nimekumiss sana,” nilimwambia.
“Kweli jamaniiii!”
 
SEHEMU YA 35

“Ndiyo! Mwili wako una joto tamu sana, yaani nilivyokukumbatia , nilihisi raha kama nimeona mlango wa pepo.

Zamaradi, unaufanya moyo wangu udunde, ndum ndum ndum....” nilimwambia.

“Jamaniiiiii”
“Wewe u mzuri mno, una tabasamu zuri, una meno mazuri, macho ya goroli, Zamaradi, umeumbika, unajua kucheka, una sura ya kitoto, umejazia, Zamaradi, hakika hakuna mwanaume anayeweza kukuacha akikupata,’ nilimwambia kwa kumchombeza.

“Jamaniiiii! Nasikia aibu huko!” aliniambia kwa kasauti kake ka kubembeleza.

“Zamaradiiiiiiii....nipo radhi nikose kila kitu, yaani pesa, kuingia peponi, nikose furaha lakini nisikukose wewe, ni mwanamke wa kipekee sana, ni mwanamke unayehitaji kuwa na furaha muda wote, unahitaji kutabasamu, kujaliwa, kusikilizwa, ni mwanamke unayetakiwa kuwa kwenye ulimwengu wako wa kipekee, Zamaradi, katika dunia hii hakuna mwanamke mzuri kama wewe,” nilimwambia, nilimsifia sana.

“Jamaniiiiiiiiiii” aliniambia, nahisi muda huo alikuwa aking’ata kidole chake.
“Zamaradi mpenzi, naomba ufungua mikono yako, unikumbatie, nikubusu, nikuonyeshee jinsi ulimwengu wa mapenzi ulivyo, nikaribishe mpenzi, nionje radha ya mate yako kwa mara nyingine,

Zamaradi, kuwa mama wa watoto wangu,” nilimwambia kwa sauti ile tamu kabisa.

“Kwani hujaoa bebi?” “Ningeoaje na wakati sikuwa nimeonana nawe? Zamaradi! Be mine mamiiiiii, unautetemesha moyo wangu....let me love you senyorita,” niliendelea kumchombeza.

Siku hiyo ndiyo nikaamini kwamba na mimi mkali kwenye maneno matamu, nilimfanya Zamaradi ajisikie kuwa mwanamke mzuri kuliko Mila Kunis, nilimwaminisha kwamba moyoni mwangu hakukuwa na yeyote yule.

Siku hiyo nilikesha nikiongea naye tu. Sijui alikuwa na bwana au peke yake, kitu nilichokuwa nikikiangalia ni mimi kuwa naye tu.

Nakumbuka siku hiyo nililala majira ya saa saba na asubuhi nikapanga kwenda benki.

Ilipofika, nikachukua begi langu na kwenda benki kwa lengo la kuchukua pesa hizo. Nilihitaji kuchukua milioni tisini kwani nilijua kungekuwa na dharura.

Sikutaka kwenda na dalali, nilikwenda peke yangu. Niliingia benki nikiwa na begi langu lililokuwa na nguo ndani, unajua kwa nini? Kwa sababu ya kubadilisha.
 
SEHEMU YA 36

Nilijua kwamba unapotoka kuchukua pesa nyingi benki na unapotoka, huwa kuna watu wanakufuata kwa ajili ya kukuua na kukuibia pesa, sasa kwa sababu nilikuwa mjanja, nilitaka niwachezee mchezo mpaka washangae.

Nilihitaji kiasi hicho cha pesa, niliambiwa nisubiri wakati wakiendelea kufanya process za mimi kupata kiasi hicho cha pesa. Baada ya saa moja, nikapewa na kuanza kuondoka.

Hapo benki, unapotoka, kwa kuwa ipo kwenye ghorofa refu, kabla ya kwenda nje kuna lifti, hivyo nilichokifanya ni kwenda kwenye lifti kama ninataka kwenda juu, humo ndani, nikabadilisha nguo zangu na kuchukua zilizokuwa kwenye begi, nikavaa na kofia kabisa kisha kuteremka kutoka kwenye lifti na kuchukua nyingine, nikaanza kushuka.

Nilitoka huku nikiwa na muonekano mwingine kabisa.

Kwa kawaida sehemu hiyo si ya kupaki bodaboda, ila kwa mbali niliwaona vijana wawili, walikuwa na elementi, walisimama pembeni ya bodaboda yao huku wakiangalia kule kwenye jengo lile la benki, nikajua tu kwamba walitonywa kuna mtu ametoa milioni tisini hivyo walitakiwa kunifanyia uninja, kumbe hawakujua kama mimi mwenyewe nilikuwa ninja.

Nikawaacha wakiendelea kumsubiri mtu aliyevalia suruali ya kitambaa na fulana nyekundu, kumbe huyu aliyetoka ambaye alivalia pensi ya jinsi, fulana ya bluu na kofia nyeusi na kubeba begi ndiye mtu ambaye walitakiwa kumfuata, ila kwa kuwa hawakugundua kutokana na maelekezo waliyopewa kuwa tofauti na jinsi nilivyokuwa, nikawa huru kuondoka bila kufuatwa na yeyote yule.
 
Kesho ni uongo hii story bado haijaisha ndio mana kuna viarosto flani tuvumiliane tu jamani hivyohivyo
Haya mamaa wewe ndio umeshka upini, una uamuzi wakunipa utamu utakavyo! Asanteh hata kwa huu utamu kidogo unaonipatia, unanichanganya vilivyo nawaza tu kama huu kidogo uko hivi je...?
 
Mh jamani
Kwahiyo hizi episode 6 jamani ni kidogo nipo2
Haya mamaa wewe ndio umeshka upini, una uamuzi wakunipa utamu utakavyo! Asanteh hata kwa huu utamu kidogo unaonipatia, unanichanganya vilivyo nawaza tu kama huu kidogo uko hivi je...?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom