SEHEMU YA 169
Usiku wakati wa kulala, Erica alimfata Vaileth chumbani na kuanza kuongea nae,
“Basi leo nimemsikia mama akiongea na simu na mama mkubwa, na walikuwa wakiongelea kuhusu wewe na Junior”
Vaileth akashtuka kidogo na kuuliza kuwa alikuwa akiwaongelea kitu gani,
“Inasemekana wewe na Junior mna mahusiano ya kimapenzi, sasa mama kasema kuwa atawachunguza”
“Mmmmh ila Erica, kuna muda huwa unakera ila kuna muda huwa unafaaa sana kwa matumizi mbalimbali. Asante sana kwa ujumbe wako”
“Ila je ni kweli kuna mahusiano yanaendelea kati yako na Junior?”
“Mmmh jamani Erica, kama ni kweli kuna siku nitakwambia mwenyewe”
“Kwahiyo sio kweli?”
“Naomba tuachane na habari hizo, kwani nahitaji kupata muda wa kupumzika kwasasa”
Erica aliagana nae na moja kwa moja alienda chumbani kwa kaka yake ili kumpa huo ujumbe, ila muda ameingia chumbani kwa kaka yake basi kaka yake nae alikuwa ametoka bafuni kuoga, kwahiyo Erick alimkuta moja kwa moja Erica yupo chumbani kwake na kumuuliza,
“Vipi una mpya gani?”
“Ni hivi, nimemkuta mama akiongea na mamkubwa na walikuwa wakiongelea swala la Vaileth na Junior. Je wewe unahisi kuwa Vaileth na Junior wana mahusiano?”
“Kwani wakiwa na mahusiano tatizo ni nini? Vaileth na mwanamke na Junior ni mwanaume”
“Mmmh jamani, ila kumbuka Vaileth ni dada yetu. Kwahiyo Junior ana mahusiano na dada!”
“Kwani wewe unatakaje? Unataka Abdi aletwe hapa ili nae uishi nae nyumba moja”
Erica aliinuka huku akicheka kicheko cha kimbea na kusema,
“Sio Abdi bhana, saivi ni mambo ya Bahati”
Halafu Erica akaondoka zake, ile kitu ilimfanya Erick ajiulize maswali mengi sana, kuwa huyo Bahati ni nani? Anajua tu kuwa Erica alipewa viatu na mwanaume ila hakumjua huyo Bahati, kwahiyo alijikuta akitamani sana kumfahamu huyo Bahati ambaye kwa muda huo ametajwa na Erica, basi alitafakari kwa muda kidogo ila hakupata jibu wala nini.
Moja kwa moja aliamua zake kulala tu.
Kulipokucha, walijiandaa kwaajili ya kwenda shuleni kama kawaida, basi Erick alienda shuleni ila siku hiyo gari lao la shule lilipata hitilafu kidogo kwahiyo dereva alisimamisha na kuanza kutengeneza gari lile, wakati dereva akitengeneza gari lile, baadhi ya wanafunzi walikuwa wameshuka na wapo pembeni ya gari wakiangalia kinachoendelea ndipo alifika binti mmoja ambaye walikuwa wakisoma nae ila Erick hakuwa na mazoea na binti huyo kwani yeye hakuwa na ukaribu kabisa na watoto wa kike, basi yule binti alimfata Erick karibu na kuanza kuongea nae,
“Naitwa sarah! Nipo kidato cha pili”
“Oooh, mimi nipo kidato cha kwanza”
“Unajua nimekuangalia sana, mbona unaonekana umekaa peke yako peke yako kwani una tatizo gani?”
“Hapana, sina tatizo lolote”
“Hupendi kuongea na watu? Ila unaonekana unatokea kwenye familia nzuri sana, unajua katika maisha niliwahi kusikia stori moja hivi kuwa mahusiano mazuri ya kimapenzi huanzia shuleni”
“Unazungumzia nini kwani?”
Lile gari lilitengemaa na wanafunzi wote walirudi kwenye gari halafu safari ya kwenda shuleni ikaendelea.
Ila walipofika shuleni, yule binti alimpa Erick ujumbe halafu yeye aliondoka zake na kuelekea darasani kwao, kwakweli Erick alimshangaa sana na hakuelewa kuwa yule binti alikuwa na maana gani.
Nyumbani siku hii walibaki Junior na Vaileth tu, ambapo Vaileth alimueleza Junior kile ambacho aliambiwa na Erica,
“Nilijua tu, yani mama yangu huwa anaacha kufatilia mambo ya maana ila yeye huwa anakazana na kufatilia ujinga tu ambao huwa haumsaidii chochote kile.”
“Ujinga upi?”
“Sasa aanze kunifatilia mimi kweli ataweza? Mbona kipindi kile hakuweza, kiukweli Vaileth umebadilisha sana maisha yangu, tena umeyabadilisha kwa kiasi kikubwa sana kwahiyo hata waseme kitu gani kwangu ni sawa ma bure tu”
“Ila tunatakiwa kuwa makini sana, kwani tukigundulika kuwa tupo pamoja ni hatari kubwa sana. Ni hatari kwangu na ni hatari kwako pia”
Muda kidogo alifika mgeni, na mgeni huyo alikuwa ni mama Junior, hakwenda kwa taarifa kwavile alitaka ajaribu kuona kuwa ni kitu gani kinaendelea.
Basi Junior alikaa na mama yake na kuanza kuzungumza nae,
“Mama, hivi bamdogo alikueleza kuwa ni mazingira gani ambayo alinikuta nayo mimi kabla ya kuchukua uamuzi wa kuja kuishi nae hapa kwake?”
“Kivipi?”
“Bamdogo alinikuta mimi nikiwa guest, na nilikuwa na mwanamke mkubwa sana. Kiukweli maisha yangu yaliharibika sana na kila kitu mlichokuwa mnanisema niliona kama ni kumpigia mbuzi gitaaa. Ila nakuuliza sasa, je maisha yale na haya ninayoishi sasa yapi ni bora?”
“Sikuelewi Junior, kwani unazungumza kuhusu nini?”
“Mama, jana nimekuja kwako kukuona nikiwa nimeongozana na Vaileth ila umeanza kunihisi vibaya, hata kitendo chako cha kufika leo hapa ni kwamba unataka kunichunguza. Hivi mama umeshindwa kunichunguza siku zote hizo ndio unichunguze leo kweli? Unajua wazi kuwa sipendagi unafki, niambie mimi wazi ni kitu gani unanihisi sio kuanza kunichunguza chunguza. Haya nikiwa na mahusiano na Vaileth, je wewe nakupunguzia kitu gani mama yangu? Kwani Vaileth sio mwanamke wa kufaaa kuwa na mimi? Watoto wa kike ndio huwa wanachungwa kwani wanaweza leta mimba nyumbani, ila mtoto wa kiume sio wa kuchungwa, nikileta watoto kwako ni baraka kuwa mtoto wako ni rijali”
Mama Junior alimuangalia mwanae na kutikisa kichwa, kwakweli hakuona kabisa umuhimu wa yeye kuendelea kuwepo kwenye eneo lile, kwani muda huo huo aliamua kuondoka tu.
Kwakweli mama Junior alitembea njiani huku akitafakari mambo mengi sana na kusema,
“Kweli mtoto wa nyoka ni nyoka, yani huyu Junior ni tabia za baba yake mtupu, kupenda wanawake, na muda wote kuona kuwa anachofanya yeye sio kosa yani anaona kuwa anachofanya yeye kipo sahihi. Yani hapa kwakweli sijazaa kabisa bali nimeingia kwenye matatizo”
Wakati akitembea mara akashikwa bega, kugeuka alimuona mtu ambaye alimfahamu vizuri sana, na kumshangaa,
“Kheee wewe kumbe upo?”
“Nipo dada, kwanza kabisa naomba unisamehe kabisa kwa yote ambayo nilikukosea”
“Kumbe bado unayo hayo?”
“Unajua, kuna muda huwa nafikiria sana kuhusu wewe na kuona kuwa kiburi nilichokufanyia basi leo kimekuja katika maisha yangu”
“Kivipi?”
“Mimi nilikuwa msichana wako wa kazi na ulinilea vizuri kabisa, ulinifanya kama mdogo wako ila sikuwa na huruma kwani niliamua kutembea na mume wako hadi kupata ujauzito, mumeo alinipangishia nyumba na kuanza kuishi na mimi kwa siri siri hadi siku ambayo wewe na mdogo wako mlikuja na kufanya fujo katika nyumba ile. Dada nikianza kukuelezea niliyopitia kwa hakika utanihurumia sana, ila kwa kifupi na mimi nilipata bahati ya kuolewa, ila unajua kilichotokea kwangu? Mume wangu pia alienda kuzaa na msichana wa kazi, yani dada huwa nalia mno kwani maisha kumbe ni duara, yanazunguka pale pale”
“Usijali, kwangu yalishaisha kitambo sana. Hajambo mwanao?”
“Hajambo, ila ninao na wengine. Mwanangu yule nilimuita James, jina moja na baba yake, yule mtoto alikataa shule, yani kanisumbua sana, kwasasa anaishi na mjomba wake, ila ana matukio mengi ambayo hayafurahishi hata kidogo. Kuna muda huwa najutia sana, na kujilaumu sana, ila ndio hivyo maji yakimwagika hayazoleki wala nini. Nimefurahi kukuona tena, kama hutojali basi naomba mawasiliano yako”
Mama Junior hakuwa na pingamizi la aina yoyote ile zaidi zaidi ya kubadilishana namba na yule mwanamke, wala hakutaka kumfikiria sana kwani kwa muda huo hata yeye alikuwa na mawazo yake ya kutosha tu.