SEHEMU YA 105
Angel alirudi kwao ila alikuwa na mawazo sana, sema akakumbuka maneno ya shangazi yake kuwa ajiweke makini na masomo ili aweze kuyakwepa yale mawazo aliyokuwa nayo.
Siku hiyo hadi wakati analala usiku ni kama alikuwa akihisi kuwa madam Hawa ana mahusiano na Samir,ila alijiuliza sana,
“Sasa kama kweli, kwanini naumia?”
Aliwaza na kukosa jibu, basi aliamua kujilazimisha tu kulala.
Kulipokucha alienda shuleni kama kawaida, ila na siku hiyo pia alimuona madam Hawa akifika na Samir halafu muda kidogo baada ya Samir kuingia darasani yule madam alifika na kumuita Samir, basi alimuangalia na watu darasani walionekana kuguna kwa siku hiyo.
Basi Husna akaanza kumwambia Angel,
“Unajua kwasasa kila mtu kaanza kupatwa na mashaka yani sio ukaribu huu wa mwalimu na mwanafunzi, huyu madam Hawa anatushangaza kwakweli”
“Kumbe na nyie mmemuona eeeh!”
“Ndio, kwanini kila siku asubuhi afike nae? Na kwanini baada ya kufika tu aje kumuita? Huwa anaenda kuongea nae nini ofisini?”
“Ila huyu madam mbona ni mtu mzima?”
“Ni mtu mzima ndio, ila kumbuka kuwa hana mume halafu huyu ni madam anayeogopewa shule nzima hii, ni kwanini aweze kuwa karibu hivyo na Samir? Hivi hujajiuliza swali hilo Angel?”
“Nimejiuliza ila nikakosa jibu”
“Basi jibu ni kuwa anatoka nae”
Wakaongea ongea pale ila Husna hakujua tu ni kwa jinsi gani jambo lile lilimuuumiza Angel.
Ilikuwa ni karibu na muda wa kutoka, walimu wakiwa ofisini waliona kwa mbali Abdi akishuka na baba yake kwenye gari kuelekea ofisini, basi walianza wenyewe kuongea,
“Uwiii jamani huyu Abdi kaamua kuja na baba yake mweeeh!”
“Ila hukumwambia kuwa aje na mama yake?”
“Nilimwambia, hata sijui kwanini anakuja na baba yake jamani!”
“Yule mama ni muelewa ila huyu baba ni mtata balaa, yani sijui itakuwaje mweeeh!”
“Hivi na siku ile aliyotoka na damu puani ilikuwaje?”
“Tulimwambia asiseme, alivyopona basi, tulimpa huduma ya kwanza ila tulimwambia kuwa asiseme, yani ugomvi huu una wazazi wasumbusu jamani hadi kero”
Baba Abdi aliingia ofisini, huku Abdi akikaa nje ya ofisi kusubiria baba yake aongee na walimu.
“Eeeeh nimeitikia wito, niambieni tatizo”
“Samahani mzee, ni hivi huyu Abdi kuna kitu kafanya shuleni hapa. Tulisikia sauti chooni, kwenda ndio tukamkuta Abdi, pamoja na binti mmoja na mvulana mwingine, Abdi alitaka kumbaka yule binti, sasa….”
Baba Abdi akawakatisha kwanza na kuwauliza tena,
“Mnasema Abdi alitaka kubaka? Jamani mnataka kuchekesha wasionuna, sasa Abdi abake kitu gani wakati hata kubalehe hajabalehe jamani, hivi walimu mna akili nyie kweli eeeh! Sasa Abdi abake vipi?”
“Tusikilize mzee kwanza, halafu mlango wa chooni umevunjwa, kwahiyo inabidi ulipe gharama za kutengeneza kitasa”
“Kwahiyo Abdi ndio kavunja huo mlango katika harakati za kubaka?”
“Hapana, ila mlango alivunja kijana aliyeenda kumuokoa yule binti”
“Hivi mnajua siwaelewi kabisa, yani siwaelewi. Mlango avunje nani na alipe nani? Hebu niitieni kwanza huyo aliyetaka kubakwa na huyo muokoaji”
Ikabidi mwalimu akamuite Ellyn a Erica kwani ulikuwa ndio muda wa kutoka, kwahiyo moja kwa moja walienda ofisini na kumkuta baba Abdi, ambapo walitambulishwa na walimu pale, kisha mwalimu akamwambia baba Abdi,
“Binti huyo hapo ambaye mwanao alitaka kumbaka, anaitwa Erica”
Baba Abdi akashangaa sana na kusema tena,
“Erica!!!”
“Ndio, anaitwa Erica, halafu huyu mvulana anaitwa Elly ndio ambaye alienda kumsaidia Erica”
“Hebu muiteni Abdi kwanza”
Walimu walimuita Abdi ambaye alikuwa nje ya ile ofisi ambaye aliingia na baba yake alimuuliza,
“Eti mwanangu, ulitaka kumbaka Erica?”
“Hapana baba, sijataka kumbaka”
Kisha baba Abdi akamuangalia Erica na kumuuliza,
“Eti ni kweli Abdi alitaka kukubaka wewe?”
“Ndio”
“Ulijuaje kama anataka kukubaka? Ulishawahi kubakwa?”
Yani walimu walichukia sana, walitamani hata kumwambia huyu mzee amuhamishe mtoto wao ili waepuke ule usumbufu wake, wakati kabla Erica hajajibu alifika mwalimu wa taalumu na kusema kuwa mzazi wa Erica yupo nje anamsubiri mtoto wake, basi mwalimu mmoja akasema,
“Eeeeh vizuri sana, mwambie aje”
Basi yule mzazi wa Erica akaitwa, alipoingia tu ofisini, macho yake yaligongana na macho ya baba Abdi kwani ni watu waliofahamiana.
ITAENDELEA