SEHEMU YA 46
Alifika sebleni na kumkuta dada yake nae akionyesha sura ya hasira ila alimpokea na kumkaribisha vizuri, sema dada yake nae aligundua kuwa mdogo wake ana matatizo basi aliomba kuongea nae kwanza ili kujua kakumbwa na matatizo gani, ikabidi watoke pale ndani ya nyumba na kuelekea kwenye bustani ili kuweza kuongea maana hata yeye aliona vyema akimwambia dada yake atapumua,
“Nini kinakusumbua mdogo wangu? Una maisha mazuri, mumeo anakupenda sana, huna mawazo kama hela ipo, tatizo ni kitu gani yani nini kinakusumbua?”
“Ni Angel dada”
“Kafanyaje Angel/ niambie mdogo wangu, usikae na kitu moyoni maana kitakuumiza zaidi natumai unaelewa nikisema hivyo”
“Naelewa dada”
“Haya, niambie”
Basi akamsimulia kwa kifupi jinsi ambavyo amemkuta Angel,
“Kheeee hatari, kwahiyo kambaka?”
“hapana hajambaka ila ningechelewa kidogo tu basi angembaka jamani mwanangu”
“Pole sana mdogo wangu, huyu Angel nae kwanini amekuwa hasikii kiasi hiko jamani? Huyo mwanaume nae amekuchanganya kwanini?”
“Nadhani dada sijawahi kukwambia kuhusu hili, kuna mwanaume alikuwa akiitwa George, nilikutana nae kipindi nasoma chuo, mwanzoni niliamini ananipenda kumbe anahitaji msichana bikra, yani alipotembea na mimi na kukuta si bikra aliniacha peke yangu nikiwa sina hata nauli, nakumbuka siku hiyo nililia sana na kulaumu kwanini nilimuamini kiasi kile nilichomuamini. Nikaja kujua ukweli kuwa huyo mwanaume ni muhuni balaa, na pale alipo ameathirika yani kaathirika kitambo sana, yule rafiki yangu Dora alitembea pia na huyu George, halafu leo nimemkuta anataka kunibakia mwanangu kwakweli nimeumia sana, kwanini mimi jamani? Kwanini mimi nafanyiwa hivi!! Yani watu wananifatilia na utu uzima huu jamani, sio wakati wangu wa kulia kwasasa, ila kwanini Angel ananitesa kiasi hiki, kwanini huyu mtoto ananieleleza sana mimi!”
“Nadhani ni vyema sasa ukamwambia Angel asili yake, anatakiwa amfahamu babake wa ukweli”
“Mmmh si ndio itakuwa balaa”
“Hapana, unatakiwa kumueleza Angel kuhusu ukweli wa maisha yake, mueleze jinsi ulivyohangaika nae, mueleze jinsi babake alivyokutenda, ili kama akiamua kuyafanya maisha yake hovyo ajue ukweli kabisa kuwa anakuumiza kwa kiasi gani, mwambie Angel ukweli”
“Nasubiri hata afike chuo ndio nimwambie ukweli maana kwasasa nitaichanganya akili yake, unajua siku zote Angel anajua huyu ndio baba yake mzazi! Kwakweli nimepata mume mwenye upendo sana, yani anampenda mwanangu hadi nafurahia kwakweli, sijui ningefanyeje mimi kama huyu asingekuwa mume wangu ila kwanini Angel ananifanyia hivi jamani!”
“Mwambie ukweli, nakwambia mdogo wangu ukweli utakuweka huru, mwambie ukweli. Si unaona kama Junior anaelewa fika kama baba yake alikuwaje”
“Eeeeh tena bora umenikumbusha dada, nilikutana na Dora, nasikia James amekufa”
“Ndio amekufa”
“Kumbe unajua dada?”
“Najua vizuri ila sikuwaambia wala nini, kwanza ni kujichoresha, kwa yule mwanaume niliondoka mwenyewe, sasa niseme kitu gani? Alikufa ndio”
“Eeeeh aliumwa nini?”
“Na wewe nawe, aliumwa nini kivipi? Si alikuwa na ukimwi yule? Ila hapa mwishoni nasikia alianza tena uhuni yani uhuni ndio ulipamba moto na amefia guest akiwa na mwanamke, sasa sijui kitu gani ila kafia guest”
“Kheee shemeji nae, hakuacha uhuni jamani loh!”
“Basi ndio naimba wimbo mmoja na Junior kila siku, baba yake kafia guest sijui nay eye anataka hivyo jamani! Katoto kale kanahitaji maombi kwakweli, peke yangu siwezi, nishamkanya hadi nimechoka jamani ila mtoto hasikii hahambiliki jamani”
“Kheee pole dada”
“Ila sio kilichonileta huku, bali kilichonileta ni watoto wa wifi yako jamani mimi nimechoka, huyu tumaini anaweza fanya tuharibu undugu kwakweli”
“Eeeeh wamefanyaje tena dada”
“Watoto ni wavivu wale sijapata kuona, ila ni malezi ambayo mama yao kawalea yani tumaini kawaendekeza sana watoto wake jamani, yule mdogo yupo darasa la pili ila hawezi kufua hata nguo yake ya ndani jamani! Malezi gani haya sasa? Kwakweli Tumaini anakera, yani watoto wake wananikera jamani, nilijua nitamkuta mumeo nilitaka niongee nae ili aongee na dada yake, mimi nimechoka jamani”
“Pole, tulipotoka kanisani kuna mahali alipitia”
“Ila jamani Mungu huyu kweli mkali, hadi mumeo nae anaenda Kanisani mmmh! Yani kabadilika kabisa kama sio yeye, ila wanaume hawaaminikagi ujue”
“Kivipi dada? Unamaanisha atakuwa ananisaliti?”
“Sina maana hiyo”
Mara simu ya mama Junior ikaita na kumfanya aipokee ila alipata habari ya kumshtua kidogo na kumuaga mdogo wake,
“Vipi tena dada?”
“Nasikia Junior huko kapiga mtu, sasa kashikiliwa polisi. Ngoja niende”
“Kheee watoto hawa jamani, tuzaage tu kutoa machango tumboni, hawa wangebaki kwenye viuno vyetu basi tungetolewa uvimbe kama kichwa cha mtu. Pole dada, utaniambia yatakayojiri”
Basi mama Junior akaondoka na mama Angel alirudi ndani.