SEHEMU YA 217
Angel alitulia chumbani kwake huku akifikiria siku hiyo alivyobambwa, ila akaja kuletewa taarifa na mama yake kuwa ajiandae maana ataondoka na bibi yake,
“Aaaah mama jamani, nyie si mmenitoka kunitoa kwa bibi yule!”
“Sitaki maneno mengi Angel, jiandae hapo ulipo na ujue kabisa kesho unaondoka na bibi yako”
Kisha mama yake akatoka na kumfanya Angel abaki amekasirika sana kwani bibi yake huyo alimfahamu vizuri sana, basi akachukua simu yake na kumtumia ujumbe Samir,
“Mwenzio nimeambiwa kuwa kesho nitaondoka na bibi, jamani umeniponza Samir, yule bibi alivyomkali yani itakuwa ngumu kwetu kuonana”
“Usijali Angel, tutaonana tu. Maana huyo bibi ni kama bibi yangu ila najua kuonana kwetu kutakuwa kwa masharti sana ila usijali”
“Sawa, yani nimekosa hata amani halafu kumkatalia mama siwezi”
“Sawa mpenzi nimekuelewa kabisa, usijali kitu”
Basi Angel aliamua tu kufanya maandalizi kama alivyoambiwa na mama yake ila kiukweli hakupenda kwenda kuishi kwa bibi yake kwani alielewa malezi ya bibi yake huyo yalivyokuwa.
Wakati akiendelea kujiandaa, mara aligonga Vaileth mlango wake na kumkaribisha kisha Vaileth alianza kuongea nae,
“Angel nasikia kesho unaondoka na bibi, ni kweli?”
“Ndio hivyo, yani nitakoma maana huyo bibi namfahamu fika alivyo na mambo yake”
“Ooooh pole mdogo wangu, jinsi huyu bibi anavyojua kufatilia mambo yani hadi nakuhurumia”
“Yani acha tu, nimechukia hapa balaa, wewe umewasikia au?”
“Ndio, nimewasikia wakiongelea basi nikamsema mmmh nimeanza kuwa Erica sasa kusikiliza yasiyonihusu”
Angel alicheka na kusema,
“Yani kale kaErica sijui tabia ya umbea katoa wapi jamani, mtoto ni mbea yule sijapata kuona, baba sio mbea, mama sio mbea ila yeye sasa akipata jambo anawashwa mdomo balaa”
“Mmmh Angel una maana gani sasa?”
“Aaaah sina maana yoyote, ila Erick na Erica kiukweli kabisa hawafanani, si sura wala sio matendo yao maana Erick ni mstaarabu, muelewa na mpole, ila Erica sasa uwiii ni mbea, anapenda kufatilia mambo ya watu, akisikia tu watu wanaongea kidogo basi yeye kashayabeba, yani yule mtoto jamani!”
“Labda kuna ndugu yenu yuko hivyo, maana mbona Erica kafanana sana na mama yako! Yani kafanana nae sana kasoro huo umbea”
“Aaaah aliyefanana na mama ni mimi bhana na sio Erica”
Basi Vaileth akacheka tu, halafu Angel akaendelea kuongea,
“Ila licha ya hivyo jamani Erica ni mbea hadi huwa siongei nae mara kwa mara wakati ni mdogo wangu ningekuwa napanga nae vitu vingi ila umbea wake hadi unakera”
Vaileth alicheka na kumuacha Angel aendelee kujiandaa.
Erick alipomaliza kuosha gari yani siku hiyo anaonekana hata hakupenda Sarah kwenda nyumbani kwao, basi alimwambia asubiri aende kuoga kwahiyo Sarah alimsubiri kule kule nje walipokuwa wakiosha magari, muda huo hata Junior alishaingia ndani na kujiandaa ila muda kupita bila ya Junior wala Erick kurejea Sarah alijiuliza kuwa tatizo ni nini, ila alipotaka kuinuka tu alifika pale Junior na kusema,
“Kheee bado upon je jamani mtoto mzuri dah! Karibu ndani jamani”
Basi Sarah aliongozana na Junior hadi ndani ambapo muda huu walimkuta mama Angel sebleni na baada ya kumuona tu Sarah alitabasamu ambapo Sarah nae alitabasamu kisha akaenda kumkumbatia huku akimuuliza,
“Eeeeh za kwenu Sarah!”
“Nzuri tu, mama anakusalimia”
“Oooh wow, naomba ukirudi usalimie pia binti yangu. Vipi lakini za tangu siku ile”
“Ni nzuri kabisa”
“Nafurahi kusikia hivyo na nimefurahi kukuona kwa leo, kumbe kweli Erick alivyosema kuwa unakuja, oooh nimefurahi sana”
“Na mdogo wangu hajambo!”
“Hajambo, kachangamka sana kwasasa”
Basi bibi Angel akaja na mtoto Ester amembeba maana alikuwa ameamka, basi yule bibi alivyofika pale Sarah alimsalimia vizuri sana na akahitaji pia kumsalimia mtoto ambapo bibi alimpa ili amsalimie ila leo wakati Sarah amekaa na yule mtoto akasema,
“Yani mama jamani huyu mtoto amekufanana hatari, leo ndio nimemuangalia vizuri, ni wewe mtupu”
Mama Angel alikuwa akitabasamu tu ila bibi Angel aliongezea na kusema,
“Ila kweli Ester kakufanania sana jamani, yani Ester kakukopi vile ulivyo hapa mwanangu umejizaa”
Mama Angel akamchukua mtoto wake huku akimuangalia vizuri na kutabasamu na wote walijikuta wakitabasamu na kufurahi.
Erick alijua wazi kuwa mdogo wake amechukia sana siku hiyo, kwahiyo alivyomaliza kujiandaa alienda moja kwa moja chumbani kwa Erica na alimkuta amejilaza, basi alianza kuongea nae kwa kumuamsha,
“Erica, Erica jamani Erica”
Erica alishtuka na kukaa kwanza huku akimsikiliza kaka yake,
“Sasa Erica umechukia nini jamani mdogo wangu!”
“Hapana sijachukia mbona”
“Erica, mimi nakufahamu vizuri sana na najua umechukia baada ya kumuona Sarah, hebu nisikilize hili kwanza”
Erica alikaa vizuri na kumsikiliza kaka yake,
“Sikia Erica, katika maisha yangu basi wewe ndiye ndugu yangu bora sana, kumbuka tumezaliwa wote na tumenyonya wote, tumecheza wote michezo yote inayojulikana, ukilia nipo, nikilia upo, nakuonea huruma na unanionea huruma. Jamani uwepo wa Sarah ndio ukuondoe amani jamani Erica! Kumbuka mimi ni nani kwako, kumbuka jinsi tulivyo mimi na wewe, yani Sarah ni mpita njia tu, tena ningependa awe rafiki yako maana ni rafiki yangu pia, akiwa rafiki yako utaona kuwa hana matatizo yoyote yale, usiwaze vibaya mdogo wangu nakupenda sana”
Kisha Erick alimsogelea mdogo wake na kumkumbatia, kitendo hiko kilimfanya Erica ajihisi vizuri, kwani katika maisha yake alikuwa akipenda sana kujihisi kuwa anapendwa ndiomana hata swala la kuwa mtoto wa mwisho alilifurahia sana kwani aliona atakuwa akipendwa mno na wazazi wake, huku wakimsikiliza na kumthamini yeye, ila baada ya kupata mdogo wake aliamua kuishi kwa kutokudeka ila bado anapenda sana kugundua kuwa anapendwa sana kwahiyo alifurahi, kisha Erick alimuomba kuwa waende pamoja kuongea na Sarah ambapo Erica alikubali na wakaenda pamoja.
Basi waliongea na Sarah pale mambo mbalimbali hadi Sarah alipoaga na mama Angel kumwambia tena Erick kuwa ampeleke, ila Sarah alikuwa akipenda sana ule muda way eye kuwa peke yake na Erick kwahiyo siku hiyo hakufurahi sana kwani aliona kama Erica anambania vile.
Muda wa kuondoka, bado Erick alimuangalia Erica na kumtaka wamsindikize kwa pamoja Sarah, kwahiyo siku hiyo walipanda kwenye gari watatu yani Erick, Erica na Sarah na siku hiyo Sarah alikaa siti ya nyuma kwani pale mbele isingewezekana kukaa watatu.
Moja kwa moja walienda hadi kwakina Sarah yani siku hiyo kwenye gari ilikuwa ni kimya kimya, tofauti na ile siku ya kwanza ambayo walikuwa wakiongea mambo mbalimbali wakati wapo Erick na Sarah tu.
Walifika nyumbani kwakina Sarah na walimkuta mama Sarah ambaye alipowaona kama kawaida alishindwa kujizuia machozi yake kwa Erick, kwani alimsogelea na kumkumbatia huku akilia, na leo alilia kwa muda mrefu kidogo kwahiyo Sarah na Erica walisimama pembeni tu wakimuangalia jinsi yule mama alivyomkumbatia Erick huku akilia, na baada ya hapo aliwalazimisha kuingia ndani kwake ili kupata chochote cha kula, ila leo Erica aliweka mgomo na kudai kuwa wana haraka sana kwahiyo ilibidi wage tu na kuondoka zao.
Wakiwa ndani ya gari Erica alimuuliza Erick,
“Kwahiyo hata siku ile ulipokwenda kumsindikiza huyo Sarah ulikula kwao? Naona tu maana hata leo bila ya mimi ulitaka kukubali, ushasahau mama huwa anasemaje?”
“Mmmh jamani Erica, mbona hata Sarah anakula kwetu kwanini sisi tushindwe kula kwao?”
“Kula sehemu ni mpaka mama akubali, uoni mimi nilikuwa nakuja na visheti nyumbani! Ingawa nilikula vingine kisirisiri ila mama alinisema sana na nilimuahidi kutokurudia tena, sisi tutakula kwakina Sarah mpaka pale mama atakapomfahamu vizuri mamake Sarah”
“Mmmh wewe nawe kwa kukuza maneno hujambo”
Basi waliendelea tu na safari na kurudi nyumbani kwao.
Baba Angel alirudi nyumbani kwake na kama alivyokuwa amemuahidi mke wake basi alirudi na zawadi ya kumpa mama yao, ambapo moja kwa moja alienda kumkabidhi zawadi hizo, hata bibi Angel alizifurahia sana kisha baba Angel sasa moyo wake ukawa mweupe kumruhusu mama yao,
“Sasa mama, moyo wangu mweupe kabisa nakuruhusu”
“Kumbe mlinikataza sababu ya zawadi jamani watoto wangu! Mmesumbuka jamani!”
“Hamna mama hata usijali kitu, inapaswa kufanya hivi kwako maana umetuhudumia sana hapa nyumbani, umetulea, umeacha mambo yako mengi sana kwaajili yetu kwahiyo yatupasa kufanya hivi mama”
“Haya, nashukuru sana wanangu”
Basi baba Angel alirudi chumbani kwake kwani alikuwa amechoka, mke wake alimfata na kumpa habari kuwa Angel ataondoka kesho na mama yao,
“Jamani, tunampa tena mama mzigo wa Angel?”
“Hamna, mama atakaa nae vizuri tu, naomba ukubali hilo mume wangu. Naelewa mama yangu alivyo”
“Hata mimi namuelewa sana”
“Unajua leo mama kamkuta Angel na Samir getini kwakweli kachukia sana, halafu anamfahamu vizuri sana Samir, hamfai mtoto wetu, nasikia baba yake ni muhuni sana kwahiyo lazima Samir atakuwa na tabia za baba yake. Halafu siku ile ulisema kuna mtu unamfananisha na Samir ni mtu gani?”
“Oooh nitakuonyesha tu siku moja, utamuona ila unamfahamu sema humfahamu kivile ni rafiki yangu”
“Oooh hapo sawa, nikajua ni ndugu yako”
Baba Angel alicheka kwa muda kidogo na kusema,
“Ila huyo rafiki yangu sio muhuni kwahiyo hawezi kuwa baba wa Samir”
“Na kweli maana duniani ni wawili wawili, ila hata hivyo mara nyingine unakuta mtoto na baba wanafanana kwa mbali sana kama wewe na baba yako mlivyokuwa”
“Oooh umenikumbusha yule mzee wangu, alikuwa ni mzee mtata, ila nilimpenda jamani baba yangu, dah angekuwepo hadi leo aangalie wajukuu zake”
“Na hivi Angel alivyokuwa anavutia unadhani baba yako anagejistahi amuache!”
“Mmmh ushaanza hivyo na maneno yako ya kijinga, hata kama baba alikuwa na tabia mbaya ila bado asingeweza kumtamani mjukuu wake, kwani Angel ni kama mjukuu wake pia. Halafu kumbuka japo fadhila za baba yangu jamani, kumbuka baba ndio alisimamia harusi yetu yote yani yeye ndiye aliyegharamia kila kitu, kumbuka pia wakati unajifungua hawa mapacha wetu ni baba yangu ndio alikuwa karibu”
“Ila Erick hujui tu, mimi nafahamu mambo mengi sana ila sikuweza kukwambia kwani sikutaka ugombane na baba yako, hujui tu ni kwanini baba yako aligharamia harusi yetu na kuhusu kuwepo wakati najifungua ilibidi iwe vile kwani ni yeye aliyekupa kazi wewe kwahiyo hakukuwa na namna zaidi yayeye kuwepo. Namshukuru kwa mazuri aliyotufanyia, ila Erick baba yako alikuwa ni kichomi, hujui ni nini alikuwa akiongea na mimi kila alipokutana nami, kuna mengi yapo kwenye moyo wangu nadhani nikisema utaona kamavile namkosea heshima marehemu mkwe wangu. Ngoja niishie hapo”
“Ndio bora uishie hapo maana sio vizuri kuwaongelea vibaya marehemu”
Muda huo waliamua kubadili mongezi na kuendelea na maongezi mengine ya jinsi ya kumfikisha mama yao nyumbani kwa siku ya kesho.