SEHEMU YA 32
Angel alienda chumbani kwa mamake sasa ila alishangaa sana siku hiyo wala mama yake hakumfokea wala hakumwambia kiukali zaidi zaidi alimwambia akae ili wazungumze, basi Angel alikaa na kuanza kuongea na mama yake,
“Eeeh niambie mwanangu Angel ulikuwa unataka simu umpigie nani?”
“Nilitaka nimpigie Hanifa mama”
“Niambie ukweli, kumbuka mimi ni mama yako Angel”
“Naelewa mama ila huo ndio ukweli”
“Haya, simu hii hapa mpigie huyo Hanifa hapa nisikie unachotaka kuongea nae”
Muda huo huo akakumbuka kile alichoahidiana na Hanifa kuwa watoroke Ijumaa, akaona akimpigia simu itakuwa ni msala kwake kwahiyo akajigelesha kupiga ile simu.
“Ila mama jamani, naomba tuache tu hata sikutaka kupiga simu”
“Kwahiyo unanidanganya mimi Angel eeeh!”
“Hapana mama”
“Haya, piga ulipotaka kupiga, au ulitaka kumpigia Samir”
“Jamani mama mbona hivyo, yani mama mambo yako kama askari hadi tunakosa uhuru humu ndani”
Basi Angel akainuka ili aondoke, mama yake akamvuta nyuma na kumnasa kofi kisha akamfokea,
“Mjinga wewe, umeona leo nimeongea nawe kwa upole basi unajifanya kuleta kiburi, mimi sio shangazi yako wa kumfanyia jeuri”
Muda huo simu ya mama Angel ikaanza kuita kwahiyo mama Angel alimwambia Angel atoke mule chumbani kwake na kupokea ile simu, ila mpigaji alikuwa ni dada yake na kuanza kuongea nae,
“Mbona unaongea hivyo mdogo wangu jamani”
“Si huyu Angel jamani, ataniua kwa presha huyu mtoto dah!”
“Kafanyaje tena?”
“sheleni kwao kuna kivulana kinaitwa Samir sijui sasa ndio kinamsumbua akili, kweli leo hii naongea halafu Angel ananiambia naongea kama askari, eti nawanyima uhuru kweli Angel wa kunijibu hivi!”
“Ila mdogo wangu mambo mengine umeyataka mwenyewe, huyo mtoto toka mdogo kazi kumsifia tu, oooh mwanangu mzuri sana, mwanangu mzuri kama malaika, haya sasa ndio anakuonyesha mambo ya uzuri wake, nilikwambia mdogo wangu ni kweli mwanao ni mzuri ila usimsifie kupitiliza, umeona sasa ameanza kukujeuria hadi wewe. Pole mdogo wangu, nisingekuwa na majanga ningesema huyo Angel aje kukaa kwangu kidogo ila na mimi mwanangu tu huyu ananitoa pumu, dawa ya Angel mpeleke kwa mama yani akikaa na bibi yake huyo atashika heshima na adabu”
“Sawa dada, nashukuru kwa ushauri wako nitaufanyia kazi. Eeeeh niambie”
“Sasa mwenzangu ni kuhusu huyu wifi yetu maana sio wifi yangu tu ila ni wifi yetu, kwakweli kuolewa ukoo mmoja ni vibaya jamani, miukoo mingine ni shida tupu jamani”
“Unamaanisha Tumaini? Kafanyaje?”
“Ndio huyo huyo, kwani mimi na wewe tunashea wifi yupi? Si ndio huyo mdogo wangu, yani ananipasua kichwa kwakweli”
“Anafanyaje dada”
“Yani kaleta mitoto yake kwangu, mwezi umepita sasa halafu yeye nasikia yupo Arusha anakula bata na mumewe”
“Khee wote wanne?”
“Ndio, watoto wenyewe kawazaa kama ngazi halafu wote kawaleta kwangu jamani, kisa nyumba zetu zipo karibu, najuta kuwafahamu, wakati huo ana dadake nae katuma wanae wawili waje kwangu jana, kwakweli Napata mawazo mimi jamani. Junior anisumbue kichwa na mawifi nao wanisumbue kichwa kwanini lakini!”
“Pole sana dada yangu jamani”
“Ongea na mumeo jamani, aongee na dada yake”
“Ila kumbuka na mumeo nae ni dada yake”
“Hamsikilizi ila mumeo atamsikiliza, kuna vitu Tumaini anamuheshimu sana kaka yake huyo, naomba umwambie jamani nimechoka, yani nimechoka la sivyo nawaleta hawa watoto na kwenu ili tusaidiane majukumu ya kulea, aliona raha kuzaa kila siku halafu kulea kunamshinda jamani loh!”
Dada wa mama Angel alionekana kuongea kwa hasira sana kuhusu wifi yao huyo ambaye wamechangia undugu yani mume wa mama Angel ni kaka wa Tumaini ambaye wamechangia baba na mume wa mama Junior ni kaka wa Tumaini kwa upande wa mama yani amechangia nae mama halafu huyo Tumaini kaolewa na kaka yao.
Basi waliongea pale na kuagana ila mama Junior alionekana kuwa na hasira sana na huyo wifi yao.